Kinachoipa nguvu kanuni hii ni sheria ya asili ambayo
hamna mtu yeyote bado anayeweza kuielezea. Imewakanganya wanasayansi wa zama
zote, wanasaikolojia wameipa sheria hii jina, “kujishauri binafsi”, na iache
iwe hivyo. Jina ambalo mtu ataiita sheria hii halina umuhimu mkubwa. Jambo
muhimu kuihusu ni kuwa, inafanya kazi kwa utukufu na
mafanikio ya mwanadamu ikiwa itatumiwa katika hali ya
kujenga.
Kama itatumiwa katika hali ya kubomoa, kwa upande mwingine itafanya
uharibifu kwa kiwango kilekile. Katika kauli hii unaweza ukapatikana ukweli
wenye maana: wale ambao huanguka chini kwa kushindwa na kumalizia uhai wao
katika umasikini, taabu na masikitiko, huwa hivyo kutokana na matumizi hasi ya
kanuni ya kujishauri binafsi.
Sababu inaweza kuwa hivyo kutokana na ukweli kwamba,
MISUKUMO YOTE YA FIKRA INA TABIA YA KUJIVIKA YENYEWE KATIKA HALI YAKE YA KITU
HALISI KINACHOWEZA KUONEKANA.
Akili ya ndani(Maabara ya kikemikali ambamo misukumo yote
ya fikra hukusanywa na kufanywa tayari kubadilishwa kuwa ukweli halisi unaoweza
kuonekana) haiwezi kutofautisha kati ya misukumo ya fikra inayojenga na ile
inayobomoa. Hufanya kazi na chochote kile tunachoilisha kupitia misukumo yetu ya fikra. Akili ya
ndani itatafsiri kuwa ukweli wazo linaloongozwa na hofu sawa sawa kama vile
itakavyotafsiri kuwa kweli wazo linalochochewa na ujasiri au imani.
Kurasa za historia ya utabibu zimejaa maelezo ya kesi za
“vifo vya kujishauri”. Mtu anaweza akajiua kutokana na fikra hasi, sawa kama
vile ambavyo angelijiua kutokana na sababu nyinginezo. Katika mji wa Midwestern
City, afisa mmoja wa benki aliyeitwa Joseph Grant aliazima kiasi kikubwa cha
fedha za benki bila ya idhini ya wakurugenzi.
Alipoteza fedha zile kwenye
kamari. Siku moja mchana mkaguzi wa
benki alikuja na kuanza kukagua hesabu. Grant aliondoka benki na kwenda
kuchukua chumba katika hoteli moja
mtaani. Walipokuja kumkuta siku tatu baadae, alikuwa amelala kitandani akilia
kwa huzuni na kuomboleza, akirudia tena na tena maneno haya; “Mungu wangu, hili
litaniua! Sitaweza kuhimili aibu hii”. Baada ya muda mfupi aliaga dunia.
Madaktari walitoa taarifa kwamba kifo kile kilitokana na “Kujiua mwenyewe
kiakili”.
Kama vile umeme utakavyozungusha matairi ya kiwanda na
kuzalisha huduma zenye maana ikiwa utatumiwa vizuri, au kukatisha uhai ikiwa
utatumiwa vibaya, na hivyo hivyo ndivyo sheria ya kujishauribinafsi
itakavyokuongoza kwenye amani na utajiri
au chini katika shimo la mateso, maanguko na kifo. Yote itategemea kiwango
chako cha uelewa na matumizi yake.
Ikiwa utaijaza akili yako hofu, mashaka na kutokuamini katika uwezo wako wa kujiunganisha na
kutumia nguvu kuu zilizo chanzo cha viumbe vyote, sheria ya kujishauri
binafsi itaichukua roho hii ya kutokuamini na kuitumia kama kielelezo ambacho
akili yako ya ndani itatafsiri kuwa katika kitu
chenye umbo lake halisi.
KAULI
HII INA UKWELI SAWA KAMA ILIVYOKUWA KAULI KUWA MBILI NA MBILI NI SAWA NA NNE!
Kama ilivyokuwa upepo ubebao meli moja Mashariki na
nyingine Magharibi, sheria ya kujishauribinafsi itakunyanyua juu au
kukushusha chini, kulingana na vile
jinsi utakavyoyaendesha mawazo(fikra) zako. Sheria ya kujishauri binafsi ambayo
mtu yeyote anaweza akaitumia kufikia urefu wa mafanikio yanayoshangaza akili
yanaelezewa vizuri katika shairi lifuatalo;
Ikiwa utafikiria umeshindwa, umeshindwa,
Ikiwa utafikiri haustahili, hustahili
kweli
Kama unapenda kushinda, lakini unawaza
hautaweza,
Bila shaka hautaweza.
Ikiwa unafikiri utapoteza, umepoteza
Kutoka duniani tunakuta,
Mafanikio huanza na utashi wa mtu-
Vyote vikiwa katika hali ya akili.
Ikiwa unawaza wewe ni bora, upo hivyo,
Unatakiwa uwaze juu ili kuinuka,
Unatakiwa kuwa na uhakika na wewe mwenyewe kabla
Unaweza kushinda zawadi wakati wowote
Vita ya maisha mara nyingi haiendi
Kwa mwenye nguvu zaidi au mbio,
Lakini mapema au baadae anayeshinda
Ni yule ANAYEWAZA(KUFIKIRI)
ANAWEZA!
Chunguza maneno yaliyotiliwa mkazo, na
utapata maana ya ndani shairi iliyokusudia. Mahali fulani mwilini mwako(pengine
katika seli za ubongo wako) imelala mbegu ya ushindi. Ikiwa itaamshwa na kutiwa
katika vitendo, hii inaweza ikakufikisha kileleni kiasi ambacho hukuwahi
kutumaini kufika.
Kama ilivyo kwa mwanamuziki mahiri anavyoweza
akasababisha mapigo mazuri zaidi ya muziki kumiminika kutoka katika nyuzi za
gitaa, ndivyo na wewe unavyoweza ukaamsha kipaji kilicholala kwenye ubongo
wako, na kukisababisha kukunyanyua juu kuelekea lengo lolote unalotamani
kukamilisha.
Abraham Lincoln alikuwa akishindwa katika
kila jambo alilojaribu kufanya mpaka pale alipopitisha umri wa miaka 40.
Alikuwa “Bwana Asiyejulikana kutoka Kusikojulikana” mpaka pale uzoefu mkubwa
ulipokuja katika maisha yake, ukaamsha kipaji kilichokuwa kimelala ndani ya
moyo na ubongo wake, na kuipatia dunia
mmoja kati ya watu wake mashuhuri.
“Uzoefu” huo ulikuwa umechanganyika na
mihemko ya huzuni na upendo. Ilikuja kwake kupitia Anne
Rutledge, mwanamke pekee aliyempenda kweli daima.
Ni ukweli unaofahamika kuwa mhemko wa mapenzi
una uhusiano wa karibu na hali ya akili ijulikanayo kama Imani. Mapenzi huja karibu sana kwenye kutafsiri
msukumo wa fikra wa mtu kwenda katika upande wake wa pili wa kiroho.
Wakati akifanya utafiti wake, mwandishi aligundua
kutokana na tathmini ya kazi na mafanikio ya mamia ya watu wenye utajiri
unaoonekana, kwamba kulikuwa na ushawishi wa mapenzi ya mwanamke nyuma ya
karibu kila mmoja wao.
Mhemko wa mapenzi katika moyo na ubongo wa
binadamu, hutengeneza mazingira yanayofaa ya uvutano wa kisumaku. Hii
husababisha kumiminika ndani kwa mitetemo ya juu na laini ambayo huelea katika
anga(ether)
Hebu tuangalie nguvu ya Imani kama
ilivyothihirishwa na mtu anayefahamika vizuri kwa kila Ustaarabu, Mahatma
Gandhi wa India. Kwa mtu huyu dunia ilishuhudia moja kati ya mifano ya
kushangaza zaidi ya uwezekano(fursa) za IMANI.
Gandhi alitawala uwezo mkubwa wa nguvu
isiyothihirika kushinda mtu mwingine yeyote aliyeishi katika wakati wake, na hii
licha ya ukweli kwamba hakuwa na zana halisi za kutawala kama vile, pesa, meli
za kivita, askari na zana za kivita. Gandhi hakuwa na pesa. Hakuwa na nyumba.
Hakumiliki hata suti moja ya nguo lakini alikuwa na nguvu.
Ni kwa jinsi gani alizipata nguvu hizo?
ALIZITENGENEZA KUTOKANA NA UELEWA WAKE WA
KANUNI YA IMANI NA KWA KUPITIA UWEZO WAKE WA KUPANDIKIZA IMANI HIYO KATIKA
AKILI ZA WATU MILIONI 200.
Gandhi alitimiza kwa kupitia ushawishi wa Imani,
kitu ambacho tawala zenye nguvu za kijeshi duniani zisingeliweza kutimiza, na
kamwe hazitoweza kutimiza kwa kutumia wanajeshi na vifaa vya kivita. Alitimiza
tendo gumu na la ajabu la kushawishi akili milioni 200 kuungana na kusonga mbele katika umoja,
kama akili moja. Ni nguvu gani juu ya dunia isipokuwa Imani, ingeliweza
kutenda kiasi hicho?.
Kaulimbiu ya wakati ujao itakuwa ni furaha ya binadamu na kuridhika. Hali
hii ya akili inapokuwa imefikiwa, uzalishaji utajiendesha wenyewe kwa ufanisi
zaidi kuliko kitu chochote kilichowahi kukamilishwa wakati watu walipokuwa hawachanganyi
au wanashindwa kuchanganya imani na matamanio binafsi pamoja na
kazi.
Kutokana na uhitaji wa imani na ushirikiano katika
biashara na viwanda, litakuwa ni jambo la kuvutia na lenye faida kulitathmini
tukio maalumu. Hili hutoa uelewa mzuri kabisa wa njia ambayo wenye viwanda na
viongozi wa makampuni hujichumia utajiri kwa kutoa kabla hawajapata. Tukio
lililochaguliwa kwa ajili ya maelezo haya lilitokea huko nyuma mwaka 1900,
wakati Shirika la Kimarekani la Chuma cha pua(United States Steel Corporation)
lilipoundwa. Kama utakavyo isoma simulizi hii, zingatia akilini ukweli huu na utafahamu jinsi wazo
lilivyobadilishwa kuwa utajiri mkubwa.
Kwanza shirika kubwa la Kimarekani la chuma
cha pua lilizaliwa katika akili ya Charles M. Schwab katika hali ya wazo
aliloliunda kupitia ubunifu wake. Pili, alichanganya imani na wazo lake. Tatu,
alitengeneza mpango kwa ajili ya kulibadilisha wazo lake kuwa katika kitu
halisi na ukweli kifedha.
Nne, aliuweka mpango wake katika vitendo kwa
hotuba yake maarufu katika Klabu ya Chuo Kikuu. Tano, alitekeleza na kuufuata
mpango wake kwa uvumilivu pasipo kuacha huku akiusaidia na maamuzi thabiti
mpaka pale ulipoanza kufanya kazi. Sita, aliandaa njia ya mafanikio kwa shauku
kali ya kufanikiwa
Ikiwa mara nyingi umekuwa ukishangaa ni jinsi
gani utajiri mkubwa unavyopatikana, simulizi hii ya kuundwa kwa Shirika la
Chuma Cha Pua la Marekani itakupa mwangaza. Kama unayo shaka yeyote kwamba watu
wanaweza Wakafikiri na Kuwa Matajiri, simulizi hii inapaswa kukuondoa
shaka hiyo kwa sababu ndani yake unaweza
ukaona wazi matumizi ya sehemu kubwa ya Kanuni 13 zilizoelezewa katika kitabu hiki.
John Lowel katika gazeti la New York
World-Telegram, kwa heshima yake hapa, imerudiwa kuchapishwa simulizi nzuri
ya kushangaza ya nguvu ya wazo.
………………………………………………………………………..
Mpenzi msomaji, usikose sehemu ya (iv) ya sura hii ya 3 ya “Kitabu cha pesa na mafanikio maarufu zaidi duniani
FIKIRI UTAJIRIKE AU THINK & GROW RICH (MSAHAFU WA MAFANIKIO)”.
Pia kwa vitabu vyako mbalimbali vya Biashara
na Ujasiriamali katika lugha ya kiswahili, bonyeza SMART BOOKS TANZANIA.
0 Response to "LILE UNALOFIKIRI(WAZA) AKILINI, ZURI AU BAYA NDILO HUTOKEA KUWA KWELI."
Post a Comment