MTOTO WANGU MALARIA ILITAKA KUMUUA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MTOTO WANGU MALARIA ILITAKA KUMUUA

SEHEMU YA 2







.........Inatoka sehemu ya- 1
Hata pamoja na kuja huu mseto bado kuna baadhi ya watu wengine wanaodai nao huwa hauwasaidii, wanapomeza dalili za malaria hazitoweki. Hili hata mimi binafsi naliunga mkono ni kweli, kwanza ni kwangu binafsi huwa ni bora hata metakelfin inanisaidia lakini siyo mseto wa alu. Lakini pia kuna watu wengine utawasikia wao wakiumwa ni Alu tu dawa zinginezo haziwasaidii. Pili ni kwa mwanangu wakati huo alikuwa na umri wa miaka 4, kuna siku alishikwa homa tukampeleka hospitalini na baada ya kupimwa alikutwa na malaria 3.

Dokta alimuandikia dawa mseto tukampa hadi dozi ilipomalizika mtoto bado homa ipo palepale na kilichokuwa tu kikimsaidia ni panadol pamoja na maji ya glucose niliyokuwa kila mara nikimpa. Karibu wiki sasa ilikuwa ikimalizika, mtoto hadi akaanza kushindwa kusimama peke yake akisimama hupepesuka na kuanguka chini. Nikawa najipa moyo labda ni zile nguvu za dawa zinamnyongonyesha lakini kila kukicha hali yake ikawa inazidi kuwa tete. 

Hakuna kitu nilichokuwa nikikizingatia kama chakula na maji, na nadhani ndivyo vitu vilivyomuweka hai siku zote dawa zilipokataa, hata akatae vipi, atapike, aharishe, bado mimi sikukubali mpaka nihakikishe angalao hata tone moja la uji au maji limeingia tumboni. Kwa hilo kwa kweli mimi sikuwa na huruma naye labda mama yake ambaye nilimpuuza alipotaka nisimlazimishie chakula.

Tulimrudisha tena kwa  yule dokta na baada ya kumuelezea, akaandika andika kwenye karatasi tukaenda chumba cha dawa na baadaye niligundua alimuandikia sindano za dawa ile ile aliyompatia kama vidonge. Ilikuwa ni sindano ya artemether, ijapokuwa mimi siyo daktari lakini nilishangaa, iweje dawa imemkataa mtu halafu tena achomwe dawa ileile?

Alichoma zile sindano kwa siku nne au tano kama sikosei lakini hali wala haikubadilika. Sikuona haja ya kuendelea tena kupoteza muda kwani mtoto usiku huo alivyokuwa anapata joto sikutegemea kama asubuhi ingefika hajakata roho, usiku kucha mimi na mama yake tukawa tunawekeana zamu ya kulala huku mwingine akimkanda kwa kitambaa cha maji kupunguza joto ambalo panado ilikuwa imeshindwa kazi huku pumzi zikimtoka kwa shida.

Alfajiri tulijihimu hospitali palepale walikomwandikia zile sindano. Mwanzoni tulibishana sana na mama yake, mimi nikitaka tuhamie hospitali nyingine lakini mama mtu yeye alikuwa akishikilia kwamba tukihamia kwingine hawajui historia ya mgojwa hivyo tutaenda kuanza upya huku mtoto akizidi kuteseka.Tulifika pale  hata kabla madaktari wenyewe hawajafika pale, tukasubiri na kuwa watu wa kwanza kumuona dokta.

Hapa kuna ugojwa mwingine hatari kushinda hata Malaria, mbaya zaidi husambaa kwa kugusana na tofauti yake tu ni virusi, usome.

Tulimweleza kila kitu akatuandikia tuende maabara kwenye vipimo. Mtoto alipimwa kuanzia typhoid, UTI, kila kitu akakutwa yupo ok. isipokuwa tu, malaria badala ya kupungua yalikuwa yameongezeka sijui wadudu karibu 8, akachukua simu akampigia mwenzake, alipofika pale walisemezana lugha ya 'kidaktari' japo niliwasikia walikuwa wanazungumza nini. Yule aliyempa mseto alimuuliza mwenziwe hii kesi watafanyaje, akamjibu dawa ni quinine tu, na hata ikiwa ingedunda tena basi wangetumia mbinu ya kumuwekea dozi kidogokidogo mpaka kuhakikisha wadudu wote wanatoweka kabisa mwilini.

Tuliandikiwa kitanda mtoto mara moja akaanzishiwa dozi ya dripu za quinine, aliwekewa kama  dripu tatu au nne hivi, sikumbuki vizuri zilikuwa ngapi. Wakati akiwekewa nusu nizimie pale kitandani, kuna wakati mtoto alibadilika ghafla akaanza kukoroma kwa sauti ambayo kwa kweli iliniogofya, nikajua hapa tayari ndiyo anakata roho, siyo hivyo tu alianza kutetemeka, mama yake alikuwa ametoka kwenda nyumbani kuchukua uji, nikaanza kusali nikijua basi tena, hata hivyo sikukaa kimya nikachukua nguo zote pale nikamfunika ili kama ni baridi basi angalao apate joto.

Sikutulia akili ikanituma labda kwa sababu ya njaa pengine na dawa yenyewe basi kwenye damu ameishiwa sukari, nikakimbia kama mwendawazimu, nikavuka barabara kwenda kutafuta glucose eti nije nimpe. Njiani nikirudi nilijua simkuti lakini Mungu mkubwa nilimkuta bado yupo anakoroma. Baada ya ile dripu kumalizika hali yake ikarudi tena kuwa nzuri nikamwamsha nikampa ile glucose kidogo badae uji akapata tena nguvu kidogo.

Baada ya zile dripu, tuliporuhusiwa, Dokta alituandikia dawa nyingine za vidonge, quinine ya vidonge pamoja na sindano nyingine alizochomwa kwenye makalio. Mtoto siku iliyofuata tu akaanza kuchangamka na mimi nikawa sasa na matumaini kuwa dawa alizopewa zilikuwa zimemsaidia.


HITIMISHO
Baada ya mapambano yangu binafsi na Malaria ya karibu miongo miwili na kupata uzoefu mkubwa kuna vitu nilivyojifunza, kwanza kuna dhana nyingi nilizokuwa nazo ambazo hazikuwa na usahihi kwa asilimia kubwa, dhana kama “nilikuwa na malaria sugu ambayo wadudu wake walikuwa kwenye ini na dawa pekee iliyotakiwa ili nipone ilikuwa ni Piperaquine” kwa kiasi fulani naweza kusema haikuwa sahihi sana kwani kama ilikuwa kweli mbona nilipotumia Sp kwa mara ya kwanza nilipona na nikakaa muda mrefu tu pasipo kuugua? .

Baada ya kuja kwa artemether pia niliweza kushuhudia malaria yakitoweka mwilini na nilikuwa nikikaa hata miezi 3 pasipo kuugua huku nikiwa katika mazingira hatarishi ya mbu. Ukweli ni kwamba mbu wenye wadudu wa malaria wanapokuuma na mwili wako ukawa hauna kinga madhubuti dhidi ya malaria ni lazima utaugua tu hata ikiwa umetoka kumeza dawa siku za hivi karibuni.

Nilijaribu kumuuliza mtaalamu mmoja wa afya kuhusiana na dawa hii ya piperaquine na akanieleza kwamba sababu haipatikani hapa ni kwamba, serikali na hata shirika la afya Duniani huwa na sera zake juu ya maswala yote yahusuyo matibabu mbalimbali na huruhusu tu dawa fulani kutumika eneo fulani kulingana na tafiti zinazofanywa kitaalamu.

Kwa mfano ikiwa sehemu fulani hamna mlipuko wa malaria  aina hiyo inayokaa katika ini basi serikali kuleta dawa kama piperaquine inakuwa kama kupoteza pesa bure, wanaangalia kwanza njia nyinginezo rahisi kukabiliana na tatizo kabla ya ile iliyokuwa ghali.

Inavyoonekana aina ya vijidudu vya malaria inayopatikana Tanzania huweza kutibika kiurahisi na dawa za kawaida. Alinieleza pia kuwa si kama hazipo kabisa la hasha, katika mazingira fulani fulani hupatikana na hasa katika mahosipitali makubwa na katika vitengo vinavyohusika na utafiti wa dawa za magojwa mbalimbali.

Jambo jingine nililogundua ni kwamba Dawa za malaria karibu zote zina tabia ya kujenga usugu kwa vimelea wanaosababisha ugonjwa huo isipokuwa quinine pekee, na hata quinine wanasema nayo hujenga usugu ikiwa itatumiwa peke yake pasipo kuchanganywa na dawa zingine. Vimelea wanaosababisha malaria huwa wana tabia ya kujigeuza kijenetiki(mutation) ambapo dawa zilizokwishazoeleka huwa hazina uwezo tena wa kuwaua, na hata wadudu watakaozaliwa baada ya hapo tena nao wanakuwa na tabia hizo hizo kama mama zao.

Kwa mfano mtu anaweza akala dozi ya quinine ya vidonge kwa mshangao malaria yakawa yako palepale, hii iliwahi kunitokea hata mimi kipindi fulani. Madaktari wenyewe wanafahamu ni katika mazingira gani wakupe dawa hiyo wakichanganya na dawa gani nyingine ndipo unakuta mtu anaweza akapona malaria sugu au kali kama watu wengi tunavyoamini. 

Vile vile Malaria huweza kusababishwa na wadudu wa aina nne na kila mmoja anasababisha malaria iliyokuwa na dalili tofauti nao ni ‘Plasmodium falciparum’, ‘Plasmodium vivax’, ‘Plasmodium ovale’ na ‘Plasmodium malariae’. Plasmodium falciparum ndiyo wabaya kushinda aina nyinginezo zote tatu kwa kusababisha malaria kali na ambayo huweza kuua katika kipindi kifupi na mgonjwa huhitaji kushughulikiwa haraka. Plasmodium vivax hawa husemekana kwamba malaria yake si kali sana, ila ndiyo husababisha yale malaria yanayojichimbia kwenye ini, na hatimaye wadudu hao huibuka baada ya muda fulani, hata miaka. Aina zingine siyo hatari sana, huja polepole na wakati mwingine hutoweka yenyewe baada ya siku kadhaa.

Kinachotakiwa baada ya kutibu malaria inafaa mtu uende tena kupima kuona ikiwa yameisha au bado yapo, ukikuta yapo basi daktari hujua akupe dawa gani nyingine kuliko ungejikalia tu na kusema tayari nimeshakula dozi. Wengi hapo ndipo mauti huwafika kwani haoni tena sababu ya kurudi hospitali kwa imani kuwa dawa aliyokwishakula inatosha, kumbe pengine wadudu wameshajenga usugu na aina ile ya dawa.

Njia mbalimbalia za kujikinga na mbu wa malaria haziwezi kukuhakikishia asilimia mia moja kwamba mbu wa malaria hawawezi kukuuma, mathalani kujifunika chandarua(neti), kunakinga lakini kuna wakati unaweza ukaweka mkono kwenye neti mbu akiwa nje akaweza kukuuma kupitia tundu la neti, dawa za mbu za kupuliza nazo ni hivyo hivyo huuwa lakini kuwamaliza kabisa wote siyo rahisi.

Njia pekee ya uhakika ya kutokomeza malaria ni kwa kuhakikisha mbu wanaangamizwa kuanzia kule wanakozaliana na kujificha. Serikali ingelianzisha kampeni na wananchi wote wakaunga mkono jambo hili lingeweza kufanikiwa, mfano mzuri tunasikia huko Zanzibar walifanya hivyo wakafaulu pia kuna nchi kama Cuba na nyinginezo nao waliweza.

Malaria ni chanzo kikubwa cha umasikini, athari zake tunazichukulia kwa uzito mdogo sana lakini ukweli ni kwamba zinachangia sana kurudisha maendeleo ya watu mmoja mmoja nyuma na hata jamii nzima, katika nyanja zote na hususani kiuchumi. Mimi ni shahidi wa hilo, nimeonja athari zake waziwazi na pengine ni kutokana na kudra za Mwenyezi Mungu tu pekee, hata makala hii pengine nisingekuwa nimeiandika, ningekuwa nimekufa siku nyingi.

Siku moja nikiwa Songea nilitoka  shuleni Matogoro nikaelekea zangu mjini maeneo ya Mfaranyaki alikokuwa anaishi mjomba wangu. Kilichonitoa shuleni siku hiyo ya Jumanne si kingine bali ilikuwa ni homa, malaria. Mwili ukiwa umechoka huku kichwa kikiwa kinagonga kama nyundo. Lengo langu lilikuwa angalao nikapumzike kwa mjomba pamoja na kupata matibabu nikiwa hapo.

Nilipofika maeneo ya stendi kuu nilishika njia moja ya uchochoro ambayo huenda moja kwa moja hadi mfaranyaki. Nakumbuka baada ya kutembea kidogo, nilihisi nguvu zikiniishia, nikatazama matofali yaliyokuwa karibu yangu nikaketi chini. Baada ya kuketi sikujua tena kilichoendelea mpaka pale nilipokuja kujikuta kitandani nyumbani kwa mjomba.

Kwa kweli kama ni kufa siku hiyo nadhani ilikuwa ndiyo siku yangu ila tu Mungu hakuwa ametaka. Nilipouliza nilifikafikaje pale nyumbani, nilielezwa kwamba ni msamaria mwema alinipeleka. Kitu cha ajabu kipindi hicho chote nikisumbuliwa na malaria, ni kwamba sikupenda kabisa kusikia habari ya kuchoma sindano wala kuwekewa dripu. Nakumbuka kwa Dr. Hyera pale Matogoro nilikataa kata kata kuchomwa sindano za quinine mpaka alipoamua kuniandikia vidonge. Pengine nafikiri na hii ndiyo iliyochangia sana mimi kupata  shida kubwa katika kupambana na malaria. 


Una chochote cha kuchangia kutokana na makala hii leo siku ya Malaria Duniani? Hebu tupe na wewe uzoefu wako hata ikiwa ni sentesi moja tu katika kisanduku cha maoni hapo chini. Asante na tuendelee kuwa pamoja katika kulisongesha gurudumu la maendeleo mbele.



*Chanzo cha picha ni mtandao, na siyo picha halisi ya mwanangu.


Ukitaka kusoma sehemu ya 1 ya makala hii "MALARIA UGONJWA HATARI....." bonyeza hapa.











0 Response to "MTOTO WANGU MALARIA ILITAKA KUMUUA"

Post a Comment