USOMAJI VITABU AFRIKA UPO CHINI SANA: SHIGONGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

USOMAJI VITABU AFRIKA UPO CHINI SANA: SHIGONGO


Mwandishi wa habari, mtoaji mada za kutia moyo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Publishers and General Enterprises ltd Bwana Eric James Shigongo, akifanya mahojiano na Shaka Ssali wa luninga ya Marekani VOA  jana katika kipindi cha Straight Talk Afrika, amesema kuwa usomaji wa vitabu Afrika upo chini sana kiasi ambacho juhudi za ziada zinatakiwa kuchukuliwa ili kuinua kiwango hich.Mada iliyokuwa ikizungumziwa ilihusu, changamoto zinazowakabili waandishi wa vitabu wa Kiafrika.

Akitolea mfano alisema kuwa, yeye binafsi ni miongoni mwa waandishi wa vitabu anayeonekana kuwa na mafanikio makubwa   lakini unapotajiwa idadi ya nakala za vitabu alivyowahi kuuza inashangaza, “Nimeuza nakala laki moja tu” anasema Shigongo . Alitoa mwito kuwa ili kuondoa hali hiyo inafaa juhudi kubwa zifanywe kupandisha utamaduni wa kusoma vitabu ambao ulishuka baada ya vyombo vya habari vya kielektroniki kuja. Alisema mbinu nyingine kuongeza kiwango cha usomaji ni kwa waandishi kuendelea kuandika hadithi  za kuvutia zenye ubunifu wa hali ya juu na zenye maudhui ya kwao wenyewe ya kiafrika.

Alipoulizwa kati ya waandishi wakongwe wa riwaya  wa Kiafrika, Chinua Achebe na Wole Soyinka, alijibu kwamba wote ni waandishi ‘wakali’ hawezi kutofautisha ni yupi anamzidi mwenzake.

Kuhusiana na kuongezeka kwa wasiojua kusoma na kuandika  aliwaasa wazazi kuhakikisha wanachukua hatua za makusudi  hata ikiwezekana kuzima TV wakati fulani kusudi kuwafanya watoto kurudisha ule utamaduni wa kujisomea vitabu uliopotea.

Anakubakli kuwa ni vigumu sana Mwandishi wa kiafrika kuuza nakala nyingi kwa mamilioni,ukitaka kuuza vitabu vingi ni lazima uzingatie mambo 3, nayo aliyataja kuwa ni, moja, kuandika vitabu vinavyouzika, pili,Stori nzuri zenye maudhui ya utamaduni wa kiafrika na tatu kuhakukisha unavunja mipaka ya lugha.

Akijibu swali  ni sababu zipi zilizomsukua kuanzisha kampuni ya uchapishaji alisema kwamba ya kwanza, alitaka kuchapisha vitabu vyake mwenyewe baada ya kuhangaika sana na miswada yake, kila alipokwenda kampuni za uchapishaji walimwambia mswada huo hautaweza kuuza na kuukataa. Aliamua “kukataa, kukataliwa”(reject being rejected). Sababu ya pili anasema ilikuwa ni kupaza sauti yake kwani tangu alipokuwa mdogo  kutoka familia masikini aliaminishwa kuwa  kila alichosema kilikuwa hakina maana yeyote, sasa akasema hapana, “Ndani yangu ninayo manbo mengi na napaswwa kuyasema ili kubadilisha maisha ya watu wengine”

Anazitaja mbinu alizotumia kukataa kukataliwa 'reject rejection' kuwa ni' baraka kutoka kwa Mungu pamoja na Kujitambua binafsi.Anasema pamoja na kutaniwa 'MADASO' jina lililomaanisha mtoto anayevaa nguo zilizochanika chanika bado alichagua kufuata mfano wa baba yake na kuamua kubadilisha njia aliyofuata baba yake badala ya kuwa masikini basi awe mwenye mafanikio kamwe aliapa hatakufa masikini.

Shigongo anamkumbuka Mjapani mmoja mwendesha baiskeli aliyekutana naye kitambo alipokuwa hana kitu akiuza karanga, Mjapani huyo alinunua karanga zote alizokuwa nazo na kisha baada ya kumtazama alimsifu kutokana na uhodari ule wa kujishughulisha na biashara, alimwambia “Wewe una akili sana” Anasema ndiye mtu ambaye hata kaa amsahau kwani alianzisha ndani yake roho ya ujasiri iliyokuja kumfanya mpaka leo kutambua kumbe maoni ya watu kuwa hawezi kufanya jambo lolote hayakuwa ya kweli.

Shigongo alisema kuwa Afrika kuna matatizo mengi na hivyo pia kuna biashara nyingi(fursa), kinachopaswa kufanywa ni sisi kubadilisha mtazamo na jinsi tunavyolitazama Bara letu, tuache kuwa na mtazamo hasi.


Watu anaosema walimsaidia na kumfikisha pale alipo mbali na Yule Mjapani  aliwataja kuwa ni, Wazazi wake hasa baba yake aliyekuwa mchuuzi wa samaki katika soko la mwaza aliyekuwa akimpa mbinu mbalimbali za kufanikiwa kimaisha. Wa pili ni mke wake, Veneranda, wa tatu ni wanawake wa Tanzania waliompiga tafu kwa kununua magazeti yake kwa wingi tangu siku anaanza mpaka leo hii na Mzee Reginald Mengi anayemtaja kuwa mshauri na "role model" wake. 

Akiielezea kanuni moja ambayo imemsaidia sana aliyopewa na baba yake huyo Mzee James ni ile kanuni ya ‘Faneli ‘kama ya kumiminia mafuta, ambapo juu ina mdomo mpana na chini ni nyembamba. Anasema kuwa baba yake alimueleza kuwa ili mtu kufanikiwa kutajirika unapaswa uingize pesa nyingi toka vyanzo mbalimbali lakini wakati wa kuzitoa au kuzitumia unapaswa uziminye zisitoke nyingi.
Mfano unaoelezea "Kanuni ya pesa ya Mzee James Shigongo aliyomwachia mwanawe Eric"
Juu pesa zinaingia nyingi chini zinadondoka kidogo sana.
Katika kitabu kipya alichoandika, anasema kuwa mafanikio siyo zawadi bali ni matokeo ya jitihada mtu anazofanya, “ Hakuna mtu anayeweza kupata mafanikio halafu ashindwe kutaja ni jinsi gani alivyofanikiwa” Alisema, pia alitanabahisha kuwa kiafrika unapofanikiwa huwezi ukajitenga na watu, familia nk. Lakini inatakiwa mtu kuwa na msimamo, huwezi ukaanza kugawa pesa na kisha zikiisha na wewe unajiunga na wale uliowagawia kuwa omba omba. Inabidi kuwasaidia mawazo na njia za kupita ili kufanikiwa na siyo kuwagawia pesa. “ Watu wanachohitaji siyo pesa bali ni taarifa, zitakazowaweka huru, waonyeshe njia ya kutoka pale walipo na kufika mahali pengine. TAARIFA  + UTEKELEZAJI MABADILIKO YA KIMAISHA.”

Akitoa mfano wa watu waliowahi kunufaika na mafunzo na semina zake alisema wapo wengi wanamiliki makampuni, wengine wapo vyuoni nk. Alitoa pia stori ya kijana mmoja ambaye alipokutana naye alimuuliza afanye nini ili aweze kufanikiwa kama yeye akamjibu kwamba anachopaswa kufanya ni kubadilika, na kujichanganya na watu mbalimbali hasa wale wenye mafanikio.

Alimwambia badala ya kukaa vijiweni  mitaa ya Manzese alikokuwa akiishi  aende kutembea maeneo ambayo angekutana na watu tofauti kama hoteli kubwa akatoa mfano hoteli ya Serena, nunua hata soda kunywa taratibu hamna atakayekufukuza. Kijana yule alifanya kama alivyoambiwa na Shigongo na matokeo yake alikuja akakutana na msichana mmoja wa kimarekani mzuri na mrembo, walipendana na mpaka sasa hivi wanaishi huko Calfornia Marekani. “ Ni lazima uondokane na mazingira uliyozoea na kukutana na watu tofauti ndipo utafanikiwa” Alisema Shigongo.


Angalia video ya shigongo akiwa 'VOA' hapa chini,


Shigongo, amewavutia watanzania wengi kutokana semina zake za ujasiriamali na kuwatia watu moyo, kwa historia yake ya kushangaza kutoka umasikini wa kutupa akitukanwa majina mabaya hadi mafanikio makubwa kama mmiliki wa kampuni ya uchapishaji vitabu na magazeti pamoja na biashara nyinginezo. 

Ana vitabu 7 mpaka sasa hivi cha kwanza “The last days of my life” na viwili vipya katika lugha ya kiingereza alivyokwenda kuzindua huko Marekani, navyo  ni “How to Move From Poverty to Success" na cha pili, "26 Secrets, How to Defeat From Enemies and Make Millions of Dollars".

0 Response to "USOMAJI VITABU AFRIKA UPO CHINI SANA: SHIGONGO"

Post a Comment