KATI YA OBAMA NA PUTIN, NI NANI ANAYEISAIDIA IS? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KATI YA OBAMA NA PUTIN, NI NANI ANAYEISAIDIA IS?

(Ni mtazamo wangu.)
Rais wa Marekani Barack Obama amenukuliwa akisema kuwa, Mashambulizi ya Urusi dhisi ya Magaidi wa IS  nchini Syria eti ni kuwadhoofisha waasi waliokuwa na msimamo wa wastani, na kuzidi kuwapa nguvu  Magaidi hao wa IS.Lakini Moscow kwa upande wake imepinga madai hayo ya Marekani na kusema kuwa  lengo lake kuu ni kuwasambaratisha magaidi hao wanaohatarisha amani ya Dunia nzima.

Kwa maoni yangu binafsi, nafikiri tatizo hili la Syria waliolilea na kuifikisha Syria pale ilipo sasa hivi pamoja na tatizo la maelfu ya wakimbizi wanaomiminikia Ulaya kutafuta hifadhi baada ya nchi zao kukumbwa na machafuko ni nchi za Magharibi zenyewe zikiongozwa na Marekani. 

Kile kilichokuwa kikidhaniwa hapo kabla kuwa kilikuwa ni msimu wa machipuo katika nchi za Kiarabu, “Arab Spring” sasa hivi kimegeuka na kuwa msimu wa machipuo ya wahamiaji wanaotoka nchi za kiarabu kukimbilia Ulaya kwa machafuko yaliyochochewa na wao wenyewe Ulaya na Marekani.

Kwa kisingizio cha kuleta Demokrasia na kuwangoa viongozi madikteta ili kuleta utawala Bora, nchi za Magharibi Marekani akiwa kinara wao, walifanikiwa kumg'oa Sadam Hussein wa Iraq, Hosni Mubarak wa Misri, Muammar  Gaddafi wa Libya, Zine el Abidine Ben Ali wa Tunisia, Ali Abdulah Saleh wa Yemen na sasa Bashar Al Assad ambaye ameshindikana kung'oka baada ya Urusi kumkingia kifua.

Ukiiondoa Tunisia, karibu nchi nyingine zote maraisi wao waliolazimishwa kuondoka madarakani hamna hata moja iliyokuwa salama sasa, hata Misri pamoja na kuurudisha utawala wa kijeshi kupitia kwa  Abdel Fattah el-Sisi bado hakujatulia kama ilivyokuwa enzi za Hons Mubarack.Sasa haya machipuo ni machipuo ya aina gani ikiwa hayaleti neema?

Marekani na washirika wake walijidai kuwasaidia waasi wa Syria wenye msimamo wa wastani ili kumuondoa Assad ikiwa ni pamoja na kupigana na magaidi wa IS lakini cha ajabu mpaka sasa hivi hakuna lolote lililofanyika, na tunaambiwa kwamba hata kikundi wanachodai kukipa mafunzo ya kupambana na IS, badala ya kupambana walikwenda kugawa silaha walizopewa kwa magaidi wengine wa Al-Nusra Front.

Obama anamlaani sana Bashar Al Assad kuwa ni muuaji, aliyewaua wananchi wake mwenyewe, hilo hamna mtu anayelipinga lakini mimi najiuliza, hivi Assad na IS ni nani aliyeua watu wengi zaidi ya mwingine?

Hata kama Assad aliua watu, kwani aliwaua katika mazingira gani? Aliamua tu kuwaua hivi hivi au ni baada ya uasi kutokea tena uasi wenyewe ule wa vikundi mfano wa IS na Al Nusra Front ambao hata ingelikuwa Marekani wenyewe wasingeliweza kuvumilia.

Marekani na washirika wake wakumbuke kuwa wale wanaowaita waasi waliokuwa na msimamo wa kadri ndiyo hao hao wakati mwingine hugeuka na kuwa wenye misimamo mikali. Mfano mzuri ninchini Libya, waasi walisaidiwa vizuri tu kumng'oa na kumuua Gaddafi lakini ni nani alijua kuwa waasi wale wale waliokuwa wakijifanya wanademokrasia kumbe walikuwa na ajenda za kidini na sasa ndiyo wanaoifanya Libya isitawalike?.

Mimi nadhani kabisa kwamba Marekani haijashindwa kuisambaratisha IS,ila inachelea kufanya hivyo kwa sababu lengo lake kuu siyo kuingoa IS bali Assad ambaye inadai ndiye mtu mbaya zaidi nchini Syria. Madai haya ya Marekani si mageni, iliwahi tena kumchukia Saddam Hussein vilevile kama inavyofanya kwa Assad, hali kadhalika na kwa Muammar Gaddafi.

Tabia hii ya Marekani kumchukia mtu mmoja na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wengi wasiokuwa na hatia ndiyo inayosababisha nchi nyingi za Kiarabu zikumbwe na misukosuko na matokeo yake ndiyo hayo sasa Ulaya inalipa kwa kushuhudia utitiri wa wahamiaji usiowahi kushuhudiwa karibu kipindi cha nusu karne iliyopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Wallid Muallem akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York alisema kuwa mashambuli ya angani pekee pasipokuwa na msaada wa mashambulizi ya ardhini  kamwe hatayaweza kuwashinda magaidi wa IS na hilo kweli linathibitishwa na mashambulizi Marekani na washirika wake ambayo wamekuwa wakiyafanya dhidi ya IS kwa kipindi kirefu sasa pasipo kuonyesha mafanikio ya maana.


Alisema Mashambulizi ya Urusi yatazaa matunda kutokana na kupata msaada wa kweli kutoka kwa jeshi la ardhini la Syria ambalo ndilo pekee linaloonyesha kupambana na magaidi hao kiukweli na siyo vikundi vidogo vidogo vyenye maslahi yao binafsi Marekani inavyodai ni waasi wa msimamo wa kadri.

Obama ana wasiwasi endapo mpango wa Urusi utafanikiwa na kuwasambaratisha IS basi Marekani wataonekana si lolote tena katika siasa za Dunia na hilo litamfanya Rais Obama hadhi yake kushuka huku ile ya Rais Putin kuwa juu zaidi. Hata katika suala la Ukraine ambalo Marekani na nchi za Ulaya wamekuwa wakiiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi Urusi itaibuka kidedea na kuonekana hata vikwazo hivyo havina maana tena.

Kwa maoni yangu binafsi, mimi naona ni bora Syria chini ya Bashar Al Assad, kuliko Syria chini ya IS, na kitendo cha Marekani kudai inawasaidia waasi wa kadiri kumngoa kwanza Assad ndipo ije iwangoe magaidi wa IS baadaye, mimi huko naona Obama anawasaidia magaidi hao dhahiri shahiri. Hana tofauti na Uturuki inayojidai kufanya mashambulizi nchini Syria ikidai inapambana na IS kumbe lengo lake ni kupambana na Wakurdi wanaodai kujitenga, kwao Wakurdi ni wabaya kushinda IS.

Viva Urusi, viva Puttin kwa kuchukua hatua ya kuwaumbua hawa wanafiki, Marekani na vibaraka wake wanaoona ni bora raia wasiokuwa na hatia waendelee kutaabika, huku wakikosa pa kukimbilia kwa kisingizio cha kumkomesha mtu mmoja tu, ASSAD.

Inauma sana kuona watu ambao walikuwa na nyumbani kwao, wanalazimika kuhama na watoto na familia zao kukimbilia usalama, wanafika kule wanakoamini kuna usalama, nako wanakataliwa, wanasababisha wenyeji wao kuwa na mjadala mkali, wawakubaki au wawakatae.

Ulaya hata ikiwa watu wenye mioyo mizuri kama kina Angela Markel watakubali vipi kuwapokea wahamiaji wanaokimbia machafuka Mashariki ya kati na Afrika ya Kaskazini lakini dalili siyo nzuri hata kidogo, raia wa kawaida wameshaanza kuchoka hawataweza kuvumilia kupokea wahamiaji kwa kipindi kirefu na itafika mahali wataonyesha hasira zao, kama siyo kwa kuanzisha maandamano ya kupinga basi watawakataa viongozi wanaotetea hilo kwa njia za kura.

Kwa hiyo suluhisho la kweli pekee la mgogoro wa Syria siyo kuweka sera nzuri za kuwapokea wahamiaji tu, bali ni kutibu mzizi wa tatizo ambao ni kusimamisha vita nchini Syria na nchi zingine kama Libya na Yemen na hili litawezekana  tu kwa nchi zote Duniani bila kujali nchi inaendeshwa na Assad au nani, kukaa na kujadili namna ya kupambana na vikundi vyote vinavyoleta machafuko kwa kisingizio chochote kile.


0 Response to "KATI YA OBAMA NA PUTIN, NI NANI ANAYEISAIDIA IS?"

Post a Comment