Hali ya madeni ya nchi ndogo ya Ulaya, Ugiriki, ni funzo kubwa kote Duniani siyo kwa ngazi ya nchi tu au Taasisi kubwa kubwa, bali hata kwa mtu mmoja mmoja kama iivyokuwa kwako wewe unayesoma makala hii au mimi binafsi.
Kuwa na madeni ni kitu cha kawaida kabisa kwa nchi au
hata kwa mtu binafsi, lakini yanapokithiri na kupindukia mipaka hugeuka
kuwa janga kubwa na kero, hata kufikia hatua ya nchi
kufilisika kabisa na kwa mtu binafsi kufikia hata hatua ya kuamua kujitoa uhai
wake.
Sababu zilizoifanya nchi ya Ugiriki kufika hapa ilipo leo
hii hazina tofauti na zile ambazo
humfanya mtu wa kawaida kufikia hatua ya kukata tamaa kwa madeni makubwa
yasiyolipika kwa urahisi. Wagiriki baada ya kujiunga na Umoja wa Ulaya mnamo
mwaka 1981 na hatimaye sarafu ya Euro hapo mwaka 2001 hapo ndipo deni lao
lilipoanza kukua kidogo kidogo mpaka pale mgogoro ulipokuwa dhahiri kabisa
mwaka 2009 na kuendelea kuitesa hadi hivi leo.
Baada ya kukumbwa na mgogoro kipesa Ugiriki iliendelea
kukopa pesa nyingi na ambazo imeshindwa
kabisa kuzilipa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo, uongozi mbovu
ulioshindwa kusimamia vyema mapato ya nchi, matajiri kukwepa kodi, malipo makubwa ya pensheni ya uzeeni pamoja na huduma za bure za afya. Kwa
ujumla Ugiriki ilikuwa inatumia pesa nyingi kushinda vile ilivyokuwa ikizalisha
yenyewe huku matumizi hayo yakiwa ni pesa za wakopeshaji.
Hapa ndipo hata mtu wa kawaida kabisa kama wewe na mimi
tunapopata funzo kubwa ya kuwa, suala la matumizi hasa ya pesa ni la kufa
na kupona kuhakikisha hutumii kiasi kinachozidi kile kinachoingia, na
tena kinachoingia kwa maana ya ‘jasho na damu’ yako na wala isije
ikawa ni pesa ulizokwenda kukopa kutoka katika taasisi ya pesa kama benki na
taasisi nyinginezo.
Baada ya Wakopeshaji wa Ugiriki yaani Nchi za Umoja wa
Ulaya EU, Shirika la fedha la Dunia ‘IMF’ pamoja na Benki kuu ya Ulaya ECB
kuiwekea masharti ya kubana matumizi
kusudi waipe mkopo wa kuikoa isifilisike, Serikali ya Ugiriki chini ya Waziri
mkuu wake Alexis Tsiprasis ilikaidi
katakata na kuitisha kura ya maoni hapo jumapili yaani leo, wananchi waamue
ikiwa wakubaliane na masharti hayo ya kubana matumizi au wayakatae na kujiondoa
kwenye sarafu ya Euro.
Hakuna njia ya mkato kuondokana na madeni kama
yanayoikabili Ugiriki, zaidi ya kukubali kubana matumizi na kufanya kazi kwa
nguvu zaidi na maarifa, kuendelea kukopa sehemu moja na kwenda kulipa kwingine
hakutosaidia bali kuzidi kulimbikiza madeni ambayo nayo yanakuwa na riba ndani
yake ambayo huzidi kufanya hali kuendelea kuwa ngumu.
0 Response to "JE UNA MADENI KAMA UGIRIKI?"
Post a Comment