Halima ni msichana anayefanya kazi ya kuuza
katika duka moja la jumla la kuuza maji, hivi karibuni alinifuata na kutaka
nimpatie ushauri ni kwa jinsi gani anaweza kukabiliana na ugumu wa maisha hasa
ukizingatia kwamba mahitaji yake ni mengi kushinda kipato anachopata kutokana
na ajira yake hiyo. Nyumba aliyopanga huko Kigogo Mbuyuni zamani haikuwa na umeme lakini sasa wameweka
umeme, anahitaji kuwa na vifaa vya ndani kama TV nk. Lakini mshahara peke yake haumtoshi.
Alikuwa tayari na wazo lake mwenyewe kichwani
la kuanzisha vibiashara vidogovidogo, ambavyo angevifanya muda wake wa ziada na
wakati akiwa katika kazi yake. Wazo la kwanza lilikuwa ni kutengeneza vitu kama
karanga za kufunga, pamoja na maandazi. Mimi nilichomwambia ni kwamba, wazo
lake hilo ni zuri na biashara zote hizo
zinawezekana kabisa kufanya kwani haziwezi zikaingiliana na ile ya bosi wake.
Nilimtia moyo na kumhakikishia kwamba athubutu tu kwani, hakuna jambo lolote
linaloweza kutokea pasipo kwanza mhusika kuchukua hatua za kulitenda.
Nilimshauri atengeneze mpango wake wabiashara japo ni kwa kuufikiria kichwani tu na wala siyo lazima auandike kwenyekaratasi, nilimfundisha kwamba, kwakuwa tayari ameshakuwa na wazo ambalo ndiyo
dhamira yake kuu, atengeneze sasa malengo, na moja nilimwambia tayari alikuwa
nalo ambalo ni kupata pesa kwa ajili ya kununulia tv, lingine kupata kiasi cha
pesa kila mwezi za kulipia gharama ya umeme, nikamweleza anaweza akaongeza na
malengo mengine aliyokuwa nayo kichwani.
Jambo lingine muhimu sana nililomweleza ni
kufikiria mpango wake wa masoko utakuwaje, nilimshauri aumize kichwa kujua ni
vipi atahakikisha bidhaa zake zinawafikia wateja, watajuaje kama anauza vitu
hivyo, atatumia mbinu zipi na mikakati kuwavutia wateja wake hao. Sikutaka
kabisa kumuonyesha mbinu hizo moja kwa moja au kumwambia afanye kitu gani kwani
nilitaka abuni kulingana na mazingira yake mwenyewe ndiyo mikakati inaweza
ikafanya kazi vizuri.
MATOKEO
YAKE.
Halima siku ya kwanza alianza kutengeneza
karanga za kufunga, na kuanza kuziuza pale kazini baada ya siku kadhaa,
aliniambia amebadilisha mkakati, na hatauzia tena pale kazini, badala yake
amebuni soko jingine huko nyumbani anakoishi, ile jioni baada ya kufunga kazi,
akifika nyumbani hutoka na kwenda kando kando ya barabara pana stendi ya
daladala, na hapo huweka karanga zake na kuanza kuuza. Nilimshauri, badala sasa
ya kuuza karanga peke yake aondeze hapo na vitu vingine kama sigara, pipi,
biskuti, ubuyu, na maji ya kufunga. Ushauri wangu huo aliufanyia kazi nabaada
ya siku chache akaniambia mambo yalikuwa yakienda vizuri.
AANZA
KUKAANGA MAANDAZI.
Biashara imeendelea kushamiri, akaja tena na
kuniambia sasa ameona aanzishe na maandazi, nilitaka nimshauri asianzishe
kwanza biashara hii, kutokana na kuona kwamba kazi zingekuwa nyingi mno jambo
ambalo lingeweza kumsababishia kuharibu ajira yake lakini yeye mwenyewe akadai
haitaweza kuathiri kabisa majukumu yake ya kazi kwani alikuwa amedhamiria
kiukweli hata ingewezekana asilale angefanya hivyo, “ usiniambie eti kazi
zitakuwa nyingi huku umasikini ukiniua, mbona kabla sijaaza, nilikuwa napata muda
wa kupiga stori za umbea nyumbani mpaka hata saa tano usiku, hebu niache huko” aling’aka Halima.
![]() |
Akikanda
unga wa maandazi
|
Nilimwambia basi ikiwa ataamua kuanzisha
maandazi ajaribu kufikiria kwamba, biashara hii, ina ushindani mkubwa, karibu
kila mwanamke wa nyumbani huifanya, sasa aumize tena kichwa na kufikiri ni kitu
gani cha pekee atakachoweza kukifanya kuwashawishi wateja wawe wanakuja kununua
maandazi yake na kuyaacha ya wale waliokwisha wazoea.
![]() |
Maandazi
yakiwa tayari kupelekwa sokoni.
|
Jibu alilokuja nalo baada ya siku moja,
aliniambia ya kwamba maandazi yake atakuwa akiyatia tui la nazi, ambalo
huyafanya yawe na ladha nzuri na ya kupendeza mtu anapoyatafuna mdomoni. Kweli
siku ya kwanza tu kutengeneza maandazi aliyapitisha pale ninapokaa na
nilipoonja moja tu, nikamwambia aniongezee mengine matano, yalikuwa matamu ‘balaa!’
CHANGAMOTO.
Siku ya kwanza alitengeneza maandazi kiasi
kama nusu kilo hivi, alipoyatua chini tu
na baada ya mimi kununua hapo matano, mtu wa pili alinunua maandazi 20 ya
familia, mtu wa tatu hakuweza kupata idadi ya maandazi aliyokuwa akiyataka,
yakawa yamemalizika.
Halima alinifuata na kuniambia huku
akitabasamu, “yamekwisha na wengine wamekosa, kesho nitajaza kindoo kizima”
Nilimwambia achukue tahadhari kwani biashara ya kuanza haitabiriki hata kidogo.
Nilimsihi aendelee kwanza kutengeneza kiasi kile kile au hata akiongeza basi
iwe ni kiasi kidogo sana mpaka atakapohakikisha ana wateja wa uhakika.
Siku iliyofuata alibeba maandazi kindoo
kimejaa mpaka juu, kama kawaida walikuja wateja wale wa jana yake kakini, mpaka
jua linazama bado kindoo kilikuwa kimejaa, walinunua watu wachache! Halima akaanza kuingiwa na wasiwasi,
alinifuata na aliponieleza nikamwambia awe mvumilivu kwani ndivyo biashara
ilivyo, huwezi kila siku mambo yakaenda vizuri. Aliyarudisha nyumbani lakini kesho
yake aliniambia kwa bahati nzuri jioni ile alikwenda kuyauza yote pale katika kijiwe cha stendi ya daladala
karibu na nyumbani kwao anakoishi.
UBUNIFU
ZAIDI.
Ili kukabiliana na changamoto ya kubaki kwa
maandazi mara kwa mara, Halima mwenyewe alibuni mkakati ambao hata mimi binafsi
alinishangaza, mwenyewe anasema kuna siku maandazi yalibaki mengi, jioni
akayatazama kwa uchungu karibu machozi yamtoke akikumbuka mtaji wake wa shida
aliouwekeza pale. Akiwa anarudi nyumbani jioni hiyo, alikuwa akiwaza na kuwazua
afanye kitu gani kitakachomhakikishia soko la bidhaa zake hizo. Maandazi ni
mazuri, matamu na yanakidhi kila haja ya mteja lakini shida ilikuwa, ni njia
ipi rahisi itakayomwezesha kuyauza?
Alipokuwa akipita maeneo ya sokoni Ilala Boma, kichwani alikumbuka jinsi ambavyo
mahali hapo muda wa asubuhi panakuwa na pilikapilika ya watu wanaofika kununua
nguo kwa ajili ya kwenda kuziuza. Lilimjia wazo la kujihimu asubuhi na mapema
kabla hajaja kazini, apitishe maandazi yake hapo sokoni na baada ya kuuza
ikifika saa moja hivi basi aende zake kazini huku ‘mzigo’ unaokuwa umebakia aje awauzie wateja wake wa
kawaida wa kila siku kazini, na hata ikiwa yatabakia tena kidogo, hayo ni
lazima yakamalizike pindi atakapokuwa amefika kijiweni kwake masaa ya jioni.
Wanawake wakiuza vitafunwa sokoni (picha
na Majira)
|
Mkakati huo Halima aliutekeleza kwa mafanikio
makubwa kiasi kilichonifanya nimtanie, “Mwanamke
wa shoka anatakiwa kuwa mbunifu namna hiyo na siyo kukaa tu na kusubiri” . Sasa
hivi, taratibu anaanza kuzoea maisha ya kuchakarika(ujasiriamali), hasubiri
tena kufanya kila kitu kwa mshahara, kazi yake inaenda vizuri, muda wa kazi
hauingiliani na wa biashara zake na soko lake la maandazi halina tena vikwazo.
----------------------------------------------------------------------------------------
----------------------------------------------------------------------------------------
*Ndugu msomaji wa blogu hii, tunapenda kukutaarifu kuwa vile vitabu vilivyokuwa vimekwisha sasa vipo tayari, na vinapatikana ukiwa mahali popote pale nchini. Ikiwa utahitaji usisite kutupigia namba zetu hapo juu. Pia kama una maoni yeyote yale juu ya makala hii au chochote kuhusiana na biashara basi, yatoe hapo chini katika kisanduku cha maoni. Asante.
0 Response to "KUTAFUTA SOKO LA BIDHA ZAKO, KUNAHITAJI UBUNIFU"
Post a Comment