1.
Jiandae kuanguka.
Unapojiandaa kwa maanguko haina maana kuwa unafahamu
kwamba utaanguka hapana. Kuna usemi maarufu usemao, “Wakati wa amani, ndiyo muda mzuri wa kufanya mazoezi kujiandaa na vita”
Usisubiri mpaka biashara ife ndipo uanze kujiuliza imekufa kufaje kwani
mafanikio au kuanguka kwa biashara yako kunakutegemea wewe na kupo chini ya
uthibiti wako, wewe ndiye utakayeamua kufeli au kufanikiwa kwake. Jiandae kwa
vyote, mafanikio, lakini pia usiache kujiandaa na maanguko.
Jiandae kuanguka lakini huku ukifanya kila jitihada
zilizopo ndani ya uwezo wako kuhakikisha unazuia usianguke na kamwe
hautaanguka. Sababu moja kubwa inayowafanya wajasiriamali kushindwa ni kwa
sababu wanaogopa kushindwa(woga), na kwa hiyo woga huo wa kushindwa
huwasababisha washindwe kuwa wabunifu katika biashara zao. Wengine hudhani
kwamba kuhofia sana kushindwa kunasaidia kumfanya mtu ajitume zaidi na zaidi
lakini hilo siyo kweli hasa kwa upande wa ujasiriamali. Inaweza ikawa kweli katika upande wa ajira.
SOMA: Kutafuta soko la bidhaa zako kunahitaji ubunifu.
Unapohofia sana maanguko, kunakufanya uwe makini kupita kiasi jambo litakalokufanya pia uogope kujaribu mambo mengi na hivyo kupoteza fursa nyingi za kukufanya ufanikiwe. Wajasiriamali wa kweli “huogelea katika bahari hiyo hiyo iliyojaa maanguko pasipo kuhofia kitu chochote”. Kujiandaa kisaikolojia kutakufanya hata ukianguka uweze kuinuka tena upya haraka bila kuchelewa.
2.
Kuwa makini sana na maamuzi unayoyafanya.
Wewe ni mjasiriamali na hivyo ndiye rubani wa biashara
yako. Kwa hiyo mafanikio ya kesho ya biashara yako yatategemea kwa kiasi kukubwa maamuzi
unayoyafanya leo. Hivyo usije ukafanya maamuzi ya kukurupuka; ikiwa una mashaka
na uamuzi unaokaribia kuufanya,, basi tafuta wataalamu wa ushauri ili uweze
kujadiliana nao juu ya hayo maamuzi.
Ni bora kuahirisha mpaka umepata suluhisho kuliko
biashara yako kuja kufa kirahisi. Kabla hujafanya maamuzi muhimu, tafuta kwanza
taarifa nyingi kwa kadiri itakavyowezekana, zitathmini vyema na kupima uzuri na
ubaya wake, jadiliana na washirika wako wa karibu na mwisho fanya maamuzi moyo
wako utakayokuambia ufanye.
3. Chunga
sana mtiririko wako wa fedha.
Kwenye
kitabu, “Mifereji 7ya pesa na siri matajiri wasiyopenda kuitoa”,
Toleo jipya la 2016, kuna Sura iliyoongezwa pale inayosema “HESABU MUHIMU KULIKO NYINGINE ZOTE KATIKA BIASHARA” Sura
hiyo imezungumzia kwa kina sana juu ya uhai wa biashara yeyote ile ambao ni
PESA TASLIMU(CASH).
Kuna vitu vingi sana kuhusiana na mzunguko wa pesa ambavyo
wajasiriamali tunavichukulia rahisirahisi kumbe vinatugharimu vibaya sana na mara
nyingi inakuwa ndiyo chanzo cha kuanguka kwetu kibiashara.
“Mzunguko
wa pesa ni sawa na damu katika mwili wa binadamu”, “pesa ni mfalme” (cash is
aking) nk. Hayo ni baadhi tu ya maneno ambayo bila shaka yeyote
ile hakuna mtu ambaye hajawahi kukutana nayo mahali katika ulimwengu wa
biashara. Hii yote ni kuonyesha ni jinsi gani pesa na hasa ‘pesa taslimu’ ilivyokuwa muhimu katika
uhai wa biashara.
Hakikisha muda wote biashara yako inaingiza pesa nyingi
kuliko vile inavyotoa. Ni lazima utumie mbinu na mikakati itakayowashawishi
wateja wako kukulipa mapema na wakati huo huo kwa upande wako kuchelewesha
malipo kwa wale wanaokudai.
5. Usiogope Mabadiliko.
Ifanye biashara yako kuendana na mabadiliko. Katika dunia
ya sasa inayobadilika kwa kasi kubwa, mjasiriamali unatakiwa uwe mbunifu kwa
kubadilisha mambo mabaya yanayoambatana na mabadiliko hayo kuwa fursa badala ya
kuyatazama kwa jicho la maafa. Kumbuka mabadiliko ni rafiki na siyo adui.
6.
Ongeza bajeti yako ya masoko na mauzo.
Lengo la kutafuta soko ni ili kuwafahamu vizuri wateja
wako kusudi uweze kuwahudumia vizuri zaidi, bidhaa au huduma unazozalisha na
mwishowe kufanya mauzo makubwa. Lakini kosa moja kubwa wenye biashara wengi
wanalofanya ni kupunguza bajeti ya masoko na mauzo kipindi mambo yanapokuwa
magumu au biashara kudorora. Badala ya kufanya hivyo zidisha bajeti yako ya
masoko kuhakikisha wateja na washindani wako wote wanaendelea kujua uwepo wako.
7. Jenga
mahusiano mazuri na wafanyakazi wako.
Waheshimu na kuwahudumia vizuri watu unaofanya nao kazi,
na wao pia utaona wakikurudishia heshima na huduma kama ulizowatendea.
Wafanyakazi ni sehemu ya biashara yako hivyo watendee kwa kadiri unavyopenda na
wao waitendee biashara yako. Wape zawadi bila ya wao kutegemea katika sikukuu
zao za kuzaliwa au hata pale wanapofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu
yao ya kila siku kazini.
8. Kuwa
makini unapoajiri mfanyakazi/wafanyakazi.
Upo usemi usemao “Ajiri taratibu lakini fukuza haraka”,
maana yake ni kuwa, kamwe usije ukachukulia rahisirshisi wakati wa kuajiri
mfanyakazi, weka umakini wa kutosha kuhakikisha unaajiri mtu sahihi. Ni bora
ukatumia hata gharama kubwa kumpata mfanyakazi aliyekuwa bora kuepusha kuja
kuiumiza biashara yako kwa muda wa kipindi kirefu kijacho.
Vivyo hivyo ikiwa mfanyakazi utaona “anazingua” usifanye
naye mzaha hata kidogo, haraka muondoe kabla mambo hayajaharibika. Usipofanya
hivyo anaweza hata akawaambukiza ubaya wafanyakazi wengine ikiwa wapo wengi na
wao wakaanza kuharibu kazi.
9.Tunza
wateja uliokuwa nao.
Kwenye biashara yupo
bosi mmoja tu, na anao uwezo wa kumtimua kazi mtu yeyote katika kampuni/biashara
kuanzia mmiliki mwenyewe kwa kuamua kutumia pesa zake mahali pengine. Mteja
ndiyo rasilimali kubwa katika biashara yako kushinda rasilimali zingine zote
kwani bila yeye na biashara nayo haipo. Wataalamu wa biashara wanatanabahisha
kwamba “NI VIGUMU MNO KUMPATA MTEJA MPYA
KULIKO KUMTUNZA MTEJA ULIYEKUWA NAYE TAYARI”
Wateja wako uliokuwa nao ndiyo kitu muhimu zaidi katika ukuaji wa biashara yako ndogo, hivyo watunze kwa kuwatendea mema na wao watakwenda kukutangaza vizuri na biashara yako kwa watu wengine huko mitaani.
Swali ninalokuachia ni hili hapa;
……………………………………………………………...
Nakutakia biashara njema, na endapo utataka kujipatia
vitabu mbalimbali vinavyotolewa na Self Help Books tembelea Blogu/ukurasa huu, SMART BOOKS TANZANIA
Mhamasishji na Mwandishi wako;
Peter A. Tarimo.
0 Response to "KUFA AU KUANGUKA KWA BIASHARA YAKO NDOGO FANYA VITU HIVI 9 KUJIEPUSHA?"
Post a Comment