Simaanishi hata kidogo ni kiasi gani cha fedha mtu anachotakiwa atoe kwa afisa anayehusika na kuandikisha vitambulisho vya kupiga kura ili ampitishe mlango wa nyuma kwenda kujiandikisha hata kama amekuta foleni ndefu kiasi gani. Wala sina maana kwamba ni shilingi ngapi mtu anazotakiwa alipwe na mgombea au chama fulani cha siasa ili aweze kumuuzia kitambulisho chake kwa madhumuni ya kuja kujiongezea wapiga kura siku ya uchaguzi.
Jana nilipokwenda kujiandikisha ili nipate kitambulisho
kwa ajili ya kuja kupiga kura, njiani na hata kabla sijaanza safari ya kuelekea
huko nilifikiri sana juu muda ambao ningeutumia mpaka namaliza zoezi hili. Niliwahi
kuwasikia watu wengine wakisema, inaweza hata ikakuchukua siku nzima kuanzia asubuhi mpaka jioni kabla
hujafanikiwa kukipata kitambulisho chenyewe.
Akilini nilijaribu kufanya hesabu kwa kufikiria kwa mfano kama mtu ataamua kukokotoa gharama zote
atakazotumia mpaka amepata kitambulisho kile inaweza ikafika gharama kiasi
gani? Nikianza na muda nikasema, kwa mfano ikiwa nitatumia masaa 6 na masaa
hayo nilipaswa niwe katika biashara yangu ambayo niliifunga muda naenda kituo
cha kujiandikisha, ni sawa na faida yote ambayo ingepatikana ndani ya masaa
hayo 6.
Kama toka asubuhi mpaka jioni huwa napata faida, mfano sh. 30,000/- ina
maana kwamba kwa hayo masaa 6 ni kadirio la sh. 15,000/- Kwa ujumla gharama
zote ambazo zingeambatana na zoezi hili zingeweza kuhesabiwa kama ndiyo dhamani
halisi kipesa ya kitambulisho kile.
Lakini bado niliendelea kujiuliza, kama basi dhamani ya
kitambulisho hiki ni sawa na muda unaotumika kukipata pamoja na gharama zote
zinazoambatana na upatikanaji wake, kwanini basi hata watu wenye uwezo tu, kwao
shilingi laki moja, mbili kwao siyo tatizo nao walikuwemo kwenye foleni ya
kujiandikisha?
Ajabu nyingine ni
kwamba, walikuwepo pia na watu wakawaida
tu ambao maisha yao hutegemea zaidi muda wao, kwao mtaji ni muda, akisha
upoteza siku hiyo basi ujue na kula hakuna tena.
Nakumbuka kwenye foleni hiyo jana tulikuwa mchanganyiko wa
kila aina ya watu, walikuwepo wanafunzi hasa washule za sekondari wengi wakiwa
ni kuanzia ‘form two’ na kuendelea, na
utawajua tu kwa stori zao mfano kuna wawili waliokuwa nyuma yangu walinivutia
sana, nilibaini kuwa walikuwa wanafunzi waliomaliza la saba katika shule ile
miaka miwili mitatu iliyopita, mara zote walikuwa wakipiga stori za walimu wao
wa zamani kwa kuwataja majina yao ya utani, jinsi walivyokuwa wakichapa bakora
na hata mwalimu mkuu alivyokuwa akimiliki gari na sasa akaja kubadilishwa cheo
na mambo yake kuzorota.
Walizungumzia pia “mademu” waliosoma nao huku wakiwataja
waliokwishaolewa na wengine wanaodai walikutana nao njiani wakiwa na watoto
walipowaambia mambo vipi wakawajibu, “We shika adamu yako, hebu niamkie” Ina maana
kwamba wasichana hukua upesi kushinda wavulana na hata kuwahi kuanza maisha
kabla yao.
Muda ule maafisa wanaoandikisha walipokuwa wakipata ‘lunch’
ndani, pale nje watu wengi tulikuwa
hatuna mbavu kwa vicheko; vijana watatu, huwezi ukawaita vijana sana kwani
wanaonekana umri wao ni zaidi ya miaka 35 hivi, wakionekana kabisa kuwa
walikuwa wamelewa pombe au ulevi mwingine wowote ule, na mavazi yao na hata haiba zao zilialiashiria kabisa kwamba
ni wapiga debe, au vijana wanaokaa katika vijiwe vya stendi za mabasi.
Awali walikuwa kwenye mistari lakini waliposikia zoezi
limesitishwa kwa muda nao mmoja wao alichomoja akakimbilia nje ya geti la
shule.Punde kidogo alirudi ameshikilia vifuko viwili laini vya lambo mikononi
ndani vikiwa na chakula. Wenzake mara
moja walimfuata kisha wakatafuta mahali wakakaa na kuanza kula ilikuwa ni ugali
na samaki wa mafungu wakukaangwa, walionyunyiziwa kitu mfano wa chachandu.
Maneno waliyokuwa wakitamka na staili zao zilimfanya kila mtu awakodolee macho.
Katika mistari pia walikuwepo Watanzania wenye asili mbalimbali wakiwamo
waarabu na hata wasomali.
Cha kujiuliza hapa ni kwamba, kitambulisho hiki thamani yake ni kiasi gani hasa mpaka watu
wahamasike kiasi hiki?. Mtu mmoja wa makamo jana wakati ule tunalumbana juu yawalioingia mlango wa nyuma alimtania yule askari polisi na kumwambia hivi; “Afande,
hivi unaweza kunijibu ni kwanini zoezi la kujiandikisha huchukua zaidi ya wiki
moja wakati siku ya kupiga kura, watu huenda siku moja tu na kura kuanza
kuhesabiwa siku hiyohiyo?. Askari alicheka tu wala hakumjibu kitu.
Ni nini kilichowasukuma watu kujitokeza namna hii?, je,
ni mwamko wa watu kutambua umuhimu wa kupiga kura, au kuna sababu nyinginezo?
Kuna wanaosema kwamba, watu wamehamasika kutokana na umuhimu wa kitambulisho
chenyewe kuwa, mbali na kutumiwa kupigia kura lakini pia kimekuwa muhimu sana
hasa katika masuala mbalimbali kama vile shughuli za kibenki na kujisajili
sehemu mbalimbali.
Watu wengi ambao walipuuzia zoezi kama hilo miaka
iliyopita kwa muda wote wa miaka mitano au kumi wameonja ‘joto ya jiwe’ kwa
kushindwa kupewa huduma kiurahisi katika taasisi mbalimbali za serikali na hata
zile za kibinafsi.
Mfano mmoja ni rafiki yangu yule niliyemtaja jana kuwa
alijihimu siku ya kwanza kabisa ya kujiandikisha, mimi nikashindwa kwenda.
Kipindi kile cha vitambulisho vya Taifa yeye alipuuzia, siku za hivi karibuni akaja
kujaribu kukifuatilia lakini vikwazo alivyokutana navyo nusu akate tamaa ya
kufuatilia.
Mpaka sasa hivi ninavyoandika haya makala ni zaidi ya miezi miwili
hajafanikiwa kukipata, kwanza kabisa tofauti na ilivyokuwa kwa watu tuliowahi
muda zoezi la kawaida lilipofanyika, sasa mtu analazimika kwanza aende Mamlaka
ya Usajili wa Vizazi na Vifo ‘RITA’ kupata cheti cha kuzaliwa kama hana. Ni
mchakato mrefu, siyo rahisi tena kama mwanzoni.
Leo taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi ni kwamba
muda wakuandikisha umeongezwa siku nne ili kila mtu aweze kujiandikisha.
Binafsi ninaamini kabisa, hakuna mtu atakayebaki tena labda iwe mwenyewe hataki
kufanya hivyo. Thamani ya kitambulisho hiki huwezi ukaithaminisha kwa pesa hata
kidogo. Usipokipata sasa kuna wakati utakuja kukihitaji hata kwa milioni
ukikose, shauri yako.
0 Response to "THAMANI YA PESA KUJIANDIKISHA KUPIGA KURA NI SHILINGI NGAPI?"
Post a Comment