Biashara ya kuwasambazia wenye maduka bidhaa
hususani yale maduka yanayouza rejareja,
ni biashara ambayo imekuwa ikifanywa na watu wengi jijini Dar es salaam na hata
katika mikoa mingine nchini. Mtu anakwenda katika maduka makubwa, au viwandani,
ananunua bidhaa kwa bei ya chini, kisha anakwenda kuziuza kwa wenye maduka ya
rejareja mitaani kwa bei ambayo yeye hupata faida.
SIRI YA KUFANYA ILI KUKUPA FAIDA NZURI.
Biashara yeyote ile ili iweze kuwa endelevu na inayolipa
inahitaji kuwa na wateja wa uhakika na wakudumu. Katika biashara hii ya
kusambaza bidhaa za jumla kwenye maduka ya rejareja, wengi wa wale wanaoifanya
kuna kitu kimoja tu wanachoshindwa kukizingatia ambacho ndicho huchangia kuiona
biashara hii kuwa ni ngumu na isiyokuwa na faida ya kutosha.
Katika biashara yeyote ile ni lazima umlenge yule mteja
wako, na kubaini ni kitu gani hasa anachokitaka. Kushindwa kubaini kile mteja
anachokitaka hasa husababisha biashara
kuwa ngumu.
Kumbuka ya kwamba mwenye duka unayekwenda kumuuzia bidhaa
ana njia nyinginezo za kupata bidhaa hizo, na mara nyingi huwa ni kutoka katika
maduka ya jumla au hata katika zile sehemu ambazo na wewe huwa unakwenda
kununua ili kuja kuwauzia.
Hivyo hapa siri kuu ipo katika bei. Kitu cha kwanza
mwenye duka anachokifikiria anapomuona mtu amemletea bidhaa hadi mlangoni, ni
je, bei yake ukilinganisha na za kule kwingine anakokwenda kununua bidhaa kama
hizo zikoje?, ni kubwa zaidi, zinalingana
au zipo chini zaidi?
Ili kupata faida hapa inakubidi uuze kwa wingi, lakini
pia kuhakikisha kuwa kule unakonunua na wewe unapata kwa bei nzuri yenye faida.
Kwa hiyo hapa kazi ipo kwako kuzunguka na kuhakikisha unapata bidhaa zako
kutoka yale maeneo wanakouza kwa bei
nafuu kabisa, lakini pia zingatia na ubora wake usije ukanunua “mchina”(feki)
wateja wakakukimbia.
Ili wateja wako wanunue bidhaa zako pasipo kusitasita
pindi unapobisha hodi madukani mwao, wanachokitaka wao ni uwauzie bidhaa hizo
aidha kwa bei ileile wanayonunulia kwingineko, au bei chini ya hiyo. Hii huwapa
kitu cha ziada kwani hawaoni ni kwa nini wapoteze muda wao wa dhamani na nauli
ya kwenda kufuatilia bidhaa ambazo wanaweza wakaletewa hadi mlangoni kwa bei
ileile au chini ya hapo.
CHANGAMOTO.
Chngamoto kubwa iliyopo katika biashara hii ni jinsi gani
mtu utafanya ili uweze kukabiliana na kikwazo hicho cha kuhakikisha wateja wako
wanapata bidha kwa bei ileile wanayoweza wakapata kwingineko katika maduka
makubwa ya jumla au hata kutoka viwandani moja kwa moja. Mbinu moja wapo 7 ambazo
unaweza ukazizingatia ni hizi hapa chini ;
1.Kubali kupata faida kidogo, kwa ajili ya kujenga soko
lako kwani biashara ni wateja kwanza na
siyo faida, faida itakuja tu baadaye utakapokuwa umekwishazoeleka vyakutosha.
2. Hakikisha unajitahidi kufa na kupona kupata punguzo
kutoka kule unakokwenda kununua kwa jumla, kwani punguzo hilo hilo laweza
likawa ndiyo faida yako, ikiwa utataka kuuza chapchap na kujenga mtandao mpana
wa soko lako.
3. Omba kupelekewa bidha mpaka unapohifadhi ikiwa
umenunua mzigo mkubwa, wauzaji wengine, au wenye viwanda huwa na huduma ya kumpelekea mteja bidhaa mpaka
anakofika kutegemeana na mazingira fulani fulani kama vile wingi wa bidhaa,
mteja wa kila mara nk. Utaona kwamba zile gharama ambazo ungelipia usafiri zinageuka
kuwa faida kwako.
Omba kufikishiwa bidhaa unapozihifadhi. |
4. Jitahidi kuwa na bidhaa za aina tofauti tofauti,
usijihusishe na aina moja tu ya bidhaa huku ukilenga zile bidhaa zinazotoka
harakaharaka hata kama ikiwa faida yake ni kidogo.Utakapouza kwa wingi ile
faida kidogo kidogo unayoidharau hatimaye huwa kubwa baada ya muda fulani.
5. Ikiwa unasambaza bidhaa zako kwa kutembea kwa miguu,
jaribu kuwa na angalao usafiri wa baiskeli, pikipiki au hata gari kama unao
uwezo huo ili kuongeza tija zaidi kwa
kuokoa muda pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba bidhaa nyingi zaidi.
6. Kuwa tofauti, jitahidi kutafuta kitu kitakachokufanya
uwe tofauti na watu wengine wanaofanya biashara ya kuwasambazia watu bidhaa
kama wewe, jambo au kitu hicho chaweza kuwa
hata unadhifu wako, namna unavyozipanga bidhaa zako au kuzifungasha,
muda unaowafikishia wateja bidhaa nk.
kuwa na angalao usafiri wa baiskeli, pikipiki au hata gari |
7.Zingatia kanuni zote za uuzaji, kama vile kauli nzuri
unapowasiliana na wateja wako, jenga mahusiano mema ukizingatia kwamba mteja ni
mfalme na kamwe hakosei.
----------------------------------------------------------------------------------
*Ndugu
msomaji wa makala hii, ukitaka kusoma makala zaidi zinazohusiana na masomo
muhimu ya Ujasiriamali tu peke yake, basi nenda moja kwa moja pembeni mwa blogu
kwenye ‘TAGS’ au pale chini kabisa
mahali palipoandikwa ‘LABELS’ na
ubonyeze kwenye LABEL/TAG yenye jina, “MASOMO
MUHIMU”.
Hali
kadhalika kama wewe ni mpenzi wa makala
zinazohusiana na Jinsi ya kuandaa Mpango/mchanganuo wa biashara basi bonyeza TAG/LABEL yenye jina la “KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA”
utapata mfululizo wa makala zote zinazohusiana na jinsi ya kuandika mpango wa
biashara.
0 Response to "BIASHARA YA KUTEMBEZA BIDHAA ZA JUMLA MADUKANI, MBINU 7"
Post a Comment