Katika makala hii nitaelezea vitu
kwa namna tofauti kidogo na makala nyingi ninazoweka katika hii blogu, sawasawa
na jinsi nilivyofanya tena katika makala nyingine moja niliyowahi
kuandika isemayo, Biasharaya duka inavyoweza kukutoa
kimaisha ukiwa mjanja.
Asilimia kubwa ya mada nilizoandika katika
makala hizi mbili ni vitu vinavyonigusa mimi binafsi moja kwa moja au kwa
maneno mengine tunaweza kusema nimeandika kutokana na uzoefu wangu mwenyewe
nilioupata kutokana na shughuli mbalimbali za ujasiriamali nilizowahi kuanzisha
katika maisha yangu tangu nikiwa mtoto nasoma shule ya msingi.
Nakumbuka wakati huo niliwahi kuanzisha biashara
ndogondogo kadhaa kwa mtaji mdogo sana niliokuwa nao, biashara kama vile ya
kuuza mafuta ya taa nyumbani muda wa jioni baada ya saa za masomo, kufuga
sungura, kuku na kilimo cha bustani za nyanya na mbogamboga kama mchicha.
Kumbuka binadamu hajifunzi kutokana na yale
mambo anayofanikiwa maishani tu peke yake, bali hata na yale anayo anguka pia
kuna mafunzo anayoyapata yanayokuja kumsaidia
mbele ya safari yake maishani.
Hivyo ndugu msomaji, nakushirikisha moja ya
mafunzo muhimu sana niliyoyapata pamoja
na uzoefu binafsi niliojikusanyia kwa
kipindi kirefu. Na ikiwa upo tayari kwa mafunzo hayo muhimu sana ya namna ya
kuanzisha biashara tangu sifuri(mwanzo) mpaka inafikia hatua yajuu ya mafanikio,
basi karibu sana tuendelee kujifunza pamoja.
Ukweli hakuna raha kama kuanzisha biashara
yako mwenyewe tokea mwanzo mpaka inafanikiwa, huweza kumfanya mtu kupata
ridhiko la kweli moyoni, unapoweza kuushinda mtihani huo, basi ujue, hata mtu
akuahidi kazi nzuri namna gani, utamwambia, “niache” na hautakata tamaa tena ya
kufanya ujasiriamali mpaka kufa kwako.
Usikatishwe tamaa na takwimu kwamba, asilimia
zaidi ya 70% ya biashara zote mpya zinazoanzishwa hufa kabla ya kutimiza mwaka
wake wa kwanza, bali weka nguvu, nia na mipango thabiti pale unapoanza. Kama alivyowahi
kusema mfanyabisahara na mjasiriamali wa Kimarekani, James Cash Penney kuwa “
Mara nyingi mwanzo ndio unaohitaji nguvu nyingi zaidi”- James Cash. Tengeneza
mpango wa biashara yako hata kama ikiwa siyo mpango rasmi ni wa kichwani tu
itakusaidia zaidi.
Jinsi
ya kuanzisha biashara tokea mwanzo(sifuri) hadi hatua ya juu kabisa ya
mafanikio: Mafunzo matano 5 muhimu kutokana na uzoefu wangu binafsi wa biashara
kwa muda mrefu.
FUNZO
LA KWANZA 1
Njia
rahisi na ya haraka ya kufanikiwa katika biashara yeyote ile mpya unayoianzisha
ni kuanguka kwanza.
Unaweza ukaniona mimi kuwa ni mtu wa ajabu
lakini ndugu yangu hivyo ndivyo mambo yalivyo popote pale. Nafahamu kabisa
kwamba hupendi kufeli, na siyo wewe mwenyewe tu bali kila mtu duniani hapendi
kuona biashara yake aliyoianzisha kwa tabu ikianguka ama kuzorota na nadhani hata
hii ndiyo sababu kubwa ni kwanini baadhi ya watu huwa hawapendi kuanzisha
biashara tokea chini kabisa wakihofia kuanguka. Wapo radhi hata kununua
biashara iliyokwisha anzishwa na mtu mwingine na kuonyesha dalili za mafanikio
kuliko waanzishe biashara mpya.
SOMA: Eepusha kufa au kuanguka kwa biashara yako, kwa kufanya mambo haya 9
SOMA: Eepusha kufa au kuanguka kwa biashara yako, kwa kufanya mambo haya 9
“Mafanikio siyo mwalimu mzuri.Tunapoanguka
tunajifunza mengi kuhusiana na sisi wenyewe, hivyo usiogope kuanguka. Kufeli ni
sehemu ya mchakato wa mafanikio”-Robert Kiyosaki
Kuwa na biashara yenye mafanikio, mtu ni lazima uwe tayari na kukubali maanguko,
unapoanguka chini, mara moja okota mafunzo uliyoyapata na kisha uinuke
kuendelea tena na safari yako. Duniani hajawahi kutokea mjasiriamali hata mmoja
ambaye alifanikiwa hivihivi tu pasipokuanguka hata mara moja.
Mimi binafsi ni mmoja wa wale walioanguka
mara nyingi, sijakata tamaa bado na ninaendeleza mapambano nikijua kabisa
kwamba siko peke yangu, ni wengi kama siyo kila mtu duniani anapaswa kupitia
milima na mabonde kabla hajafanikiwa.
Tukiangalia mfano mwingine, Thomas Edison,
mgunduzi mkubwa na mjasiriamali wa wakati wote(huwezi ukataja ugunduzi wa simu unayotumia leo hii pasipo kumhusisha
yeye) alifeli mara elfu kumi(10,000) ndipo hatimaye akaja kugundua taa ya
umeme ya balbu wewe na mimi tunayotumia leo hii pale jikoni au sebuleni nyakati
za usiku.
Lakini yeye mwenyewe Edisoni alitamka maneno
haya, “Sijafeli, bali nimegundua njia elfu kumi ambazo hazifanyi kazi”-Thomas Edison.
Kwa mantiki hiyo basi, tunaweza tukaema
kwamba, maanguo katika biashara siyo mabaya kwa kiasi kile ambacho watu
tumekuwa tukiyatazama. Katika dunia ya biashara na uwekezaji ni lazima tukubali
kwamba tunaweza tukajifunza mambo mengi zaidi kutokana na kuanguka kuliko tavyoweza
kujifunza kutokana na kufanikiwa.
Habari za mafaikio tu peke yake huweza kuwavutia
zaidi wapumbavu na wale wavivu, na pindi wanapoingia kwenye biashara au
uwekezaji kichwakichwa hujikuta
wakianguka vibaya. Kubali kuanguka na kila mtu huanguka katika jambo fulani kwa
wakati fuani maishani mwake, lakini kamwe usije ukakubali kutokujaribu.
Haijalishi utafeli mara ngapi, lakini uzoefu
utakaoupata kutokana na kuanguka huko una thamani kubwa. Kama mgunduzi Thomas
Edison, hauwezi ukajua ni kitu gani kinachofanya kazi au ni kipi kisichofanya
kazi ikiwa hautafeli, wala huwezi kufahamu udhaifu wako na nguvu zako ni zipi.
Haujashindwa mpaka wewe mwenyewe umeamua
kukubali kwamba umeshindwa, umejisalimisha huku mikono ikia juu kama mwanajeshi
vitani aliyeamua kujisalimisha kwa adui.
Kwa kila anguko utakalokutana nalo, kuna njia
mbadala ya kutokea, ni lazima uitafute njia hiyo. Hata gari linapokutana na
kizuizi barabarani, dereva hujitahidi kutafuta njia ya mchepuko ili kukikwepa
hicho kizuizi kusudi safari iendelee kama kawaida.
Kuanguka katika biashara. |
FUNZO
LA PILI 2
Kuianzisha
biashara na kuiendeleza ni mchakato wa muda mrefu, hakuna mafanikio ya miujiza.
Mpendwa msomaji wangu, sina lengo la
kukukatisha tamaa, hata daktari anapokutibia malaria angelisema asikupe quinine
au chloroquine kwa kuwa eti ni chungu utatapika, sidhani kama ungepona, ni
wengi tungekuwa tumeshakufa kitambo, asante sana madokta kwa kutokuwa na huruma
hata kidogo kwa hilo.
Niliwahi tena kuandika makala iliyosema, “Hakunautajiri wa miujiza kwenye mitandao, fanya kazi” miaka kadhaa iliyopita
nikisisitiza jambo hili kwa vijana ambao kutwa kucha wao walikuwa wakichakura
kwenye mitandao ya kompyuta wakisaka taasisi au vyama walivyodhani vinagawa
utajiri kwa njia za kimiujiza.
“Katika mchezo wa ujasiriamali, mchakato
ni muhimu zaidi kuliko magoli(malengo), unapoanza kuijenga biashara unaianza
safari au mchakato, mchakato huu una mwanzo na mwisho na katikati ya mwanzo na
mwisho kuna changamoto nyingi. Utashinda ikiwa tu utabakia kuwa mwaminifu kwa
mchakato huo”- Rich Dad.
Hayo siyo maneno yangu bali ni ya mtaalamu wa biashara na mwandishi mashuhuri
wa Rich Dad Poor Dad, Robert Kiyosaki.
Zipo simulizi nyingi sana za kusisimua juu ya
kupata pesa za haraka haraka, kutajirika ndani ya muda mfupi, pesa za chapchap,
utajiri wa miujiza, pesa za majini, pesa za majoka nk. Stori hizo ukikaa
vijiweni ndipo unapoweza kuzisikia sana zikizungumzwa, kupata utajiri na pesa
nyingi kwa kupitia njia za mkato. Wengine hata hudai eti kuna wataalamu(waganga
wa jadi) waliokuwa na uwezo wa kukupa utajiri, ila sharti lake kubwa ni lazima
kwanza kuku alishwe punje za mahindi.
Inasadikiwa kwamba idadi ya punje za mahindi
kuku huyo atakazoamua kumeza basi na ujue ndiyo idadi ya miaka yako iliyosalia
hapa duniani. Inasemekana ikiwa hata kama kuku huyo ataamua kudonoa nusu punje
ya mhindi kisha akasita kuendelea kula, tambua fika una miezi sita 6 tu
iliyobakia ya wewe kuendelea kuishi hapa duniani.
Lakini wakati simulizi au hidhi hiyo
ikiendelea kijiweni, hebu mwambie huyo msimuliaji akupeleke au tu hata
akuelekeze aliko huyo mganga kusudi siku moja uende huko. Ataanza, Ooo…, sijui,
namimi niliambiwa na mtu kuwa mganga anapatikana huko iringa milimani….OO…na
Ooo.. oo.. kibao zisizokuwa na mwisho.
Kiuhalisia utakapoamua kumtafuta mtaalamu
kama huyo au Sangoma, huwezi kumpata kamwe, na hata kama utapelekwa, basi ujue
ni kwa matapeli watakaoenda kuishia kukutapeli hela zako kidogo zote ulizokuwa
nazo huku utajiri wenyewe ukiusika redioni.
Achana kabisa na upotofu kama huo, ukweli
ninaokuambia ndugu yangu ni huu hapa chini a uzingatie,
“HAKUNA MAFANIKIO YA MIUJIZA, ILI UFANIKIWE
NI LAZIMA UFANYE KAZI KWA JUHUDI NA MAARIFA. NJIA YA MKATO NDIYO NJIA NDEFU
ZAIDI YA KUFIKA KULE UENDAKO”-Peter Tarimo.
Kila mtu angependa kuwa kama, Said Salim
Bakhresa, Reginald Mengi, Mohamed Dewji(MO), Rostam Aziz, Bill Gates, Mark
Zuckerberg, Aliko Dangote na wengineo lakini ni wangapi kati yetu tupo tayari
kupitia michakato waliyopitia Mabilionea na Mamilionea hawa ?
SOMA: Je ungependa uwe kama Bakhresa, Mengi, Mo na Rostam aziz?
SOMA: Je ungependa uwe kama Bakhresa, Mengi, Mo na Rostam aziz?
Tukiwaondoa wachache kama vile Mark
Zuckerberg aliyefanikiwa kuwa tajiri ndani ya muda wa miaka mitano 5 tu,
wengine wote, mafanikio makubwa ya biashara zao yalionekana baada ya miaka kui
10 na kuendelea. Ujasiriamali unaweza ukalinganishwa na kazi ya udaktari wa
binadamu. Dokta ili aweze kuitwa dokta kweli anapitia mchakato mrefu na kazi
ngumu ya kujifunza na kusoma usiku na mchana. Na ujasiriamali ni hivyohivyo.
Achana kabisa na mafanikio ya miujiza ndipo
utakapokuwa katika nafasi nzuri ya kuelekea mafanikio. Kabla sijamalizia funzo
hili la pili, napenda nikukumbushe tu pia kwamba, biashara yeyote ile duniani,
huanzia na wazo kisha mipango ya mtu ndani ya akili yake
kabla hata hajaamua kuandika mahali au kumuelezea mtu mwingine. Haiwezekani tu
ukaanza biashara bila kupanga utakavyofanya biashara yenyewe.
Waswahili husema, “Usione vyaelea, vimeundwa” mtu unaweza ukaona biashara ya mtu
imefanikiwa ndani ya kipindi kifupi sana, lakini kumbe huelewi mtu huyo
ilimchukua muda gani kufanya maandalizi na mipango ya biashara yenyewe, pengine
ilimchukua miaka mitano au hata 10 huwezi kujua.
Hivyo jifunze kupanga, ingawa dhana hii
inaweza ikaonekana kukinzana na fundisho namba 3 tunalokwenda kulianza sasa
hivi lakini mipango haiwezi kukuzuia kuanza mara moja na tena itakusaidia kwani
siyo lazima mipango au bajeti yako iwe ni ya fedha halisi uliyokuwa nayo
mfukoni. Kuchanganua biashara kunakuwezsha kuijua biashara kwa kina zaidi kabla
hata haujaianza rasmi.
Kwa kuhitimisha fundisho hili la pili,
Wajasiriamali wote waliofanikiwa walipitia michakato tofauti na hata muda
walioutumia pia unatofautiana, hivyo ni juu yako na wewe kutambua kwamba
unatakiwa kuanza mchakato wako mwenyewe na siwezi pia kukutabiria kama itakuchukua
muda gani mpaka unafanikiwa.
FUNZO
LA TATU 3
Wakati
muafaka wa kuanza biashara hautakaa utokee, ukisubiri taa zote ziwake kijani
utakesha kwenye mataa.
Ukisubiri ukamilishe kila kitu ndipo uweze kuanzisha
biashara, kamwe hautakaa ufanye biashara maisha yako yote. Jambo hili nina
ushuhuda nalo mimi binafsi katika biashara hii ya kuuza vitabu na kutoa ushauri
wa kibiashara kwa watu mbalimbali. Nimewahi kuwauzia watu wengi vitabu vyangu
kikiwemo kitabu cha Michanganuo ya
Biashara na Ujasiriamali, Siri ya
mafanikio ya biashara ya duka na kile cha Mifereji 7 ya pesa.
Kuna wateja wengine hata baada ya kuwatumia
vitabu mikoani waliko waliamua kufunga safari ya kuja Dar es salaam tuonane ili
niweze kuwapa ushauri wa kina zaidi. Hawakuamini kama kile nilichoandika kwenye
vitabu peke yake kingetosha kuwasaidia katika safari yao ya ujasiriamali.
Katika vitabu vyangu karibu vyote kuna kitu kimoja au tuseme mtindo nilioutumia
kuandika ambao kama umewahi kuvisoma basi unaweza ukagundua. haijalishi utasoma
kurasa ngapi, tayari unakuwa umeshaanza kupata ile ‘spirit’(hamasa ya kuanza
kufanya biashara)
Nashukuru kwani naweza kusema kwamba asilimia
kubwa ya mirejesho ya wateja niliowahi kuwauzia vitabu vyangu wamefanikiwa,
Siyo siku nyingi alikuja kijana mmoja akapaki bajaji yake ya kubebea mizigo
mbele ya ofisi yangu, ilikuwa imesheheni vitu mbalimbalii vya kwenda kuuza
gengeni na dukani.
Nilimfahamu kwa mara ya kwanza alipofika tena
ofisini kwangu miaka 2 iliyopita begani
akiwa ameshika furushi la vitu vya kuuza gengeni kwake akataka nimuuzie vitabu
vya ujasiriamali. Kwa kweli alinishangaza kwani kijana muuza genge kununua vitabu vyote
3 vya shilingi elfu 34 halikuwa jambo la kawaida. Mara hii ya pili baada ya
kumkaribisha akaniambia hivi, “Brother hujatoa tena vitabu vya aina
nyingine, kwa kweli vile vimekuwa msaada mkubwa sana kwangu”
Kwa miaka hiyo 2 aliweza kutanua biashara
yake kutoka genge mpaka kuwa duka kamili huku genge likiendelea kuwa pembeni,
akanunua na hiyo bajaji ya mizigo achilia mbali mafanikio mengine ambayo
pengine sikufanikiwa kuyajua. Kijana huyu ni mmoja kati ya wengi wanaonipa
mrejesho chanya kwa mafunzo mazuri wanayoyapata katika vitabu na blogu hii.
SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?
SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?
Lakini katika upande mwingine wa shilingi
kuna baadhi ya wateja ambao sasa ndio nilitaka kuwazungumzia ambao wao hata
ninapokutana nao hawana furaha na ninapojaribu kuwauliza maendeleo yao
kibiashara hunipa majibu ya kukatisha tamaa, huniambia mpaka sasa hawajaanzisha
chochote na hata biashara yenyewe bado kutokana na sababu mbalimbali, kuna
wanaosema mazingira ya kuanza bado hayajakaa vizuri, huku wengine wakidai
wanasubiri muda muafaka ndipo waweze kuanza. Lakini mara zote mimi huwauliza,
ni lini muda huo muafaka utakapofika?
Dhana ya kuanzisha biashara yenye mafanikio
nimeielezea kwa njia nyepesi sana katika kitabu, KANUNI YA KUJIFUNZA ELIMU YA
PESA NA MAFANIKIO, kitabu hiki kinapatikana bure kwa msomaji yeyote wa blogu
hii ingawa baadaye kitaanza kuuzwa. Ili mtu ufanikiwe katika biashara,
hauhitaji maneno maneno mengi sana, wala stori au porojo nyingi zisizokuwa na
manufaa. Ni vitu vichache mno unavyotakiwa uwe navyo au uvijue ndipo uweze
kufanikiwa (Tafadhali jipatie kitabu hicho bure hapa kama ulikuwa bado hujakisoma)
Ukishindwa kanuni hii ya kuanzisha biashara
hata kama hauna kila kitu unachohitaji, nakushauri wala usije ukajisumbua bure
kununua vitabu lukuki, havitakusaidia na mwisho wa siku utajikuta haujaanza kitu
chochote. Wewe anza na chochote kile ulichokuwa nacho mkononi vingine vitakuja
vyenyewe mbele ya safari. Kumbuka kuna vitu vitatu, wazo, timu ya watu na mtaji. Usije ukasubiri kuwa navyo vyote
vitatu ndipo uanze biashara, hata kama unacho kimoja tu wewe anza. Njia pekee
ya kuweza kuanza ni kuachana na maneno matupu(kuongeaongea) na kuanza kutenda
vitendo halisi. Unatakiwa utekeleze kwa vitendo na tenda sasa wakati ndio huu.
FUNZO
LA NNE 4
Usiweke
mategemeo yako kwenye mambo mazuri tu, jiandae na mabaya pia.
Kibinadamu tulivyoumbwa sisi ni watu wa
kusali na kuomba tupate mambo mema tu, tunasahau kwamba pia kuna mikosi, bahati
mbaya na matatizo mengi yanayoambatana na neema hizo. Na hivyo ndivyo ilivyo
hata katika ujasiriamali, tegemea mambo mazuri, faida na kila kitu lakini pia
usisahau kujiandaa na hasara na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Mafanikio katika ujasiriamali ni kama ua zuri la waridi ambalo ili ulipate
basi hauna budi kwanza uchomwe na miiba ya mti wenyewe wa waridi. Unapoanzisha
biashara ni lazima uelewe kuna uwezekano wa kuanguka au kufanikiwa nusu kwa
nusu.
Sababu kubwa ya kukushauri ujiandae kuanguka
ni kwamba, ikiwa itatokea kweli ukaanguka, basi kuanguka kwako hautakuchukulia
kama balaa kwani ulishajiandaa tayari, utainuka na kuanza tena safari. Ikiwa
utachukulia kuanguka huko kama janga, basi na huo ndio utakaokuwa mwisho wako
wa kufanya ujasiriamali na kwenda kutafuta ajira.
Na njia bora ya kujiandaa na mabaya ni kwa
wewe kuwa na njia mbadala(Plan B). Jiulize, “Hivi kama mradi huu hautafanikiwa
nitafanyaje? , je nitaachana nao?, nitaanzisha mradi mwingine?, nitabadilisha
mikakati ya mwanzo?.
Kuingia kwenye biashara ni kama vile kuingia
kwenye msitu mnene usiojua njiani utakutana na kitu gani, hivyo ni bora
ukajiandaa mapema kabla ya safari kwa kutengeneza mpango wa biashara au dira
hata ikiwa mpango wenyewe utauweka akilini tu.
SOMA: Sababu 5 kwanini uandike mpango wa biashara yako.
SOMA: Sababu 5 kwanini uandike mpango wa biashara yako.
Kuanzisha biashara toka mwanzoni kabisa mpaka
juu kileleni siyo mchezo! Kuna nyakati utatakiwa kujinyima usingizi ili
kukamilisha majukumu ya biashara. Utahitajika kujitolea chochote kile
ulichokuwa nacho kusudi uweze kupenya kipindi kigumu cha mwanzo. Wengine kama
kina Bill Gates, Steve Jobs na wengineo walidiriki hata kutoa sadaka elimu yao
kusudi tu waweze kufanikisha biashara zao. Mchakato wote huo ulivyokuwa mgumu
kama wewe ni mtu mwenye roho nyepesi utajikuta ukiachana na biashara.
FUNZO
LA TANO 5
Mafanikio
yako au kuanguka kwako katika biashara vyote 2 vinamtegemea mtu mmoja tu ambaye
ni WEWE.
Funzo la 5 na la mwisho ambalo pia ni kama
ushauri kwa wale wanaotarajia kuanzisha biashara au kwa waliokuwa katika
biashara tayari ni kwamba, hata uwe na kila kitu kama mtaji wa kutosha, timu
nzuri sana ya wasaidizi, wazo bora kabisa la biashara na mpango mzuri, lakini
ikiwa hautakuwa na mtazamo sahihi wa akili, maana yake kuwa na utayari mzuri wa
akili, kushikilia ndoto zako hata ikiwa utakutana na vikwazo vigumu namna gani
hautaweza kufanikiwa.
Mwisho kabisa nakusihi, tegemea changamoto
nyingi kabla haujafanikisha safari yako ya ujasiriamali, kitu cha msingi ni
hiki hapa, “USIOGOPE KUANGUKA, BALI
OGOPA SANA KUKATA TAMAA. Hatma ya maisha yao unayo wewe mwenywe, ziamini
ndoto zako na kuhakikisha unapigana kufa na ukupona kusudi siku moja ndoto hizo
zije kuwa kweli.”
……………………………………………………………….
Mpenzi msomaji wa blogu hii ya
jifunzeujasiriamali, huu ndio wakati mzuri kabisa wa wewe kutumia muda wako
wa thamani kujifunza kitu bora
kilichokuwa na manufaa makubwa kwako, siyo muda tu peke yake, angalia pia na
thamani ya pesa yako, ugumu uliopitia kuipata haiingii akilini kabisa wewe
kuitumia kwa kitu kisichoongeza thamani katika maish yako.
Linapokuja suala la kujifunza mbinu
mbalimbali za biashara na ujasiriamali, kwanini usiokoe muda na pesa zako kwa
kupata kila kitu hapa? Kitabu cha MICHANGANUO
YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, ndani yake kina kila kitu mjasiriamali yeyote
anachohitaji ili kufanya biashara yenye mafanikio.
Kina kozi zote muhimu za kuanzisha na kuendeleza biashara, namna ya kuandika mchanganuo wa biashara pamoja na michanganuo/mipango halisi ya biashara mbalimbali unayoweza kuitumia kama kielelezo au kukuhamasisha. Bei ya kitabu hiki ni sh. 20,000/= kwa kitabu cha kawaida cha karatasi. Softcopy kwa njia ya email ni sh. 10,000/=
Kina kozi zote muhimu za kuanzisha na kuendeleza biashara, namna ya kuandika mchanganuo wa biashara pamoja na michanganuo/mipango halisi ya biashara mbalimbali unayoweza kuitumia kama kielelezo au kukuhamasisha. Bei ya kitabu hiki ni sh. 20,000/= kwa kitabu cha kawaida cha karatasi. Softcopy kwa njia ya email ni sh. 10,000/=
Kama utapenda pia tuna vitabu vingine kama
vile, cha BIASHARA YA REJAREJA, na kingine kiitwacho MIFEREJI 7 YA PESA. Kwa maelezo zaidi kuhusu vitabu vyote tembelea, SMARTBOOKSTZ
Tuna Masomo ya Semina juu ya Michanganuo ya biashara
pia yanayotolewa kwa mtindo wa blogu ya kulipia ambapo ni shilingi elfu 10 tu
kuunganishwa na semina hiyo, bonyeza link hiyo kuingia kwenye blogu kama umeshalipia.
Vitabu hivi vyote vinapatikana katika ofisi
yetu iliyopo MBEZI KWA MSUGURI,
jirani kabisa na stendi ya daladala.
Kwa watu wa mikoani tunawashauri waagizie
watu wanaokuja Dar es salaam, au njia nyingine tunaweza pia kuwatumia kupitia
mabasi ila gharama za usafiri zitaongezeka.
Tunazo pia softcopy za vitabu hivyo vyote kwa
yeyote anayependa kuvisoma kupitia e-mail yake. Tuma pesa na email tutakutumia.
Namba zetu za simu ni, 0712 202244 au 0765 553030
jina Peter Augustino Tarimo
0 Response to "MAFUNZO MATANO (5) YA JINSI YA KUANZISHA BIASHARA TOKA MWANZO MPAKA MAFANIKIO"
Post a Comment