Mabenki na taasisi mbalimbali za fedha
zinazotoa mikopo Tanzania, zimekuwa zikitolewa lawama na malalamiko lukuki
kutoka kwa wateja wao pasipo wateja hao kufahamu vyema jinsi sheria na kanuni
mbalimbali za nchi zilizoziweka benki na taasisi hizo zinavyofanya kazi. Ingawa
kweli yapo baadhi ya malalamiko na lawama zinazotolewa kwa haki kabisa na
wakopaji kama vile mambo ya rushwa, huduma mbaya nk. Na wala hapa sina nia ya
kutetea upande wowote bali kuelezea hali halisi jinsi ilivyo.
Malalamiko ya walio wengi hujikita zaidi
kwenye masharti wanayokumbana nayo pindi wanapoamua kwenda kuomba mikopo, iwe
ni mikopo ya biashara zao, kuendeleza ujenzi wa nyumba/makazi, kulipia
masomo/chuo au shule, kununulia vifaa kama magari, mitambo nk.
SOMA: Kuendesha biashara na mtaji kidogo ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.
SOMA: Kuendesha biashara na mtaji kidogo ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.
Mabenki na taasisi nyingine zote za fedha
zipo kwenye biashara kama yalivyokuwa makampuni mengine yeyote yale ya
kibiashara au watu binafsi, wanafanya biashara ya kukopesha fedha na malengo
yao ya msingi kabisa ni kutengeneza faida kwa kutoza gharama(riba) kwenye zile
huduma wanazozitoa kwa wateja wao. Hakuna kampuni au mfanyabiashara anayekubali
kupata hasara wala kuingia kwenye makubaliano ya biashara yenye mashaka
yasiyokuwa na uhakika wa kurudisha mtaji uliowekezwa na faida.
Baadhi tu ya malaamiko na lawama hizo
wanazotupiwa taasisi za mikopo zikiwemo benki, ni kama hizi zifuatazo;
· Benki
siyo rafiki wa watu wadogo(masikini)
· Benki
na taasisi za fedha zina masharti magumu
· Benki
zina riba kubwa
· Maafisa
mikopo wengi huwabana sana wateja kwa masharti magumu siyo kwa maslahi ya benki
au taasisi, bali kwa maslahi yao binafsi hasa ya kutengeneza mazingira ya
kupatiwa rushwa.
· Baadhi
ya taasisi na mabenki hupendelea mteja aje akwame marejesho mwishoni karibu na
kumaliza mkopo kusudi wao waje wauze dhamana zake, na hasa kama ikiwa dhamana
zenyewe ni nyumba, kiwanja au gari. Wanunuzi huwa wao wao wenyewe maafisa au
huwatuma watu wao kinyemela kwa kupanga nao dili.
· Taasisi
na mabenki mengi wana tabia ya kutokuweka bayana gharama mbalimbali na faini za
mikopo kabla, na mteja huja kubaini wakati tayari amekwisha tia saini fomu za
mkopo.
· Taasisi
na mabenki mengine huwahadaa wateja (Mithili ya mchinjaji anavyomrushia kuku
mahindi au mtama kusudi tu apate kuingia ndani na kumbe lengo lake siyo
kumlisha bali amkamate na kumchinja kama kitoweo) kwa ahadi tamutamu
kupitia matangazo ya biashara na ukishachukua mkopo tu ndipo utakapojua ubaya
au uzuri wao.
Kwanini
basi wateja hutoa malalamiko hayo yote kwa mabenki na taasisi za mikopo?
Ni hulka ya binadamu tuseme karibu wote,
kwamba hatupendi kulipa deni. Mtu angependelea baada ya kukopa basi arejeshe
baada ya muda atakaotaka yeye mwenyewe, na hata kama ikiwezekana basi asilipe
deni hilo kabisa. Kulipa deni mara nyingi huleta maumivu fulani kwa yule anayelipa
deni, ingawa ni wajibu wake na haki kufanya hivyo.
SOMA NA HII: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha na benki?
SOMA NA HII: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha na benki?
Kutokana na sababu hiyo, Serikali na mamlaka
za nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, zimeweka sheria na taratibu kuwa
mabenki na taasisi za fedha kote nchini kufuata taratibu maalumu ili
kuhakikisha kwamba mitaji yao ambazo ni fedha na amana za watu walizohifadhi
katika mabenki na taasisi hizo hazipotei kirahisi na zinazunguka kwa ajili ya
watu wengine nao waje wakope hapo baadaye ikiwa ni pamoja na taasisi na mabenki
hayo kujiendesha, kulipa wafanyakazi wake pamoja na kulipa kodi na gharama
mbalimabali za uendeshaji biashara.
Hitaji
muhimu zaidi (mashart) Maafisa Mikopo wa Benki, Saccos na taasisi nyingine za
mikopo wanayotaka mkopaji atimize kwanza kabla hajapewa mkopo wa biashara.
Dhana iliyojengeka miongoni mwa wakopaji
wengi ni kwamba hitaji kubwa na la msingi kushinda yote benki au taasisi
wanalohitaji toka kwako ni DHAMANA YA
MKOPO, lakini ukweli wenyewe ni kuwa wala Dhamana ya mkopo siyo kitu cha
kwanza wanachokiangalia, kuna vigezo vingine muhimu zaidi wanavyotaka wavijue
ndipo waweze kutambua ikiwa unazo sifa zinazostahili kupewa mkopo. Vigezo hivyo
ni hivi hapa chini;
1. Kipato
chako.
Wanahitaji kujua unapata shilingi ngapi kwa
siku, wiki, mwezi au mwaka na chanzo/vyanzo vya kipato hicho ni kitu gani. Je
ni biashara au ajira?. Mathalani ni biashara, watataka kujua ikiwa biashara
hiyo ni yakwako, halali, imesajiliwa kisheria na ni endelevu. Ndiyo maana
watakutaka uwaonyeshe hati mbalimbali mbali zinazoweza kuthibitisha mambo hayo kama
vile leseni ya biashara, namba ya mlipa kodi TIN nk.
2. Mwenendo
na historia yako ya ulipaji madeni siku za nyuma.
Wanataka wafahamu ikiwa una rekodi nzuri ya
ulipaji madeni, siyo kwa taasisi husika tu bali na kwa taasisi nyinginezo au
mabenki uliyowahi kukopa. Kwa mfano serikali ya Tanzania chini ya Benki kuu BOT
imeanzisha wakala(taasisi maalumu)
ambayo kazi yake ni kufuatilia na kutunza kumbukumbu zote za wakopaji kutoka
taasisi na mabenki yote nchini zikiwemo hata mamlaka za umeme na maji kama
Tanesco na Dawasco. Benki au taasisi zinapotaka kutoa mkopo kwa mteja
huwasiliana na mamlaka hiyo kupata taarifa za mteja husika ikiwa alishawahi
kusumbua sehemu nyingine au la. Taarifa zako zikisoma una alama nzuri basi
inakuwa rahisi kukukopesha.
Ufanyeje
ili kutokuwekewa alama mbaya kwenye taasisi hiyo inayotunza historia ya
wakopaji mikopo na madeni?
Lipa madeni yako yote kwa wakati, Usikope
kutoka taasisi au mabenki mengi tofauti kwa wakati mmoja hasa ikiwa wewe bado
ni mkopaji mdogo. Kufanya hivyo mara nyingi kutawafanya maafisa wa benki
kukutilia mashaka na hata wengine tu kutokana na udhaifu wa kibinadamu wanakuwa
na wivu, ni kwa nini ukakope kwa washindani wao, hivyo hutafuta njia ya
kukukomesha na ikitokea tu umefanya kosa hata kama ni dogo la bahati mbaya basi
watakuripoti kwenye taasisi hiyo kusudi wakukomoe.
Upo ushahidi wa watu waliofanyiwa hivyo
hapahapa Tanzania na kwa kuwa wakopaji wengi uelewa wao juu ya taasisi hiyo
bado hawajawa nao basi wengi wataumizwa bila kujua.
SOMA: Unaogelea ndani ya maji baridi huku ungali unakufa kwa kiu.
SOMA: Unaogelea ndani ya maji baridi huku ungali unakufa kwa kiu.
Kwa nchi za wenzetu zilizoendelea jambo hili
lipo wazi sana na huwezi ukasingiziwa alama mbaya uwongo kwani unapewa fursa ya
kujua maafisa wa benki wanachokuripoti na kama watakuhujumu kwa kukutolea
taarifa za uwongo ili kukukomoa, unakuwa na uwezo wa kukata rufaa kwenye hiyo
taasisi. Kosa kwa mfano la kuchelewesha marejesho siku moja au mbili sidhani
kama linaweza kukufanya uwekewe alama mbaya za kukufanya usindwe kwenda kukopa
mahali pengine.
3. Tabia
yako ya uwekaji akiba.
Watapenda kufahamu kama unatabia ya kuweka
akiba, na ndiyo maana mabenki au taasisi nyingi humtaka mkopaji kabla ya kupewa
mkopo kwanza awe ameshafungua akaunti katika benki au taasisi husika angalao
miezi sita au mwaka kabla, ili kuona mwenendo wake wa kujiwekea akiba ikiwa ni
pamoja na kufahamu mzunguko wake wa pesa katika biashara au mshahara upoje.
Ikiwa mzunguko huo wa fedha ni mzuri (chanya) basi uwezekano wa kupata mkopo unakuwa mkuwa
zaidi.
4. Deni
ulilokuwa nalo.
Kama ilivyo kwa historia ya ulipaji madeni ya
nyuma, pia wanaangalia ni deni kiasi gani ulilokuwa nalo kwa wakati huo. Inawezekana
umechukua mkopo mahali pengine na bado haujamalizia. Inakubidi taarifa hizo
uwape mapema na hata ikiwezekana uonyeshe ni kwa jinsi gani mkopo unauomba
dhamana zake hazitaingiliana na mikopo mingine uliyokuwa nayo kusudi
kuwashawishi kuwa utakapokuja kushindwa kulipa mkopo hawatapata shida ya kuuza
dhamana ulizoziweka.
Kinyume na hapo ukiwaficha kuwa huna deni
mahali pengine wakaja kugundua kwa njia zao wenyewe ikiwemo ile taasisi ya
kuweka kumbukumbu za wadaiwa basi utachukuliwa kama mtu usiyekuwa na sifa za
kupewa mkopo.
5. Dhamana
ya mkopo.
Na mwisho kabisa ndiyo wanaangalia ikiwa
unayo dhamana itakayotumika kulinda mkopo ikiwa utafika mahali mkopo
ukakushinda kulipa. Mara nyingi dhamana huwa ni mali ulizokuwa nazo hasa zisizohamishika
kama vile nyumba, kiwanja au shamba, lakini pia dhamana yaweza kuwa ni vyombo
vyako vya ndani, gari, mashine, fedha ulizoweka katika akaunti ya kudumu ya
benki, pia unaweza ukadhaminiwa na mtu mwingine aliye na mali au anayefanya
kazi sehemu inayotambulika.
HITIMISHO.
Kabla ya kutoa malalamiko kwa taasisi za
mikopo na mabenki, wakopaji inatupasa kwanza kufahamu kuwa, mkopo/mikopo siyo
ruzuku wala zawadi, bali sheria za nchi zinatutaka turejeshe mikopo tunayokopa
iwe ni ya benki, saccos, ama taasisi nyingine yeyote ile ya pesa.
Ndiyo maana unaposhindwa kulipa mkopo
uliokopa maafisa wa benki au taasisi husika huwa na mamlaka kisheria ya kuja
kukufilisi kwa kuuza mali zako ulizoziweka kama dhamana iwe ni nyumba, gari,
kiwanja , shamba, vyombo vya ndani au mali nyingine yeyote ile unayomiliki na
kisha mkopaji kuanza kulalamika na kuyaona mabenki au taasisi za mikopo ni
wabaya wasiokuwa na huruma.
SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara unayoipenda.
SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara unayoipenda.
Kwa upande wa mabenki nayo na taasisi za
kifedha, wajitahidi kuwaelimisha wateja wao maswala mbalimbali, wasifikirie
kuwa wateja wa kawaida wanaelewa kila kitu, wengine hawana uelewa kiasi hicho.
Wasisubirie tu kuja kuwakomoa siku za kuomba mikopo. Vile vile maafisa mikopo
wengine kusema ukweli ni kero kubwa hasa linapokuja suala la “kitu kidogo” ni bora kabisa mabenki na
taasisi zote wakasisitiza kwa dhati kubainisha gharama zote zinazotakiwa kwa jumla ndipo
mtu apewe mkopo na kuwe na uwezekano wa mteja kuonana na meneja iwapo ataona
afisa mkopo anamuwekea vizingiti visivyokuwa na umuhimu.
Inafika mahali mtu ukichukua mkopo wa mwanzo
usipompa afisa chochote baada ya kuondoka pale dirisha la benki, basi ujue
kabisa na huo ndio utakaokuwa mkopo wako wa mwisho katika benki au taasisi hiyo.
Atakujengea vigingi vya ajabu na longolongo kibao mpaka uonekane wewe hufai
kabisa kukopeshwa tena.
…………………………………………………………………..
Msaada zaidi kwa Mkopaji.
Ili uweze kupata mkopo kwa urahisi zaidi
kutoka taasisi za fedha na benki kuna vitu unavyopaswa kuzingatia navyo ni kama
hivi hapa chini;
Kabla haujakwenda kukutana na afisa mkopo wa
benki au taasisi unayotaka kukopa, kwanza kaa chini utafakari na kupanga mambo
mbalimbali ambayo unajua ni lazima watu wa benki au taasisi watakwenda
kukuuliza. Usifike pale ukaanza tena kubabaika. Njia rahisi itakayokuwezesha
kupanga kila jambo kuhusiana na biashara yako na ukapata kila jibu la swali
unaloweza ukaulizwa na afisa wa benki ni kupitia utafiti
au mchanganuo wa biashara ambao siyo lazima umtafute mtaalamu
aliyebobea kukufanyia, labda kama ni biashara kubwa kubwa za mamilioni ya pesa.
Kwa biashara zile ndogo tu za kawaida au za kati wewe binafsi unaweza ukafanya
utafiti na kuchanganua biashara yako kwa mahitaji ya kuiendesha kwa ufanisi
zaidi na hata kujibu baadhi ya maswali utakayoulizwa na wadau kama benki au
wabia.
Kuchanganua biashara pia itakuwezesha kupata
jibu la swali muhimu sana kwako wewe binafsi la ni kiasi gani cha mkopo utakachohitaji
katika kuuongezea nguvu mtaji wako. Jibu hili litakuwezesha kukwepa
kuomba mkopo mkubwa kupita mahitaji yako au mdogo kushinda mahitaji, jambo
linaloweza kukusababishia matatizo hapo baadaye.
Unaweza wewe mwenyewe hata pasipo kuandika
kwenye karatasi kufanya utafiti wa biashara yako na kutengeneza kichwani mpango/mchanganuo
ambao utakupa majibu mengi yatakayosaidia hata katika uendeshaji wa biashara
husika.
Biashara yeyote ile ina vipengele ambavyo ni
lazima vipitiwe wakati wa mwenendo mzima wa kuiendesha, vitu kama vile, una malengo yapi na
biashara hiyo, umiliki wa biashara upoje, mtaji wa biashara ni kiasi gani na
utaupata vipi, ni watu gani watakaohusika katika biashara hiyo, matarajio ya
mauzo yapoje, utauza bidhaa/huduma shilingi ngapi, utazalisha au kununua bidhaa
kiasi gani, wateja wako watarajiwa ni kina nani, utajitangaza vipi kuwafikia
wateja watarajiwa, faida yako baada ya wiki, mwezi na mwaka unakadiria inaweza
kuwa kiasi gani nk.
Ni mambo ya msingi kabisa mfanyabiashara na
mjasiriamali yeyote hujiuliza hata ikiwa hataki kuandika kitu kinachoitwa mpango rasmi wa biashara, na vitu vyote
hivyo hupatikana baada ya mtu kufanya utafiti na utafiti haimaanishi ule wa
kitaalamu la hasha, hata kwa mtu mwenyewe kuzunguka na kuchunguza mtaani,
tayari huo ni utafiti.
Kitabu
cha Michanganuo ya biashara na Ujasiriamali kimeelezea vizuri
sana mada hizi mbili za “Kufanya utafiti wa biashara na masoko”
pamoja na Namna ya kutayarisha mpango au mchanganuo wa biashara” katika
viwango vyote, yaani kwa mtu anayependa kuandika mchanganuo rasmi au hata yule
mtu wa kawaida kabisa anayependa tu kufahamu vitu hivyo kwa ajili ya uendeshaji
mzuri wa biashara yake ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa vipengele mbali
mbali kama hivyo ambavyo watu wa mikopo wanaweza wakakuuliza unapotaka kwenda
kuomba mkopo benki au taasisi yeyote ile.
Kitabu hiki mbali na kuwa na kozi hizo za
Utafiti na namna ya kuandaa Michanganuo ya biashara, Michanganuo yenyewe halisi
unayoweza kuitumia kama kielelezo au mifano unapojifunza, vile vile kina masomo
mengine karibu yote ya ujasiriamali kuanzia, Ujasiriamali wenyewe na jinsi ya
kuanzisha biashara, Uendeshaji wa biashara: namna ya kutafuta masoko, mifumo
mbalimbali ya biashara, utunzaji na uwekaji wa kumbukumbu za biashara yeyote
ile, namna ya kutangaza bidhaa au huduma zako, jinsi ya kusimamia vizuri
biashara yako, mbinu bora za kufanya mauzo na njia mbalimbali halali watu
wanazotumia kutajirika haraka.
Bei ya kitabu hiki kikiwa katika mfumo wa
kielektroniki kwa njia ya E-mail ni shilingi elfu kumi,
10,000/=
Kitabu cha kawaida cha karatasi bei yake ni
Shilingi elfu ishirini, 20,000/=
Wasiliana na sisi kwa namba, 0712
202244
Tunapatikana pia kwenye;
0 Response to "MKOPO WA BENKI AU TAASISI ZA FEDHA: SOMA HAPA NA HUTAKAA UWALAUMU TENA!"
Post a Comment