“Mwanzoni nilifikiri ni utani tu lakini baada ya ugomvi ule kukolea ndipo
nilipobaini kumbe ulikuwa ni ugomvi dhahiri” Anasimulia Shaban Saleh ambaye hivi karibuni
katika duka moja maeneo ya Buguruni Malapa jirani na stendi ya daladala nusura
mwenye duka na mteja wake wazichape “kavu kavu” kisa kikiwa ni sarafu mpya ya
shilingi mia tano ambayo imeletwa mbadala na ile noti ya zamani ya shilingi 500,
na ambayo pia ililalamikiwa mno kwa ubora wake hafifu.
Kisa kilianza hivi, Mteja baada ya kufika dukani alimpa mkononi
yule muuzaji sarafu moja huku akimwambia, “Nipe sigara moja aina ya embsi . Muuzaji
pasipo kuitazama ile sarafu na huku kama kawaida yake akidhani ni sarafu
aliyoizoea ya shilingi miambili, aliitupilia katika droo lake la pesa na kisha haraka haraka akachomoa sigara aina ya embasi
na kumkabidhi yule mteja pasipo kumrudishia chenji. Mteja alikaa kimya
akisubiri chenji yake lakini alishangaa kumuona muuza duka naye akiwa kimya bila
dalili yeyote ya kumrudishia chenchi yake.
Ndipo yule mteja alipoamua kumuuliza muuzaduka chenji
yake na ugomvi ukaanzia palepale, muuzaduka akishikilia kwamba sarafu aliyopewa
ilikuwa shilingi mia mbili, iweje aseme ni shilingi mia tano?. Kwa upande
mwingine yule mteja alijitahidi kumuelewesha muuzaji kwamba alichompa ni
shilingi mia tano kwa msisitizo kiasi kwamba alitaka hata kuingia ndani hadi
kwenye droo ya pesa akaionyeshe pesa yake lakini muuzaduka akamzuia.
Katika hali ile ya taharuki kubwa watu walianza kusogea
karibu, na kuanza kumshauri muuza duka akubali kukagua pesa zake . Ilibainika
kumbe yule muuzaduka hata uwepo wa kitu kinachoitwa sarafu ya mia tano hakuwa
nao sembuse kukubali kuwa alipewa
shilingi mia tano na mteja. Ilibidi juhudi za ziada zifanywe na wale
wasuluhishi akiwemo bwana huyu Shaaban kumuelimisha juu ya uwepo wa sarafu mpya
y ash. 500 na ndipo muuza duka sasa alipokubali, na alipoangalia vizuri katika
droo lake la pesa aligundua kulikuwa na sarafu mpya inayong’aa lakini isiyokuwa na tofauti kubwa na sarafu ya
shilingi mia mbili.
Watu wengi walitoa maoni yao wakisema kwamba sarafu hii
mpya ya sh. 500 itaibua sintofahamu kubwa hasa kwa wafanya biashara hata kuliko
ilivyokuwa kwa noti inayoondolewa kutokana na kwanza, kufanana mno na ile ya
shilingi mia mbili kwa ukubwa na hata kwa umbo, “Ni heri hata wangeiwekea pembe
mithili ya ile sh. 5 ya zamani ingelikuwa afadhali” Alisema mwananch mmoja
ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja katika eneo la tukio. Pili
wengine wanadai itakuwa mzigo kutokana na kuwa zamani hata benki waliweza
kukupa hata mia tano za shilingi elfu hamsini na ukazibeba bila usumbufu lakini
kwa sasa hivi haitawezekana hata kutembea na shilingi elfu kumi za sarafu
mifukoni mwa nguo tena.
0 Response to "SHILINGI 500 MPYA YA SARAFU NI MAJANGA KWA WAFANYIBIASHARA!"
Post a Comment