ZOEZI LA KUJIANDIKISHA VITAMBULISHO VYA KURA NA HADITHI YA NGEDERE KUCHIMBA MIHOGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

ZOEZI LA KUJIANDIKISHA VITAMBULISHO VYA KURA NA HADITHI YA NGEDERE KUCHIMBA MIHOGO


Leo majira ya saa tano asubuhi niliamua kwenda kituo cha kujiandikisha kupiga kura ikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya siku ya mwisho iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi. Sababu iliyonifanya nisiende siku za mwanzomwanzo haikuwa nyingine bali ni foleni kubwa iliyokuwepo siku hizo za mwanzo.

Siku ya kwanza kabisa kuna rafiki yangu mmoja aliniambia tujihimu alfajiri ili tuwe watu wa mwanzo kabisa kupewa vitambulisho lakini mimi nikashindwa, yeye alifanya hivyo na kweli muda wa saa sita nilimuona akirudi na kitambulisho nikajuta kwanini sikwenda. Hata hivyo nilijipa moyo kuwa siku za mwisho huenda foleni ikapungua nikaenda kiulaini kumbe utabiri wangu huo haukuwa sahihi.

Nikiwa na matumaini makubwa kwamba nitakuta watu wawili watatu tu kituoni, kwa mshangao nilikuta msururu wa watu ambao kwa kukadiria hata siku ya mwisho ya kesho  ingelikuwa vigumu watu wale kumalizika kwani licha ya foleni niliyoikuta bado watu walikuwa wakimiminika nyuma yangu.

Nikajipa moyo na kujisemea moyoni “Potelea mbali siku ya leo  naandika ndiyo imekwisha  bila kufanya kazi, nitachukulia kama vile ni siku ya mapumziko tu, mbona sikukuu sifanyi kazi na sijutii?” Masaa yalipita nikashitukia inafika saa 8, nilipogeuka kutazama pale nilipoanza kujiunga mtarini niligundua sijasogea hata mita moja na nusu, na nikicheki mbele  mpaka nifike getini kuna kama mita kumi hivi !

Mlangoni palikuwa na askari polisi aliyekuwa akiwaruhusu watu kila baada ya muda fulani kuisha. Walikuwa wakiruhusiwa watu ishirini, kumi mstari wa wanawake, na kumi mstari wa wanaume.Lakini kilikuwa kikipita kitambo kidogo mpaka watu waruhusiwe na cha ajabu ni kwamba mistari ilikuwa inaanzia kwenye geti la shule , watu wanaoruhusiwa huingia ndani wakaenda kutengeneza mistari mingine ndani ya uzio wa shule ndipo waweze kuingia ndani madarasani mlipokuwa na vyumba vya kujiandikishia.

Askari alikuwa hatulii sana getini, kuna wakati alikuwa akionekana kuzunguka nyuma ya madarasa na kuacha mistari peke yake. Wakati fulani alionekana ameketi nje ya geti akila chipsi na dada mmoja anayeonekana kama vile ni mke wake au pengine ni mpenzi wake. Alikaa hapo muda mrefu kiasi kwamba watu kule ndani waliisha wakatakiwa wengine 20 waende lakini askri wa kuwahesabu kulikuwa hakuna.

Tulipojaribu kumuita akajibu, “Si mnaniona nakula jamani, jichagueni wenyewe watu 20 muingie, nyie si watu wazima” Basi kitendo tu cha kutamka vile kundi la watu zidi ya 30 lilizama ndani ya geti haraka, ikabidi askari yule alazimike kuwakimbilia na kwenda kuwarudisha baadhi yao.
Foleni  ya kujiandikisha vitambulisho vya kupiga kura(picha na Eatv.tv, haihusiani na habari yenyewe)
Mambo yaliendelea hivyo lakini sasa ilionekana mistari haisogei kabisa, lakini ukichungulia kule ndani kuna watu wanaotokea nyuma ya yale madarasa na kuingia ndani ya vyumba vya kujiandikisha. Kwa kweli uvumilivu ulitushinda, mimi nilikuwa mbele kabisa nikawaambia wenzangu, “Kama mbwai na iwe mbwai, mimi kitaeleweka huko huko ndani ya geti, naingia zangu”. Baadhi ya watu walinifuata, kwa hasira tukazama ndani bila kuitwa. Kumbuka askari wakati huo hakuwa mlangoni alionekana anazunguka nyuma ya madarasa  na alikaa huko muda mrefu.

Pale nje ya vyumba  tulipokewa na viongozi nadhani wa serikali za mitaa waliokuwa wakisimamia hilo zoezi lakini hatukujali hata walipotuuliza ni kwanini hatukufuata utaratibu, kila mtu akaanza kubwatuka kivyake. Mzee mmoja aliwatolea uvivu akaeleza kila kitu, wasiwasi wake juu ya mazingira ya rushwa yaliyokuwa yakionekana waziwazi. Punde kidogo yule askari  naye alifika pale, naye akaanza kujibishana na umati wa watu waliokuwa wamechoshwa na foleni ile.

Kijana mmoja alifoka na kuwaambia ameshuhudia watu wanane wenye asili ya kiasia wakiingizwa ndani kupitia mlango wa nyuma ilhali wengine tukiwa tunasubiri katika foleni. Lakini yule polisi naye alifoka huku akidai tuoneshe ushahidi  kama kweli kulikuwa na rushwa iliyotendeka pale. Hatimaye busara za baadhi ya watu pale wakiwemo wazee zilisaidia kupoza moto ule na hali ikarudi kuwa kawaida safari hii kila mtu akiapa kutokukubali mtu anayepita kinyume cha utaratibu kuingia ndani ya vyumba vya kujiandikisha hata ikiwa ataletwa na askari ama viongozi wa mtaa waliokuwa pale.

Sasa hadidhi ya Ngedere kuchimba mihogo inakujaje?. Tukiwa bado pale nje ya vyumba vya kujiandikisha badala ya nje ya geti kama hapo mwanzoni, kiongozi mmoja wa serikali ya mtaa alitutaka radhi na kusema kuwa, waandikishaji ulikuwa ni muda wao kupata chakula hivyo tuvute subira mpaka wamalize ndipo zoezi liendelee tena. Kauli ile ilijibiwa na malalamiko mengi miongoni mwao yakiwa, “Hata sisi tuna njaa, watugawie nasisi tule”, “Wanalipwa pesa nyingi na serikali, wavumilie njaa mbona sisi tupo hapa tangu asubuhi tumekula nini?, “Wangekula kwa zamu wachache wakiendelea na kazi wengine wanakula”

Lakini tulisubiri mpaka wote walipomaliza kula ndipo zoezi likaendelea tena. Mzee mmoja aliyekuwa amekasirishwa sana na kitendo kile cha watu kuletwa kupitia mlango wa nyuma baada ya kupata kitambulisho chake na kutoka pale nje alianza kuwaasa waliokuwa katika mistari kwa kuwaambia; "Nyie msije tena mkakubali  kuwa kama ngedere. 
Ngedere akitafuna mhogo.
Ngedere wanapokuwa wakingoa mhogo, mmoja anashika shina la mhogo na kisha wengine huja nyuma kila mmoja akimshika mwenzake kiunoni na kumvuta, kwa namna hiyo huunganisha nguvu ili kazi ya kuungoa mhogo ule iwe rahisi zaidi. Mara tu mhogo unapongoka,  ngedere wote wa mbele hubinuka na kuanguka chali  huku ile mihogo ikirushwa nyuma yao kwa ngedere waliokuwa nyuma”

Yule mzee alikuwa akimaanisha kwamba, wakati mwingine usipokuwa makini, unaweza ukajikuta unawapisha watu waliokuja nyuma yako katika jambo lolote lile kwenye maisha.

Ingawa tulikuwa tumechelewa kuchukua hatua mapema wakati watu wakiingizwa milango ya nyuma, hata hivyo tulifanikiwa kuzuia hali ile na sasa foleni ikawa inaanzia pale pale ndani ya geti la shule badala ya nje ya geti la shule ambapo ilikuwa rahisi ‘kupigwa michanga’ ya macho kwa watu kuingizwa kinyemela pasipo kuwazuia kiurahisi. 

0 Response to "ZOEZI LA KUJIANDIKISHA VITAMBULISHO VYA KURA NA HADITHI YA NGEDERE KUCHIMBA MIHOGO"

Post a Comment