Siyo jambo la kawaida kwa blogu hii kuandika habari/makala
zinazohusiana na maswala ya imani,
isipokuwa tu pale suala lenyewe linapokuwa linahusiana na ujasiriamali moja kwa
moja, hivyo ndugu msomaji unayesoma hapa,ikiwa pengine wewe siyo wa imani ya Kikristo
tafadhali usikwazike kwa kufikiri pengine labda tuna nia ya kujaribu kutaka
kukubadilisha imani uliyokuwepo.
Tunaandika jambo lolote lenye maudhui ya ujasiriamali
hata likiwa lina uhusiano na dini gani, kifupi hatubagui watu kwa msingi wowote
ule na tunaheshimu dini na imani zote hapa Duniani zinazomtaja Mwenyezimungu.
Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, kuhusiana na Mchungaji
huyu, Obadia Alex, ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili, kuna jambo moja
ambalo niliona ni vizuri wajasiriamali wakajifunza kutoka kwake, jambo lenyewe
halihusiani kabisa na imani yake bali na biashara yake ya kuuza DVD na CD za
nyimbo anazoimba.
Bwana huyu nimewahi kumuona mara nyingi tu maeneo ya
Buguruni sheli, sokoni na hata maeneo ya Rozana akiwa na kigari chake cha tairi
mbili, mfano wa mkokoteni wa kubebea vitu, akiusukuma na huku ikisikika sauti
kubwa ya nyimbo za injili ambazo zinapigwa na dvd player iliyokuwa ndani ya
mkokoteni huo. Ndani ya mkokoteni huohuo kuna jenereta ya umeme inayotumika kuendeshea
mitambo yake hiyo ambayo pia kuna kipaza sauti anachotumia kutoa matangazo
mbalimbali sambamba na muziki huo.
Muimbaji
wa nyimbo za injili, Obadia Alex
|
Matangazo anayoyatoa yana ujumbe unaohamasisha watu
wanunue CD yake iliyokuwa na nyimbo kumi, ukiwamo wimbo maarufu na ambao ndio
huutumia zaidi kuuzia cd hiyo uitwao “MAMBO
MAGUMU” pamoja na wimbo wa kwanza uliobeba albamu unaoenda kwa jina la “WEMA WA BWANA”. Sina uhakika kama huwa anatembea maeneo
yote ya jiji la Dar, na nilipanga nimuombe kufanya naye mahojiano lakini
nilipokutana naye nikanunua CD hiyo ilikuwa usiku saa 1 pale sheli, na sikuweza
kumsimamisha muda mrefu.
Nilichojifunza kutoka kwa Mjasiriamali huyu na ambacho kilinisukuma kuandika makala hii
kusudi na wengine nao waweze kujifunza ni “UBUNIFU”.
Kwa kweli kijana yule anastahili kuitwa mbunifu kwani staili ile ya kuuza kanda
ama tuseme CD ni ya kipekee. Sijawahi kumuona mtu mwingine anauza kazi yake
mwenyewe ya sanaa hasa katika upande huu wa muziki na video kwa mtindo ule,
inawezekana wapo lakini hawatakuwa
wengi.
Nadhani changamoto nyingi wanazokumbana nazo wasanii wachanga
ndizo zilizomsukua akaweza kubuni njia hiyo, wasanii wengi wachanga hulalamika
mara nyingi kazi zao kuuzwa nakala nyingi na wale wanaozisimamia huku
wakiwalipa kiasi kidogo kisicholingana na nakala zilizouzwa.
Ijapokuwa njia anayoitumia inaweza ikawa, ngumu, ndefu na
itakayomchukua muda mwingi, lakini anao uhakika wa kurudisha gharama zake
alizotumia wakati akiandaa kazi yake. Nimewahi kuona wasanii kadhaa walioamua
kuuza kazi zao wenyewe lakini hawakutumia “approach” kama ya huyu bwana, Wengi huzunguka nazo mitaani wakiwa
wamezishika tu mkononi, sasa wateja hawawezi kupata nafasi ya kusikiliza kile
kilichokuwemo ndani ya CD hizo zaidi ya kuona picha iliyokuwepo juu ya kasha la
CD au DVD.
Mbali na kuwa na uhakika na mapato yatokanayo na kazi
yake, msanii huyu pia atakuwa na uwezo mkubwa wa “kucontrol”(kudhibiti)
biashara yake, hawezi kupata ‘stress’ zisizokuwa na msingi na hali
hii ya uthibiti, ni muhimu mno hasa katika
ngazi ya kuanza biashara kwani mjasiriamali anakuwa bado mtaji wake ni mdogo na
hivyo changamoto ndogondogo tu zinakuwa na uwezo mkubwa wa kuidumaza biashara
au hata kuiua kabisa ikiwa hana udhibiti wa kutosha na kila mazingira
yanayohusiana na biashara yenyewe.
Ikiwa kwa mfano(siyo idadi halisi anayouza) anao uwezo wa kuuza hata nakala 5 tu kwa siku,
anao uhakika wa kupata 5×5000 =
25,000/-, na fedha hizi anazipokea taslimu (cash) pasipo kupitia sijui kwa
wakala wala nani.
Sikiliza na kuangalia nyimbo zake hapa chini;
MAMBO MAGUMU(VIDEO)
Sikiliza na kuangalia nyimbo zake hapa chini;
MAMBO MAGUMU(VIDEO)
0 Response to "HEBU SOMA ALICHOKIFANYA MUIMBAJI HUYU WA INJILI OBADIA ALEX"
Post a Comment