Kujenga banda bora na la kisasa la kufugia
sungura ndiyo kitu cha kwanza kabisa mfugaji wa sungura anayetaka kuanza
kuwafuga sungura anachotakiwa kuanza nacho. Mafanikio ya biashara ya ufugaji wa
sungura hutegemea kwa kiasi kikubwa mabanda au vizimba vinavyotumika kuwatunza
sungura.
Banda la kutunzia sungura halihitaji kuwa la
gharama kubwa sana ikiwa ndiyo kwanza unaanza lakini pamoja na hivyo linapaswa
kuwa imara kwa ajili ya usalama na maisha bora kwa sungura wako. Hivyo ujenzi
wa rahisi wa mabanda ya sungura yanayokidhi sifa hizo unapaswa ufanywe kwa
kutumia malighafi na vifaa vinavyoweza kupatikana kwa urahisi kwenye mazingira
uliyopo.
Aina
za mabanda ya sungura (vizimba vya kufugia sungura)
Ujenzi wa mabanda ya sungura hauna kanuni
maalumu, kikubwa tu ni sungura kupata eneo salama na la kutosha kuishi raha
mustarehe, lililokuwa na hewa ya kutosha, eneo la kucheza hasahasa kuruka, kusimama
wima na kujinyoosha huku kukiwa na
urahisi wakufanya usafi katika banda kwani sungura wanataka usafi, na
hawatakiwi kabisa kuishi katika eneo lililokuwa chafu.
Dhana ya banda bora la kisasa ni kutimiza
matakwa hayo ya nafasi ya kutosha , usalama na usafi, hivyo banda lako la
sungura au nyumba ya kuishi sungura wako
unaweza ukaiijenga vyovyote vile utakavyoamua kwa kutumia malighafi na vifaa
utakavyomudu kupata ilimradi tu umetimiza vigezo na masharti hayo.
Mabanda ya sungura unaweza ukayaweka katika
mafungu tofauti kulingana na aina ya sakafu au pia unaweza kuyapanga kulingana
na aina ya ufugaji wa ndani au wa nje.
SOMA: Soko la Sungura Tanzania linakua kwa kasi kuliko uzalishaji wenyewe wa sungura.
SOMA: Soko la Sungura Tanzania linakua kwa kasi kuliko uzalishaji wenyewe wa sungura.
Mabanda
yenye sakafu ya waya.
Aina hii ya mabanda, sakafu wanakokaa sungura
hutengenezwa kwa waya mesh au wavu ambao huruhusu kinyesi na mkojo kupita kwa
urahisi na kwenda kudondokea juu ya bati au chombo kama trei lililolala
mshazari hatimaye uchafu huo hukingwa na kukusanywa kwenye vyombo maalumu kwa
ajili ya kuuzwa hasa mkojo au kinyesi kutumika kama mbolea.
Uzuri au faida kubwa ya aina hii ya mabanda
ni kwamba mfugaji unapata urahisi mkubwa wakati wa kufanya usafi wa mabanda na
mabanda hubakia kuwa masafi muda wote.
Ubaya wa aina hii ya ujenzi wa mabanda ya
waya ni sungura kukosa raha, kwani sungura kwa asili yake hawajaumbwa kuishi juu ya sakafu ya waya,
asili yao ni kukanyaga juu ya sakafu ngumu kama ardhi na ndani ya mapango
wanayopendelea kuchimba wenyewe juu ya ardhi. Unapotumia aina hii ya mabanda
basi unashauriwa kutenga eneo dogo uweke sakafu ngumu kama mbao au bati kwa
ajili ya sungura kupumzika au kukanyaga pasipo usumbufu.
Mabanda
yenye sakafu ngumu.
Mabanda yenye sakafu ya namna hii ndiyo
sungura wanayopendelea zaidi na tena sungura hufurahi zaidi endapo sakafu
itakuwa ya udongo kusudi waweze kuchimba mashimo ya kujificha lakini
haishauriwi kabisa kutumia udongo kwani watakupa tabu sana pindi wakizaa au
wakati utakapotaka kuwashika.
Hukimbia na kuingia kwenye mapango hayo
kujificha na hata wakati mwingine wanaweza wakachimba mashimo yenye urefu
mkubwa wakapitiliza na kwenda kutokeza mbali na lilipokuwa banda lenyewe. Hii
ni hatari pia kwani wanaweza wakapotea, kuibiwa au kuliwa na wanyama wa porini.
Ukiweka sakafu ngumu basi inabidi utumie
malighafi ngumu kama sementi/zege, mbao au bati na juu unaweka matandiko ya
nyasi ngumu au nyuzinyuzi za katani, maranda ya mbao hayafai sana kwani
yanaweza kuharibu mapafu ya sungura.
Faida kubwa ya aina hii ya sakafu ni sungura
kujisikia raha zaidi watembeapo juu yake lakini ubaya wake upo katika kuweka
banda katika hali ya usafi. Wakati wa kufanya usafi bandani itakubidi uhamishe
sungura wote kwenda eneo jingine ndipo uweze kufanya usafi vizuri jambo
linaloongeza ugumu wa kuwashughulikia.
Banda dogo la sungura lenye sehemu ya ndani na nje. |
Mabanda
ya nje na ya ndani.
Kama ilivyokuwa kwa kuku sungura pia wanaweza
wakafugwa ndani tu au nusu ndani nusu nje. Sungura ni wanyama wanaopenda wakati
mwingine kujificha hivyo hata kama unawaweka banda la wazi la nje lakini ni
lazima ndani ya banda hilo uwawekee eneo au maumbo wanayoweza wakajificha ndani
yake wanapojisikia hawako salama sana. Mabanda ya ndani yanaweza yakatumika kwa
ajili ya sungura kupumzika na kulala, kisha ya nje wakatumia kucheza na kula.
Ukubwa
(saizi ya mabanda ya sungura)
Sungura wanahitaji kulala, kula , kunywa maji,
kucheza, kujificha na kujisaidia haja kubwa na ndogo. Eneo linalopendekezwa la
kizimba au banda la kufugia sungura ni mita za mraba 12au wastani wa meta za
mraba 1, ina maana kwa wastani upana unatakiwa kuwa mita 1 na urefu mita 1 au
futi 6 kwa 2.
Sungura anahitaji pia eneo kwa ajili ya
kucheza, kwa hiyo jumla ya eneo lote lisipungue futi za mraba 40 mpaka 60.
Sungura anaposimama wima anatakiwa masikio yake yasiguse juu kwenye paa hivyo
urefu kutoka chini kwenye sakafu hadi juu kwenye paa unatakiwa kuwa sentimita
60 mpaka 90. Hayo ni makadirio tu ya chini, sungura wanahitaji eneo kubwa hata
zaidi ya hilo ili kujinafasi kwa uhuru zaidi.
Mpenzi msomaji, kama ulikuwa hujagundua faida
za kufuga sungura, hebu soma makala hii isemayo Sungura wa mbegu na wa nyama wanapatikana Mbezi Kwa Msuguri kwa bei nafuu. Ushauri wangu kwako:- fuga sungura wana faida kubwa na hawahitaji
eneo kubwa kama wanyama wengine, sungura pia wanakula vitu ‘simple’ sana kama
vile, nyasi na maganda ya vyakula kama ndizi, kunde, matikiti na maboga, tena
kwa kiasi kidogo tu kwa siku. Uzaaji wao ni wa haraka na watoto wengi kuanzia 6
mpaka 8 kwa wakati mmoja. Soko halina shaka unauza kuanzia manyoya, mpaka
mkojo.
Unaweza kuanza hata na sungura wawili tu dume
na jike na kama utapenda kuanza leo, nakushauri anza na banda kwanza walao la
sungura wawili na kisha ukimaliza ndipo utafute sungura kwa ajili ya mbegu. Sungura wazuri na wanaolipa ni wale wa kisasa au chotara ambapo huwa na uzito mkubwa tofauti na sungura wa kienyeji.
Asante kea somo ila kwenye maelezo yanayohusu ukubwa wa eneo katika bada ,hivyo vipimo fafanua kwa sungura mmoja anahiaji sqm ngapi?
ReplyDelete