UNAJUA BIASHARA YA CHIPSI KUKU, SODA INAVYOLIPA DAR? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UNAJUA BIASHARA YA CHIPSI KUKU, SODA INAVYOLIPA DAR?

Bila shaka kama wewe ni mkazi wa jiji la Dar es salaam au hata ulishatembelea hapo, ni lazima tu umewahi kula chipsi, kama siyo chipsi kuku basi itakuwa ni chipsi mayai au hata chipsi kavu huku ukishushia kwa kinywaji baridi na kinaweza kikawa labda ni soda, juisi au hata maji ya chupa. Lakini umewahi kujiuliza ni kwanini chakula hiki kimekuwa kinapendwa hivi na watu wengi?
 
Chipsi mayai, kuku na soda baridi.
Ingawa uandaaji wenyewe wa chipsi siyo rahisi sana  kwa yule anayeifanya kazi hiyo, lakini kwa mlaji chipsi huonekana kuwa chakula rahisi sana, kutokana na maandalizi yake kutokuchukua muda mrefu kwani zinakuwa zimekwishakaangwa tayari ni kupasha tu, na pia anaweza akabeba na kuondoka nazo “take away” bila kuchafuka kwa  michuzi  wala mafuta ikiwa zitafungashwa vizuri katika mfuko wa plastiki au karatasi ya aluminiamu maarufu kama ‘foil paper’.

Mbali na sababu hizo mbili, chipsi ni chakula kitamu sana, ziwe zimekaangwa kwa mayai, kuandaliwa na kuku, samaki au mishikaki, ukishushia na kinywaji bariidi kama soda au juisi unapata burudani ya aina yake.

Chipsi hazina rika, hupendwa na kila mtu, watoto, vijana watu wazima na hata wazee, wanafunzi ndiyo  kabisaa usiseme, hata husababisha mara nyingi kuwaingiza vishawishini wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari  na kuishia kupata mimba wakiwa bado hawajahitimu masomo yao. Utasikia watu wakisema “huyu alidanganywa kwa chipsi na soda”.

Chipsi  mayai iliyokauka.
Jijini Dar es salaam karibu kila mahali utakuta mabanda ya kuuzia chipsi, kwenye maeneo ya kuuzia vyakula kama, migahawani, grocery za bia, mabaa na kuzunguka maeneo mbalimbali ya shule na vyuo.

Kwa ujumla mahitaji ya chakula hiki, chipsi ni makubwa sana kushinda vile mtu unavyoweza  kufikiria, na wateja kuna vitu vikubwa vitano vinavyowafanya wanunue chipsi mahali fulani na kuacha mahali pengine, vitu hivyo ni hivi hapa; kwanza Usafi, pili huduma nzuri, tatu ni ufungashaji mzuri, nne ubora na tano ni bei.

1.  USAFI.
Usafi ni kigezo kikubwa sana kwa mteja kupenda kununua chipsi mahali fulani na kuacha pengine. Unaweza kukuta mahali fulani wateja hawakauki na wanaweka hadi foleni kusubiria chipsi ili-hali jirani tu kuna mabanda mengine yanayouza chipsi kama hizohizo. Usafi kuanzia wahudumu wenyewe, vyombo mpaka meza na mahali wateja wanapoketi wakila ni muhimu sana. Usafi unatakiwa kufanywa kila siku na kwa ukamilifu wake.

2. HUDUMA NZURI KWA MTEJA
Ukarimu wa watoa/mtoa huduma, ni jambo muhimu mno, wateja hawataki ukali ukali usiokuwa na maana, mteja muda wote anatakiwa achukuliwe kama mtoto mdogo, kamwe haitakiwi aonekane mkosaji, hata ikiwa ana makosa. Kuchukuliwa kwa upole, anaweza akaomba aongewzewe 'vichipsi' kidogo na muuzaji mwenye busara atampa japo punje moja ama mbili naye ataridhika na kesho atarudi tena. 

3. UFUNGASHAJI.
Zamani wauza chipsi wengi walizoea kufungia wateja chipsi wakitumia makaratasi ya magazeti yaliyotumika au mifuko ya plastiki maarufu kama mifuko laini. Lakini kwa sasa hivi muelekeo umebadilika baada ya watu wengi kuwa na elimu ya kutosha juu ya madhara ya mifuko ya aina hiyo. Wateja sasa wanapendelea zaidi chipsi zilizofungashwa kwa karatasi ya aluminium(foil). Ukiziweka zinavuta wateja.

4. UBORA.
Ubora hapa ninamaanisha chipsi na mayai au kuku kukauka vizuri, mishikaki iliyoiva sawasawa, kachumbari iliyotayarishwa katika hali ya usafi pamoja na viungo vingine kama vile tomato sauce, pilipili, karafuu nk.

5. BEI.
Kuna wanaoangalia pia bei, ikiwa ni bei ya wastani basi wapo tayari kununua lakini inapokuwa juu sana ya wastani, utawasikia wakisema “anafikiri anawauzia watalii hapa”.

Chipsi  mishikaki na kachumbari. 
Lakini ukiacha utamu wote huo wa chipsi na vivywaji baridi kuna kitu kimoja cha hatari sana, kinachohusina navyo.Vyakula hivi ni muuaji wa taratibu (silent killer). Ulaji wa chipsi mayai, kuku wa kisasa, chumvi kupita kiasi, sukari kupindukia, mafuta mengi na hata nyama nyekundu unahusishwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa makuu ya tabia yakiwamo, kisukari, shinikizo la juu la damu, kansa na kiharusi.

4 Responses to "UNAJUA BIASHARA YA CHIPSI KUKU, SODA INAVYOLIPA DAR?"

  1. Asante kwa elimu nzuri. Swali langu je faida ni asilimia ngapi ya mapato.?

    Mfano katika mauzo ya 300,000. Faida inaweza kuwa sh. Ngapi hapo?

    ReplyDelete
    Replies
    1. OK. Niwaweka mchanganuo next time katika blog hii kufahamu hilo

      Delete
  2. Kuhusu suala la biashara hizi nidili sana.

    ReplyDelete
  3. Ni kweli mr. Adam ukisimamia fresh haiwezi kukutupa hata kidogo

    ReplyDelete