BIASHARA 1 NZURI INAYOLIPA TANZANIA UNAYOWEZA KUFANYA KIPINDI HIKI KIGUMU CHA FEDHA 2017 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA 1 NZURI INAYOLIPA TANZANIA UNAYOWEZA KUFANYA KIPINDI HIKI KIGUMU CHA FEDHA 2017

Ingawa Serikali ya Tanzania kupitia taasisi na  wizara zake mbalimbali ikiwemo, Benki kuu na wizara ya Kilimo, mifugo na  uvuvi inadai kwamba hali ya kiuchumi siyo mbaya, lakini kiuhalisia katika maisha ya kawaida ya Mtanzania hali ni tofauti kabisa. Wananchi wengi wanalalamikia hali ngumu kipesa na kudorora kwa biashara kunakosababishwa na watu wengi kukosa uwezo wa kununua mahitaji mbalimbali.

Katika hali kama hiyo wajasiriamali wengi wamejikuta wakipunguza morali wa kufanya biashara, kuanzisha biashara mpya na hata wafanyakazi katika makampuni mbalimbali na biashara wakijikuta vibarua vyao vikiota nyasi kutokana na biashara au makampuni hayo kuamua kupunguza wafanyakazi ili kupunguza gharama za uendeshaji au hata kuamua kuzifunga kabisa biashara zenyewe.


Kimbilio pekee linabakia ni kwa zile biashara ama shughuli ambazo zenyewe kulingana na asili yake haziwezi zikaathiriwa kwa kiasi kikubwa sana na hali ngumu ya kifedha au tuseme mdororo wa kiuchumi kama huu unaoinyemelea Tanzania mwaka huu wa 2017. Ikiwa basi unapanga kuanzisha biashara au kubadilisha biashara uliyokuwa nayo sasa hivi kutokana na hali kuwa ngumu, bila shaka utapenda kufikiria kuanza biashara ambayo haitaathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali hiyo mbaya ya mzunguko mdogo wa pesa.

Biashara hizo hazishuki sana kipindi cha matatizo ya kiuchumi zipo nyingi lakini hapa nimeamua kuweka msisitizo mkubwa zaidi katika biashara moja tu ambayo ndiyo isiyoweza kutikiswa kabisa ijapokuwa pia nitataja na baadhi ya biashara zingine kadhaa.

BIASHARA NZURI TANZANIA YA KUFANYA WAKATI WA HALI MBAYA KIUCHUMI (HALI NGUMU YA FEDHA)

Biashara ya vyakula na vinywaji.
Hakuna shaka yeyote kwamba biashara namba moja ambayo kamwe haiwezi kuyumba iwe ni katika kipindi cha mdororo wa kiuchumi au hata katika kipindi cha vita ni biashara ya kuuza vyakula. Vyakula katika maana zote, yaani vile vilivyopikwa na hata vile ambavyo bado havijapikwa kama nafaka, nyama, samaki, mbogamboga, matunda na vinywaji vya aina zote kuanzia maji, juisi nk.

Watu hawana chaguo jingine wanapoumwa na njaa na hasa hasa katika majiji makubwa kama Dar es salaam, Mwanza, Arusha, Morogoro na Mbeya. Ni lazima watanunua vyakula wakapike au vyakula ambavyo tayari vimeshapikwa kama wali, chipsi, supu, chai ndizi, na vyakula vinginevyo. Mtu anapokuwa na kiu pia ni lazima atafute maji anywe au kinywaji kingine atakachoamua mwenyewe.

Sina maana kwamba sasa basi kila mtu aachane na biashara yake aliyokuwa akiifanya zamani na kuhamia katika biashara hizi za vyakula, hapana, ila hapa nataka tu kuonyesha ni jinsi gani biashara ya vyakula isivyoweza kuathiriwa na hali mbaya ya kiuchumi na hivyo kwa yule ambaye anapanga kuanzisha biashara na anaona ipo fursa anayoweza kuipata kupitia biashara ya vyakula na vinywaji basi aweze kuifanya kwani ikumbukwe kwamba hata biashara ikiwa na fursa kubwa kiasi gani, lakini vigezo vingine vingi vitahusika kusudi mtu uweze kuifanikisha kwa faida vikiwemo vigezo vya, ujuzi, mtaji wa kutosha nk.

SOMA: Ijue biashara nzuri yenye uwezowa kulipa faida mara mbili 2 ya mtaji wako uliowekeza.

Nilitangulia kusema kwamba listi au orodha ya biashara zinazoweza kufanyika kipindi cha hali ngumu kipesa au kiuchumi ukiachana na hii ya chakula na vinywaji ambayo ndiyo kubwa kuliko zote ni ndefu na ningetaja biashara nyingine angalau nazo kwa uchache, kwahiyo ni hizi hapa chini;

Biashara ya kukodisha vifaa na vyombo mbalimbali.
Wakati hali za kiuchumi za watu zikia siyo nzuri sana watu huwa hawapendi kununua vitu vipya ovyoovyo, kwa mfano mtu anapotaka kufanya ujenzi mdogo tu badala ya kwenda kununua nyundo atachagua kwenda kuazima au kukodi ili kupunguza gharama. Hali ni hiyohiyo kwa vifaa na vyombo kama, maturubai, viti, vyombo vya shughuli kama za harusi, misiba, vifaa vya kufanyia kazi za ujenzi nk.

Biashara ya ufundi wa kurepea vitu(kukarabati vitu vilivyoharibika)
Mtu badala ya kutupa kiatu chake kilichochakaa au nguo, huamua kupeleka kwa fundi kuikarabati  tena upya.

Biashara ya huduma za afya.
Wakati huu unaposoma hapa ukiwa mzima wa afya, kuna  mtu fulani, mahali fulani ana tatizo la kiafya au anaumwa. Magonjwa na homa mbalimbali huwa hayajui kama kuna hali ngumu ya kiuchumi, huibuka siku yeyote. Kama wewe una rasilimali za kutosha, ujuzi, nguvukazi na mtaji unaweza ukaanzisha biashara yeyote inayohusiana na huduma za afya kama vile zahanati, hospitali, duka la kuuza dawa, huduma za matibabu kwa kutumia miti shamba, tiba lishe, ushauri wa kiafya, kuuza dawa za mimea, kuanzisha kituo cha mazoezi ya viungo(Gymn), kuanzisha blogu ya maswala yahusuyo afya, vyakula,  ushauri nk.

Biashara ya huduma za mazishi.
Pamoja na hali kuwa ngumu kipesa lakini haiwezi kuzuia watu kufa na baada ya msiba ndugu na jamaa haijalishi wana hali gani kiuchumi, watachangishana au kutumia mifuko mbalimbali ya kufa na kuzikana ili kukamilisha shughuli ya kumuaga na kumsetiri mpendwa wao.

……………………………………………………………….

Mpenzi msomaji wa blogu hii, tulikuwa na semina inayohusu namna ya kuandika mpango au mchanganuo wa biashara  kwa takribani miezi 3 iliyopita. Semina hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa mtindo wa masomo yaliyowekwa katika blogu maalumu ya kulipia kwa sasa imemalizika lakini masomo yake yote bado yataendelea kubakia katika hii BLOGU YA SEMINA YA MICHANGANUO.

Kwa mtu yeyote atakayependa kupata masomo yote ya semina hiyo kwa sasa anatakiwa kulipia kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, shilingi elfu 30 ikiwa ni kitabu cha kawaida cha karatasi au shilingi elfu 10 kama ni kitabu cha PDF kwa njia ya e-mail. Baada ya kununua kitabu atatupatia anuani yake ya email(GMAIL) kwa ajili ya kumuunganisha kwenye hii BLOGU YA MASOMO YA MICHANGANUO

Vitabu vyetu vingine vinapatikana, kile cha SIRI YA MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA pamoja na MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA. Ukivihitaji tembelea SMARTBOOKSTZ au tuwasiliane kwa namba za simu 0712 202244  au  0765 553030


4 Responses to "BIASHARA 1 NZURI INAYOLIPA TANZANIA UNAYOWEZA KUFANYA KIPINDI HIKI KIGUMU CHA FEDHA 2017"

  1. Nataka kuendeleza biashara yangu ya kilimo hasa katika kipindi hiki cha mdororo wa kiuchumi.0754397743

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ndugu Alex, kilimo hasa kile cha kibiashara nyakati kama hizi ambazo mzunguko wa fedha umekuwa mdogo kinaweza kuwa mkombozi kutokana na sababu kwamba binadamu ni vigumu mno kuishi pasipo kupata mlo. Chagua zao lenye soko kubwa na lisiloharibika katika muda mfupi baada ya kuvunwa au kama huharibika upesi mfano matunda bai chagua lile lililokuwa na uhitaji mkubwa kisha hakikisha unatafiti vyema soko lake.

      Delete
  2. Mimi ni kijana wa miaka 19 lakini ninapenda sana niwe na maendeleo na pia napenda sana kujihusisha na mambo ya kilimo ila bado sijapata mtaji je nifanye nini kwani napenda sana mafanikio na nachukia umasikini na kuwa tegemezi kwa mtu...

    ReplyDelete
    Replies
    1. Vizuri Bernard, katika umri mdogo kama huo wako kuwa na malengo na maono ya kufika mbali kama hayo bado upo katika mstari mzuri kabisa. Sijajua kama bado upo masomoni au umeshamaliza, lakini ikiwa husomi basi huu ndio wakati wako muafaka wa kuanzisha kitu. Usiweke suala la mtaji mbele kupita kiasi, anzisha kitu kwanza.

      Kwa kesi ya kilimo kama tayari unalo shamba anza kulima kidogo ili utakapomfuata mtu au taasisi ya mkopo waamini kweli unahitaji mtaji wa kupanua kilimo ulichokusudia kikutoe

      Unaweza pia ukatafuta shughuli ya kukuingizia kipato kidogo kama ajira au kibarua au biashara ndogo, halafu baada ya kupata fedha kiasi fulani ndipo ukaenda kuwekeza katika kilimo. Cha msingi kuwa mvumilivu.

      Delete