UTAJIRI HUANZA NA WAZO, UKOMO WA UTAJIRI MTU HUPANGA MWENYEWE AKILINI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UTAJIRI HUANZA NA WAZO, UKOMO WA UTAJIRI MTU HUPANGA MWENYEWE AKILINI


HOTUBA NZURI BAADA YA MLO WA JIONI KWA AJILI YA DOLA BILIONI MOJA

‘Mnamo jioni ya Desemba 12, 1900 baadhi ya vigogo wa fedha wa Taifa wapatao themanini walikusanyika katika ukumbi wa klabu ya Chuo Kikuu Barabara ya Tano kumpa heshima kijana mdogo kutoka Magharibi, ni wageni wachache waliogundua kuwa walikuwa wanakwenda kushuhudia  tukio muhimu zaidi Marekani katika historia ya viwanda.

‘J. Edward Simmons na Charless Stewart Smith, mioyo yao  ikiwa imejawa na shukrani kwa ukarimu kupita kiasi walioonyeshwa na Charles M. Schwab katika ziara yao hivi karibuni walipotembelea Pittsburgh, walikuwa wametayarisha chakula cha jioni kumtambulisha mtu wa chuma cha pua mwenye umri wa miaka 38 kwa Jumuiya ya mabenki ya Mashariki.

‘Lakini hawakutazamia yeye kuingia kwa kukurupuka katika ule mkutano. Walimpa angalizo, kwa kweli kwamba hisia za ndani za watu wenye maringo wa New York zisingeliweza kusikiliza atakachokisema, na hivyo ikiwa asingependa kuwaudhi Stilimans na Harrimans na Vanderbbilts, ni bora angejiwekea ukomo mwenyewe kwenye dakika kumi na tano au ishirini za maongezi mepesimepesi na kuacha mambo yaende kama yalivyo.

‘Hata John Pierpont Morgan aliyekuwa ameketi mkono wa kulia kwa Schwab kama alivyokuwa mgeni wa heshima kwake, alitarajia  kuzungumza kidogo tu kwa madaha kuikoga meza ya hafla ile kuwa alikuwepo. Na kwa kadri vyombo vya habari na umma walivyokuwa wanahusika, tukio zima lilikuwa la muda mchache kiasi kwamba halikutajwa popote katika magazeti siku iliyofuata.

‘Hivyo waandaaji wawili na wageni wao waalikwa walikula kivyao kupitia mizunguko ya kawaida saba au nane. Kulikuwa na mazungumzo machache na hata yale kidogo yaliyokuwepo yalizuiliwa. Ni watu wa benki na mdalali wachache waliokuwa wamewahi kukutana na Schwab ambaye ajira yake ilikuwa imechipua katika mabenki ya Monongahela na hakuna aliyemfahamu vizuri.

‘Lakini kabla jioni haijamalizika, yeye - wao pamoja na Mkuu wa pesa Morgan waligeuka marafiki ghafla, na mtoto wa Dola billioni moja, Shirika la chuma cha pua la Marekani(United States Steel Corporation) alikuwa anakwenda kutungwa.

‘Labda ni kwa bahati mbaya kwa ajili ya historia, kwamba hamna kumbukumbu kamwe ya hotuba ya Charles Schwab kwenye chakula hicho cha jioni iliyowahi kutunzwa. Alirudia baadhi ya sehemu za hotuba hiyo katika siku ya baadaye iliyofanana na ya mkutano wa Chicago wa watu wa benki. Na bado tena baadaye wakati serikali ilipoleta madai ya kuivunja kampuni ya chuma cha pua(steel trust), alitoa tafsiri yake mwenyewe, kutoka upane wa ushahid, wa maoni yaliyomchochea Morgan wazimu wa kuingia katika shughuli ya kiuchumi.

‘Pengine hata kama ile ilikuwa ni hotuba “nyepesi” kwa namna fulani isiyofuata sarufi(kwa mambo madogomadogo ya lugha kamwe hayakumsumbua Schwab), ilijaa semi za kuchekesha na mafumbo, lakini mbali na hayo ilikuwa na nguvu ya kiumeme na athari kwenye bilioni tano za makadirio ya mtaji uliowasilishwa na wanahafla ya chakula cha jioni.

‘Baada ya kumalizika na mkusanyiko ukiwa bado kwenye mapumziko, ingawa Schwab alikuwa amezungumza kwa dakika tisini, Morgan aliongozana naye kwenye dirisha la mapumziko ambapo walininginiza miguu yao hewani kutoka juu kwenye viti visivyoburudisha. Walizungumza kwa saa moja zaidi. Maajabu ya haiba ya schwab yalikuwa yamefunguliwa kwa nguvu zote, lakini kilichokuwa muhimu zaidi na cha kudumu ilikuwa ni programu yenye kueleweka aliyoieleza kwa ajili ya uendelezaji wa chuma cha pua.

‘Watu wengine wengi walikuwa wamejaribu kumshawishi Morgan kuunda kampuni ya chuma cha pua kwa kuunganisha pamoja makampuni ya biskuti, waya na magurudumu, sukari, raba, whiski, mafuta au na mchanganyiko wa bazoka. Mcheza kamari John W. Gates, alimshawishi lakini Morgan hakumuamini. Moore boys, Bill na Jim, madalali wa Chicago ambao walikuwa wameunganisha kampuni ya viberiti(match trust) na kampuni ya uokaji(cracker corporaton) walimshawishi lakini walishindwa.

‘Elbert H. Garry, wakili anayeheshimika nchini, alitaka kumshawishi lakini hakuwa na uwezo wa kutosha kumvutia. Mpaka pale ushawishi wa Schwab ulipomchukua J. P Morgan hadi kwenye kilele ambacho kutoka hapo aliweza kupiga taswira ya matokeo thabiti ya mradi wa kiuchumi wa uhakika zaidi kuwahi kuanzishwa, mradi uliochukuliwa kama ndoto ya kiuendawazimu ya mpumbavu anayetaka pesa za haraka haraka.

‘Mvutano wa pesa uliokuwa umeanza kizazi kimoja nyuma, kuvutia mamilioni ya makampuni madogo na wakati mwingine yaliyoendeshwa  bila ufanisi katika muunganiko wa kampuni kubwa zenye ushindani, ulikuwa ukijiendesha katika sekta ya chuma cha pua kupitia  haramia mchangamfu wa biashara John W. Gates.

‘Gates tayari alikuwa ameanzisha kampuni ya chuma na waya ya Kimarekani(The Americana Steel and wire Company) kutokana na msuruu wa kampuni ndogondogo, na pamoja na Morgan walikuwa wameanzisha Kampuni ya Shirikisho ya chuma cha pua(The Federal Steel Company). The National Tube na American Bridge ni makampuni mengine mawili zaidi Morgan aliyojihusisha nayo, na Moore Brothers walikuwa wametelekeza biashara za viberiti na pipi kuunda “American  Group-Tin Plate, Steel Hoop, Sheet  Steel na The National Steel Company.

‘Lakini kwa upande wa Kampuni kubwa la Andrew Carnegie, kampuni iliyomilikiwa na kuendeshwa na wabia hamsini na tatu, hiyo miunganiko mingine ilikuwa midogomidogo. Wangeweza kuungana kwa thati ya mioyo yao lakini wengi wao hawakuweza kupenya kushindana na kampuni ya Carnegie, na Morgan hili alilifahamu.

‘Mzee wa Kiskoti, Andrew Carnegie, mtu asiyetabirika alilifahamu hili pia. Kutoka kilele kitukufu cha “Skibo Castle”(makazi yake ya kifahari) alikuwa ameona kwanza kwa mshangao na halafu kwa uchungu majaribio ya kampuni ndogondogo za Morgan kuingilia biashara zake. Majaribio yalipozidi kuongezeka, tabia ya Carnegie iligeuka kuwa hasira na ulipizaji kisasi. Aliamua kuiga kila kiwanda kilichomilikiwa na washindani wake.

‘Mpaka sasa hakuwa amevutiwa na waya, mabomba, magurudumu wala mabati. Badala yake aliridhika kuwauzia kampuni hizo chuma cha pua ghafi na kuwaacha watengeneze maumbo yeyote wayatakayo.Sasa alikuwa na Schwab kama msaidizi wake mkuu na luteni mwenye uwezo, alipanga kuwafilisi maadui zake.

‘Hivyo ilikuwa ni hiyo hotuba ya Charles Schwab, Morgan alipoona jibu la tatizo lake la muunganiko. Kampuni  bila ya Carnegie-mkubwa wa wote - isingeliweza kuwa kampuni hata kidogo, kama mwandishi mmoja alivyosema, “ ni sawa na mkate wa zabibu usiokuwa na zabibu”.

‘Hotuba ya Schwab usiku wa tarehe 12 Desemba, 1900, bila shaka ilibeba hitimisho, ingawa haikuwa ahadi, kwamba kampuni kubwa ya Carnegie ingeliweza kuletwa chini ya hema ya Morgan. Alizungumza juu ya hali ya baadaye ya dunia kwa chuma cha pua, juu ya kujipanga kwa ufanisi, juu ya ubobezi katika nyanja mbalimbali, juu ya kuzifunga kampuni na viwanda vinavyofanya vibaya na kuelekezea nguvu zaidi katika rasilimali zenye tija, juu ya uchumi katika usafirishaji wa mawe yenye madini, juu ya uchumi katika idara za nguvukazi na utawala, juu ya masoko ya kigeni.

‘Zaidi ya hapo aliwaeleza maharamia wa biashara miongoni mwao, kasoro za tabia yao ya uharamia. Aliwaeleza kwamba, malengo yao, yalikuwa ni kujenga ukiritimba, kupandisha bei na kujilipa wenyewe faida nono nje ya stahili zao. Aliulaumu kwa nguvu zake zote mfumo huo.

‘Aliwaambia wasikilizaji wake, kutokuona mbali kwa sera kama hiyo kunasimama kwenye ukweli kwamba kulikuwa kunazuia soko katika zama ambazo kila kitu kilikuwa kikililia kutanuka. Kwa kurahisisha bei ya chuma cha pua, alisema, soko linalotanuka daima lingeweza kutengenezwa; matumizi zaidi ya chuma cha pua yangeliweza kubuniwa na sehemu kubwa ya biashara ya dunia ingeliweza kushikwa. Ukweli ingawa hakufahamu, Schwab alikuwa nabii wa uzalishaji wa kisasa wa bidhaa kwa wingi(mass production)

‘Kwa hiyo hafla ya chakula cha jioni katika klabu ya Chuo Kikuu ilifikia tamati. Morgan alikwenda nyumbani kufikiria juu ya utabiri wa kutia matumaini wa Schwab. Schwab alirudi Pittsburgh kuendesha biashara ya chuma cha pua ya Andrew Carnegie, wakati Gary na wengine waliobakia walirudi kwenye soko la hisa kupoteza muda na mambo madogomadogo kwa matumaini ya kile ambacho kingelifuata.

‘Haukupita muda mrefu. Ilimchukua Morgan kiasi cha muda wa wiki moja kutafakari wazo Schwab alilokuwa ameliweka mbele yake. Baada ya kujihakikishia mwenyewe kuwa hakukuwa na matatizo ya kifedha ambayo yangeliweza kuja kutokea, alituma ujumbe kumuita Schwab - na kumkuta kijana akiwa na aibu kiasi. Schwab alidokeza ya kuwa Bwna Carnegie asingefurahishwa ikiwa angekuta Rais wake wa kampuni anayemuamini amerubuniwa na kukubali kuonyesha mapenzi kwa mfalme mkuu wa Wall Street, mtaa ambao Carnegie alishaapa kutokujihusisha nao. Hatimaye mjumbe aliyetumwa W. Gates, alipendekeza kwamba ikiwa Schwab angelikwenda katika hoteli ya Bellevue Philadelphia, J.P Morgan naye pia angeliweza kutokea pale wakutane.

‘Hata hivyo Schwab alipowasili, Morgan kwa bahati mbaya alikuwa mgonjwa nyumbani kwake New York, na hivyo kutokana na shinikizo la mwaliko wa mzee huyu, Schwab ilimbidi aende New York na kujiwasilisha mwenyewe katika mlango wa maktaba ya bwana fedha.

‘Siku hizi wanahistoria fulani wa uchumi hueneza imani kwamba tangu mwanzo mpaka mwisho wa ‘sinema’, jukwaa liliandaliwa na Andrew Carnegie - kwamba chakula cha jioni, hotuba maarufu, mkutano wa Jumapili usiku kati ya Schwab na Mfalme wa pesa, yalikuwa ni matukio yaliyopangwa na Canny Scot(Andrew Carnegie). Ukweli ni ikinyume kabisa. Wakati Schwab alipoitwa kuja kukamilisha mapatano, hakufahamu hata ikiwa “bosi mdogo” (kama Andrew Carnegie alivyokuwa akiitwa kwa utani), angeliweza hata kidogo kusikiliza ofa ya kuuza, hasa kwa kundi la watu ambao Andrwew aliwachukulia kama watu waovu.

‘Lakini Schwab alikwenda kwenye mkutano akiwa na karatasi sita zilizoandikwa vizuri kwa mkono wake mwenyewe, aliwakilisha akilini mwake thamani halisi na uwezo tarajiwa wa faida wa kila kampuni ya chuma cha pua aliyofikiria kama ni nyota muhimu katika dunia mpya ya chuma.

‘Wanaume wanne walitafakari juu ya tarakimu hizo usiku kucha . Kiongozi Mkuu, bila shaka alikuwa ni Morgan,  akishikilia msimamo katika imani yake kwenye haki ya utukufu wa pesa. Pamoja naye alikuwa rafiki yake Kabaila, Robert Bacon, msomi na mtu muungwana. Wa tatu alikuwa John W. Gates ambaye Morgan alimbeza kama mcheza kamari na alimtumia kama zana. Wanne alikuwa Schwab ambaye alifahamu zaidi kuhusu mchakato wa kutengeneza na kuuza chuma cha pua kuliko mtu mwingine yeyote yule aliyekuwepo katika kundi. Kupitia mkutano ule tarakimu za Pittsburgh kamwe hazikuhojiwa. Kama angesema kampuni ilikuwa na thamani kiasi fulani, basi ingelikuwa na thamani kiasi hichi hicho na siyo zaidi.

‘Alikuwa na msimamo pia juu ya kujumuishwa katika muunganiko zile kampuni alizozitaja tu. Alikuwa ameanzisha Shirika ambalo kusingelikuwa na kuigizwa, wala hata kuwaridhisha marafiki walafi waliotaka kutua makampuni yao juu ya mabega mapana ya Morgan. Hivyo aliibwaga nje kiufundi idadi ya makampuni makubwa  ambayo ‘matapeli’ wa Wall Street walikuwa wakiyatupia macho yao yenye njaa.

‘Kulipopambazuka, Morgan aiamka na kuunyoosha mgongo wake. Swali moja tu lilibakia…

“Unafikiri unaweza ukamshawishi Andrew Carnegie kuuza?” Aliuliza.
“Naweza kujaribu” Alisema Schwab.
“Ikiwa utaweza kumfanya auze, nitatimiza ahadi” Alisema Morgan.

‘Lakini mpaka kufikia hapo. Carnegie angeweza kuuza? Ni kiasi gani cha pesa angeweza kuhitaji? (Schwab aliwaza juu ya $320,000,000) Angechukua malipo katika mfumo gani? Katika mfumo wa hisa za kawaida au hisa za upendeleo? Dhamana? Pesa taslimu? Hakuna mtu ambaye angeweza kuchukua kiasi cha Dolla bilioni tatu katika pesa taslimu.

‘Kulikuwa na mchezo wa golfu mwezi Januari katika mbuga ya barafu ya St. Andrews links huko Westchester. Andrew akiwa amejivika lundo la sweta  kujikinga na baridi, na Charles Schwab akizungumza kwa uhodari kama kawaida ili kujitia moyo. Lakini hakukuwa na neno lolote kuhusiana na biashara walilozungumza mpaka pale wawili hao walipoketi chini sehemu nzuri tulivu kwenye kibanda cha Carnegie kilichokuwa jirani.

‘Kisha kwa ushawishi uleule aliowapumbaza mamilionea themanini kwenye klabu ya Chuo Kikuu, Schwab alimwaga ahadi zenye kuvutia za kustaafu kwa faraja, ahadi za mamilioni ya kumtosheleza Mzee mafao yake uzeeni. Carnegie alisalimu amri, akaandika tarakimu juu ya karatasi na kumpa Schwab akisema, “Vizuri, hiyo ndiyo bei tutakayouza”

‘Tarakimu zilikuwa zinakadiriwa kufikia  Dola $400,000,000 na ilifikiwa kwa kuchukua $320,000,000 kiasi cha msingi na kuongeza hapo $80,000,000 ili kuwakilisha mtaji ulioongezeka thamani kwa kipindi cha miaka miwili ya nyuma.

‘Baadaye wakiwa ndani ya meli(Trans Atlantic Liner) Carnegie alimwambia Morgan kwa masikitiko “Natamani ningekutajia $100,000,000 zaidi”
“Kama ungetaja, ungeliweza kuipata” Morgan alimjibu kwa uchangamfu.

‘Schwab mwenye umri wa miaka 39 alipata dhawabu yake. Alifanywa kuwa Rais wa Shirika jipya na kubakia katika uthibiti wake mpaka mwaka 1930’

Simulizi hii ya kusisimua ya biashara kubwa ilijumuishwa humu ndani ya kitabu kwa sababu ni mfano halisi wa njia ambayo kupitia hiyo Shauku inaweza ikabadilishwa kuwa katika kitu halisi kinacholingana nayo Ninafikiria baadhi ya wasomaji watahoji kauli hiyo kwmba ni kwa vipi Shauku tupu isiyoweza kushikika inaweza kugeuzwa kuwa kitu halisi. Bila shaka wengine watasema, ‘Huwezi ukaigeuza hali ya kutokuwepo kitu chochote kuwa kitu chochote!’ Jibu lipo ndani ya simulizi hii ya Shirika la Chuma cha Pua la Marekani(United States Steel)

Shirika hilo kubwa liliundwa katika akili ya mtu mmoja. Na mpango ambao Shirika liliutumia kwa viwanda vya chuma cha pua uliolipa shirika uthabiti kipesa ulibuniwa katika akili ya mtu huyohuyo mmoja. Imani yake. Shauku yake, Ubunifu wake, Uvumilivu wake vilikuwa ni viungo vya kweli vilivyounda Shirika la Chuma Cha Pua la Marekani, viwanda vya chuma cha pua na mashine zilizochukuliwa na Shirika baada ya kusajiliwa kisheria ilikuwa ni jambo dogo, lakini tathmini ya kina itabainisha ukweli kwamba thamani iliyokadiriwa ya mali zilizochukuliwa na Shirika iliongezeka kwa kadirio la dola milioni mia sita kwa hesabu tu ile iliyowaunganisha chini ya usimamizi mmoja.

Kwa maneno mengine, wazo la Charles M. Schwab ukijumlisha na Imani ambayo aliipandikiza kwenye akili ya J.P. Morgan na wengineo, liliuzwa kwa faida ya karibu $600,000,000. Siyo kiasi kidogo cha pesa kwa wazo moja!

Ni nini kilichotokea kwa baadhi ya watu waliochukua hisa zao za mamilioni ya dola ya faida iliyotokana na uuzwaji huu ni suala ambalo hatuhusiki nalo kwa sasa. Jambo muhimu katika mafanikio haya ya kushangaza ni kwamba yanatoa ushahidi usiopingika wa ukamilifu wa filosofia iliyoelezwa katika kitabu hiki.

Zaidi ya hapo, utendaji kazi wa filosofia umedhihirishwa kutokana na ukweli kwamba Shirika la Chuma Cha Pua la Marekani lilipata mafanikio. Lilikuwa moja kati ya Mashirika tajiri zaidi na lenye nguvu Marekani, likiajiri maelfu ya watu, kubuni matumizi mapya ya chuma cha pua na kufungua masoko mapya, hivyo kuonyesha kwamba, $600,000,000 za faida ambazo wazo la Schwab lilizalisha, zilikuwa halali.

Utajiri huanzia katika hali ya fikra. Ukomo wa utajiri hupangwa tu na mtu ambaye ndani ya akili yake fikra hutiwa katika vitendo. Imani  huondoa ukomo. Kumbuka hili wakati unapokuwa tayari kujadiliana na Maisha kwa chochote kile kiwacho unachokihitaji  kama bei kwa kuwa umepitia njia hii. Kumbuka pia kwamba, mtu aliyeunda Shirika la chuma cha pua la Marekani kiuhalisia hakuwa anajulikana kabisa wakati huo. Alikuwa tu “Msaidizi” wa Andrew Carnegie, mpaka pale alipozaa wazo lake maarufu. Baada ya hapo, alipanda haraka kwenye nafasi ya Madaraka, Umaarufu na Utajiri.
.......................................................................................................

Inafuata >>>>Sura ya NNE>>>>>>   Usikose.

Pia kwa vitabu mbalimbali, vya Biashara, Ujasiriamali, Michanganuo na Mafanikio kwa ujumla tembelea ukurasa huu hapa >> SMART BOOKS TANZANIA.







0 Response to "UTAJIRI HUANZA NA WAZO, UKOMO WA UTAJIRI MTU HUPANGA MWENYEWE AKILINI"

Post a Comment