Katika makala zetu siku za nyuma niliwahi
kuandika makala iitwayo, NI KITABU GANI HAUTAKISAHAU MAISHANI?. Kitabu ambacho
mimi siwezi kukisahau maishani, siyo lazima wewe ama mtu mwingine naye iwe hivyo hivyo, kila mtu
anaweza akawa na mtizamo wake tofauti kuelekea kitabu/vitabu fulani.
Tanzania na Duniani kwa ujumla wake, vimewahi
kuandikwa vitabu vingi vya kila aina, kuanzia vile vya Dini, elimu na maarifa
mbalimbali mpaka vile vya hadithi na riwaya. Kuna vitabu vikubwa na vidogo
vilivyoandikwa katika lugha mbalimbali kutoka katika mabara yote ya dunia
kuanzia Asia, Ulaya Amerika, Afrika na Australia.
Vitabu ndiyo chimbuko la Ustaarabu duniani
kote, kwa mfano inasemekana maandishi ya kwanza kabisa yalianza kutumiwa huko
Sumeria ya kale katika karne ya 3 -7 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo (IRAQ YA LEO) kati kati ya mito ya Tigris
na Euphrates katika mfumo uliojulikana kama ‘pictographic’ au maandishi yanayowakilisha picha za
vitu halisi badala ya herufi kama hizi tunazotumia leo hii.
Mpaka kufikia maendeleo ya sasa ukiachilia
mbali teknolojia ya kompyuta na mtandao wa intaneti vilivyoibuka hivi karibuni
tu, ni vitabu na maandishi ya aina mbalimbali yaliyokuwa yakitumiwa katika kurithisha
maarifa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine ijapokuwa pia katika jamii nyingine
ambazo hazikuwa na maendeleo makubwa kiteknolojia mfano maeneo mengi ya Afrika,
Australia na hata Amerika walikuwa
wakitumia njia za masimulizi kueneza na kurithishana maarifa kutoka kizazi hata
kizazi.
Katika tasnia ya biashara na Ujasiriamali hapa Afrika ya mashariki na hususani
nchini Tanzania, vipo vitabu vingi tu vinavyohusiana na taaluma hizo lakini kwa
bahati mbaya sana vingi vimeandikwa katika lugha ya kiingereza, na utakuta mara
nyingi mtu anapotaka kusoma kitabu fulani basi ni sharti awe na
kamusi(dictionary) pembeni kwa ajili ya kutafsiri(translate english to Swahili).
Tatizo hili la lugha ya kiingereza kwa hapa
Afrika ya Mashariki lipo kwa sisi Watanzania zaidi kuliko nchi zingine kama
Kenya na Uganda, na hii imetokana hasa na mfumo wetu wa Elimu tangu enzi zile
za Mwalimu ambapo tumekuwa “Mshika mawili”,
kiswahili tunataka na kiingereza nacho tunakitaka kwa wakati mmoja, mwishowe
tunajikuta kila moja hamna tunayoimudu barabara. Huwezi ukamkuta mtu Kenya au
Uganda akisoma kitabu cha kiingereza na huku pembeni eti kaweka na kamusi ya
kiswahili.
Kwa kweli ili maarifa ya aina yeyote yale mtu
aweze akayapata yakamwingia vizuri zaidi kichwani na hatimaye akawa na uwezo wa
kuyatafsiri kivitendo(translation of
knowledge into action) kwa urahisi pasipo kuhangaika na kamusi wala ‘google
translator’, basi hana budi kuijua bara bara lugha anayoitumia
kujifunzia.
Vitabu vingi vizuri vya Biashara,
Ujasiriamali na maendeleo binafsi, siyo siri, vimeandikwa katika lugha ya
kiingereza. Sina maana kuwa hamna vya kiswahili vilivyokuwa vizuri, la hasha,
vipo ingawa siyo vingi kama ilivyokuwa vya kiingereza.
Ikiwa uwezo wako katika lugha ya kiingereza
ni mzuri kwa kweli hauna shida ya kusoma vitabu vizuri, vipo vingi sana hata
nikisema nivitaje hapa patakuwa hapatoshi. Tukianza na kitabu maarufu zaidi
duniani cha pesa na mafanikio “THINK
& GROW RICH” au kwa ‘jina la utani’ “MSAHAFU WA MAFANIKIO”,
kitabu hiki kinapatikana bure kabisa mtandaoni pasipo kulipa hata senti
hamsini,download kitabu hicho hapa free, ukitaka katika lugha ya kiingereza au
katika mitandao mingine kinapopatikana.
Lakini tukirudi katika mada yetu kuu iliyokuwa ikisema, “Kwa
maisha ya mafanikio: Soma vitabu hivi vya Biashara na Ujasiriamali kwa Kiswahili”,
bila shaka ndugu msomaji utakuwa na shauku ya kutaka kuvijua hivyo vitabu ni vipi,
na mimi sikukudanganya kwani dhima yangu kuu ni kuhakikisha kila
ninachokiandika humu kwenye blogu ni sahihi na kimefanyiwa utafiti wa kutosha
kabisa.
Umuhimu wa kusoma au kujifunza maarifa iwe ni
ya kisayansi, ya kibiashara, ya kihandisi, ya kitabibu, ya kiufundi au ya aina
nyingine yeyote ile katika “LUGHA YAKO YA MAMA” nikiwa
namaanisha ile lugha yako uliyojifunza toka utotoni ni mkubwa sana kwani
humsaidia mhusika kuelewa haraka na kwa urahisi zaidi tofauti na kutumia lugha
ya pili au ya tatu. Kuna mifano mingi kwa mfano Wachina, Wajerumani, Wakorea,
Wajapani, Wavietnam na hata Warusi, huzitumia lugha zao za mama kujifunza
maarifa ya aina zote kuanzia fasihi, sayansi na teknolojia, biashara, ufundi
mpaka aina zote za ufundi na uhandisi. Na wanafanikiwa kufanya vizuri hata
kuwashinda waanzilishi wenyewe wa teknolojia hizo Waingereza na Wamarekani.
Kitabu cha “Think & Grow Rich” licha ya
kuwa unaweza ukakisoma kwa lugha ya
kiingereza pia unaweza ukakisoma katika lugha ya Kiswahili fasaha kabisa
bila ya kuwa na kamusi pembeni ya
kiingereza-kiswahili(English to Swahili) kupitia blogu hii ya
jifunzeujasiriamali. Kitabu hiki kitakufunulia siri nyingi na mbinu mbalimbali
matajiri wengi na watu mbalimbali waliwahi kufanikiwa kimaisha, njia
walizopitia mpaka kufikia pale walipofikia.
Vitabu vingine vya Ujasiriamali, Biashara, Pesa
na Mafanikio katika lugha adhimu ya Kiswahili pia unaweza ukavipata kutoka
kampuni ya Self Help Books PublishersLimited. Vitabu kama vile, “Jifunze Michanganuo ya Biashara na
Ujasiriamali”, “Siri ya Mafanikio ya Biashara ya Rejareja”
na “Mifereji
ya Pesa na Siri Matajiri wasiyopenda kuitoa”. Mbali na vitabu vya Self
Help Books, pia kuna waandishi wengine wengi tu wa Kitanzania, vitabu vyao
vimeandikwa kwa Kiswahili na unaweza ukavipitia ikiwa vitakupendeza. Tuachane
na ile kasumba mbaya ya kudharau kila kinachofanywa na Watanzania wenzetu.
Mfano mmoja ni mtu mmoja tena mwandishi mwenzangu aliyenishangaza sana kwa
kudiriki kuandika katika blogu yake kuwa yeye hasomi tu hovyo hovyo vitabu
vilivyoandikwa na waandishi wa hapa nchini.
Akataja baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na
waandishi wa ngambo akidai ndivyo yeye hupenda kuvisoma. Kwa maoni yangu huyu
hawezi kuwa mwandishi mzuri kwani mwandishi unapaswa usome kazi za watu wengine
hata ikiwa unaamini kiwango chao ni kidogo ndipo utaweza kujua wewe unao uwezo
gani. Kumbuka ile kanuni maarufu ya soko isemayo, “Katu usiwadharau washindani wako”
Narudia tena kusema kuwa, kama wewe upo
vizuri katika lugha ya kiingereza, una uwezo wa kuitumia pasipokuwa na
vipingamizi vinngi ikiwa ni pamoja na uwezo hata wa kufikiri kwa kutumia lugha
hiyo, siyo kusoma tu na kuandika pekee, basi unaweza ukajisomea vitabu
vilivyoandikwa katika lugha hiyo na vikakupa manufaa yaliyokusudiwa bila ya
kutumia nguvu nyingi na muda. Ushauri wangu ni kwamba ukitaka kujifunza kitu
kwa urahisi na haraka zaidi basi tumia ile lugha unayoielewa vizuri zaidi na
mara nyingi huwa ni ile lugha ya mama uliyoanza kujifunza muda mfupi baada ya
kuzaliwa kwani ndiyo ubongo wako uliyoizoea zaidi.
Njia mbadala, unaweza ukaamua basi ikiwa kile
unachotaka kujifunza kipo katika lugha fulani tofauti na ile lugha yako ya mama
madhalani katika kiingereza, basi suluhisho ni wewe kuhakikisha unajifunza
vyema na kukizoea kiingereza ili wakati wa kukitumia basi usipate vikwazo.
0 Response to "MAISHA YA MAFANIKIO?: SOMA VITABU HIVI VYA BIASHARA NA UJASIRIAMALI KWA KISWAHILI"
Post a Comment