1. Anza kwa kuwa na mtazamo
sahihi akilini wa kijasiriamali.
Kwanza kabisa anza wewe mwenyewe
kuiandaa akili yako kisaikolojia kuwa na mtazamo wa
kijasiriamali(entrepreneurial mindset) kwani mafanikio yeyote yale ama utajiri
huanza na mtazamo sahihi, maneno sahihi na mpango sahihi. ”Miongoni mwa watu zipo tofauti ndogo
lakini tofauti hizo ndogo matokeo yake huzaa tofauti kubwa. Tofauti hizo
ndogo ni mitizamo na tofauti kubwa ni ikiwa mitizamo hiyo ni hasi au
chanya.”-maneno hayo yaliwahi kutamkwa na mwandishivitabu na mfanyabiashara
mashuhuri W. Clement
Stone.
Ni dhahiri kabisa kwamba
kuanzisha biashara, ni lazima ipo siku itakubidi ufanye uamuzi mgumu wa kuamua
kuachana kabisa na ajira uliyokwisha izoea na ambayo inakupa ulinzi kifedha,
utakuwa sasa unahama rasmi kutoka kuwa mwajiriwa na kuwa mwajiri hivyo inakupasa
ujiandae kiakili na changamoto zote zinazoambatana na hatua hiyo ya awali ya
kuanza biashara kuanzia mizizini.
Thomas Jefferson, Rais wa tatu wa
Taifa la Marekani naye aliwahi kusema hivi; “Hakuna chochote kiwezacho
kumzuia mtu mwenye mtazamo sahihi wa mawazo kutimiza malengo yake; na
hakuna chochote kile juu ya Dunia kinachoweza kikamsaidia mtu mwenye mtazamo
potofu wa akili”
SOMA: Njia za kujiingizia kipato cha ziada nje ya kazi yako ya msingi.
SOMA: Njia za kujiingizia kipato cha ziada nje ya kazi yako ya msingi.
Kuanzisha biashara ndogo, iwe ni
katika muda wako wa ziada, nje ya kazi ama kama shughuli yako ya kudumu
masaa yote inakupasa kuwajibika au kubeba majukumu na ili kuifanikisha kwa
mafanikio unatakiwa kujijengea stadi au tabia za kijasiriamali kama vile,
uvumilivu, mbinu za uongozi, stadi za mawasiliano, stadi za mauzo, majadiliano
nk. Somo zima la stadi na tabia za ujasiriamali limeelezewa kwa kina sana
katika kitabu chetu kiitwacho “MICHANGANUO YABIASHARA NA UJASIRIAMALI” kukipata bonyeza maandishi hayo.
2. Andika Mpango wa
Biashara.
Hatua inayofuata katika kuanza
biashara muda wako wa ziada ni kuandika mchanganuo wa biashara kutokana na wazo
lako la biashara uliyoichagua. Unaweza ukawa tayari unao mpango wako wa
biashara kichwani na ni lazima utakuwa nao kwani kitendo tu cha kufikiria
kuanza biashara tayari ni hatua moja ya kuanza kupanga. Ninachosisitiza hapa ni
kuandika katika karatasi. Mpango wa biashara unaweza ukaandika vyovyote vile
hata kama ikiwa hautafuata zile taratibu rasmi za kuandika mpango wa biashara.
Unaweza ukaorodhesha yale mambo
ya msingi tu yatakayosaidia katika kufanikisha biashara yako kama vile, una
malengo gani na biashara yako, biashara itakuwa mahali gani, mtaji wako
ni shilingi ngapi na utaupata kutoka wapi, ni nani utakayemuachia majukumu ya
biashara wakati haupo, ni kina nani unaotarajia kuwauzia bidhaa/huduma
zao, ni akina nani wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya, ni mbinu gani
utakazotumia kujulisha wateja juu ya uwepo wako, unatarajia bidhaa/huduma zako
utauza shilingi ngapi, faida unayotegemea kuipata katika kipindi fulani,
chaweza kikawa ni siku, wiki, mwezi au hata mwaka nk.
Kwa kifupi unapaswa kufanya
tathmini nzima na kwa kina jinsi unavyotarajia kuianzisha na kuiendesha
biashara yako ndogo ungali bado na majukumu mengine ya kazi au ajira.
3. Tafuta msaidizi au mbia
mwenye malengo na biashara.
Kabla hujachagua mbia wa biashara
au msaidizi, ni lazima uhakikishe kwanza, kuwa huyo utakayekwenda kushirikiana
naye katika biashara anayo maono
na ndoto sawa na za kwako.
Anapaswa kuzifahamu barabara changamoto zinazoweza kutokea kwenye biashara
mnayotaraji kuifanya na anatakiwa pia kuwa tayari kutoa mchango wake uliokuwa
sawa na wa kwako kuhakikisha uhai wa biashara.
Wafanyabiashara wakubwa na
waliofanikiwa sana kama akina Bill Gates, Steve Jobs, Mark Zuckerberg na
wengineo wengi katika nyakati tofauti wamewahi kukiri kwamba mafanikio
yao makubwa kwa kiasi kikubwa yametokana na kutengeneza ubia mzuri tangu hatua
za awali kabisa za kuanza kwa miradi yao.
Jambo lingine la kuzingatia
unapomchagua mtu wa kusaidiana naye kwenye biashara kama mbia ni nguvu
alizokuwa nazo huyo mwenzako; ni lazima uchague mtu mwenye uwezo ambao wewe
hauna; kwa mfano kwa kuwa wewe bado utakuwa kwenye ajira au shughuli
nyingine itakuwa ni jambo la busara kumpata mtu ambaye yeye muda wake wote
atautumia katika biashara yenu kusudi aweze kujaza pengo lile litakalotokana na
kukosekana kwako pale muda wa kazi.
Ikiwa biashara yako utaamua
kuifanya na mbia, basi hakikisheni mnaweka ua wa kisheria ili kuepukana na
matatizo yanayoweza kuja kujitokeza hapo baadaye. Labda uwe umeamua kufanya
mwenyewe ukamuweka mfanyakazi lakini ikiwa ni mbia mkataba wa kisheria ni kitu
cha lazima na mara nyingi sana kwa watu wanaoanzisha biashara ndogo “part time”
wakiwa wangali bado kazini au katika majukumu mengine tofauti, huwa
wanawatafuta wabia na siyo kuendesha peke yao au kuajiri mfanyakazi. Na uzoefu
kote duniani unaonyesha kuwa biashara ndogo ukiwa kazini hushamiri na kupata
mafanikio makubwa unapoifanya kwa ubia na mtu mwingine.
4. Sasa Anza Biashara yako bila
kuchelewa.
Wahenga hawakukosea waliponena, “Asiyeanza,
kamwe hatamaliza” Kuanza biashara ni kama vile mtu unapotengeneza
mashua na kuanza safari baharini huku ukiwa mkononi una ramani, mpango, pamoja na timu
ya wasaidizi pembeni. Unatakiwa
kusafiri pamoja na kutokuwa na uhakika asilimia mia moja wa usalama dhidi ya
dhoruba wala hali ya hewa isiyotabirika. Endapo mashua yako itazama
baharini, kuna mawili, ukatishe kabisa safari na kuachana nayo, ama
uamue kurudi ufukweni, ukatengeneze mashua nyingine na kuanza safari tena upya.
Kwa nini nasema uanze biashara
yako bila kuchelewa?, nasema hivyo kwa sababu waajiriwa wengi wamekuwa wakiota
kuanzisha biashara zao ndogo wangali bado wakiendelea na ajira zao lakini kitu
kikubwa ambacho mara zote kimekuwa kikiwavuta shati kwa nyuma wasianze kimekuwa
ni “WOGA”. Huendelea tu kufanya mipango siku hadi siku wakisubiri kila
kitu kitengemae, kumbe haitafika siku hata moja kila kitu kikatimia ndipo
uanzishe jambo.
Katika kitabu cha Gwiji, Robert
Kiyosaki, “Before you Quit
your Job, 10 Real Life Lessons…..” anabainisha
kwamba, vipo vipengele vitatu unapoanzisha biashara, cha kwanza ni mpango
sahihi, cha pili ni timu sahihi na cha tatu ni mtaji(pesa). Katika hili
Kiyosaki anaelezea kwamba, hutokea mara chache sana vipengele hivi vitatu
vikapatikana vyote kwa pamoja wakati mtu anapoanzisha biashara.
Anaendelea kutanabahisha kwamba;
“Ni jukumu lako mjasiriamali
kuchukua kipengele kimojawapo na kuanza kufanya biashara, vingine viwili
vinavyobakia utakutana navyo mbele ya safari. Kuvipata vipengele viwili
vilivyosalia inaweza ikakuchukua mwaka au hata zaidi ya miaka 10; swala ni
kwamba, anza na kile ulichokuwa nacho” – Robert
Kiyosaki.
Hata kama hauna mtaji wa kutosha,
anza tu na kile ulichokuwa nacho kwani makampuni unayoyasikia yakitamba
duniani leo hii kama vile, ‘Yahoo’, ‘Google’, ‘facebook’ na hata ‘Dell ‘yote
hayakuwa na fedha za kukodi vyumba kwa ajili ya ofisi, badala yake walianzia
katika mabweni ya shule na vyuo. Siyo hao tu, kina ‘Amazon’, ‘Ford motors’ na
‘Apple’ wao ofisi zao zilianzia katika magereji ya kutengenezea magari
5. Pangilia ratiba zako na gawa
majukumu kwa mbia wako.
Hatua ya tano ni wewe kupangilia
ratiba zako kwa kufahamu muda utakaokuwa ukijihusisha na biashara yako. Je,
utakuwa ukijihusisha usiku, muda baada ya masaa ya kazi, ama mwishoni mwa juma
wakati wa ‘weekend’? Ili biashara yako iweze kusimama ni lazima uipe muda wa
kuishughulikia, na uuheshimu muda huo kwani kitu kikubwa kuliko vyote
utakachopaswa kuwekeza katika biashara yako ikue ni muda. Ili kupata muda, panga
ratiba, jua malengo yako ni yapi, panga na kuutumia muda kikamilifu, ainisha
vikwazo na fursa kisha tengeneza mikakati.
Ikiwa unaye mbia hapa sasa ndipo
mahali anapotakiwa kuonyesha uwajibikaji wake. Mbia atakusaidia kutimiza baadhi
ya majukumu huku wewe ukielekeza nguvu zaidi kwa yale majukumu ya msingi zaidi
yanayoifanya biashara iweze kukua. Hakikisha mnagawana sawa majukumu na kila
mmoja kuwajibika kwa kila jukumu atakalopangiwa kulifanya.
6. Panga muda au lengo
utakapoacha kazi yako.
Baada sasa umekwisha anza
biashara yako ndogo, hatua inayofuata itakuwa ni kuweka lengo la muda
utakapoachana na kazi yako au ajira uliyokuwa nayo. Bila shaka yeyote ipo
siku moja utakwenda kuacha kazi na kuamua muda wako wote uutumie katika
kuijenga biashara yako. Jambo hili la kupanga tarehe ya kuondoka unaweza
ukalifanya kwa kutumia vigezo tofauti, kwa mfano unaweza ukatumia kigezo cha
kiwango fulani cha ukuaji wa biashara au kigezo kingine chochote kile
kilichofikiwa. Hata hivyo bila ya kuzingatia kigezo chochote ulichochagua, ni
lazima ujiwekee muda utakapoachana na kazi yako na kuamua sasa kuelekeza nguvu
zako zote na muda kwenye biashara yako.
7. Endelea kuwekeza kwenye
biashara yako mpaka utakapofikia malengo yako ya ujasiriamali.
Kumbuka ya kwamba kuwa na
biashara endelevu siyo kazi unayoweza ukaifanya kwa siku mbili ama tatu, ni
mchakato endelevu. Ili iendelee kuwepo inabidi uendelee kuifanyia ubunifu mpaka
pale ambapo itakuwa imekua kubwa kiasi ambacho siyo lazima tena uwepo wewe
ndipo iweze kuishi.
Kitu kingine muhimu sana na
usichopaswa kamwe kukisahau ni kwamba, kama mjasiriamali, ni lazima ujifunze
kuishi bila ya kutumia mapato yatokanayo na biashara yako ili kuhakikisha
mzunguko chanya wa pesa unakuwepo mpaka pale biashara itakapokuwa kubwa vya kutosha.
…..……………………………………………………….
Kwa msaada zaidi wa jinsi mtu
unavyoweza ukafanikiwa katika mchakato mzima wa kuanzisha biashara ukiwa
bado unaendelea na kazi au majukumu yako mengine ya msingi, ninapendekeza
kitabu chetu kiitwacho “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRIMATAJIRI
WASIYOPENDA KUITOA” Toleo
jipya lililoboreshwa na kuongezewa vitu, 2016, nina uhakika
kitazidisha uwezekano wako wa kufanikiwa. Kukipata kitabu hicho, bonyeza
maandishi makubwa ya jina la kitabu hapo juu. Kinapatikana kwenye mifumo
yote, kama kitabu cha kawaida cha karatasi(hard copy) na pia katika mfumo
wa kitabu-pepe(soft copy)PDF file
Pia kupata vitabu vingine vya
self help books ltd kupitia email kwa njia ya simu yako ya mkononi, tablet au
hata kompyuta ya kawaida, tembelea ukurasa huu maalumu uitwao SMART BOOKS TANZANIA.
Mwandishi na mhamasishaji wako;
Peter A. Tarimo
Asante sana Mentor, umekuwa msaada sana kwangu soon nataraji kujiunga niweze kusoma vitabu vyako..
ReplyDeleteWaandishi wengi huishia ku inspire watu tuu lakini hawatoi practical oriented financial educational kama Robert Kiyosaki.
Nashukuru na karibu sana ndugu Mulaki, unachosema ni kweli watu wanahitaji kuwa inspired lakini pia wajengewe uwezo wa kuyatia katika matendo yale wanayojifunza
Delete