Mwaka 1996 nikiwa
ndiyo naenda kuanza kidato cha tano katika shule ya sekondari ya wavulana
Songea Boys Secondary school, maarufu kama BOX 2, sikuwa nafahamu mtu anapougua
malaria huwa anajisikiaje, zaidi ya kuzisoma dalili zake katika vitabu na
kufundishwa na mwalimu wa somo la baiolojia na sayansi kimu.
Nilikuwa natoka
Mkoani Kilimanjaro, wilayani Rombo ambapo ugojwa huu kwa wakati ule haukuwa
umeenea sana, nadhani hata mpaka hivi sasa unapolinganisha na maeneo mengineyo
kama Dar es salaam na mikoa ya Kusini bado malaria siyo tishio sana. Ulikuwa
ukisikia mtu anaugua malaria basi ujue katoka nayo Dar au mikoa ile iliyokuwa na kiwango kikubwa cha
Maambukizi ya malaria. Hata tulipokuwa tukisoma shule ya msingi na O lelel
mwanafunzi akiugua homa basi ujue ni mafua, tumbo la kuendesha, surua au ugonjwa
mwingine wowote lakini siyo malaria.
Wiki mbili tu baada
ya kuanza kidato cha tano, nikiwa 'boarding' katika mabweni ya Uhuru nilianza
kujisikia mwili kuchoka, homa, na kutaka kulala kila mara hata ikiwa usiku
nililala mapema kiasi gani. ‘Prepo’ za
usiku sikuwa kabisa na hamu nazo, wenzangu wakienda mimi nabaki ndani ya neti.
Chakula ambacho ilikuwa ni dona na maharage kasoro siku za 'weekend' ambazo tulipikiwa wali na nyama maarufu kama mpunga, asubuhi saa nne tulipewa uji, na vitafunwa mtu unajitegemea mwenyewe ambapo wengi tulipendelea kununua kwa mamantilie viazi vitamu au mihogo ya kuchemshwa iliyojulikana sana kwa jina maarufu kama“Mayao” ‘Ulokoni’ ulokoni maana yake ni nje ya maeneo ya shule.
Chakula ambacho ilikuwa ni dona na maharage kasoro siku za 'weekend' ambazo tulipikiwa wali na nyama maarufu kama mpunga, asubuhi saa nne tulipewa uji, na vitafunwa mtu unajitegemea mwenyewe ambapo wengi tulipendelea kununua kwa mamantilie viazi vitamu au mihogo ya kuchemshwa iliyojulikana sana kwa jina maarufu kama“Mayao” ‘Ulokoni’ ulokoni maana yake ni nje ya maeneo ya shule.
Siwezi kuisahau kamwe
siku ambayo shuleni kulikuwa na ‘Debe’ yaani Disko, Wakati wenzangu
‘wakijirusha bwaloni na mademu wa "Tamsala" (mademu
wa tamsala au tamso walikuwa ni wanafunzi wasichana kutoka shule jirani ya
wasichana songea girls) mimi
nilikuwa nimelala hoi ‘Dom’(bwenini) nikiugulia
malaria, huku nikizisikia kwa mbali ngoma kali za wakati huo kama vile 'Salanoki na Famille Kikuta za General Defao', Twisted wa Keith Sweat, 'Macarena wa Los del Rio', 'End of The Road wa Boys II Men' na nyinginezo nyingi. Bweni letu lililoitwa Uhuru halikuwa mbali sana na Ukumbi huo hivyo kuyafanya masikio yangu kuzisikia vyema ngoma hizo.
Nilikula kwa tabu
sana huku kiungulia kikinisumbua mara kwa mara na tumbo kujaa gesi. Baadaye
nilikuja kubaini kwamba hali ile ilitokana na malaria. Nilidhoofika sana na
kila nilipokuwa naenda zahanati ya shule au hospitali mjini kupima waliniambia
nina wadudu wa malaria wawili au watatu. Kwa kweli hali ile ilikuwa ngeni sana
kwangu. Dawa pekee wakati huo iliyokuwa rahisi kupatikana ilikuwa ni vidonge
vya Chloroquine
na mara kwa mara ndivyo nilivyokuwa nikipewa hospitalini nikichanganyiwa na 'antibiotic' nyingine iitwayo Septrine kama sikosei(mimi sina
taaluma ya udaktari au madawa naweza kuwa nimekosea spelling).
Chloroquine
zilinitesa zaidi ya homa yenyewe ya malaria, kwanza nilipatwa na muwasho mkali
hasa maeneo ya siri na mwili mzima, muwasho uliofanana na vitu
vinavyochomachoma mithili ya sindano au miiba midogomidogo. Hali hiyo
inasemekana ni mzio, ‘allergy’ inayotokana
na vidonge hivyo na huwapata baadhi ya watu tu, kwani nilishangaa sana kuona
kuna wanafunzi wengine walikuwa wakitumia hawapatwi na muwasho wowote.
Kupunguza muwasho
ijapokuwa kwa upande wangu wala sikuona kama inanisaidia lolote madokta walipendekeza
mtu utumiapo chloroquine basi utumie sambamba na Vidonde vingine
vilivyojulikana kama Piriton. Mara ya kwanza kula
chloroquine nilipata nafuu lakini wala hazikupita wiki mbili hali ile ikarudi
tena, niliendelea kuteseka na malaria kwa kipindi kirefu huku nikitumia
chloroquine mara kwa mara, kwa kipindi karibu cha mwaka mmoja mzima.
Kwa kweli
nilichanganyikiwa, sikujua nitumie dawa gani, wenzangu wengine walinishauri
labda ningetumia quinine ingenisaidia. Sikuthubutu kuzitumia pasipo kuandikiwa
na daktari hivyo ikanibidi niende kwa dokta mmoja aliyejulikana kwa jina, Dokta
Hyera aliyekuwa na zahanati yake maeneo ya pale Matogoro karibu na Songea TTC
Chuo cha ualimu. Dr. Hyera alinipima nikamuelezea historia ya malaria yangu kisha
aliniandikia kutumia vidonge vitatu ambavyo baadaye nilikuja kugundua kwamba
vilikuwa SP, Sikumbuki vilikuwa Fansida au Metakelfin lakini kwa wakati ule
dawa hizi ndiyo zilikuwa zinaanza anza kutumika, hazikuwa zimezoeleka sana.
Nilishangazwa sana, kwani
siku chache baada ya kutumia dawa zile nilijisikia tena mwenye afya njema kama
nilivyokuwa kabla sijaondoka Kilimanjaro. Sasa nilikuwa nimeshaingia kidato cha
sita lakini nikiwa karibu mwaka wote wa kidato cha tano nikiwa sijasoma
kikamilifu.
Tatizo la malaria pale shuleni halikuwa likinisumbua mimi peke yangu, nilichojifunza ni kwamba wanafunzi wengi waliotoka mikoa isiyokuwa na maambukizi mengi ya malaria karibu wote walikuwa wakisumbuliwa kama mimi, lakini wale waliozaliwa palepale Ruvuma au kutoka mikoa kama Morogoro na Dar. hawakuwa wakisumbuliwa kwa kiasi kikubwa.
Tena wapo wanafunzi wengine hata walifikia hatua ya kuhama shule kwenda kusoma katika shule za mikoa walikotoka. Kila mara ungesikia kuna mwanafunzi kalazwa hoi katika zahanati ya shule na hata wakati mwingine kuna waliofariki kwa malaria kali.
Tatizo la malaria pale shuleni halikuwa likinisumbua mimi peke yangu, nilichojifunza ni kwamba wanafunzi wengi waliotoka mikoa isiyokuwa na maambukizi mengi ya malaria karibu wote walikuwa wakisumbuliwa kama mimi, lakini wale waliozaliwa palepale Ruvuma au kutoka mikoa kama Morogoro na Dar. hawakuwa wakisumbuliwa kwa kiasi kikubwa.
Tena wapo wanafunzi wengine hata walifikia hatua ya kuhama shule kwenda kusoma katika shule za mikoa walikotoka. Kila mara ungesikia kuna mwanafunzi kalazwa hoi katika zahanati ya shule na hata wakati mwingine kuna waliofariki kwa malaria kali.
Hamna hata siku moja
nililala pasipo kufunga chandarua(neti), lakini labda nafikiri neti za wakati ule
hazikuwa zikiwekewa dawa kama ilivyokuwa siku hizi. Tangu kutibiwa na Dr. Hyera
nikaanza kutumia metakelfin na kuachana na chloroquine. Sasa hivi nikawa nakaa
muda mrefu kidogo pasipo kupata malaria na nilipotumia dawa nilipona haraka
kuliko enzi za klorokwin. Lakini athari nilizozipata kipindi hicho, kiuchumi na
kimaisha kwa ujumla mpaka leo hii bado zinanitesa, hazijafutika.
Baada ya masomo
nilirudi nyumbani Kilimanjaro, huku mwili ukiwa umedhoofu sana. Nakumbuka hata
mama yangu mzazi alishtuka kuniona, nikaanza dozi moja ya kula malimao, dozi
hii niliambiwa na mtaalamu mmoja wa dawa lishe kwamba ingesafisha sumusumu zote
mwilini zilizotokana na madawa ya malaria niliyokuwa nikitumia karibu miaka 2. Kwa siku nilipaswa kula zaidi ya malimao 12,
sikumbuki vizuri ilikuwa ni dozi ya malimao mangapi tena lakini kama
ningemaliza dozi nzima si chini ya malimao 120.
Dozi hii nayo almanusura
imalize uhai wangu kwani baada tu ya kuitumia kwa muda wa siku nne hivi, siku
moja tukiwa shambani mimi dada yangu na mama yangu, ghafla nikasikia kizunguzungu na kuanguka chini, niliamka baada ya dakika kama 5 hivi, baadaye niligundua
huenda ikawa ni ile asidi ya malimao
ilikuwa imezidi kwenye damu na kwa kuwa mwili ulikuwa umedhoofu,( nilifikisha
kilo 45, kutoka kilo 70) yakanizidi nguvu.
Nilisitisha dozi mara moja na hali ile haikuja kunirudia tena mpaka hivi leo. Nikawa sasa nakula vyakula vya kawaida tu mpaka mwili uliporudi hali yake ya kawaida. Nilikaa nyumbani karibu mwaka mzima wala sikusikia dalili yeyote ile ya malaria isipokuwa tu siku za mwanzo baada ya kurudi nilisikia dalili na baada ya kupima nikaenda kununua Sp duka moja na nilipotumia zile dalili zikatoweka. Nadhani walikuwa ni wadudu wa malaria niliotoka nao Songea.
Nilisitisha dozi mara moja na hali ile haikuja kunirudia tena mpaka hivi leo. Nikawa sasa nakula vyakula vya kawaida tu mpaka mwili uliporudi hali yake ya kawaida. Nilikaa nyumbani karibu mwaka mzima wala sikusikia dalili yeyote ile ya malaria isipokuwa tu siku za mwanzo baada ya kurudi nilisikia dalili na baada ya kupima nikaenda kununua Sp duka moja na nilipotumia zile dalili zikatoweka. Nadhani walikuwa ni wadudu wa malaria niliotoka nao Songea.
Baadaye nilihamia
jijini Dr es salaam, ambako nilianza tena upya kusumbuliwa na malaria. Nikiwa
naishi mitaa ya Manzese, nakumbuka nilianza tena kuzisikia dalili kama zile
zile nilizokuwa nazipata nikiwa Songea, sikuhangaika wala kwenda kupima
nikaanza matumizi ya dozi ya SP. Baadae niligundua kitu kimoja kwamba kumbe ile
dozi ya Sp mtu ulitakiwa kurudia pindi ambapo wiki moja ilikuwa imemalizika
lakini mimi baada ya dozi ya kwanza tu sikuwa narudia tena hadi dalili
zilipokuwa zikinirudia tena. Vile vile unatakiwa kula idadi ya vidonge kulingana na uzito wako.
Hali ile kumbe ilikuwa ikinifanya malaria isiishe
kikamilifu jambo lililofanya niwe naumwa mara kwa mara. Nilipata ushauri kutoka
kwa watu wengi, wengine wakinishauri kutumia dawa chungu kama mchunga,
muarobaini ama majani yeyote yale ambayo ni machungu. Mboga zangu zikawa kila
wakati ni mchunga na hata nilienda kwa Wamasai ambao walinipatia dawa chungu.
Juhudi zote zile
ziligonga mwamba, nikawa kila mara natumia dozi ya Malaria ambayo mara nyingi
ilikuwa ni metakelfin(SP). Chloroquine japo wakati huo ilikuwa haijapigwa
marufuku rasmi hata ungelinishikia panga katu nisingeliitia mdomoni kwangu tena nikikumbuka vile ilivyokuwa ikinitesa kwa muwasho.
Kitu
kilichonistaajabisha sana ni kwamba, wakati naanza kutumia Metakelfin(SP) kwa
Dr, Hyera nikiwa pale Songea kabla sijamaliza shule, dawa hiyo ilinitibu vizuri
sana! Lakini baada tu ya kuwa nimeitumia kwa muda fulani tangu niliporudi
nyumbani Kilimanjaro na baadaye Dar. SP ilianza kuonekana hainisaidii chochote.
Nilianza kuingia
kwenye mtandao wa intaneti wakati huo tena intaneti ikiwa ndiyo kwanza ipo
katika hatua zake za mwanzo kwa hapa kwetu, Google haikuwa maarufu kama ilivyokuwa sasa,
nakumbuka nilikuwa nikitumia sana 'search engine' ya Yahoo, nikaanza kutaipu neno
malaria. Nilijifunza Malaria kwa kina sana, nikazifahamu dawa zote zinazotumika
kutibu malaria kuanzia 'Halfan' mpaka dawa moja ambayo nilifikiria pengine ndiyo
ambayo ingeliweza kuwa suluhisho la malaria yangu iitwayo'Piperaquine'.
Kwa mujibu
wa website mbalimbali nilizotembelea ni kwamba Piperaquine iliyokuwa kundi moja
na dawa zingine kama Quinine na chloroquine, inafanya kazi tofauti kidogo, na
sifa yake kuu ni kwamba ina uwezo wa kuviua vijidudu vya malaria vinavyojificha
kwenye ini na ambavyo kwa dawa za kawaida haviwezi kuuwawa. Huwa tu malaria
inatoweka kwenye damu lakini mayai ya wadudu hao hujichimbia katika ini na huja
kuibuka baada ya kipindi fulani na kuanza tena kumpa mgonjwa dalili za malaria.
Gonjwa jingine hili hatari linaloenezwa na mbu kama hukulisoma nalo lisome hapa.
Gonjwa jingine hili hatari linaloenezwa na mbu kama hukulisoma nalo lisome hapa.
Niliamini kabisa
kwamba malaria yangu haikuwa ya kawaida nikajisemea “Ni lazima malaria yangu itakuwa
kwenye ini”. Sasa nilianza kufanya utafiti mwingine wa kuipata dawa
hiyo, kila duka la dawa nililokwenda nikawa naambiwa dawa ile 'piperaquine'
haipatikani, lakini kila nilipoingia kwenye mitandao nilikuwa nikipata
maelekezo yake kuwa ndiyo dawa pekee iliyokuwa na uwezo wa kufuta malaria sugu
ya kwenye inni. Nilishangaa sana kwanini serikali ya Tanzania haikuwa imeona
umuhimu wa kuagiza dawa hii ambayo nilidhani ndiyo uliokuwa muarobaini wa
malaria inayojirudia rudia.
Nilifikia hata hatua
ya kutaka kuiagiza dawa hiyo mtandaoni kutoka Marekani au Ulaya lakini kikwazo kilikuwa ni jinsi ya kupata
Credit/Debit Card, kumbuka wakati huo miaka ya 2003 kurudi nyuma hata mabenki
ya hapa sijui kama kulikuwa na moja iliyokuwa na huduma ya namna hiyo. Sina uhakika kama kulikuwa na benki iliyokuwa na huduma hizi za Master Card na VISA. Nusu nifunge safari ya kwenda jiji
la Nairobi nikidhania labda ningekwenda kuikuta dawa hiyo katika 'mapharmacy' makubwa huko.
Nilipokuwa nafanya
juhudi hizi zote siyo kwamba sikuwa na imani na madaktari au hospitali za hapa nyumbani, la
hasha ila nilishajiaminisha mwenyewe kwamba tatizo la malaria kama mtu
usipokuwa makini mwenyewe, ukasema utegemee hospitali unaweza ukapoteza maisha.
Kwanza nilikatishwa tamaa na dawa ya Sp ambayo mwanzoni ilikuwa ikinitibu vyema ilipoanza kukataa kunitibu vizuri, pili niliona sasa ikiwa serikali haioni umuhimu wa kuagiza Piperaquine dawa pekee ambayo niliamini ndiyo ingeliweza kuniponya malaria yaliyokuwa yakinisumbua kwa takribani miaka mine sasa, basi hakuna tena umuhimu wa kwenda hospitalini.
Kwanza nilikatishwa tamaa na dawa ya Sp ambayo mwanzoni ilikuwa ikinitibu vyema ilipoanza kukataa kunitibu vizuri, pili niliona sasa ikiwa serikali haioni umuhimu wa kuagiza Piperaquine dawa pekee ambayo niliamini ndiyo ingeliweza kuniponya malaria yaliyokuwa yakinisumbua kwa takribani miaka mine sasa, basi hakuna tena umuhimu wa kwenda hospitalini.
Mwishowe niliamua
kwenda hospitali ya Magomeni na Dokta mmoja nilimuelezea tatizo langu kwa
kirefu, alinishauri kwanza nisiwe tena natumia dozi yeyote ya malaria pasipo
kwanza kupima na pili nihakikishe baada ya kumalizia dawa atakazoniandikia
nirudi tena hospitalini nikafanye vipimo kuangalia ikiwa malaria imemalizika.
Tangu siku hiyo
nikaanza kufuatilia yale aliyonielekeza yule dokta huku nikihakikisha najilinda
vilivyo na mbu. Ijapokuwa tatizo la malaria halikumalizika kabisa lakini
nilipata ahueni kubwa na ndipo nilipobaini kuwa kumbe dhana nyingi nilizokuwa
nazo juu ya malaria huenda nyingine hazikuwa sahihi sana.
Nilichogundua mimi
binafsi ni kuwa mwili wangu ni miongoni mwa wale watu ambao kinga yao ya
malaria ipo chini sana jambo linalosababisha mara tu mtu aumwapo na mbu mwenye
vijidudu vya malaria basi mwili hauna uwezo wa kujikinga nao, na hili nililigundua
tangu nikiwa Songea pale ambapo kuna baadhi ya wanafunzi tuliosoma nao walipokuwa
wakikusikia ukilalamika una malaria
walikuwa wakishangaa na hata wengine wakisema walikuwa hawajui malaria inauma
vipi.
Ukaja ujio wa dawa ya
Artemisinin pamoja na mseto wake na dawa nyinginezo, mara ya kwanza kabisa
zilianza kuletwa artemisinin peke yake vidonge ambavyo havikuchanganywa na dawa
nyingine yeyote ile.(Nimesema mimi siyo
mtaalamu wa dawa hivyo inawezekana majina haya naweza nikawa nakosea spelling).
Baada ya kusikia kuna dawa ya malaria ya Kichina imeingia mpya na inatibu
haraka pasipokuchosha mwili sana mara moja nikaanza na mimi kuitumia.
Ni kama
vile vile ilivyokuwa kwa ujio wa SP. Matibabu ya malaria kwa kutumia Artemither
yalikuwa ni ya kushangaza mno, ukianza tu kumeza vile vidonge vya mwanzo,
taratibu dalili zilikuwa zikitoweka mpaka unamaliza dozi malaria nayo kwaheri
huku husikii uchovu wowote kama zilivyokuwa dawa zingine.
Mshangao mwingine
tena ulinikuta baada ya kipindi kifupi tu, kila nilipopata malaria nikatumia
Artemether nilishangaa mbona siponi kama zamani?. Hali kama hiyo hiyo nayo
ilimkuta mke wngu ambaye kwa wakati huo alikuwa mjamzito Daktari mmoja
akapendekeza aitumie kwani haina madhara makubwa. Ulikuwa ni mtihani, mama
aliendelea kulalamika maumivu ya kichwa na mgongo hata mara baada ya kumalizia
ile dozi. Haraka sana nilimwahisha hospitalini wakamuwahi kwinini na ndiyo
ikawa salama yake.
Nilijiuliza haya
malaria kwanini ni kigeugeu hivi? Hata dalili zake unaweza leo ukasikia kichwa
kinauma siku nyingine yanakuja kwa staili nyingine mfano badala sasa ya kichwa unashangaa ni
tumbo tu linauma na kuendesha, wewe kama hautakwenda hospitalini kupima maabara
unaweza ukdhania labda umekula chakula kichafu ukaanza kumeza flajin
kumbe ni mdudu wa malaria. Siku nyingine utasikia tu kiungo labda mguu, mkono,
shingo au hata kiuno kikivuta wewe bila kupima ukaanza kusema “oo..nililala
vibaya”, kumbe tayari ni mdudu wa malaria.
Baadaye serikali nayo
ilianza kutangaza kuwa matumizi ya zile dawa za Artemether peke yake bila ya
kuchanganya na dawa nyingine yeyote yalikuwa hayafai tena kutokana na wadudu
wenyewe wa malaria kutengeneza usugu. Zilianza kutumika dawa mseto ambazo sasa
artemether ya kichina huchanganywa na dawa nyinginezo kuifanya iwe na uwezo
mkubwa zaidi wa kupambana na mdudu wa malaria na moja kati ya hizo ni ile
iitwayo ALU.
0 Response to "MALARIA, UGONJWA HATARI, ULIOJAA MAAJABU NA CHANZO KIKUBWA CHA UMASIKINI.HUUA KULIKO UKIMWI-1"
Post a Comment