Kama wewe ni abiria mkaazi wa maeneo ya Buguruni, TABATA Gongo
la mboto, Kiwalani ama hata eneo lolote lile ambalo ni lazima utumie barabara
ya Uhuru, ni lazima umekwisha ionja adha
hii ya dimbwi kubwa la maji machafu mithili ya bwawa la samaki lililozuka kwenye
barabara maeneo ya Shule ya Uhuru katikati ya Sekondari ya Benjamin Wiliam Mkapa
na makutano ya Shule ya Uhuru.
Nikiwa kwenye basi aina ya costa lililokuwa likielekea Mnazi Mmmoja likitokea maeneo ya Tabata, basi lilipofika tu katika eneo hilo katikati ya bwawa, ghafla injini ya gari ilizimika ndiposa kasheshe ilipoanza. Kila abiria kuanzaia dereva wa basi, kondakta mpaka wanafunzi wa shule, kila mmoja alisema lake ilimradi tu wakionyesha hasira zao kwa utawala hasa viongozi wa serikali waliochaguliwa na wananchi.
“Nawashangaa
sana hawa viongozi, kuanzia ngazi ya mtaa, kata mpaka huko juu, wakija kuomba
kura, utawasikia wakitoa ahadi kibao kwa unyenyekevu mkubwa, lakini ona sasa,
dimbwi hili kila masika lipo na hamna anayeshughulika nalo”
Alisema mama mmoja kwa uchungu.
“Magari
ya kunyonya majitaka ya Halmashauri ya jiji yako wapi?, ni mafuta kiasi gani
yanahitajika, si waseme wananchi tujitolee wenyewe kuchanga hela ya mafuta waje
wayanyonye kuliko kutaabika namna hii…” Naye baba mmoja wa
makamo hivi alitamka.
Kijana mnwingine naye alihamaki, “Si ingelikodishwa hata pampu ya
dizeli maji yakaelekezwa kwenye chemba ambazo hazijaziba, mbona ni kazi ya dakika chache tu……! Hawa serikali kwa
kweli hawatujali kabisa sisi wananchi tuliowaweka pale”.
Alidakia dada mwingine na kusema; “Ni kwa sababu viongozi wenyewe
hawapiti hapa, wangeshaamuru patengenezwe siku nyingi, mbona ujio wa Obama
barabara yote ilifagiliwa kwa wiki moja iweje washindwe haka kadimbwi? Wenzetu
hupita Nyerere road kwa raha zao na mavingora”
“Ni
aibu kubwa, kwanza wangebadilisha hata na jina lenyewe, Uhuru road likawa
Madimbwi road” Kijana
mmoja mwanafunzi wa sekondari naye alidakia.
![]() |
Bwawa
la maji machafu ya mvua katikati ya barabara Shule ya Uhuru jijini Dar es
salaam.
|
Kwa kweli ilikuwa ni shughuli pevu, abiria kushuka
tutembee kwa miguu haikuwezekana, na wala kusukuma gari napo haikuwezekana pia.
Kila mtu aliganda garini akimsubiri kondakta na dereva wake wangeamua nini.
Kondakta alijaribu kushuka kwenda kusukuma peke yake lakini pasipo mafanikio
yeyote.
Kwa bahati njema, dereva na kondakta wake waliomba msaada
kutoka basi jingine wakafunga mnyororo uliosaidia kuikokota costa mpaka “ufukweni”
mwa lile bwawa ndipo sasa na sisi tukashuka kutoka garini. Lakini iliwabidi
kondakta na dereva wake walowe maji chapachapa kuanzia unyayoni mpaka maeneo
mengine ya mwili katika pilika pilika zile za kuufunga mnyororo.
Kwa kweli hasara ya kiuchumi na muda inayowapata wananchi wanaotumia barabara hii haimithiliki achilia mbali ile hasara wanayokula wenye magari yanayozimika pindi tu yanapojaribu kuyavuka maji hayo.
Sidhani kama gharama za kuyaondoa maji yale zinaweza zikazidi
hasara inayopatikana kila siku. Foleni ya daladala unapotokea Mnazimmoja au Posta
ndiyo hata usiseme! Inaanzia pale
Bakhresa jirani na KCB Bank, ukijakufika Karume, unakuwa hoi bin taaban! Na tayari wakati huo unakuwa umekwishatumia
zaidi ya saa moja ukiwa ndani ya gari. Kwa mjasiriamali mogomdogo hiyo ni
hasara kubwa !
Picha ni kwa hisani ya Mjengwa Blog
0 Response to "BWAWA LA MAJI KEEPLEFT SHULE YA UHURU: ABIRIA WATOA SULUHISHO."
Post a Comment