Habari hii ni kutoka tovuti ya idhaa ya
kiswahili ya Redio DW Ujerumani
Kiongozi wa Kanisa Katoliki
Duniani Papa Francis ameyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kulazimisha demokrasia
yake kuenea katika mataifa mengine pasipo kuheshimu asili ya siasa za wazawa.
Kiongozi
wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ameyakosoa mataifa ya Magharibi kwa
kutaka kuiuza aina ya demokrasia yake kwa mataifa mengine pasipo kuheshimu
asili ya siasa za wazawa, huku akipongeza kuchaguliwa kwa meya wa kwanza
Muislamu jijini London.
Katika
mahojiano hayo na gazeti la Kanisa Katoliki la nchini Ufaransa La Croix , Papa
Francis amesema Ulaya inapaswa kuunganisha vyema suala la wahamiaji na kampeni
ya kusambaza kile kinachoitwa demokrasia ya Kimagharibi kwenye mataifa
wanakotoka wakimbizi hao.
Papa
Francis ameliambia gazeti hilo na hapa namnukuu: "Kulingana na kitisho cha
ugaidi wa Kiislamu, tunapaswa kuhoji namna demokrasia ya mataifa ya Ulaya
ilivyopelekwa katika mataifa ambayo yalikuwa na nguvu, kama nchini Iraq au
Libya, ambako kulikuwa na muundo mzuri wa kikabila." Mwisho wa kunukuu.
Ameongeza
kwamba hakuna hatua zinazoweza kupigwa pasipo kuzingatia tamaduni hizo.
Akitolea mfano siasa za Libya, Papa Francis anasema "kama Walibya
walivyosema hivi karibuni, tulikuwa na Gaddafi mmoja ila sasa wapo 50",
akirejelea rais wa zamani wa taifa hilo, Muammar Gaddafi, ambaye
aliondolewa madarakani na kuuawa mwaka 2011.
Mara
kadhaa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amekuwa akishambulia kile anachokiita
"ukoloni wa kitamaduni" ambapo mataifa yaMmagharibi yanalazimisha
maadili yake kuenea katika mataifa yanayoendelea kwa malipo ya misaada ya
kifedha.
Amesema
suala la wakimbizi wa "maghetto" halikuwa baya, lakini limepotoshwa
katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Ametolea
mfano wa shambulizi la bomu la mjini Brussels la mwezi Machi kuwa magaidi hao
walikuwa ni raia wa Ubelgiji, wakiwa ni watoto wa wahamiaji waliokulia katika
maghetto.
Katika
hatua nyingine, Papa Francis amepongeza kuchaguliwa kwa Sadiq Khan kama meya wa
kwanza Muislamu wa jiji kubwa la London nchini Uingereza. Anasema kuwa na hapa
nanukuu "Jijini London, meya mpya aliapishwa katika Kanisa Kuu na pengine
alipokelewa na Malkia. Hii inaonyesha umuhimu wa Ulaya kurejesha uwezo wake wa
kushirikiana." Mwisho wa kumnukuu.
Siku 10
zilizopita Papa Francis aliyakosoa tena mataifa ya Ulaya kwa kutoa majibu
yasiyoridhisha juu ya utitiri wa wahamiaji wanaokimbia vita na umaskini
Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Mwandishi:
Sylvia Mwehozi /RTRE
Mhariri:
Mohammed Khelef
0 Response to "PAPA FRANCIS I: TULIKUWA NA GADDAFI MMOJA SASA TUNA (50) HAMSINI"
Post a Comment