Ni leo nikiwa kwenye basi nilikuwa nikitafakari kwa kina kabisa maisha yangu, siyo maisha nikiwa tu hapa Dar es salaam, hapana, tafakari hiyo ilinipeleka tangu nilipokuwa mchanga kabisa, tangu nilipoanza kuwa na fahamu pengine nilipokuwa shule ya chekechea(vidudu au nursery).
Nilijaribu kukumbuka vitu vingi, hasa watu waliokuwepo
wakati ule lakini sasa hivi hawapo tena wameshatangulia mbele za haki. Kwa
kweli nilipopiga picha vizuri nilihisi kama vile namuona marehemu bibi yangu,
mama zangu wadogo, na watu wengine wengi tu ambao kwa kweli nasikitika mno
sitaweza tena kuwaona uso kwa uso hapa duniani labda akhera na mimi itakapofika
siku yangu.
SOMO: Mama hubeba watoto wao miezi 9 lakini mioyo yao huwabeba milele.
SOMO: Mama hubeba watoto wao miezi 9 lakini mioyo yao huwabeba milele.
Tukiachana na hayo hebu twende moja kwa moja kwenye kile
nilichotaka kueleza leo hii hapa katika mfululizo wa makala zetu hizi za
kujirudishia tena ukuu wako uliotoweka(make yourself great again). Hitimisho la
tafakari yangu hiyo niliyoanza kukueleza iliishia siku mimi nitakapozeeka ikiwa
Mwenyezi Mungu ataniacha hai mpaka umri huo maanake siku hizi inavyosemekana
sisi wa Mataifa yanayoendelea kama Tanzania wastani wa umri wetu kuishi ni kitu
kama miaka 45 tu na hata ikizidi hapo ni kwa bahati, sijui lakini kama kauli
hiyo inao ukweli kiasi gani.
Nilijaribu kufikiria maisha waliyoishi babu na bibi,
namaanisha kutoka pande zote mbili, bibi na babu wazaa baba na babu na bibi
mzaa mama. Na hii siyo kwa upande wangu tu peke yake, nilijaribu pia kufikiria
kwa upande wa kaya zilizokuwa majirani na hao wazee. Kwa kweli ukweli mchungu
sana na ambao nadhani hata wewe unayesoma hapa unaweza usiukubali lakini
nadhani ndiyo hali yenyewe halisi ni kwamba, hebu watazame au wakumbuke bibi na
babu jinsi walivyoishi.
Pointi ninayotaka niiwasilishe hapa hata ikiwa kwa upande
wako ilikuwa kinyume lakini kwa asilimia kubwa ya watu wataniunga mkono. Babu
na bibi enzi zao hawakuwa na tofauti yeyote na ulivyokuwa wewe leo hii,
walikuwa nao na wazazi wao, walipofikisha umri wa kuoana wakaoana kwa nderemo
na vifijo huku wazazi wakishuhudia kwa furaha kabisa. Baada ya harusi, waliondoka wakaenda kuanzisha
familia zao na kuwaacha wazazi wao. Babu na bibi nao walifuata mlolongo uleule
waliofuata wazazi wao.
Ukweli mchungu ninaouzungumzia hapa sasa ndiyo nausema.
Babu na bibi baada ya kuwazaa mama na baba yako, baba na mama yako nao
walifuata mlolongo uleule kama kawaida, baba na mama wakaenda kuanzisha familia
zao na kuwaacha wazazi wao peke yao, siyo baba na mama yako tu peke yao waliowaacha
wazazi wao bali pia na ndugu zao wengine ambao ni mama na baba zako wadogo,
wajomba zako na mashangazi wote walikwenda kuanzisha familia(miji) yao na
kuwaacha bibi na babu wapweke wakati mwingine wakiwa kijijini hawana msaada wa
kutosha. Kuna nyakati hufika hata bibi na babu wanatafutiwa mfanyakazi wa
kuwaangalia na kuwapikia utadhani hawajazaa, hapo ndipo uchungu unaponishika.
Uchungu unakuwa mkubwa zaidi pale mmoja kati ya babu au
bibi anapofariki dunia na kumwacha mwenzake. Kwa kweli hapa unakuta anayebakia
mara nyingi huwa hawezi tena kuishi miaka mingi kutokana na upweke. Hukumbuka
enzi za ukuu wake alipokuwa na mwenza wake, watoto na hata ndugu na jamaa
wengine wa karibu, wakishirikiana hili na lile.
Sasa tuhamie kwa baba na mama yako. Nao usifikiri wako
salama kwenye hili, la hasha, inasemekana kuwa hii ni sheria ya maumbile
haimwachi mtu hata mmoja. Hapa ndipo utaanza kuhisi uhalisia wa hiki
ninachokiandika hapa. Nakuomba ujaribu kufikiria mara ya mwisho kuonana na
wazazi wako ni lini kama unaishi mjini na wazazi wapo kijijini au mkoa mwingine?.
Nadhani bila shaka yeyote asilimia 90% au naweza kusema asilimia kubwa ni
lazima watanijibu, ni siku nyingi pengine hata mwaka, miaka 2 na zaidi
hawajaonana na wazazi wao zaidi ya kuwasiliana kwa simu.
SOMO: Dhana potofu ya ushirikina ni hatari kuzidi ushirikina wenyewe.
SOMO: Dhana potofu ya ushirikina ni hatari kuzidi ushirikina wenyewe.
Baba na mama yako penda usipende watafuata nyayo zilezile
walizopitia babu na bibi yako, huu ni ukweli mchungu sana mimi na wewe tunaopaswa
kuukubali isipokuwa tu kwa mazingira machache sana na ambayo nitayaelezea
mwishoni wakati wa kuhitimisha makala hii.
Tuje kwako sasa au kwangu, piga darubini miaka kadhaa
ijayo, kuna uwezekano unaweza ukaja kukwepa kuwa sawasawa na walivyokuwa bibi
na babu na mama na baba yako? Jibu ni wewe mwenyewe unayeweza kuwa nalo. Je
kuna uwezekano mtu ukabadilisha sheria hii watu waliyoamua kuibatiza kuwa ni
sheria ya maumbile isiyoweza kubadilishwa na mwanadamu? Hivi ni kweli hii ni
sheria ya maumbile? Tafadhali ndugu msomaji wangu ikiwa una jibu au maoni
mengine yeyote yale yaweke hapo chini kwenye kisanduku cha maoni.
Mpenzi msomaji makala hii ina sehemu 2 na hii ni sehemu
ya 1, sehemu ya pili itaendelea, tafadhali nakuomba usiikose. Nitakuja na suluhisho, ninini cha
kufanya na ikiwa hii kweli ni sheria ya maumbile isiyoweza kuvunjwa kamwe. Soma sehemu ya pili 2 hapa.
ILE SEMINA KUBWA YA MICHANGANUO YA BIASHARA inakaribia
kuanza kuchanganya na uandikishaji bado unaendelea kwa kiigilio cha shilingi
10,000/= Ingeshaanza siku nyingi kuchanganya lakini tunacheleachelea kusudi
jahazi litakapong’oa namga rasmi basi abiria wawe ni wa kutosha, tusiwaache
wengine wakininginia mlangoni. Kwa mawasilianao zaidi tuwasiliane kwa namba 0712 202244
0 Response to "UKWELI MCHUNGU KILA MTU ANAOPASWA KUUKUBALI MAISHANI KABLA YA KUIAGA DUNIA-1"
Post a Comment