Kitengo chetu cha ushauri hupokea maswali na changamoto mbalimbali kila siku na kuwajibu wahusika na mara nyingi hufanya hivyo kupitia simu ya mkononi au sms, isipokuwa kwa wale wanaotuma kwa email huwa maswali au ushauri wao tunawajibu kwa email au pamoja na kuuweka hapa kwenye Blogu ya jifunzeujasiriamali lakini pasipo kuanika majina yao kabisa, tunatumiaga vifupi vya majina yao au majina yasiyokuwa halisi. Hapa chini ni ushauri alioomba mwanafunzi mmoja wa chuo kutoka Singida;
Habari, naitwa C…… niko singida kwa sasa,
ni mwanafunzi wa chuo. Nmesoma makala zako nikawiwa kukufatilia. Niko kwenye
wakati mgumu wa kuanzisha biashara, nahitaj msaada wa mawazo ili kuweza kuvuka
hatua hii
Pole
ndugu C….., na nashukuru sana kwa kupitia makala zangu, lakini napenda
kukuambia pia kwamba hauko peke yako, ni watu wengi wanapitia kipindi kigumu
pengine hata kushinda wewe, hebu fikiria mtu ambaye hata nafasi ya chuo
hajaweza kuipata na pia hana hata uwezo hususan mtaji wa kuanzishia japo
kabiashara ka kuuza karanga.
SOMA: Natengeneza sabuni, shampoo, batiki na unga wa lishe lakini mambo bado ni magumu nifanyeje?
SOMA: Natengeneza sabuni, shampoo, batiki na unga wa lishe lakini mambo bado ni magumu nifanyeje?
Nimefurahi kusikia
wewe upo chuoni na bado unalo wazo la kuanzisha biashara. Jambo hili
linawezekana kabisa japo inakubidi uwe "Smart" kidogo, nikimaanisha
kwamba inakupasa kama utaanzisha biashara yeyote ile ungali bado chuoni
ni lazima uhakikishe unatengeneza mfumo madhubuti utakaokuwezesha kutekeleza
mambo hayo mawili kwa wakati mmoja vinginevyo unaweza ukajikuta unafanya vibaya
pande zote mbili, kwenye masomo na kwenye biashara pia.
Kutengeneza mfumo huo
kuna gharama zake ambazo ni lazima ziwe aidha katika maana ya rasilimali fedha
au rasilimali muda. Biashara ili iweze kusonga mbele ni lazima itahitaji
uwekeze muda wako au fedha vinginevyo haiwezekani kabisa kuendesha biashara.
Ukiwa na rasilimali ya fedha unaweza ukaanzisha biashara fulani na ukamtafuta
mtu akawa anaiendesha hata ikiwa wewe binafsi hautakaa pale kila wakati na wewe
kazi yako kubwa itakuwa ni kuja na kukagua mahesabu yako kikamilifu tu, poteza
hata saa moja au saa moja na nusu kwa siku ili uhakikishe mtaji wako upo salama
na faida iliyopatikana siku hiyo.
Kwa upande wa
rasilimali ya muda, inakubidi mtu uutumie muda wako karibu wote kwa siku
kuendesha na kusimamia biashara yako ndogo uliyoianzisha kwa kuwa hauna
rasilimali pesa ya kutosha kuajiri mtu. Shughuli zote pengine kuanzia kufuatilia
bidhaa kama ni biashara ya kuuza bidhaa mpaka shughuli ya kumuuzia mteja
itakubidi uifanye wewe mwenyewe. Mchakato mzima wa biashara kuanzia asubuhi
mpaka jioni unaotumika mpaka biashara inatengeneza faida ndiyo tunaoweza kusema
ni mfumo wa biashara yako.
Ninavyofahamu mimi
ukishakuwa mwanafunzi au mwanachuo kama wewe, rasilimali ya muda ni lazima
itakuwa adimu sana kwa upande wako, sijajua kwa upande wa rasilimali ya fedha
upoje mfukoni mwako, na hiyo nadhani itakuwa ni siri yako sipaswi hata kujua.
Lakini hebu
"tuassume" tuchukulie labda mfukoni kwako upo vizuri kidogo,
nikimaanisha kwamba unao mtaji wa kutosha kuendesha biashara, kazi ya kuweka
mfumo wa biashara yeyote ile inayolingana na mtaji huo uliokuwa nao itakuwa
rahisi sana ilimradi tu ubuni wazo la biashara iliyokuwa na uwezo wa
kutengeneza faida na biashara ya namna hiyo mtu unachunguza katika mazingira
yaliyokuzunguka kuna mahitaji gani ya watu yanayotakiwa sana, watu wanashida
zipi zinazohitaji kutatuliwa? ukishabaini basi unaweza kutafuta eneo na kuweka
biashara itakayotatua zile shida za watu.
Kumbuka mchakato wote
huo utahitaji fedha kuukamilisha na kwa kila hatua inabidi utumie fedha hiyo
kwa umakini wa hali ya juu sana kwani fedha hiyo ikipotea inaweza kuwa vigumu
sana kuipata tena nyingine ndani ya muda mfupi. Wakati huo huo hakikisha ratiba
zako za masomo haziingiliwi kabisa.
Hebu tuchukulie sasa
wewe ni mwanachuo, tayari rasilimali-muda inajulikana 'automatic' kuwa ni adimu
kwako halafu pia ukute na rasilimali-fedha nayo huna ya kutosha kuanzisha
biashara, nikimaanisha hata ikiwa utaanzisha biashara basi ni kwa kuungaunga
tu. Hii ni hatari lakini pia zipo mbinu mtu unazoweza ukazitumia japo kwa kweli
nachelea sana kukushauri kwa dhati kabisa kuzitumia lakini 'anyway' nitajaribu
kuzielezea ili mwenyewe upime.
Najaribu kukumbuka
mifano hai niliyowahi kuiona mwenyewe kwa macho yangu vipindi mbalimbali
nilipokuwa nasoma, kwa mfano tulipokuwa shule ya sekondari, O level mimi
binafsi nilianzisha biashara ndogondogo nyingi lakini kwa kweli mafanikio yake
hayakuwa ya kuridhisha sana kutokana na ugumu wa kubalance muda wa masomo na
muda wa biashara. Nilijaribu kuuza vitu vidogovidogo kama majalada ya madaftari
na vitabu, siku zingine nilipeleka maembe, na hata kuna wakati nililima bustani
za mbogamboga na nyanya niliporudi nyumbani jioni kwa kuwa nilikuwa Day.
Shughuli zote hizo
tatizo kubwa nililokutana nalo lilikuwa ni mtaji kidogo. Nakumbuka hata
nilianzisha kutengeneza maandazi alfajiri nikamtafuta kijana aliyekuwa akienda
kuniuzia sokono mchana lakini napo sikupata mafaniio ya kuridhisa kutokana na
faida iliyokuwa ikipatikana kutokutoshelea kumlipa mfanyakazi na mimi mwenyewe.
Kuna mfano wa kijana
mwingine aliyekuwa amenitangulia kidato yeye alikuwa na biashara ya kupiga
picha akitumia kamera yake ndogo ya YASHICA,
kupiga picha wakati huo ilikuwa ni dili kubwa hasa nyakati za sherehe na siku
za miisho ya wiki. Kwa kuwa kupiga picha kulikuwa hakuhitaji muda mwingi kijana
yule aliweza kupata faida nzuri iliyomuwezesha hata kujilipia ada ya shule
mwenyewe.
Wakati nikiwa A level
nilishuhudia wanafunzi mbalimbali waliokuwa na biashara, wachache waliweza
kufanikiwa kubalansi masomo na biashara na kuna mmoja aliyekuwa na biashara ya
usafirishaji(daladala) alipomaliza form six akajiunga na chuo kikuu bado
biashara yake iliendelea kushamiria akaja kununua mpaka malori ya kusafirisha
mizigo kwenda mikoani. Kwa sasa hivi ni mwanasheria mzuri tu huku biashara zake
zikiendelea kama kawaida.
Nimekuonyesha
mazingira yote hayo ili uweze kuona changamoto unazoweza kukutana nazo pindi
utakapoamua kuanzisha biashara ungali ukiwa bado upo chuoni unasoma. Hata hivyo
kuna unafuu kidogo chuoni siyo sawa sawa na shule za sekondari au msingi, chuoni
unaweza kuwa “flexible” zaidi, kwa maana nyingine unakuwa na uhuru zaidi kwa
maana ya muda na hata masomo siyo mengi na magumu kama ilivyokuwa mashuleni.
Vyovyote vile iwavyo
kwa ushauri wangu mimi, wewe anzisha biashara, ila hakikisha unachagua biashara
“simple” ambayo utafanya kama majaribio kwanza kuona kama unaweza ukatengeneza
mfumo wako wa kujiingizia pesa pasipo kuathiri muda wako wa masomo. Tuchukulie
hata labda umeanzisha duka lako dogo na kumuweka mtu wa kukuuzia, ambalo unakuwa na uwezo wa kufika pale kila siku jioni na kukagua mahesabu yako, huo
ni mfano tu, inaweza kuwa ni biashara nyingine yeyote ile.
Narudia tena ikiwa
utaanzisha biashara utakayomuweka msaidizi, kama kwa kweli hautakuwa na mfumo
unaoleweka wazi wa kujua kwa uhakika hesabu zako za siku zimeendaje, basi
nakuomba acha kabisa usianzishe biashara bali endelea na chuo chako.
Na vilevile ikiwa
hauna uwezo wa fedha za kuanzisha biashara utakayomuweka mtu wa kukusaidia
unaweza ukaanzisha biashara rahisi isiyokula muda wako wa masomo, nina mfano
mwingine wa rafiki yangu mmoja yeye akiwa chuoni aliweza kubuni biashara ya
stationary kwenye bweni lake akawa anawatolea photocopy na printing wenzake na
wakati mwingine kuwaunganisha na intaneti, biashara ile ilimgharimu fedha
kidogo tu kwa ajili ya kununulia kompyuta, printa na baadhi ya software, lakini
aliweza kujiingizia kipato kikubwa pasipo kuingilia kabisa muda wake wa masomo
chuoni.
Unajua fursa ya kusoma
mara nyingi huja mara moja tu na huja kuwa vigumu sana kuweza kurudia mwaka au
darasa tofauti na biashara ambayo hata kama utaanguka mwaka huu lakini unaweza
ukajaribu tena na tena miaka mingine mpaka umefanikiwa. Unaweza ukasema “Mbona
kuna mabilionea kibao tu “walio drop out” kama kina Steve
Jobs, Mark Zuckerberg, Bill gates, Larry Ellison na hata Ted Turner na mambo
yao bado yakawa supa, lakini hao ni kama tone moja la maji katika bahari kubwa,
ni mmoja katika watu 1000, siyo kila mtu anaweza kuwa na bahati waliyokuwa nayo
hao.
SOMA: Ungependa kuwa kama Bakhresa, Mengi, Dewji na Rostam? fuata njia hizi 10
SOMA: Ungependa kuwa kama Bakhresa, Mengi, Dewji na Rostam? fuata njia hizi 10
Najua tatizo kubwa
mwanachuo au mwanafunzi yeyote analoweza kukutana nalo ni ufinyu wa rasilimali
za kuanzia hasa pesa na muda wa kutosha kuhudumia biashara, lakini mbinu pekee
unayoweza kuitumia kutatua matatizo hayo ni kwa njia ya kutumia rasilimali
kidogo ulizokuwa nazo kwa nidhamu ya hali ya juu, nikiwa na maana rasilimali ya
fedha na muda. Jibane, acha matumizi yasiyokuwa na ulazima kwako, kujibana huko
ni kuanzia matumizi ya fedha mpaka muda. Achana na starehe kama kula vyakula
vya gharama kubwa, vileo, kutazama tv, kuperuzi mitandao ya kijamii kupita
kiasi nk.
Mwisho kabisa rafiki
yangu C………, napenda nikuambie kuwa biashara ukiwa bado chuoni ni kitu
kinachowezekana kabisa na tena unajiandaa kwa ajili ya mazingira halisi ya
ufinyu wa ajira lakini zingatia sana mazingira niliyokueleza hasa kutokubinya
kwa namna yeyote ile muda wako wa masomo au hata kuamua kuachana na chuo
uendelee na biashara. Jitahidi kwa kadiri uwezavyo kuifanya biashara yako kuwa
inajiendesha yenyewe aidha kwa kuweka msaidizi makini au kwa kuanzisha aina ya
biashara itakayokugharimu muda kidogo sana lakini yenye faida ya kutosha pia.
………………………………………………………………
Tumekuwa kwa muda mrefu sasa tukitoa ushauri kwa watu mbalimbali
kupitia simu na ujumbe wa simu za mkononi na hata kupitia e-mail. Ni mara
chache ushauri tunaowapa watu tunauweka hapa katika blogu ya
JIFUNZEUJASIRIAMALI kama tulivyouweka huu hapa na nyingine chache.
Kwa kuwa wengi wa wale wanaotaka ushauri huwa wanarudi kwa mara
nyingine tena kuomba ushauri(unaweza kuwa tofauti na ule wa mwanzo au wakati
mwingime unakuwa unahusiana na ule wa mwanzo) tumeonelea yakwamba ili kuboresha
kitengo hiki basi tuweke huduma ya kuchangia ushauri huo ili kuweza kuutoa kwa
kina na kwa muda mrefu zaidi kwa yule anayehitaji.
Hatutaondoa ushauri wa bure wa kawaida wa mara moja kama huu au
tuliyokwishatoa kwa wasomaji wengine hapana, ila kutakuwa na chaji, shilingi
elfu 5 tu kwa yule atakayehitaji ushauri wa kina kabisa pamoja na huduma ya
COACHING katika kipindi kisichopungua miezi 6. Unapotoa shilingi elfu 5,
unapata fursa ya kuzungumza na mshauri au kocha kwa muda usiopungua dakika 15
siku hiyo, halafu utaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu kabisa na mshauri
kupitia jumbe za simu, e-mail na hata
simu kila utakapokuwa na swali au kuhitaji kushauriwa tena ndani ya miezi 6.
Ili kuwa mwanachama wa huduma hii, nitumie ujumbe unaoelezea ni
ushauri gani unaohitaji halafu utanipa muda kama saa moja au zaidi ya hapo
kulingana na nafasi yako wa kuandaa majibu. Karibu na muda tutakapoanza
mazungumzo ndipo utatuma pesa shilingi 5,000/= kwenye namba 0712 202244 au 0765 553030, na kisha tutaanza
mazungumzo yetu ukiwa sehemu tulivu isiyokuwa na kelele nyingi.
0 Response to "KUANZISHA BIASHARA NIKIWA CHUONI NASOMA NIPENI USHAURI NINA WAKATI MGUMU"
Post a Comment