Mimi binafsi siku za nyuma niliwahi kuunguliwa moto na biashara yangu ya kioski iliyokuwa Kariakoo maeneo ya Msimbazi, kila kitu kiliteketea kuanzia mafriji, mali zote na pesa. Tena isitoshe nilikuwa na mkopo mahali fulani katika hizi taasisi za fedha lakini wala wazo la kudai taasisi walao inifikirie au hata kunisamehe marejesho ya mkopo ingawa taasisi hiyo ilikuwa na kitu kinachoitwa bima sikufikiria kabisa wala kuwafikishia taarifa hizo.
Baadaye nilipokuja kuelewa vizuri maswala ya bima
yanavyofanya kazi ndipo nilipokuja kugundua kumbe nilikuwa na haki ya kudai
kampuni inayotoa bima kwa ile taasisi inilipe kwa ajili ya janga la moto lililoikumba
biashara yangu. Nilijikuta najikamua kisawasawa mpaka nikamaliza marejesho ya
mkopo ule ambao wakati janga linatokea sikuwa hata nimefikisha nusu ya
marejesho.
Matatizo kama hayo huwakumba wajasiriamali wengi, lakini
kitu wasichokijua kabisa ni kwamba bima mtu unaweza ukakata kwa kitu chochote,
kuna bima za maisha , elimu, biashara, magari moto na kila aina, isitoshe
haziangalii ukubwa wa shughuli, unakata bima na kuilipia kulingana na ukubwa wa biashara /shughuli
yenyewe. Kwa kweli mimi sioni hasara ya kutoa kwa mfano shilingi laki moja kwa
mwaka mzima, hata kama ikiwa janga halitatokea ukilinganisha na hasara
inayopatikana endapo itatokea bahati mbaya biashara au shughuli yeyote ile
ikakumbwa na mkasa utakaosababisha hasara isiyomithilika kama moto wizi,
mafuriko, ulemavu, kifo nk. BIMA NI ULINZI KWA BIASHARA YAKO.
Hivi karibuni katika Redio ya CAPITAL FM inayorusha
matangazo yake jijini Dar es Salaam
kulikuwa na mahojiano mazuri sana kuhusiana na umuhimu wa Bima na elimu ya pesa
ambapo Kamishna mkuu wa Bima nchini Tanzania Bwana Israel Kamuzora alikuwa akifafanua jinsi ambavyo bima
inavyoweza kusaidia kuinua uchumi na kuutokomeza umasikini. Chini tumeweka
sehemu tu ya mahojiano hayo kwa sauti pamoja na maelezo hayo pia katika
maandishi yakiwa yametafsiriwa sawasawa kama alivyoyatamka.
“……fundi magari…, au mjasiriamali unayeuza uza vitu
sokoni, sasa ukiugua kwa wiki moja mtaji wote umekufa, kwanza wateja wamekuja
hawakukupata mahali unapokaa kuuza mchicha, haupo, kwa hiyo watapata mteja
mwingine, kwa hiyo umepoteza soko, lakini jambo la pili, ule mtaji wako
unaoutumia katika kufanya biashara, ule mdogomdogo, woote umekwenda, kwasababu
umekwenda kutibiwa, utafanyaje?. Kwa hiyo kuna Bima ambayo ukilazwa hospitali inakulipa gharama
ile ambayo kiwango kitakusaidia ili utakapotoka hospitali, kila siku kile
kiwango, utakapotoka hospitali kwa siku
ulizolazwa hospitali, utakapotoka hospitali upate pesa itakayokurudisha katika biashara,
inaitwa “Hospitalization Cover” kwa kiingereza.
Kwa hiyo zipo Bima nyingi zimeanza kutoka za watu wa
kipato cha chini. Nyingine ni Bima ya kilimo, sasa hivi kuna makampuni matano
ya Bima, yameingia katika kuuza bima kwa wakulima. Umeenda kulima shamba, na
ulipokwenda kulima shamba, dalili zote zilionyesha kwamba mvua itanyesha, na
ukapanda mbegu. Mvua ya kwanza ikanyesha, ya pili pengine nayo ikanyesha,
lakini ya tatu na ya nne ya kukuzia zile mbegu, haikuja. Kwa hiyo yale mahindi
kama yalikuwa yameanza kuota yamefika mahali paku…Sasa utafanyaje!. Na wewe
ulikuwa umeingiza pesa katika kulima. Umekwenda kununua mbegu, umeweka mbolea,
nguvu zako na mategemeo yalikuwa pale.
Kwa hiyo mbinu ya namna hiyo sasa imeingia tayari katika
soko. Kwa hiyo hii ndiyo tunaonyesha kwamba, bima inaanza sasa kusaidia ukuaji wa uchumi na kufuta
umasikini. Ukweli ni kwamba watu wachache wana elimu ya Bima, na hili huwezi
kumlaumu yeyote kwa sababu mitaala ya ufundishaji katika mashule na katika
vyuo, hata chuo kikuu, ni watu wachache sana wanakumbana na elimu ya mipangilio
ya fedha, inaitwa “Financial Planning”.
Watu wachache sana wana uelewa wa mambo ya fedha, na ni elimu yetu ndivyo
ilivyo, si Tanzania tu, ee..ni Duniani…ee.. I mean, tuseme Afrika, huko Ulaya wamesha
rekebisha rekebisha mitaala, watoto wadogo wanaelewa ee….masuala ya kununua,
kwa mfano “Shares” (hisa) ee….Katika
makampuni, wanafundishwa habari ya Bima, na Bima wanaiona nyumbani kwao
ikifanyika.
Mfano nchi kama za wenzetu zilizoendelea, hakuna mtu
anayekwenda kutibiwa hospitali kwa fedha, kwa hiyo tangu mtoto anapokuwa na
miaka miwili anamsikia mama yake ndani ya nyumba anauliza , “Kadi yangu ya matiabu ya
hospitali ya bima iko wapi”, haulizi, “Fedha iko wapi”. Sasa elimu ya namna
hiyo, ee…kule ulaya kwa mfano, ee…, hakuna mtu ambaye ananunua kitu, ee… na
mafeedha…..amebeba mfuko wa fedha kwenda
kununua……ni fedha ni ndogo anabeba fedha
kidogo tu kununua gazeti na mahitaji madpogomadogo.
Watu wanatumia kadi, au sio, sasa huku kwetu, elimu hiyo
ndiyo inaingia. Kwa hiyo elimu ya mambo ya fedha, huku kwetu, bado iko chini
sana! Na sisi tumeona kwamba pamoja na
huduma nzuri ya Bima, ambayo inatakiwa Watanzania waweze kuipata, hawaipati”.
0 Response to "BIMA NA ELIMU YA MIPANGILIO YA PESA: NI WATU WACHACHE SANA WENYE UELEWA"
Post a Comment