Kama kuna jambo linalotugharimu maishani na kutufanya
wengi wetu kuendelea kudidimia katika bahari ya umasikini,
basi ni hili suala la kudharau pesa ndogondogo na kudhani hazina athari yeyote
kubwa kiuchumi katika maisha yetu ya kila siku.
Ukweli huu kwa kweli mimi binafsi ijapokuwa nilikuwa naujua lakini ilikuwa ni juju tu na kinadharia zaidi mpaka hivi leo asubuhi nilipokutana na tukio moja lililonifanya nibaki nikistaajabu na kujiuliza, “Hivi kweli kwa kipindi chote hiki nilichoishi hapa duniani kuna jambo ninalolifanya na linalonigharimu kiasi hiki pasipo mimi mwenyewe kushtuka hata chembe?” Tukio lenyewe tena wala si kubwa na la ajabu sana ni maisha ya kawaida kabisa ila tu cha ajabu hapo ni funzo lenyewe linalotokana na tukio hilo.
Ilikuwa leo asubuhi yapata kama saa mbili na nusu hivi,
nikiwa katika eneo langu la biashara, nikamsikia jirani yangu tuliyepanga fremu
eneo moja, yeye ni kinyozi akiniita kuniuliza tufanyeje, kwani umeme, ‘LUKU’ ulikuwa
tayari umekwisha. Alikuwa ameongozana na
mteja aliyekuwa anataka kunyoa. Mteja huyo hakuwa mgeni machoni pangu, ni
mfanya biashara maarufu sana wa kusafirisha mizigo kwenda mikoani. Sina haki ya
kumtaja jina lake hapa kwani sijamuomba wala kumpa taarifa kuwa nitaandika
makala itakayomhusu.
Tukiwa watatu tukijadili njia rahisi na ya haraka ya
kupata umeme, kwenda kituo cha mafuta au kununua kwa njia ya simu, mara alifika
dada mmoja,(simfahamu) akawa anamuulizia kinyozi mwingine mwenzake na huyu niliyekuwa
najadili naye suala la LUKU.Kinyozi huyu mwingine yeye huwa shughuli zake zaidi
siyo kunyoa bali ‘hudili’ zaidi na kusuka ‘Dread’ za akina mama. Alimjibu ya
kwamba hajafika, dada akamuomba ampigie simu ili awahi kuja kwani alihitaji
kusuka ‘dread’ kwa ajili ya shughuli itakayofanyika leo hii hii.
Yule kinyozi aliinua simu yake akaiweka sikioni kana
kwamba anampigia yule kinyozi mwenzake kama yule dada alivyomuomba, huku
akizunguka zunguka aliitoa simu sikioni na kuitazama kisha akatamka, “Huyu bwana
hapatikani, naona bado atakuwa amelala, na leo kulivyokuwa na mawingu atafika
hata saa nne hapa”
Masikini dada wa watu hakuwa na la ziada zaidi ya
kujiondokea kimya kimya huku akiwa amejikatia tamaa. Sijui kama labda kulikuwa
na msusi mwingine aliyekwenda kusuka kwake au aliamua aende zake kwenye
shughuli bila kusuka dread, hakuna aliyefahamu tena hilo.
Baada tu ya kutupa kisogo yule ‘mdada’, kinyozi alitamka, “Hata ningelimpigia kweli,
akajua ni huyu dada, asingelikuja ng’o!, tunamjua vizuri huyu dada hatoi hela,
akitoa sh. 1500/- au sh. 2000/- huondoka akilalamika kutwa. Bora nimemdanganya
aondoke zake asituletee mikosi asubuhi asubuhi hii.”
Sasa hapa ndipo nilipopata somo lenyewe, baada tu ya yule
kinyozi kumaliza kuzungumza yule tajiri wa malori ya mizigo yaendayo mikoani,
sikutarajia kabisa alichokisema, kwanza alistushwa sana na kauli aliyokuwa
ameitoa yule kinyozi, kisha akasema, “Hiyo elfu mbili siyo ndogo, unafikiri
akitoa hivyo mara siku 30 au miezi miwili ni sh. ngapi?, kama unakubali kuipokea
inamaana inatosha, huna sababu ya kuidharau, hamna hela ndogo”
Nilitafakari hali ya kiuchumi bwana yule aliyokuwa nayo
nikajaribu kuilinganisha na shilingi elfu mbili anazosema siyo ndogo kwa kweli
nikastaajabu sana, lakini nilipata jawabu ni kwa nini watu wengine hufanikiwa
katika maswala ya pesa na wengine kubakia vilevile miaka nenda miaka rudi. Ni
kutokana na kuthamini kila senti wanayoipata.
Huyu mfanyabiashara alishangazwa sana na kuona watu wa
hali ya chini kabisa wakidharau shilingi elfu mbili mpaka kufikia hatua ya
kumdanganya mteja ilimradi tu “amewaondolea nuksi asubuhi asubuhi ya kuwaletea
elfu mbili”
0 Response to "USIDHARAU PESA HAKUNA PESA NDOGO"
Post a Comment