Katika Jiji la Dar es salaam, wezi na
matapeli kila kukicha huvumbua njia mpya za kutekeleza uhalifu wao ilimradi tu
wamejipatia pesa pasipo kuvuja jasho jingi. Wakati polisi wakihangaika kuwasaka
wezi wanaonyemelea wateja kwenye ATM mashine ili kukopi namba zao za siri na
hatimaye kuja kuwaliza, kuna wimbi jingine la wahalifu ambao wao kazi yao ni
kuwaliza wahudumu katika vibanda vya kuweka
na kutolea pesa maarufu kama Tigo pesa, M-pesa,Airtel money na Ezy pesa.
Leo hii asubuhi, maeneo ya Buguruni stendi ya Muhimbili,
jamaa mmoja nusura achomwe moto na wananchi wenye hasira kali baada ya jaribio
lake la kuiba na kutokomea na pesa kiasi cha shilingi laki mbili na elfu
ishirini kugonga mwamba. Shuhuda wa tukio hilo mwanausalama(lakini siyo wa
jeshi la polisi) na ambaye pia kukosa kuwepo yeye huyu kibaka sasa tungelikuwa
tunamwita marehemu anasimulia mkasa wenyewe
kama ifuatavyo;
“Nilikuwa nimekaa karibu na kibanda cha kutolea pesa na kuweka pesa katika simu za mkononi,
mara akaja kijana mmoja na kumtaka mhudumu amuwekee shilingi laki moja na elfu
sabini katika simu. Baada ya kumtajia namba yule dada alitaka kwanza apewe pesa
lakini kijana alimwambia asiwe na wasiwasi bali aweke kwanza. Dada aliweka na
kutaka sasa apewe pesa lakini kijana badala ya kumlipa alimtaka aongeze tena
kiasi kingine cha shilingi elfu hamsini ndipo amlipe, naye akafanya hivyo.
Dada alianza kuingiwa na wasi wasi baada ya kijana yule kutokuonyesha
dalili zozote za kulipa pesa zaidi ya kushika bahasha mkononi huku akijisachi
sachi kama mtu aliyepoteza pesa. Ikabidi dada yule atuombe msaada watu
tuliokuwa karibu pale huku tayari akiwa amekwishamkwida shati na kumnyanganya
ile bahasha aliyokuwa nayo mkononi. Tulipoifungua ndani mlikuwa na udi na unga
unga mfano wa dawa ya kienyeji.
Kumbe wala mfukoni hakuwa na simu, zile pesa zilitumwa
kwa mtu mwingine tapeli mwenzake, dada alijaribu kumpigia simu wala
hakupokelea, haraka akapiga simu mtandao uliotumika kutuma zile pesa lakini nao
wakamjibu kuwa pesa zilizotumwa zimekwishatolewa.
Raia wengi walikuwa wamekwishaanza kujaa pale, na alijitokeza
kijana mmoja akamrukia yule kibaka kwa hasira akitaka kumtoa koromeo huku
akidai ni juzi tu mdogo wake anayemuuzia kibanda cha pesa aliibiwa kiasi
kikubwa cha pesa kwa mtindo huo. Baada ya kuona vile ilinibidi nimzuie na
kumuachanisha lakini watu walijawa na hasira wakidhani mimi ni kibaka mwenzake.
Ikabidi nijitambulishe, ‘jamani mimi ni mwanausalama, na
ikiwa mtamuua huyu mtuhumia mbele yangu sitakuwa nimetimiza wajibu wangu, na
isitoshe kumuua siyo suluhisho kwani huyu dada hataweza kuzipata pesa zake
zilizokwishaibiwa. Inabidi huyu akawaonyeshe hao wezi wenzake aliowatumia hizo
pesa, ni lazima anawajua’
Kibaka
akichomwa moto na wananchi wenye hasira kali.
|
Pamoja na kujitambulisha lakini watu hawakujali kitu,
mmoja akasema leteni petrol na mara moja ikaletwa , kuona vile ikabidi nitumie
nguvu za ziada kumsukumiza yule kibaka mle ndani ya kibanda alikokuwa yule dada
na kuufunga ule mlango. Raia mmoja akasikika akisema, ‘sasa umeamua kumingiza huyo
mwizi huko ndani ili akambake dada wa watu kabisa siyo?’
Mara bosi wa yule dada naye alifika pale, nikamkabidhi na
kumsihi asikubali watu wamuue yule mwizi mikononi mwake kwani itamletea
matatizo baadaye, badala yake akaripoti polisi waje wamchukue na ndipo hata
pesa zake zinaweza zikapatikana. Mimi niliondoka na kuwaacha lakini wakati huo
wote yule kibaka alikuwa amenywea utafikiri alikuwa amemwagiwa maji. Baadaye
nilirudi pale kuulizia hatima ya mkasa ule nikaambiwa polisi walifika pale na
kuondoka na mtuhumiwa pamoja na wale walioibiwa pesa zao."
Alimalizia kusimulia mwanausalama huyo kutoka jijini mbeya aliyefika hapa Dar kwa safari ya kikazi.
Alimalizia kusimulia mwanausalama huyo kutoka jijini mbeya aliyefika hapa Dar kwa safari ya kikazi.
0 Response to "WIZI NA UTAPELI VIBANDA VYA KUTOA/KUWEKA PESA, TIGO VODA AIRTEL NA ZANTEL"
Post a Comment