Ukibuni kitu au unapobuni kitu/wazo la kutengeneza
bidhaa/huduma nzuri, tegemea kwa asilimia kubwa watu wengine kuibuka na vitu
vya kwao vinavyofanana na kile ulichokifanya,watafanya kitu kinachoitwa 'kukopi na kupesti'. Nazungumzia hasahasa kwenye
tasnia ya biashara. Ukiwa tu na wazo zuri la biashara, ukaliweka katika vitendo
na watu wengine wakagundua kuwa wazo hilo lina uwezekano wa kuzalisha faida
nzuri, utashangaa utitiri wa watu wengine watakavyoibuka na kulitumia wazo
lilelile ulilolianzisha wewe.
Kuna
kuiga kwa aina 2, kuiga kubaya(unakopi idea, kitu cha mtu mia kwa mia kama
kilivyo) na kuiga kuzuri kunakojenga(kuiga kiubunifu).
Kuiga au kukopi kwa njia hiyo ya kwanza kuna
madhara makubwa kiuchumi siyo tu kwa kampuni au yule aliyeibiwa bali hata na
kwa jamii na serikali kwa ujumla, kwani uigaji wa namna hii huua vipaji na
ubunifu ukizingatia mbunifu alipoteza muda wake mwingi na gharama kufanya
ubunifu huo. Hii ndiyo sababu serikali nyingi na hata Umoja wa Mataifa wenyewe
jambo hili hawalitaki kabisa na zimewekwa hata sheria mbalimbali kama vile ile
ya hatimiliki, hakimiliki na ulinzi wa alama za biashara kusudi kukomesha na
kuzuia vitendo vya namna hiyo.
Unaweza
ukaiga(kukopi na kupesti), lakini ni lazima uhakikishe unaongeza ubunifu wenye
tija kwa watumiaji.
Kuna ule msemo maarufu sana duniani usemao; “You
can’t reinvent the wheel”(Huwezi ukagundua upya gurudumu) wakimaanisha,
mtu kutaka kugundua kitu kipya kabisa hapa duniani leo hii ni jambo gumu sana.
Vitu vingi vimekwisha kugunduliwa na kilichobakia sasa ni kuviongezea ubunifu
kusudi kuviboresha zaidi na kuvifanya viwe na uwezo wa kufanya kazi nyingi au kuwa na matumizi mengi zaidi ya vile vya awali.
Kuiga kitu kwa asilimia mia moja ni kosa na
tena hata ni aibu kubwa kwa yule anayeiga. Ushindani haumaanishi kukopi mawazo
ya mtu mwingine mazima kama yalivyo, bali ni kutoa kitu tofauti na kilichokuwa
na manufaa zaidi kwa walaji au watumiaji kushinda kile cha mshindani/washindani
wako.
Unaweza ukakuta mtu au kampuni fulani imeiga
mawazo ya mtu/kampuni nyingine lakini ikiwa katika kuiga huko kuna
kitu(thamani) kilichoongezwa pale, huwezi ukalaumu na kudai kuwa kaiba wazo la
mwingine.
Katika
mifano ifuatayo huwezi ukaiita ni kukopi na kupesti.
1)
Kuiga au kutengeneza bidhaa za aina moja.
Kampuni inaweza ikatengeneza bidhaa au huduma
zinazofanana na za kampuni nyingine lakini kukawa na tofauti katika alama(features)
au formula(kanuni ya utengenezaji). Mfano mzuri tunaweza tukaupata kutoka
makampuni ya vivywaji baridi ya hapahapa kwetu nyumbani Tanzania ya Cocacola,
Pepsi, Azam cola na Sayona. Wakati Azam na Sayona wanatoa vinywaji vyao vyenye
asili ya cola hukuwasikia Cocacola na Pepsi wakilalamika au kwenda mahakamani
kudai wameibiwa wazo la soda zao za cola.
Lakini kama Azam na Sayona pengine wangeliziita
soda zao majina yaleyale ya “cocacola au pepsi” au kutumia chupa zinazofanana
kila kitu na zile za kwao, basi bila shaka hapo ni lazima pangetokea mgogoro
mkubwa. Vilevile ijapokuwa vinywaji
vyote hivyo hutumia kiasili kimoja yaani “cola” lakini bidhaa zao zina tofauti
kubwa katika ladha na hata utakuta formula(kanuni ya uchanganyaji vile viungo)
anayotumia kila mmoja ni tofauti na ya mwenzake.
Kingine ni kwamba ujio wa kampuni hizo mbili.
Azam na sayona ulisababisha mapinduzi makubwa katika bei za soda na hata
vifungashio vyake(packaging). Zamani kabla ya hapo bei za soda zilikuwa na
ukiritimba mkubwa lakini makampuni yalipoongezeka wakaanza kushindana vikali
mpaka watu tukaanza kupata soda za 500 mpaka 300 ilihali soda ilishafika mpaka
700. Chupa nazo badala ya zile za kioo zilizokuwa zimezoeleka sasa tukashuhudia
za plastiki(takeaways) zikitumika kwa wingi. Zamani ilikuwa kupata soda
iliyotiwa ndani ya chupa ya plastiki ni ‘ishu’ na hata ulipoipata, bei yake
ilikuwa haikamatiki, 1000/= mpaka 1500/= na kuendelea. Leo hii ukitaka mpaka ya sh.
500/= unapata bila shida yeyote.
2) Kuiga
kazi za ubunifu wa mawazo(Intellectual properties)
Kazi hizi ni kama vile za uandishi, utunzi wa
muziki, filamu, alama mbalimbali kama logo nk. Mfano mzuri ninao mimi mwenyewe.
Nilipotoa kitabu, “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA”
Kitabu kilitoka sambamba na kampeni niliyoipa jina la; “KUELEKEAUTAJIRI” Kuna
watu wengi waliojaribu kuiga wazo lile. Katika blogu kadhaa niliona baadhi ya
insha “articles” zangu zikiwa zimekopiwa nyingine nzimanzima kama zilivyo,
wengine wakaanzisha blogu zilizokuwa na maudhui kama yaleyale.
Wapo hata waliotunga vitabu vilivyokuwa na
maudhui sawasawa na ya kile kitabu nilichotunga, kwa mfano mimi nilisema;
Mifereji 7 ya Pesa” wengine wakaita, Mifereji 10 ya pesa, mifereji 12 ya kipato
nk. Mfano mwingine ni makala maarufu nilizoandika katika website ya
jifunzeujasiriamali wakati huo ikijulikana kama “Kuelekeautajiri”, kama
vile; “Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa
kiuchumi?”, “Natengeneza sabuni, shampoo,
batiki na Unga wa lishe lakini sioni unafuu wowote wa maisha” na hata makala
iliyosema “Rasilimali adimu kuliko zote
duniani, ikipotea imepotea huwezi tena ukaipata maisha yako yote”
Waliokopi makala hizo wengine walikopi kama zilivyo lakini pia kuna
waliobadilisha heading kidogo au hata kubadili kabisa maneno lakini maudhui
yakabakia kuwa ni yaleyale. Mimi binafsi kwa upande wangu hilo halikunipa shida,
kwanza nilifurahi na kutiwa moyo kwani ndilo lililokuwa lengo langu kuu,
kuhamasisha watu wengi kwa kadiri inavyowezekana kuchukua hatua ya kupigana na
umasikini kwa vitendo hasa kupitia shughuli zinazohusisha mawazo au akili zao
huku zikiwapa kipato.
Hata katika kitabu hichohicho kama ulikisoma kuna mahali nilitoa ‘ruksa’
ya kukopi, nikihamasisha juu ya kitabu kingine, “MICHANGANUO YA BIASHARA NAUJASIRIAMALI” niliandika maneno haya na hapa nanukuu, “Michanganuo yetu ni ruksa kabisa mtu yeyote
yule kuiga, ilimradi tu usiige kama ‘mbumbumbu’ kwa asilimia mia moja”
mwisho wa kunukuu. Kwa vyovyote vile nisingeliweza kukasirika au kumzuia mtu
yeyote yule ambaye angetumia “kuiga kuzuri” au “kukopi kiubunifu” kazi
zangu.
Na zaidi ya hapo niligundua tena kwamba, kumbe kile nilichokuwa
nikikifanya kilikuwa ni kitu kizuri na ndiyo maana watu wengine nao wakaanza
kukopi ‘idea’ yangu. Matokeo kwa ujumla ya kampeni ile na Kitabu hicho cha
Mifereji 7 ya Pesa bila shaka yeyote mimi huwa siachi kusema kuwa
pengine ndiyo yaliyokuja kuleta mwamko uliokuwepo sasa wa watu wengi hasa
bloggers na waelimishaji mbalimbali kupitia vitabu, kwenye magazeti na semina
kutoa elimu ya ujasiriamali, kujikomboa kiuchumi na maendeleo binafsi kwa
jamii.
Kampeni ile ilisambaa mithili ya moto wa
nyika, nikawa napigiwa simu nyingi sana watu wakitaka kufahamishwa zaidi juu ya
kampeni ile “kuelekeautajiri”. Nilifanya kosa moja kubwa sana na ambalo
nitalijutia siku zote, baada ya kuona watu wakinisumbua sana juu ya kampeni
hiyo, niliamua kuisitisha ghafla(soma makala hii kwanini nilisitisha kampeni hiyo) na kubadilisha jina na hata muonekano mzima wa blogu zangu nikidhania
pengine watu walikuwa wamenielewa vibaya. Baada ya kubadilisha majina na kuita “jifunzeujasiriamali”
hakuna tena mtu aliyehangaika kunifuatilia.
Muziki
na Filamu.
Muziki na filamu navyo ni hivyo hivyo,
hauwezi ukakopi muziki au filamu ya mtu mwingine kama ilivyo na ukabaki salama.
Lakini maudhui ni ruksa na hata mtindo na vionjo hauwezi ukamlaumu mtu eti
kaiga vyakwako. Rege kapiga Bob Marley, rege kapiga Lucky Dube, rege kapiga
Jimmy Cliff, rege hiyo hiyo kapiga Alpha Blondy. Lakini hamna hata mmoja
aliyelalamika kuibiwa mtindo huo na mwenzake.
Lucky Dube kwa mfano alipiga wimbo uitwao “One love” jina linalofanana sawasawa
na la wimbo wa Bob Marley nao unaoitwa jina hilohilo, lakini ukizisikiliza
rekodi hizo zote mbili wala hazifanani kabisa kimdundo japo zote ni reggae na
hata mashairi hayafanani isipokuwa jina tu na pengine maudhui yake yanaweza
yakafanana.
Cheki pia, hata kuna filamu kama vile, Tarzan,
au Titanic, filamu hizo zimewahi kuchezwa na watu tofauti wengi na ijapokuwa
maudhui na majina zinafanana lakini tofauti zake ni kubwa.
“Templates”(Themes)
za blogu na tovuti.
Hizi ni violezo au kwa maana nyingine unaweza
ukazifananisha na daftari lililokuwa tupu halijaandikwa bado kitu chochote ndani.
Baadaye daftari hilo unapoandika na kuchora vitu ndani yake tunalinganisha na
unapoweka ‘contents’, vitu, maandishi, picha, sauti nk. kwenye
blogu/mtandao/tovuti/website, vyovyote vile utakavyoita na hatimaye vitu hivyo
visomwe, kusikilizwa au kuonwa na watu/hadhira.
‘Theme hizi/templates’ hutengenezwa na watu
mbalimbali wenye ujuzi wa lugha ya kompyuta(coding) na kisha baadaye kuziuza au
kuzitundika bure mtandaoni kwa mtu yeyote atakayehitaji basi aweze kuzitumia.
Blogu nyingi hapa Tanzania hutumia hizi templates za bure.
Sasa tukichukua mfano, A blogu yake ametumia
template ya bure, B naye akija akatumia template ileile, A hawezi kwa namna
yeyote ile kulalamika na kudai kuwa eti B kakopi wazo lake. Wakulalamika hapa
angekuwa ni yule mtengenezaji wa hiyo template lakini mtengenezaji mwenyewe
keshasema template yake itumiwe na mtu yeyote anayeihitaji tena bure.
Hata za kununua bado huwezi ukamlaumu mtu
kwani watu tofauti wanaweza wakanunua template hiyo hiyo moja. A kitu ambacho
angeliweza kukifanya ili awe na haki ya kudai watu wasikopi template yake ni
kutengeneza template yake kuanzia moja “from the scratch” akitumia “code” zake mwenyewe na isitoshe
akaikatia hatimiliki, kwa hapa kwetu ni pale BRELLA.
Kwa mfano tovuti yangu hii, jifunzeujasiriamali.com, template yake niliitengeneza
mwenyewe tangu mwanzo bila usaidizi wowote na hata watu wengine siku hizi
huniuliza “mbona huibadilishi, imepitwa na wakati, kwanza siyo mobile friendly”
lakini huwa nawajibu “nitabadilisha tu taratibu” na kweli sina haraka nayo
kwasababu moja tu, “inanikumbusha mbali
sana, kipindi sijui chochote kuhusu maswala ya mitandao na wala sina laki tano
za kumlipa mtaalamu wa tovuti.”
Unapokuwa umeuwekea ubunifu wako hatimiliki,
unayo haki ya kumshitaki mtu yeyote anayekuibia na kukopi ‘idea’ au kitu chako
na akakulipa pesa nzuri.
Usije ukaogopa kutumia template ya bure au
hata ya kununua mtandaoni iliyokwisha kutumiwa na mtu mwingine tayari kwa
kuhofia eti utaonekana umekopi na kupesti, hakuna kitu kama hicho katika dunia
hii ya utandawazi. Ilimradi imekuvutia, wewe download au nunua, jiwekee
blogu/website yako ipendeze.
Unapokopi kitu/idea ya mtu mwingine, epuka
kukopi pale kwenye kitovu(roho) ya ule ubunifu ilipo. Roho au kitovu cha
ubunifu kwa mfano kwenye soda za cola kipo katika formula(kanuni) ya
uchanganyaji wa viungo, jina halisi la soda na vitu kama nembo. Kwenye utunzi
au kazi yeyote ile ya maandishi roho ipo kwenye yale maandishi na mpangilio
wake mzima na wala siyo katika maudhui yake ndiyo maana ukikopi kazi ya mtu
mwingine neno kwa neno ni kosa kubwa. Kwenye blogu au tovuti roho ipo kwenye
‘contents’, kile kilichomo ndani, na kama ni template basi ipo kwenye
hatimiliki yake.
Hakuna kitu “Search engines” mfano
google wanachokichukia kama mtu kukopi kazi iliyokwishatolewa na mtu mwingine
pasipo kuomba idhini ya mwenyewe. Lakini hata siku moja sijawahi kusikia google
wamempiga mtu ‘penalty’ kisa eti katumia template aliyokwishatumia mtu
mwingine, watakupiga penati wakibaini umekopi maandishi ya mtu mwingine.
Magari
na vyombo vya moto.
Mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa
miaka ya 2000 kulizuka ushindani mkali baina ya makampuni makubwa ya magari
duniani. Volkswagen ndiyo iliyoanza kwa kuja na ubunifu wake ambapo iliamua
kuitoa tena upya gari yake ndogo aina ya “Beetles” iliyopata umaarufu mkubwa
sana miaka ya 60 na 70 huko nchini Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Lilikuwa ni wazo zuri sana na wakafanikiwa kuliteka soko kwa kasi ya ajabu!
Kila mtu alikuwa na shauku ya “ku-experience way back” lakini katika muonekano
na hisia mpya.
Haikuchukua hata muda mrefu, wapinzani wao
BMW nao wakaona wasibakie nyuma. Wazo ni lilelile lakini wao wakaitoa tena upya
gari yao ndogo iliyowahikutamba miaka ya 60 na iliyojulikana kama Mini Cooper
S, Mini Cooper zilitamba sana nchini Uingereza miaka hiyo ya 60. New Mini
Cooper S lilikuwa ni wazo lilelile waliloanzisha Volkswagen.
Washindani wengine FIAT nao hawakukubali
kuchelewa, mara moja kwa kutumia wazo lililoanzishwa na Volkswagen la kurudisha
mtindo wa zamani wa magari, wakalizalisha tena upya gari lao dogo la Kiitaliano,
Fiat 500, gari lililotamba mno miaka ya 50 na 60.
Wateja hupendelea sana vitu vya namna hii,
hasa ushindani wa kiubunifu usiomuumiza mtu mwingine lakini unaochochea
maendeleo na ndiyo maana ukaona makampuni yote matatu ya magari yakitumia wazo
lilelile moja lililoanzishwa na Volkswagen bila kujali ni nani aliyelianzisha.
Kibaya hapo ni kama mmoja wao angelitoa gari
linalofanana kila kitu kwa asilimia mia moja na mwenzake. Lakini kila mmoja kwa
kutumia wazo la kuzalisha tena upya magari yao ya zamani na katika muonekano
mpya wa kisasa, hakukuwa na tatizo lolote hapo na huwezi ukawalaumu BMW wala
FIAT kwa kudai wamekopi na kupesti.
HITIMISHO.
Kuiga kupo kila mahali na kutaendelea kuwepo
nyakati zote. Nchi zilizoendelea wangezuia kabisa kuiga, sidhani nchi kama hizi
za kwetu huku kungelikuwa na maendeleo yeyote. Njia za kuzuia ‘uigaji mbaya’ zipo kama vile,
kuuwekea ubunifu hatimiliki, hakimiliki kwa kazi za utunzi na usanii, kulinda
kwa kusajili alama za biashara nk. Njia hizi hupunguza tu na wakati mwingine
kuzuia kwa muda watu kukopi kazi za watu wengine. Simaanishi kwamba hazisaidii
hapana, lakini kufanya kwake kazi vizuri kunategemea zaidi wazo au kitu
kilichobuniwa iwe ni kweli umekibuni na wala siyo kwamba na wewe ulikikopi
kutoka mahali pengine na kisha ukadai umekibuni.
Njia pekee na ya uhakika zaidi inayoweza
ikakusaidia kupambana na waigaji watakaokopi kazi zako ni kuhakikisha unakuwa
bora muda wote katika biashara au chochote kile unachokifanya. Waigaji
watakapobaini haukatishwi tamaa wala kutikisika na kukopiwa kazi zako, basi
wenyewe ‘watasarenda’ na kukuacha ukisonga mbele kifua mbele.
Kwa upande mwingine, ‘kuiga kuzuri’, ndiko kunakoleta ushindani na hatima yake maendeleo
kupatikana kwani vinginevyo duniani kusingelikuwa na kitu kipya. Vitu vingi
vipya ni vilevile vya zamani vilivyoboreshwa au kuongezewa madoido(features)
zaidi.
........................................................................................................
Mpenzi msomaji wa blogu hii ya Jifunzeujasiriamali, kuna mambo mengi zaidi na makubwa yanayotarajiwa kuja nyuma ya blogu yako hii, hivyo nakuomba sana usikose kuwa na sisi kila mara. Pia ikiwa utahitaji vitabu kutoka kwetu juu ya ujasiriamali na biashara basi usisite kuwasiliana nasi au tembelea ukurasa huu wa SMARTBOOKSTZ. 'Jipatie free of charge' kitabu cha 'Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio' pamoja na vitabu vingine vizuri 25 kwa kujiunga hapa na kuweka e-mail yako
........................................................................................................
Mpenzi msomaji wa blogu hii ya Jifunzeujasiriamali, kuna mambo mengi zaidi na makubwa yanayotarajiwa kuja nyuma ya blogu yako hii, hivyo nakuomba sana usikose kuwa na sisi kila mara. Pia ikiwa utahitaji vitabu kutoka kwetu juu ya ujasiriamali na biashara basi usisite kuwasiliana nasi au tembelea ukurasa huu wa SMARTBOOKSTZ. 'Jipatie free of charge' kitabu cha 'Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio' pamoja na vitabu vingine vizuri 25 kwa kujiunga hapa na kuweka e-mail yako
Mawasiliano yetu ni haya yafuatayo;
SIMU: 0712 202244, 0765 553030 na 0689 303098
TELEGRAM: 0712 202244 au @petertarimo
E-MAIL: jifunzeujasiriamali@gmail.com
Unasema kuiga kiubunifu siyo vibaya, wewe hujawahi kukopiwa kitu ukaona machungu yake, niliwahi kufunga biashara yangu ya nguo mwananyamala hivi hivi baada ya jamaa mmoja kuona nilivyokuwa nauza akajaniwekea pembeni biashara kama ileile. Ningekuwa mchawi ningemloga.
ReplyDeleteKwanza hebu naomba ondoa hilo neno 'uchawi' kwanza maanake hizi imani imani mara nyingi sana ndizo hutufunga hata tusiwe na ujasiri wa kuthubutu kufanya vitu. Ikiwa unaamini uchawi ni dawa basi hata ujasiri wa kupambana nae kibiashara usingeliweza kuwa nao.Ulipaswa kujiamini na siyo kukimbia na kumwacha. Wewe tayari alikukuta na wateja wako, ni mbinu gani aliyoitumia kuwateka? Ikiwa ulikuwa unawapa huduma stahiki kwa bei stahiki sidhani kama huyo jamaa angelikuwa na ubavu wakukungoa, badala yake yeye ndiye angelifunga virago baada ya miezi michache. Ulipaswa uwe mvumilivu kidogo na siyo siku mbili tatu tu ukakimbia. Asante
ReplyDelete