Kitabu cha zamani kuliko vyote duniani. |
Hebu jaribu kuirudisha akili yako nyuma miaka kama 25 hivi iliyopita na linganishe na wakati huu tuliokuwa nao katika suala zima la kujipatia maarifa ya aina mbalimbali. Bila shaka utagundua kwamba miaka hiyo ya nyuma ilikuwa mtu ukihitaji maarifa ya namna yeyote yale basi ni sharti uyapate aidha kwa kusimuliwa kwa mdomo au kwa kuyasoma mahali hususani kutoka katika vitabu mbalimbali. Hizo ndiyo zilizokuwa njia kuu za kujipatia maarifa.
Tunaporudi nyuma zaidi kihistoria, utaona kwamba miaka
hata kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, njia kuu iliyokuwa ikitumika kuhifadhi
maarifa ya aina yeyote ile iwe ni ya kidini, kisayansi, kitabibu, kifasihi na
hata kijamii ilikuwa si nyingine bali ni
kwa njia ya maandishi na picha ambavyo vilihifadhiwa katika mfumo wa vitabu na
vitabu vyenyewe haijalishi vilitengenezwa kwa aina gani ya karatasi, wakati
mwingine yalitumika mawe, ngozi, vipande vya mifupa, vyuma, ardhi, kwenye
miamba na hata katika vipande vya mbao.
Moja ya vitabu vya kale zaidi duniani. |
Karatasi za kawaida zilipokuja kugunduliwa pamoja na mashine
za kupiga chapa utengenezaji wa vitabu ukawa rahisi zaidi. Kitu cha kushangaza
kabisa ni vitabu vya dini vya Quran Tukufu na Biblia Takatifu, kuna watu
wanaofikiria labda vitabu hivi katika zama za mitume na manabii vilikuwa vile
vile kama vilivyokuwa leo. Vitabu hivi vitakatifu viliandikwa kimaajabu katika
karatasi zisizokuwa za kawaida hata kidogo, wakati mwingine katika ngozi za
wanyama, mawe, miamba na hata katika magome ya miti.
Lakini kutokana na
tekinolojia ya wakati huo kuwa ndiyo iliyokuwepo, basi watu wa nyakati hizo
waliithamini mithili ya sisi tufanyavyo leo hii kwa vitu kama facebook,
twitter, wassap na mtandao mzima wa Intaneti. Na hiyo ndiyo sababu iliyofanya
vitabu hivyo pamoja na vitabu vya maarifa mengine ya kidunia viweze kuhifadhiwa
kwa ustadi namna hiyo mpaka na sisi huku leo hii tukavikuta na
vikatustaajabisha.
Kuhifadhi maarifa yeyote yale katika chombo chochote kile
iwe ni kwenye vitabu vya kawaida, au katika kompyuta kunabakia kuwa na maana
ileile iliyokuwepo enzi za manabii na mitume Biblia Takatifu na Quran Tukufu
vilipohifadhiwa. Njia zote ni lazima alama zitumike, iwe ni maandishi ya kawaida
au ya kielektroniki, ni vyombo tu ndivyo hubadilika kwa mfano ilikuwa
ngozi, ikaja karatasi na sasa imeingia kompyuta lakini dhana ya kuhifadhi inabakia
kuwa ni ileile.
Wazo la makala hii limenijia baada ya kufikiria dhana iliyoanza
kuenea kwamba vitabu na hasa vya karatasi siku zake zinahesabika, maana yake ni
kwamba itafika kipindi watu hawatasoma tena vitabu vya karatasi. Mimi hili
silipingi na wala silikubali kama lilivyo. Mawazo yangu ni kuwa, vitabu vya
karatasi vitaendelea kuwepo kwa karne nyingi zijazo sambamba na vile vya
kielektroniki, hakuna atakayemmeza mwenzake. Zipo sababu nyingi zikiwemo za
kihistoria lakini pia za kiuchumi na hata sababu za kitekinolojia.
Kwa mfano kihistoria watu ni vigumu sana kushawishika
kwamba kitabu cha kielektroniki ni sawa sawa na cha karatasi, watu
wameshajijengea mazoea ya muda mrefu karne kwa karne. Kiuchumi, maeneo mengi
Duniani ni masikini na yataendelea kubakia kuwa masikini kwa kipindi kirefu
bila ya watu wake kuweza kumudu teknolojia hizi za kisasa. Kuhifadhi maandishi
ya karatasi ni rahisi na hudumu kwa muda mrefu bila ya kuharibika kutokana na
sababu mbalimbali kama vile, hali ya hewa nk. hivyo maandishi ya karatasi
yataendelea kuwepo.
Tukiacha vitabu hivyo vitakatifu, maarifa mengine yote
yaliyosababisha kutokea maendeleo makubwa zaidi duniani yakiwemo yale ya
kompyuta na intaneti yote yalihifadhiwa kwa namna moja ama nyingine kwenye
vitabu. Hivyo kusema kwamba mafanikio ya ustaarabu wote na maendeleo ya mwanadamu yameletwa na vitabu ni sahihi
kabisa.
0 Response to "VITABU: CHANZO CHA MAENDELEO NA MAFANIKIO MAKUBWA YA BINADAMU DUNIANI"
Post a Comment