Utasikia mara nyingi watu wakizungumzia hatari kubwa iliyokuwepo kwenye biashara za magari hususani biashara ya usafirishaji, na wengi utawasikia wakidai kwamba biashara hiyo inaweza ikakupa ugojwa wa moyo ikiwa itatokea ajali na chombo chenyewe ambacho ni gari kuharibika kiasi ambacho ni vigumu kutengenezeka tena au zikahitajika fedha nyingi mno kwa ajili ya matengenezo.
Kwa upande mwingine wapo watu wanaoisifia sana biashara
ya uwekezaji kwenye majumba na kudai kuwa biashara hii haina hatari kubwa(low
risk business) kama ilivyokuwa kwa biashara za magari kutokana na ukweli kwamba
nyumba ni rasilimali inayoongezeka thamani kadiri muda nao unavyozidi kupita
tena hakuna hatari kubwa inayoweza kutokea mfano ajali za mara kwa mara kama
ilivyokuwa kwa magari.
Biashara za magari hasa zile za ubebaji abiria na mizigo zina
faida kubwa endapo mtu utatumia mbinu zinazostahili. Wapo wafanyabiashara hapa
Tanzania waliofanikiwa sana kutokana na biashara hii baada ya kuanza na gari
moja mpaka kufikisha magari zaidi ya mia moja. Moja kati ya mbinu hizo
wanazozitumia wafanyabiashara hao ni kukubali kukabiliana na hatari zote
zinazoweza kutokea kipindi biashara ikiendelea, lakini mtu anapokubali
kukabiliana na hatari hafanyi hivyo kichwa kichwa tu hapana, ni lazima upime
hatari zenyewe na kuweka mipango thabiti ya kuzipunguza au kuziondoa.
Watanzania wengi wenye asili ya kiasia kwa mfano miaka ya
nyuma walionekana kushamiri sana kwenye biashara hizi tofauti na Wazawa
kutokana na tabia yao ya kuzingatia kikamilifu kanuni zinazoongoza biashara
hii. Hata hivyo baadhi ya Wazawa nao walikuja kubaini mbinu walizokuwa
wakitumia Waasia nao wakazitumia na sasa hivi wengi wanafanya vizuri sana
katika sekta za usafirishaji abiria na mizigo.
Biashara za usafirishaji zinahitaji mtu kuwa na mtaji wa
kutosha, lakini utakuta kwa mtu anayeanza mara nyingi anakuwa hana mtaji wa
kutosha. Mbinu mojawapo watu wanayoweza wakaitumia ili kukabiliana na kikwazo
hiki namba moja ni mbinu ya kwenda kukopa mkopo benki. Na hii huwa rahisi ikiwa
mhusika tayari anamiliki angalao gari moja iwe ni basi, lori, tax au pikipiki.
Chombo ama Gari hilo moja linaweza likatumika kama
dhamana benki kwa kuwapelekea watu wa benki kadi ya gari, wanaweza kwa mfano
wakakukopesha gari jingine hivyo ukawa na magari mawili, magari hayo mawili
yatatumika kukusanya faida ambayo ndiyo itakayotumika kulipia marejesho ya
mkopo uliochukua mpaka unamaliza. Baada ya hapo kama utarejesha vizuri Benki
wanaweza wakakukopesha zaidi, kwa mfano wanaweza wakakuongezea magari mengine
mawili jumla yakawa manne.
Kuna mbinu zingine zinazotakiwa ziende sambamba na hiyo
ya kukopa kama vile kukatia vyombo vyako bima za uhakika ambapo kwa bahati
mbaya ikitokea ajali au uharibifu wowote basi wewe hutaumiza kichwa hata kidogo,
vilevile unahitajika usimamizi usiokuwa na shaka hata kidogo kuhakikisha mapato
yatokanayo na magari hayavuji ovyo bila kusahau kuepuka kununua vyombo(magari)
makuukuu. Nunua magari mapya tu na yakisharudisha faida yauze kabla hayajachoka
sana kusudi upate pesa nzuri.
Kama ulianza siku
moja na mwenzako aliyekwenda kuwekeza katika nyumba labda tuseme ni
nyumba ya kupangisha, mwenzako huyo katika kipindi kifupi anaweza akawa
anakutazama na kujiuliza “ Hivi kweli huyu ndiye tuliyeanza naye siku moja kwa
mtaji unaolingana, iweje yeye awe mbali kiasi hiki na mimi hata bado sijajenga
nyumba ya pili?”
Kwa ujumla biashara za usafirishaji japo zinamtaka mtu
kuchukua hatari kubwa na nyingi lakini kama utakuwa makini zinao uwezo mkubwa
wa kumtajirisha mtu ndani ya kipindi cha muda mfupi sana tofauti na biashara
nyingine hata na uwekezaji kwenye majengo ukiwamo ingawa uwekezaji katika
majengo au majumba hauna hatari nyingi sana na ni uwekezaji wa uhakika ambao faida yake haiwezi kuja haraka sana, inachukua
muda kidogo.
..............................................................................................
Karibu kwenye SEMINA YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YAKO, kwa maelekezo zaidi fungua link ya maandishi hayo hapo juu
Vile vile vitabu vyote kutoka Self Help Books viapatikana katika mifumo yote yaani Hardcopy na Softcopy kwa maelezo ya kila kitabi fungua blogu ifuatayo SMART BOOKS TZ. Usikose kudownload pia kitabu cha kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio bure kabisa.
Kwa mawasiliano, maswali au jambo lolote lile, tumia namba za simu; 0712202244 au 0765553030
0 Response to "JINSI WANAOCHUKUA HATARI KUBWA KWENYE BIASHARA YA MAGARI WANAVYOFANIKIWA HARAKA"
Post a Comment