Tarehe 28 Agosti mpaka 30, lilifanyika kongamano la Wiki
ya Huduma za Kifedha na Uwekezaji linalofanyika kila mwaka katika viwanja vya
Mnazi mmoja jijini Dar es salaam ambalo lengo lake kuu kwa mujibu wa Meneja
mauzo wa kampuni ya Nuebrand EC inayoandaa kongamano hilo, Cathreen Bukuku ni kuongeza uelewa wa masuala yahusuyo fedha,
kwani watanzania wengi wamekuwa
hawatumii njia salama na zilizokuwa rasmi katika shughuli zao za kila siku za
ujasiriamali.
Katika kongamano hilo lililoaza siku ya Ijumaa, wajasiriamali
wengi walifika wakiwa na hamasa kubwa ya kutaka kusikiliza na kujifunza yale
waliyokuwa wameahidiwa katika kongamano hilo. Washiriki walikuwa wengi hasa
wanawake idadi yao ilionekana kuzidi ile ya wanaume, wengine hata walifika
wakiwa na watoto wao wadogo migongoni ilimradi tu wasikose yale yaliyokuwa
yametangazwa kutolewa katika kongamano hili.
Jubilee
Life Insurance, washiriki.
|
Kongamano hili limedhaminiwa na kampuni ya NUEBRAND
ikishirikiana na Shirika la PESCODE na limeshirikisha Wajasiriamali, wasiokuwa
wajasiriamali, Taasisi mbalimbali za fedha kama mabenki pamoja na
mashirika/kampuni za Bima.
Amana
Bank, moja ya washiriki.
|
Nilipata bahati ya kuzungumza na mtu mmoja mwanaume wa makamo ambaye nilikutana naye getini
wakati wa kujiandikisha ili tupewe kibali pamoja na fomu maalumu ya kuingilia
katika kongamano hilo, akanifanya nicheke na kufurahi sana. Kaka yule wakati
akiomba ile fomu ambayo pamoja na vitu vingine ilikuwa pia na ratiba ya
masomo ambayo yangetolewa ndani ya
mabanda mbalimbali, alikuwa akitoa msisitizo mkubwa kwa wale wahudumu akitaka
kuelekezwa banda ambalo lilikuwa na somo la kutengeneza Wine ya Rosella.
Wahudumu walimuelekeza
kuwa kwa siku ile somo hilo lilikuwa likitolewa katika banda la Tembo,
kwani mabanda yalikuwa yamepangiwa kila
moja na masomo yake lakini katika siku zote tatu kila banda linakuwa limepata
masomo yote yaliyokusudiwa. Kwa mfano ikiwa banda la Tembo siku ya kwanza
limeanza na somo la kutengeneza wine ya rosella basi siku inayofuata muda ule
ule litafundishwa somo jingine ambalo lilikwishafundishwa katika mabanda
mengine siku iliyopita na Wine ya rosella watakwenda kufundishwa banda jingine
madhalani Simba au Swala.
Katika mabanda mengine kwa wakati huo walikuwa na masomo
mbalimbali ya utengenezaji bidhaa mfano, chai ya rosella, juisi ya rosella,
ukaushaji wa mbogamboga na matunda nk.
Mimi binafsi kilichonipeleka pale siku hiyo ilikuwa ni
namna ya kutengeneza Mchanganuo wa Biashara pamoja na Shindano la kuandika
mchanganuo wa biashara lakini pia nilivutiwa sana na utengenezaji wa wine ya rosella
kwa hiyo nikaamua niende banda lilelile aliloamua kwenda yule kaka kwani masomo
yote hayo yalikuwepo siku hiyo.
Baada tumeshapewa tikiti zetu, fomu, kalamu,
maji ya kunywa, kijibandiko mkononi kuashiria umesajiliwa pamoja na vipeperushi
kadhaa, mimi na rafiki yangu Yule tulianza safari ya kuelekea kwenye banda letu
la Tembo tulilochagua, huku tukiendelea kuzungumza hili na lile.
Aliniambia hivi; “Unasikia bwana, mimi nina muda mchache
sana na sijui kama kesho naweza tena kuhudhuria hapa, kilichonileta hapa mimi
si kingine bali ni hicho ‘KILAJI’ tu” Akimaanisha kutengeneza wine. Nilicheka
na kumuambia si utani hata mimi ijapokuwa pia nilivutiwa na mchanganuo wa
biashara lakini pia hiyo wine nilikuwa na hamu kubwa sana ya kufahamu namna ya
kuitengeneza. Sote tulicheka mara tukajikuta tumefika banda la Simba.
Tulikaa na kuanza kumsikiliza Mkufunzi kutoka kampuni
moja ya Bima ambaye alikuwa amekwisha anza tayari kuelezea, hivyo sikupata
fursa ya kufahamu jina lake, na hata baada ya kumaliza sikukumbuka tena
kuulizia jina lake na kampuni aliyokuw a ameiwakilisha. Alikuwa akielezea
namna Bima mbalimbali zinavyofanya kazihasa Bima ya vitu, bima ya magari, na bima ya nyumba ambayo alisema hii
hujumuisha pia na vitu vilivyomo ndani kwa mfano, samani, Tv, Compyuta, simu za
mkononi nk.
Mtaalmu huyo alizitaja hatari mbalimbali ambazo biashara, mtu au hata wateja wanazoweza
kukumbana nazo kuwa ni pamoja na moto, wizi, majanga mbalimbali ya asili nk.
Lakini pia alibainisha kwamba zipo hatari nyinginezo kwa mfano katika biashara
ambazo huwezi ukazikatia bima madhalani, hatari inayotokana na ushindani katika
biashara, kuondokewa na mfanyakazi/wafanyakazi na kutokuwa na ujuzi wa kutosha
katika biashara husika nk.
Aliongeza kuwa, hatari
mbalimbali katika biashara au maisha kwa ujumla unaweza ukakabiliana
nazo kwa kutumia moja kati ya njia kuu nne zifuatazo;
1. Kwa
kuondokana nazo kabisa, hii ni kwa kuamua kuachana kabisa na biashara husika.
2. Kukubali,
hii ni kwa kukubaliana na matokeo njia ambayo ni hatari sana hasa kwako
mwenyewe kani hapa ndipo hukuta mtu anaamua kujiua au kupata msongo mkubwa wa
mawazo ambao hatimaye hupelekea kumuua.
3. Kupunguza
hatari, kwa njia malimbali kama kuweka walinzi, fire extinguisher, nk.
4. Na
njia ya nne ambayo ndiyo muafaka zaidi ni Kuhamisha Hatari/Transfer risk au kwa
maana nyingine kukata bima (INSURANCE)
Unaipa kampuni ya bima kazi ya kukulindia mali zako ikiwa hatari
itatokea basi usije ukapatwa na msongo wa mawazo.
Mtaalamu huyo alisisitiza kwamba Bima ni kitu muhimu
sana maishani kwa mtu mwenyewe kama bima
za maisha na afya pia katika vitu na mali kama kwenye biashara zetu, nyumba na
magari. Watu huja kugundua umuhimu wa bima wakati wameshachelewa, yaani wakati
wamekwishapata hasara baada ya majanga kutokea.”Angalia usijekumbuka shuka kungali
kumekucha”
Baada ya somo la Bima kumalizika, tulipumzika saa moja na
baadae tulirudi kuendelea na somo jingine jipya ambalo sasa lilikuwa ni “JINSI YA KUANDAA MCHANGANUO WA BIASHARA”.
Mwalimu/mkufunzi katika somo hili alikuwa Bwana Luther Monko Majoji kutoka
taasisi ya VICOBA ya PESCODE. Bwana
Luther alianza kwa kuelezea maana ya Mchanganuo wa Biashara kuwa ni, Maelezo ya kina yanayoelezea hali halisi ya
biashara kule inakotoka, ilipo na kule
inapopaswa kuwepo wakati ujao.
Alifuatia na kuelezea
umuhimu wa kuandika Andiko la Biashara au kwa lugha nyingine Mchanganuo/mpango
wa Biashara kabla au wakati umeshaanza biashara. Alisema kwamba umuhimu wa
kuandika mpango wa biashara, ni
kumuwezesha mjasiriamali kuwa na dira sahihi ya biashara yake, kubaini
kabla matatizo na vikwazo mbalimbali vinavyoweza kuja kutokea hapo baadaye na
hivyo kuchukua hatua mapema au kuamua kuachana na biashara hiyo kabisa endapo
vikwazo hivyo ni vikubwa mno kuvimudu. Umuhimu mwingine ni kufahamu hali ya
soko ikiwa kweli lipo na litalipa, sekta husika pamoja na vipengele vingine
muhimu kama fedha, usimamizi na ratiba ya uzalishaji.
Umuhimu mwingine ni katika kuwavutia wawekezaji pamoja na
wadau mbalimbali kama vile mabenki na taasisi za mikopo wakati utakapohitaji
kukopa au kuongeza mtaji wa biasara yako ili iwezekukua zaidi. Wadau hao
watahitaji uwashawishi ni namna gani umejipanga
kwa kuwaonyesha mchanganuo wako na siyo kwa maneno matupu.
Vile vile mchanganuo wako wa biashara utakusaidia ikiwa
utakopa fedha benki au kutoka taasisi yeyote ile, uweze kuzielekeza katika zile
shughuli za kibiashara ulizokusudia kuzifanya pekee na wala siyo kwingineko kokote
kule ukizingatia ya kwamba hela ya mkopo siyo yakwako ni ya watu, na faida
unayoipata unatakiwa kwanza uhakikishe unarejesha mkopo pamoja na riba yake
wakati huo huo unatakiwa pesa hiyohiyo ukuze mtaji pamoja na gharama nyinginezo
kama vile mishahara na kodi ya pango.
Alisema pia ya kwamba mchanganuo unakufanya ufahamu ikiwa ni kiasi gani cha fedha kinachohitajika
katika biashara iwe mpya au ya zamani iliyokwisha anzishwa.
MTIRIRIKO WA MCHANGANUO WA BIASHARA.
Bwana Luther akielezea kwa kifdupi jinsi mtiririko wa
mpango wa biashara unavyopaswa kuwa alisema kuwa mpango wa biashara unaanza na;
1. JALADA
LA NJE, ambapo juu yake utaandika aina ya biashara, anuani na jina la
muandaaji.
2. Muhtasari,
ufupisho wa mambo yote yaliyopo ndani ukijumuisha, dira malengo, bidhaa, soko,
fedha, utawala pamoja na bajeti.
3. Malengo
ya biashara.
4. Masoko.
5. Usimamizi
6. Fedha
na
7. Ratiba
ya uzalishaji bidhaa au huduma.
Hatimaye somo la mchanganuo wa biashara lilimalizika na
tukapewa maelekezo juu ya shindano la kuandika mchanganuo ambapo kila mshirikia
aliyependa kushiriki alitakiwa mara baada ya kumaliza semina akachulue fomu ya
kushiriki mlangoni na kisha atakwenda kuandaa mchanganuo wa biashara yake na
kisha tarehe 15 au 15 Septemba atatakiwa kurudisha fomu katika kijiji cha Makumbusho Kijitonyama Dar
es slaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni. Washindi katika shindano hili
watapewa ruzuku kwa ajili ya kuendeleza biashara zao ambapo wa kwanza atapewa
kitita cha shilingi za Kitanzania 2,000,000/= wa pili sh. 1,500,000/= na watatu
sh. 1,000,000/=
Hebu sikiliza sauti(audio) ya mkufunzi huyo Bw. Luther Monko Majoji akitoa mada.
Hebu sikiliza sauti(audio) ya mkufunzi huyo Bw. Luther Monko Majoji akitoa mada.
UTENGENEZAJI WA MVINYO WA ROSELLA (WINE)
Somo lililofuata lilikuwa ni namna ya kutengeneza mvinyo
wa Rosella kwa vitendo, somo lililowasilishwa na, Bibi Stella Matutina
Mwombeki, mama mjasiriamali anayemiliki kampuni ya kutengeneza mvinyo (wine ya
rosella) iitwayo “MATUTINA NATURAL PRODUCTS” iliyo na makazi yake huko Mbezi
Beach jijini Dar es salaam, aliianzisha tangu mwaka 2007 na hujihusisha pia na
utengenezaji wa vitu vingine kama vile,garlic paste, ukaushaji wa mbogamboga na
viungo.
Alianza kwa kuuliza swali, “Ni nini maana ya neno
mjasiriamali?. Washiriki mbalimbali walinyosha vidole na mmoja akajibu,
“Mjasiriamali ni mtu mwenye ujasiri wa mali ambaye hutumia ubunifu kuanzisha
biashara”. Mkufunzi alikubaliana naye kuwa alikuwa sahihi, baada ya kutoa maana
yake, na kusema kuwa; “Mjasiriamali ni mtu anayeanzisha biashara
kwa lengo la kupata faida na wakati huohuo kuwa tayari kupata hasa endapo
itatokea”
Baada ya hapo alianza kuelezea namna ya kuandaa wine ya
rosella, na kusema kuwa Rosella ni maua ya mti wa rosella au kwa jina jingine
hujulikana kama Choya na ambao hupatikana zaidi katika mikoa ya Singida
na Dodoma lakini pia hata hapa Dar es salaam huweza kuota lakini unahitaji maji
mengi sana.
Akielezea zaidi kwa vitendo Bi Stella alisema kuwa
angefundisha kutengeneza wine ya rossela katika lita tano kutokana na ufinyu wa
vifaa vilivyokuwa pale pamoja na muda, ila vipimo ambavyo angetupa pale ni
vipimo vinavyotosha kuandaa wine katika lita 20 hivyo katika lita 5 itabidi
kugawanya vile vipimo ya lita ishirini katika sehemu nne za lita tanotano.
Mahitaji
ya kutengeneza wine katika lita 20
· Rosella
grammu 200
· Maji
lita 20
· Sukari
kilo 6
· Ndimu
4 au kama ni limao ziwe 2
· Majani
ya chai vijiko vya chai 4
· Hamira
vijiko 4 vya chai.
Vifaa.
1. Dumu
au ndoo yenye mfuniko wa kufunga vizuri.
2. Jiko
la mkaa, au la gesi.
3. Sufuria
la kuchemshia maji.
4. Ndoo
2
5. Mwiko
1
6. Vijiko
viwili vya chai.
7. Kisu.
8. Chujio.
9. Mrija
wa kutolea hewa.
Alitutia moyo kwa kusema kuwa kila kitu kinawezekana,
kwani yeye alipoanza alianza na lita 20 na hakuanza kuuza mbali bali aliwauzia
watu wa karibu waliomzunguka. Akizidi kubainisha alituambia hivi; “Msiogope
Wine inalipa”
Vile vile alitutajia faida za Rosella na wine kwa ujumla
kwa kusema kwamba, mmea wa rosella unaojulikana kwa jina la kisayansi kama “Rosella
Hibiscus Sabdarifer”, una faida nyingi katika mwili wa binadamu kama
vile;
· Huongeza
damu mwilini.
· Hushusha
shinikizo la juu la damu ‘high blood pressure’ na kuondoa mafuta mabaya mwilini
au ‘cholesterol’
· Husaidia
kupunguza athari zitokanazo na unywaji pombe(Hangover)
· Husaidia
kupunguza unene.
· Huchochea
kinga za mwili, kutokana na kuwa na vitamin c kwa wingi na pia husaidia kutibu
mafua.
· Chai
yake ikinywewa mara kwa mara husaidia kuzuia maambukizi ya kibofu cha mkojo
pamoja na kurahisisha usagaji wa chakula tumboni.
Chai
ya Rosella.
|
Alizitaja pia faida za wine mwilini kuwa ni; kusaidia mwili
usizeeke haraka, akitoa mfano alisema kuwa watu duniani walikuwa wakishangaa ni
kwanini Wafaransa hawazeeki au kufa haraka wala kupata magonjwa ya mara kwa
mara, wataalamu wakafanya research (utafiti) na kubaini kuwa ni kwa sababu
Wafaransa hupendelea zaidi kutumia wine. Kila mtu katika nyumba yake utamkuta
ana wine na huitumia kidogo kabla na baada ya chakula kwa kiasi kidogo na wala
siyo kunywa kwa ajili ya kulewa.
Faida nyingine alizitaja kuwa ni pamoja na;
· Kusafisha
mafuta mwilini hasa yale yanayozunguka moyo.
· Inasafisha
ini, figo na kutoa gesi tumboni.
· Hupunguza
unene, mfano kina mama wenye matumbo yaliyomwagika hasa baada ya kuzaa
wakitumia kidogokidogo hupungua, alitoa ushuhuda yeye mwenyewe kuwa alikuwa mnene
sana baada ya kuzaa lakini alipotumia sasa yupo fiti.
· Huondoa
msongo wa mawazo(stress/tension)
· Huongeza
CD4.
· Huongeza
nguvu za kiume.
· Husaidia
kina mama wanapofikia umri wa kukoma hedhi(menopause)
· Husafisa
kizazi.
· Husaidia
kutibu kikohozi
· Hutibu
Pressure na
· Wine
iliyokomaa pia hutumiwa kuoshea vidonda.
Baad ya kuelezea faida za wine na rosella tuliendelea na
somo letu ambapo sasa alianza kuelezea vitendo, au jinsi ya kuchangavya vile
vitu.
· Tumia
chumba maalumu kisiwe na mwanga sana ambacho hamna mtu atakaye ingia mara kwa
mara.
· Kwanza
unachemsha maji(zingatia sana usafi)
· Toboa
mfuniko wa chombo na uweke mrija wa hewa kisha ziba kwa nta ya mshumaa eneo
ulikotobolea huo mrija wa hewa. Unaweza ukatumia ‘air lock’ ambazo hutoka nje
ya nchi au mpira unaotumika kwa ajili ya dripu.
· Kata
ndimu/limao na kisha ukamue juisi yake kwenye kikombe.
· Koroga
hamira, hamira tumia hamira maalumu za wine zinazopatikana katika
masupermarket, hizi ni hamira kama za mandazi ila ni spesheli kwa wine, zina
flavor/ladha ya wine.
· Tia
rosella yako kwenye yale maji ya moto yanayochemka na kisha yakishabadilika
rangi kuwa juisi uipue.
· Kabla
hujaanza kutia mchanganyiko wa vitu vyako kwenye hiyo juisi acha kwanza ipoe
kidogo, joto la kadri kama nyuzijoto 30c hivii. Ikiwa hutaki wine, ni juisi tu,
basi hapa unaweza ukaweka sukari na baada ya kupooza katika friji ukaanza
kuinywa kama kawaida.
· Chuja
juisi yako ya rosella.
· Chuja
majani chai.
· Anza
kuweka juisi ya ndimu, mchanganyiko wa majani chai na maji au ile juisi ya
rosella iliyochujwa kwa chujio, halafu weka mchanganyiko wa hamira huku
ukikoroga kwa mwiko.
· Ukimaliza
funika chombo chako na kisha ncha ya pili ya ule mrija wa hewa unauingiza
kwenye chombo kingine kama ndoo au chupa
yenye maji kusudi hamira itakapoanza kuchachua kutoa hewa basi hewa ile itoke
kama povu ndani ya chombo hicho pasipo kuruhusu hewa kuingia ndani ya hombo
chako cha wine.
· Wine
mpaka iwe tayari kutumiwa inakaa miezi 9. Baada ya mwezi mmoja, unafunua chombo
chako kisha unaichuja kwa kitambaa safi au mfuko, halafu unairudisha tena
katika chombo kilichosafishwa vizuri na kuifunika kwa ule mfuniko wenye mrija
wa hewa. Baada ya miezi 2 tena unafanya vile vile, kila baada ya miezi 2 mpaka
mwezi wa 9 inakuwa haina hewa tena. Ukianza kuiuza ikiwa na miezi labda 2 au 3
inakuwa bado na hewa na chupa utakayoweka inaweza ikalipuka au kupasuka
kutokana na hewa.
· Baada
ya miezi 9 unaichuja vizuri kabisa, unaweza hata ukatumia kifaa kiitwacho ‘filter’
kinachouzwa, itaonekana ‘clear’ pasipo kuwa na uchafu wa aina
yeyote tayari kwa ‘kuipack.’ (Ufungashaji) katika chupa zilizokuwa safi na
kuweka lebo tayari kwa kuuzwa au matumizi.
*Aidha siyo lazima ikae miezi 9 lakini
miezi 9 ndiyo muda ambao inakuwa imechachuka vizuri zaidi na hewa yote imetoka.
Wine haiharibiki wala haina tarehe ya mwisho ‘expire
date’ endapo utaifunika vizuri isiingize hewa. Ukienda ulaya zipo hata
zenye umri wa miaka 300 na kadiri inavyokuwa na miaka mingi ndivyo thamani yake
nayo inavyokuwa kubwa.
Bibi Stella anasema kwamba chupa za kupack wine yake
huagiza Afrika ya kusini, zamani walikuwa wakizipata Sido lakini kwa sasa
hawana. Anasema ‘package’ ufungashaji ndiyo siri kubwa itakayo kufanya uuze
wine yako. Kwa mfano alisema ukipaki wine yako katika chupa labda ya
plastiki inaweza isipate wateja kwani wine ina heshima yake na wanywaji wake
huvutika zaidi zinapokuwa katika chupa maridadi za kioo.
Alipoulizwa kama wine yake huuza katika Supermarket kubwa
kama Nakumatt alisema bado yeye hajawa tayari kusupply huko kwani hajajipanga
vyakutosha, alisema unaweza ukapeleka oda huko
una chupa zako labda 100 wakakuambia ulete lita elfu 10 katika masupermarket
yote ya Nakumatt, unapeleka mara ya kwanza ya pili huna, watakuona mbabaishaji.
Pia alisema inatakiiwa unapoanza kuzalisha basi uwe na
kazi nyingine ya kukuwezesha kuishi kwani itabidi usubiri miezi 9 na inakubidi
ili usije ukakaukiwa na wine basi utengeneze angalao kila mwezi au baada ya
miezi 2 au 3.
Wakati wote zoezi hili lilipokuwa likiendelea yule rafiki
yangu, “mzee wa kilaji” tuliyekutana mlangoni, mara tu somo la wine
lilipoanza ‘aliruka’ akaenda kukaa kiti cha mbele karibu na mkufunzi, na mara
kwa mara nilimuona akinyosha mkono akiuliza maswali kwa umakini wa hali ya juu!
Hata kabla somo halijamalizika vizuri baadhi ya washiriki
walianza kujinunulia wine ya Matutina hasa iliyokuwa ikiuzwa sh. 4,500/= kwani
pia ilikuwepo na kubwa ya sh. 10,000/=
Bibi stella kuhusiana na wale wasiokunywa pombe au wenye
imani zinazokataza kutumia vileo alisema kuna wine isiyokuwa na kilevi na
hutengenezwa kama hihii ya kilevi lakini kuna chombo maalumu ambacho hupatikana
nje ya nchi ambacho hutumika kuondoa Alcohol mpaka inabadilika na kuwa
0%Alcohol. Hata yeye katika sampuli alizoleta pale darasani kwa ajili ya
kutuuzia kulikuwepo pia na hiyo wine isiyokuwa na kilevi.
Kwa kweli muonekano wa chupa za wine za huyu mama hauwezi
ukautofautisha na ule wa wine zingine zitokazo nje ya nchi kama vile za Afrika
ya kusini, Ufaransa na hata Uholanzi.
Wine zake kwa sasa alisema huzisambaza katika maduka ya
reja reja ya kawaida na supermarket ndogondogo jijini Dar es salaam hasahasa
katika maeneo ya Mwenge, Tegeta, Tangibovu na Tabata Segerea huku akijipanga
kwa ajili ya kuuza katika masupermarket makubwa na nje ya nchi, bidhaa zake
zina ubora uliopitishwa na vyomb vyote husika serikalini kuanzia, Manispaa,
TRA, TFDA naTBS.
Mbali na kutengeneza mvinyo Bibi Stella pia
hujishughulisha na kilimo cha rosella, ana mashine ya kukaushia ambapo pia huitumia
kukaushia rosella kwa wajasiriamali wengine wasiokuwa na kifaa hicho kwa
malipo,ukiwa na rosella yako anakukaribisha uende ukakaushe kwake pamoja na
huduma zozote zingine zinazohusiana na rosella.
Alitutia moyo kwamba hakuna jambo lisilowezekana ukiwa na
nia ya dhati, na ikiwa kuna mtu yeyote ambaye angependa kufahamu zaidi juu ya
utengenezaji wa wine au hata soko la wine basi ni ruksa kumpigia simu kumuuliza
kwa msaada wowote ule, au anaweza akafika kiwandani kwake Mbezi Beach, Tangi
Bovu na pia alitupa namba zake za simu ambazo ni 0756368844 na 0782368844,
STELLA MATUTINA MWOMBEKI.
Msikilize Stella Mwombeki mwenyewe hapo chini alipokuwa akitoa mada juu ya namna ya kutengeneza mvinyo/wine ya Rosella. (SEHEMU YA 1)
Picha za semina ni kwa hisani ya tovuti ya Amana bank pamoja na blogu ya charaz.blogspot.com
0 Response to "SHINDANO LA MCHANGANUO WA BIASHARA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA NA UWEKEZAJI, WAJASIRIAMALI WALIVYOHAMASIKA."
Post a Comment