Nikiwa katika harakati zangu za ujasiriamali mitaani leo
nilipita mahali fulani mara nikasikia mabishano makali yaliyokuwa yakiendelea
baina ya vijana waliokuwa wamesimama kibarazani mwa duka moja. Mmoja wao
aliyeonekana akiongea kwa msisitizo mkubwa alikuwa akijaribu kuwaaminisha
wenzake kwamba Gonjwa hatari la Ebola limeletwa na wazungu ili kuja kuwapunguza
Waafrika.
Aliendelea kudai kwamba Wazungu siyo watu wazuri, kwani
hata Ukimwi nao ndio hao hao waliouleta. Akitoa sababu ni kwa nini madai hayo
ni kweli alisema kuwa, haiwezekani wakashindwa kupata dawa. “Kwanini Wazungu
wanaopatwa na ebola wakipelekwa kwao wanapatiwa dawa na hatimaye hupona lakini
waafrika wanaachwa wakifa?, aliuliza kijana huyo kwa hasira akimaanisha baadhi
ya wale madaktari waliopona baada ya kupewa madawa ya majaribio.
Nilishindwa kujizuia baada ya kusikiliza upotoshaji ule
uliopitiliza, nikasogea karibu na mimi nikawa miongoni mwa wanamjadala. Nilimuuliza
yule mtoa mada ikiwa kama alikuwa anafahamu kwa mara ya kwanza ugonjwa huu
ulikoanzia lakini hakuonekana kuvutiwa na swali langu. Niliendelea kumuuliza ikiwa kama hao Wazungu ndio wanaowatuma Waafrika kula wanyama pori jamii ya nyani, popo na hata sokwe.
Mjadala huu ulinikumbusha mambo mengi, Waafrika tunayowasingizia
Wazungu kuwa ndiyo waliotusababishia. Hata matatizo ya kiuchumi yanayotokana na
ufisadi uliokithiri mpaka hivi karibuni tumekuwa tukiendelea kuulaumu ukoloni
wa wazungu kwamba ndio uliotusababishia hata baada ya miaka zaidi ya 50 ya
uhuru kupita.
Utakumbuka hata chanjo za magojwa mbalimbali zimekuwa
zikikataliwa maeneo mbalimbali kama Nigeria, hata na hapa Tanzania kuna wakati
watu walizua madai ya ajabu kama hayo ya kupinga.Matokeo ya ujinga huo
tumeshuhudia wenyewe juzi juzi katika janga hilihili la Ebola linaloendelea
huko Afrika ya Magharibi, Kusinimashariki mwa nchi ya Guinea wahamasishaji takribani saba wakiuwawa kinyama kwa silaha za jadi
wakati walipokuwa wakihamasisha jamii kujikinga na Ebola kwa kile kinachotajwa kuwa ni hofu juu ya wahamasishaji hao kutumwa na Wazungu kuja kueneza ebola kusudi wagonjwa wanapowekwa karantini basi wapate kuchukua viungo vyao mbalimbali kama maini figo na moyo kwa ajili ya kwenda kuwatibu wazungu.
Mtoto
mgonjwa akitoroshwa kituoni na ndugu zake huku wakiwa wamembeba.
|
Tatizo kubwa kwetu sisi Waafrika ni ujinga na kukumbatia
imani potofu zisizokuwa na misingi yeyote ile ya kisayansi. Ugojwa wowote ule
unaosababishwa na virusi ni vigumu sana kuutibu hata na kwa hao Wazungu
wenyewe. Ndio maana wanafanya kila liwezekanalo usiweze kuenea katika nchi
nyingi zaidi. Lakini binafsi nadhani kwa kiasi wenzetu Wazungu walivyokuwa
makini na pasipokukumbatia imani za kishenzi kama tufanyavyo sisi Waafrika hata
ugojwa huu ufike kwao hautaweza kusambaa kama vile ulivyofanya huku kwetu
Afrika.
Mazishi ya mtu aliyekufa kwa ebola.
|
Tusipokuwa makini na upotoshaji wa watu wachache
kama kijana Yule Waafrika tutaendelea
kuandamwa na majanga mengi ambayo uwezo wa kuyathibiti tunao wenyewe. Majanga
kama vile Ebola, Ukimwi, mauaji ya Albino na vikongwe, watu kuchunwa ngozi nk. Tutaendelea
kuwasingizia Wazungu kuwa ndio wanaotusababishia kumbe ni sisi wenyewe.
Tunadai eti ni kwa nini wazungu wasigundue dawa ya ebola
na kama ungelilipuka huko kwao basi wangefanya juu chini kupata dawa. Madai haya
siyo kweli hata kidogo kwani wanasayansi hawana mipaka wala hawabagui rangi,
kazi ya kuvumbua dawa hufanywa na wanasayansi na wala siyo wanasiasa.
Ingelikuwa hivyo ndivyo basi hata magonjwa kama malaria
na mengineyo kibao yaliyopatiwa dawa na wazungu hao hao basi yasingelikuwa mpaka leo hii yamepatiwa ufumbuzi kwani hata
mengine kama Malaria wala huko kwao siyo ‘ishu’ sana kama ilivyokuwa huku
Afrika.
Gunduzi za kisayansi hazina mipaka ya kiitikadi wala
kigezo kingine chochote kile, Muislamu, Mkristo, Mbudha, mhindi, Asiyekuwa na
dini yeyote, wote wananafasi sawa ya kubuni na kugundua kitu chochote chini ya
jua. Halikadhalika ndivyo hivyo hivyo ilivyo kwa mataifa liwe ni kutoka
Magharibi, Mashariki, au Mashariki ya kati. Sasa kinachokuja kuleta tofauti tu
ni ELIMU. Mataifa ya Magharibi
yameendelea ni shauri ya kuzingatia suala la elimu.
Boko Haram "Elimu ya Magharibi ni Haramu" wakiwa wamebeba silaha kali za kivita zilizotengenezewa huko huko Magharibi. |
Na ukitaka kujua ukweli kwamba Elimu na maarifa hayabagui, angalia Uchina ipo Magharibi? Mbona sasa inakaribia kuipiku Marekani kwa teknolojia. India haipo Magharibi lakini hata hazijapita siku mbili wameiduwaza Dunia baada ya kufanikiwa kurusha chombo kwenda kuizunguka sayarinyekundu ya Mars.
Irani, taifa tena la Kiislamu kutokana na kuanza
kuzingatia elimu na maarifa wamefikia hata hatua ya kuunda Nyuklia na ni hivi
karibuni tu, tumeambiwa nao wamezindua dege lao lisiloendeshwa na rubani
maarufu kama Drawns. Sasa huo umagharibi na Umashariki sijui Uislamu na Ukristo
uko wapi hapo?
Dawa mseto hii tunayoitumia leo hii hapa, (mchanganyiko
wa mti wa Artemisinin na viasili vinginevyo) haijagunduliwa Magharibi
na wazungu. Ni Wachina, tena Wamarekani wenyewe na ujanja wao wote iliwabidi
watumie mbinu kali za kijasusi kwa miaka karibu 10 kuweza kupenya ndani ya
ngome ya jeshi la kikomunisti la China wakati huo kusudi waweze kupata siri za
mti wa Artemisia unaozalisha dawa hiyo.
Wachina baada ya kuigundua hawakukubali ijulikane na Mataifa ya Magharibi hasa
Marekani.
Na ikiwa basi sisi Waafrika tumechoka na tiba za Wazungu
na tunadhani ya kuwa wanatuletea magonjwa yasiyotibika kwa kisingizio cha
chanjo na vifaa vingine vya tiba, basi hatuna haja ya kuwa wala na hospitali,
tuamue kurudi kwenye miti yetu ya asili kama kikombe cha Babu na wengineo.
Tusijidanganye kama wanavyofanya Boko Haramu na ISIS,
kuwa eti kila kitu cha Kimagharibi ni haramu (sikatai kweli kuna vitu vingine ni haramu) wakati huohuo wakitumia Mtandao wa intaneti
kama njia yao kuu ya kujitangaza na kueneza propaganda za itikadi zao. Sasa
najiuliza kwani kompyuta, simu, mtandao wa intaneti na hata silaha wanazotumia kuulia watu, siyo
teknolojia za Kimagharibi? Kwanini basi
wasirudi kwenye asili wakatumia zana za
enzi zile kama majambia, visu na hata njia za mawasiliano kama kupeleka habari
kwa barua kwa kutumia wakimbia kwa miguu, farasi, ngamia na njiwa?
Tusiwe kama Ngamia kujichimbia kichwa mchangani akidhania
yu salama, il-hali kiwiliwili kingali nje. Boko haram, au hata kikundi/mtu mwenye
itikadi nyingine yeyote ile, badala ya kuwa mnafiki na kudai eti elimu, iwe ya
kimagharibi, mashariki au kokote kule ni haramu anaweza akaitumia elimu hiyo
hiyo anayoipinga kwa mazuri ya kujenga
imani yake hiyo.
Hamna elimu haramu wala mbaya kutoka upande wowote ule wa Dunia ilimradi tu inatumiwa kwa lengo la kujenga na wala siyo kubomoa. Kila upande una mazuri yake na ndiyo maana Shirika la elimu na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO huwa linahifadhi maeneo yote Duniani ya kihistoria na yanayowakilisha tamaduni mbalimbali pasipo kubagua Magharibi, Mashariki, Kusini wala Kaskazini, dini, rangi wala kabila.
Hamna elimu haramu wala mbaya kutoka upande wowote ule wa Dunia ilimradi tu inatumiwa kwa lengo la kujenga na wala siyo kubomoa. Kila upande una mazuri yake na ndiyo maana Shirika la elimu na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO huwa linahifadhi maeneo yote Duniani ya kihistoria na yanayowakilisha tamaduni mbalimbali pasipo kubagua Magharibi, Mashariki, Kusini wala Kaskazini, dini, rangi wala kabila.
*Mpendwa msomaji wa makala hii, kwanza nikushukuru kwa kutembelea blogu hii ya jifunzeujasiriamali. Pia napenda kukujulisha kwamba baada ya kimya kidogo kilichotokana na kazi kubwa ya ‘kuredisign’ tovuti, blogu na cover za vitabu kusudi viweze kuwa na muonekano mpya, sasa tumerudi tena kuendelea na jukumu la kubadilishana na wewe mawazo zaidi kuhusiana na namna ya kuboresha biashara zetu ndogondogo kwa lengo la kuondokana na umasikini hasa wa kipato unaotutesa watu wengi.
Kuna watu wengi wametoa mapendekezo yao nini kifanyike, na moja
lilikuwa ni hilo tulilomaliza la kubadilisha majina. Wapo pia mlioshauri, kwa
nini blogu hii isingezungumzia masomo ya ujasiriamali tu peke yake tukaachana
na habari mbalimbali, hili nalo tumelizingatia ila, habari zitawekwa hasa zile
zenye mahadhi yanayohimiza ujasiriamali, biashara na ubunifu na usisahau pia
kuwa wengi katika timu ya watendaji wetu ni wana fani ya uandishi-habari hivyo ‘jasiri
haachi asili’
Kwa wewe ambaye unapendelea zaidi masomo ya ujasiriamali na biashara, basi ukiingia humu kwenye blogu moja kwa moja tembelea ukurasa 'page' (label) iliyoandikwa "Masomo" pale juu kabisa, na humo utapata mfululizo wote wa masomo yote muhimu.
Kwa wewe ambaye unapendelea zaidi masomo ya ujasiriamali na biashara, basi ukiingia humu kwenye blogu moja kwa moja tembelea ukurasa 'page' (label) iliyoandikwa "Masomo" pale juu kabisa, na humo utapata mfululizo wote wa masomo yote muhimu.
Ahadi zote tulizotoa, kama kutoa mfululizo wa makala zinazohusu
mafanikio ya watu maarufu na wasanii, kitabu cha think and grow Rich katika lugha ya Kiswahili, vyote sasa siyo tu, ukae mkao wa kula bali nakuambia, anza
kula sasa hivi, vyote vimekwisha wiva.
0 Response to "EBOLA: TUACHANE NA DAWA ZA KIZUNGU TURUDI KWENYE ASILI, KIKOMBE CHA BABU NA MUAROBAINI?."
Post a Comment