HUNA MUDA WA KUTOSHA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA? TUMIA NJIA HIZI 3 RAHISI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HUNA MUDA WA KUTOSHA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA? TUMIA NJIA HIZI 3 RAHISI

Kwanza nimshukuru Mwenyezi mungu kwa siku nzuri ya leo, siku moja baada ya kuanza rasmi kwa semina yetu ya MICHANGANUO YA BIASHARA, au tuseme kwa maana nyingine semina ya kujifunza jinsi ya kuandika mpango wa biashara. Nawashukuru na kuwapongeza pia washiriki wote tuliokuwa pamoja leo, ninaamini yale yote tuliyojifunza pamoja kwenye Blogu maalumu ya MICHANGANUO pamoja na mengine kwa njia za simu, email na hata sms yanaonyesha mwelekeo wa semina yetu utakavyokuwa ingawa tulishapanga kabla mwelekeo mzima utakavyokuwa. 

Hamna tofauti na Mpango wenyewe wa biashara ulivyo kwani unapanga lakini ni lazima kujitokeze baadhi ya vitu vitakavyokwenda tofauti na jinsi ulivyopanga, hilo ni lazima na halipaswi kuchukuliwa kama kisingizio cha kuacha kupanga kwani kwa kadiri utakavyoacha kupanga ndivyo mambo nayo yatakavyotokea kwa namna ya kushitukiza zaidi(kwa dharura) na usiyoweza kuidhibiti kirahisi.

SOMA: Sababu kuu 5 kwanini uandike mpango wa biashara.

Mfano ni mshiriki mmoja kutoka Arusha baada ya kujiunga nikamtumia e-mail, alinipa taarifa kwamba haoni email nilizomtumia wala ile ya kuactivate kujiunga na blogu ya masomo, baada ya kuhangaika kidogo nilikumbuka kitu nikamwambia acheki kwenye Spam folder, na kweli haikuchukua dakika 2 ‘akanitext’ kuwa ameshaziona.

Mshiriki mwingine kutoka Mwanza yeye alinijulisha ugumu wa kupakua(kudownload) masomo kwenye blogu ya michanganuo kwa kuwa yeye anatumia simu ya mkononi, hapo nikapata tena wazo kwamba badala ya kuweka masomo kwa mtindo huo wa kudownload peke yake, basi nitaweka pia kwa mtindo wa ‘post’ masomo mengine ya ziada tutakayoanza kuweka baada ya yale 11 ya msingi.

NJIA RAHISI 3 ZA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YAKO KAMA UMEBANWA NA HUNA MUDA MWINGI WA KUTOSHA

Makala hii nilipanga kuzizungumzia njia tatu unazoweza ukazitumia kuandika mpango wa biashara yako kwa urahisi zaidi bila ya kupoteza muda mwingi wala kuumiza sana kichwa.

1. Njia ya kwanza ni ya kutumia kielezo(Business plan template), hiki ni kama mfano wa mpango wa biashara uliokwisha andikwa na kupangwa sehemu zote muhimu, wewe kazi yao ni kufuta(kudelete) maandishi yaliyojazwa mle na kupachika yakwako yanayoendana na biashara yako unayoiandikia.

SOMA: Ni kina nani hasa wanaohitaji mpango wa biashara?

Kielezo au Template siyo kama document za kawaida za ‘Word’, eneo unalofuta kuweka maneno yako ni maalumu haliingiliani na eneo au kipengele kingine kinachofuata au kilichopita. Kwenye blogu ya MICHANGANUO tume ‘upload’ template hiyo ambayo imeandikwa kwa kiswahili ikiwa na sehemu zote muhimu za mpango wa biashara na katika kila sehemu inakuelekeza uweke maneno gani au ni nini cha kufanya.

2. Ukurasa mmoja wa Mchanganuo.
Huu unafanana kidogo na Muhtasari tendaji kwenye mchanganuo kamili wa biashara lakini wenyewe unakuwa na vitu vingi kidogo. Ukurasa mmoja wa mchanganuo ni maelezo yanayoihusu biashara yako nzima kwa kifupi kabisa ndani ya dakika 15 hivi. Unaweza ukaielezea dhamira, malengo na mikakati ya biashara yako kwa ufasaha ndani ya muda mfupi wakati ukisubiri kuandika mpango kamili wa biashara na msomaji akakuelewa vizuri.

SOMA: Andika mpango wa biashara yako kwa kiswahili.

Faida za Ukurasa mmoja wa mchanganuo kwanza ni, Haraka, Rahisi, Unaweza kuwashirikisha watu wengine kwa urahisi, na Una uwezo wa kumvutia au kumhamasisha msomaji asiyekuwa na muda mwingi wa kusoma mchanganuo mzima wa biashara.

Kwenye blogu ya MICHANGANUO tumeweka(uploading) mfano wa ukurasa huu uliokuwa pia na maelekezo ambao unaweza ukaudownload na kujaza taarifa zako zinazohusiana na biashara unayotaka kuiandikia ‘ukurasa mmoja wa mchanganuo’. Ukurasa huu pia unaweza kuwa kama muongozo kwako mwenyewe katika uendeshaji wa biashara yako kwa ufanisi.

3. Njia ya 3 ni kutumia programu au software za kuandika mpango wa biashara.
Zipo programu nyingi mitandaoni unazoweza kununua na kuzitumia katika kuandika mchanganuo wako wa biashara kwa urahisi na katika muda mfupi sana. Unachotakiwa kufanya ukishanunua programu hiyo ni kujaza taarifa na namba za hesabu zako na kisha kazi ya kupanga na kukokotoa unaiachia programu hiyo ambayo mwishoni inakutolea mpango mzima wa biashara uliokamilika.

Ni njia nyepesi sana lakini wewe kama binadamu ni lazima uhakikishe taarifa na namba unazoipa ‘software’ hiyo ni sahihi na zinaendana na biashara unayoiandikia kulingana na utafiti uliofanya. Ni lazima utafiti uufanye mwenyewe, programu haina uwezo wa kufanya utafiti kwa hiyo hapo utaona kwamba kutumia software hizi mtu ni lazima uwe na uelewa walao kidogo wa michanganuo ya biashara na ni kitu gani kinachotakiwa kuwekwa ndani yake.

SOMA: Njia sahihi ya kufanya utafiti wa soko la biashara

Kwa leo naishia hapa lakini rai yangu kubwa kwanza kwa wale ambao tayari wameshajiunga na Darasa la semina hii ni kwamba, tuendelee kuwa pamoja kila siku hasa hapa kwenye blogu hii ya jifunzeujasiriamali kwani ndiyo mahali pekee ninapopatumia kutoa taarifa nyingi kuhusiana na masomo ya semina yetu ingawa pia siyo kila kitu hasa yale masomo muhimu nitayaweka hapa. Kwa yale masomo muhimu yanayohusiana na mipango ya biashara tutakutana kulekule kwenye Blogu yetu maalumu ya Michanganuo.

Pili ni kwa wale wote wenye nia ya kujua kwa thati kabisa namna ya kuandaa michanganuo ya biashara, nasema kuandaa kwani najua wapo watu wengine hawapendi kabisa kuandika, lakini wangependa tu kuifahamu michanganuo ya biashara namna ilivyo na inavyoandaliwa, kwani kujua peke yake kichwani kunakupa uwezo mkubwa wa kuchanganua biashara na kuifanya kwa weledi tofauti na mtu mwingine asiyejua biashara inatakiwa iwe na vitu gani, kumbuka mchanganuo wa biashara ni malezo yote, a-z yanayoihusu biashara hivyo kusumbua kichwa chako kuyafikiria tu achilia mbali kuandika kweye karatasi kunatosha kabisa wewe kukupa uzoefu wa kipekee wa kuifanya.

Ningependa kuwatia moyo kwamba huu ndio wakati muafaka wa kujifunza namna ya kuandaa mpango wa biashara. Hata ikiwa kwa sasa ratiba yako ipo ‘tight’ unahofia pesa yako kupotea bure kutokana na hautapata muda wa kutosha kufuatilia semina, ondoa kabisa hofu hiyo kwani, kila kitu kinarekodiwa kwenye blogu ya Michanganuo na zaidi ya hapo masomo yanatumwa kwenye email yako ambapo yana uwezo wa kukaa hata kitukuu wako akaja kuyakuta labda tu itokee bahati mbaya google waje “wakolapsi” ama kuzima huduma ya Gmail.

Karibu njoo ujiunge na ikiwa hufahamu utajiunga vipi na semina basi fungua page hii hapa, JINSI YA KUJIUNGA NA DARASALA SEMINA YA MICHANGANUO YA BIASHARA. Au unaweza kuwasiliana na mimi kwa sms au simu, 0712 202244  au  0765 553030

Asante sana
Peter Augustino Tarimo
Mhamasishaji na mkufunzi wako.

0 Response to "HUNA MUDA WA KUTOSHA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA? TUMIA NJIA HIZI 3 RAHISI"

Post a Comment