MAFUNZO MATANO (5) YA JINSI YA KUANZISHA BIASHARA TOKA MWANZO MPAKA MAFANIKIO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAFUNZO MATANO (5) YA JINSI YA KUANZISHA BIASHARA TOKA MWANZO MPAKA MAFANIKIO

Katika makala hii nitaelezea vitu kwa namna tofauti kidogo na makala nyingi ninazoweka katika hii blogu, sawasawa na jinsi nilivyofanya  tena katika makala nyingine moja niliyowahi kuandika isemayo, Biasharaya duka inavyoweza kukutoa kimaisha ukiwa mjanja.

Asilimia kubwa ya mada nilizoandika katika makala hizi mbili ni vitu vinavyonigusa mimi binafsi moja kwa moja au kwa maneno mengine tunaweza kusema nimeandika kutokana na uzoefu wangu mwenyewe nilioupata kutokana na shughuli mbalimbali za ujasiriamali nilizowahi kuanzisha katika maisha yangu tangu nikiwa mtoto nasoma shule ya msingi.

Nakumbuka wakati huo niliwahi kuanzisha biashara ndogondogo kadhaa kwa mtaji mdogo sana niliokuwa nao, biashara kama vile ya kuuza mafuta ya taa nyumbani muda wa jioni baada ya saa za masomo, kufuga sungura, kuku na kilimo cha bustani za nyanya na mbogamboga kama mchicha.

Kumbuka binadamu hajifunzi kutokana na yale mambo anayofanikiwa maishani tu peke yake, bali hata na yale anayo anguka pia kuna mafunzo anayoyapata yanayokuja kumsaidia  mbele ya safari yake maishani.

Hivyo ndugu msomaji, nakushirikisha moja ya mafunzo muhimu sana  niliyoyapata pamoja na uzoefu binafsi niliojikusanyia  kwa kipindi kirefu. Na ikiwa upo tayari kwa mafunzo hayo muhimu sana ya namna ya kuanzisha biashara tangu sifuri(mwanzo) mpaka inafikia hatua yajuu ya mafanikio, basi karibu sana tuendelee kujifunza pamoja.

Ukweli hakuna raha kama kuanzisha biashara yako mwenyewe tokea mwanzo mpaka inafanikiwa, huweza kumfanya mtu kupata ridhiko la kweli moyoni, unapoweza kuushinda mtihani huo, basi ujue, hata mtu akuahidi kazi nzuri namna gani, utamwambia, “niache” na hautakata tamaa tena ya kufanya ujasiriamali mpaka kufa kwako.

Usikatishwe tamaa na takwimu kwamba, asilimia zaidi ya 70% ya biashara zote mpya zinazoanzishwa hufa kabla ya kutimiza mwaka wake wa kwanza, bali weka nguvu, nia na mipango thabiti pale unapoanza. Kama alivyowahi kusema mfanyabisahara na mjasiriamali wa Kimarekani, James Cash Penney kuwa “ Mara nyingi mwanzo ndio unaohitaji nguvu nyingi zaidi”- James Cash. Tengeneza mpango wa biashara yako hata kama ikiwa siyo mpango rasmi ni wa kichwani tu itakusaidia zaidi.

Jinsi ya kuanzisha biashara tokea mwanzo(sifuri) hadi hatua ya juu kabisa ya mafanikio: Mafunzo matano 5 muhimu kutokana na uzoefu wangu binafsi wa biashara kwa muda mrefu.

FUNZO LA KWANZA 1
Njia rahisi na ya haraka ya kufanikiwa katika biashara yeyote ile mpya unayoianzisha ni kuanguka kwanza.

Unaweza ukaniona mimi kuwa ni mtu wa ajabu lakini ndugu yangu hivyo ndivyo mambo yalivyo popote pale. Nafahamu kabisa kwamba hupendi kufeli, na siyo wewe mwenyewe tu bali kila mtu duniani hapendi kuona biashara yake aliyoianzisha kwa tabu ikianguka ama kuzorota na nadhani hata hii ndiyo sababu kubwa ni kwanini baadhi ya watu huwa hawapendi kuanzisha biashara tokea chini kabisa wakihofia kuanguka. Wapo radhi hata kununua biashara iliyokwisha anzishwa na mtu mwingine na kuonyesha dalili za mafanikio kuliko waanzishe biashara mpya.

SOMA: Eepusha kufa au kuanguka kwa biashara yako, kwa kufanya mambo haya 9

“Mafanikio siyo mwalimu mzuri.Tunapoanguka tunajifunza mengi kuhusiana na sisi wenyewe, hivyo usiogope kuanguka. Kufeli ni sehemu ya mchakato wa mafanikio”-Robert Kiyosaki

Kuwa na biashara yenye mafanikio,  mtu ni lazima uwe tayari na kukubali maanguko, unapoanguka chini, mara moja okota mafunzo uliyoyapata na kisha uinuke kuendelea tena na safari yako. Duniani hajawahi kutokea mjasiriamali hata mmoja ambaye alifanikiwa hivihivi tu pasipokuanguka hata mara moja.

Mimi binafsi ni mmoja wa wale walioanguka mara nyingi, sijakata tamaa bado na ninaendeleza mapambano nikijua kabisa kwamba siko peke yangu, ni wengi kama siyo kila mtu duniani anapaswa kupitia milima na mabonde kabla hajafanikiwa.

Tukiangalia mfano mwingine, Thomas Edison, mgunduzi mkubwa na mjasiriamali wa wakati wote(huwezi ukataja ugunduzi wa simu unayotumia leo hii pasipo kumhusisha yeye) alifeli mara elfu kumi(10,000) ndipo hatimaye akaja kugundua taa ya umeme ya balbu wewe na mimi tunayotumia leo hii pale jikoni au sebuleni nyakati za usiku.

Lakini yeye mwenyewe Edisoni alitamka maneno haya, “Sijafeli, bali nimegundua njia elfu kumi ambazo hazifanyi kazi”-Thomas Edison.
Thomas Edison, mgunduzi wa taa(balbu ya umeme) alifeli mara elfu moja

Hebu jaribu kufikiria watu wote mashuhuri duniani waliofanikiwa katika nyakati tofati wakiwemo hata na wa hapa kwetu Tanzania, fuatilia historiazao vizuri, ni lazima utakuta kuna mahali walikutana na anguko na siyo mara moja, ni mara mbili, tatu au zaidi ya hapo.

Kwa mantiki hiyo basi, tunaweza tukaema kwamba, maanguo katika biashara siyo mabaya kwa kiasi kile ambacho watu tumekuwa tukiyatazama. Katika dunia ya biashara na uwekezaji ni lazima tukubali kwamba tunaweza tukajifunza mambo mengi zaidi  kutokana na kuanguka kuliko tavyoweza kujifunza kutokana na kufanikiwa.

Habari za mafaikio tu peke yake huweza kuwavutia zaidi wapumbavu na wale wavivu, na pindi wanapoingia kwenye biashara au uwekezaji kichwakichwa  hujikuta wakianguka vibaya. Kubali kuanguka na kila mtu huanguka katika jambo fulani kwa wakati fuani maishani mwake, lakini kamwe usije ukakubali kutokujaribu.

Haijalishi utafeli mara ngapi, lakini uzoefu utakaoupata kutokana na kuanguka huko una thamani kubwa. Kama mgunduzi Thomas Edison, hauwezi ukajua ni kitu gani kinachofanya kazi au ni kipi kisichofanya kazi ikiwa hautafeli, wala huwezi kufahamu udhaifu wako na nguvu zako ni zipi.

Haujashindwa mpaka wewe mwenyewe umeamua kukubali kwamba umeshindwa, umejisalimisha huku mikono ikia juu kama mwanajeshi vitani aliyeamua kujisalimisha kwa adui.

Kwa kila anguko utakalokutana nalo, kuna njia mbadala ya kutokea, ni lazima uitafute njia hiyo. Hata gari linapokutana na kizuizi barabarani, dereva hujitahidi kutafuta njia ya mchepuko ili kukikwepa hicho kizuizi kusudi safari iendelee kama kawaida.

mafnikio na maanguko katika biashara vyote vina nafasi sawa asilimia 50% kwa 50%
Kuanguka katika biashara.
Nadhani mpaka hapo funzo langu la kwanza limekufungua macho kutambua umuhimu wa kuanguka katika mchakato mzima wa mafanikio ya biashara. Kukubali maanguko ndani ya mchakato wa kujifunza ndiyo njia sahihi kila aliyewahi kufanikiwa katika biashara aliyopitia. Shida ipo tu ni kwa namna gani unayakubali hayo maanguko, lakini bila shaka nadhani utakuwa umeshajifunza namna ya kuyapokea maanguko au kufeli ndani ya funzo hili la kwanza.

FUNZO LA PILI 2
Kuianzisha biashara na kuiendeleza ni mchakato wa muda mrefu, hakuna mafanikio ya miujiza.

Mpendwa msomaji wangu, sina lengo la kukukatisha tamaa, hata daktari anapokutibia malaria angelisema asikupe quinine au chloroquine kwa kuwa eti ni chungu utatapika, sidhani kama ungepona, ni wengi tungekuwa tumeshakufa kitambo, asante sana madokta kwa kutokuwa na huruma hata kidogo kwa hilo.

Niliwahi tena kuandika makala iliyosema, “Hakunautajiri wa miujiza kwenye mitandao, fanya kazi” miaka kadhaa iliyopita nikisisitiza jambo hili kwa vijana ambao kutwa kucha wao walikuwa wakichakura kwenye mitandao ya kompyuta wakisaka taasisi au vyama walivyodhani vinagawa utajiri kwa njia za kimiujiza.

“Katika mchezo wa ujasiriamali, mchakato ni muhimu zaidi kuliko magoli(malengo), unapoanza kuijenga biashara unaianza safari au mchakato, mchakato huu una mwanzo na mwisho na katikati ya mwanzo na mwisho kuna changamoto nyingi. Utashinda ikiwa tu utabakia kuwa mwaminifu kwa mchakato huo”- Rich Dad. Hayo siyo maneno yangu bali ni ya mtaalamu wa biashara na mwandishi mashuhuri wa Rich Dad Poor Dad, Robert Kiyosaki.

Zipo simulizi nyingi sana za kusisimua juu ya kupata pesa za haraka haraka, kutajirika ndani ya muda mfupi, pesa za chapchap, utajiri wa miujiza, pesa za majini, pesa za majoka nk. Stori hizo ukikaa vijiweni ndipo unapoweza kuzisikia sana zikizungumzwa, kupata utajiri na pesa nyingi kwa kupitia njia za mkato. Wengine hata hudai eti kuna wataalamu(waganga wa jadi) waliokuwa na uwezo wa kukupa utajiri, ila sharti lake kubwa ni lazima kwanza kuku alishwe punje za mahindi.

Inasadikiwa kwamba idadi ya punje za mahindi kuku huyo atakazoamua kumeza basi na ujue ndiyo idadi ya miaka yako iliyosalia hapa duniani. Inasemekana ikiwa hata kama kuku huyo ataamua kudonoa nusu punje ya mhindi kisha akasita kuendelea kula, tambua fika una miezi sita 6 tu iliyobakia ya wewe kuendelea kuishi hapa duniani.




Lakini wakati simulizi au hidhi hiyo ikiendelea kijiweni, hebu mwambie huyo msimuliaji akupeleke au tu hata akuelekeze aliko huyo mganga kusudi siku moja uende huko. Ataanza, Ooo…, sijui, namimi niliambiwa na mtu kuwa mganga anapatikana huko iringa milimani….OO…na Ooo.. oo.. kibao zisizokuwa na mwisho.

Kiuhalisia utakapoamua kumtafuta mtaalamu kama huyo au Sangoma, huwezi kumpata kamwe, na hata kama utapelekwa, basi ujue ni kwa matapeli watakaoenda kuishia kukutapeli hela zako kidogo zote ulizokuwa nazo huku utajiri wenyewe ukiusika redioni.

Achana kabisa na upotofu kama huo, ukweli ninaokuambia ndugu yangu ni huu hapa chini a uzingatie,

“HAKUNA MAFANIKIO YA MIUJIZA, ILI UFANIKIWE NI LAZIMA UFANYE KAZI KWA JUHUDI NA MAARIFA. NJIA YA MKATO NDIYO NJIA NDEFU ZAIDI YA KUFIKA KULE UENDAKO”-Peter Tarimo.    

Kila mtu angependa kuwa kama, Said Salim Bakhresa, Reginald Mengi, Mohamed Dewji(MO), Rostam Aziz, Bill Gates, Mark Zuckerberg, Aliko Dangote na wengineo lakini ni wangapi kati yetu tupo tayari kupitia michakato waliyopitia Mabilionea na Mamilionea hawa ?

SOMA: Je ungependa uwe kama Bakhresa, Mengi, Mo na Rostam aziz?

Tukiwaondoa wachache kama vile Mark Zuckerberg aliyefanikiwa kuwa tajiri ndani ya muda wa miaka mitano 5 tu, wengine wote, mafanikio makubwa ya biashara zao yalionekana baada ya miaka kui 10 na kuendelea. Ujasiriamali unaweza ukalinganishwa na kazi ya udaktari wa binadamu. Dokta ili aweze kuitwa dokta kweli anapitia mchakato mrefu na kazi ngumu ya kujifunza na kusoma usiku na mchana. Na ujasiriamali ni hivyohivyo.

Achana kabisa na mafanikio ya miujiza ndipo utakapokuwa katika nafasi nzuri ya kuelekea mafanikio. Kabla sijamalizia funzo hili la pili, napenda nikukumbushe tu pia kwamba, biashara yeyote ile duniani, huanzia na wazo kisha mipango ya mtu ndani ya akili yake kabla hata hajaamua kuandika mahali au kumuelezea mtu mwingine. Haiwezekani tu ukaanza biashara bila kupanga utakavyofanya biashara yenyewe.

Waswahili husema, “Usione vyaelea, vimeundwa” mtu unaweza ukaona biashara ya mtu imefanikiwa ndani ya kipindi kifupi sana, lakini kumbe huelewi mtu huyo ilimchukua muda gani kufanya maandalizi na mipango ya biashara yenyewe, pengine ilimchukua miaka mitano au hata 10 huwezi kujua.

Hivyo jifunze kupanga, ingawa dhana hii inaweza ikaonekana kukinzana na fundisho namba 3 tunalokwenda kulianza sasa hivi lakini mipango haiwezi kukuzuia kuanza mara moja na tena itakusaidia kwani siyo lazima mipango au bajeti yako iwe ni ya fedha halisi uliyokuwa nayo mfukoni. Kuchanganua biashara kunakuwezsha kuijua biashara kwa kina zaidi kabla hata haujaianza rasmi.

Kwa kuhitimisha fundisho hili la pili, Wajasiriamali wote waliofanikiwa walipitia michakato tofauti na hata muda walioutumia pia unatofautiana, hivyo ni juu yako na wewe kutambua kwamba unatakiwa kuanza mchakato wako mwenyewe na siwezi pia kukutabiria kama itakuchukua muda gani mpaka unafanikiwa.

FUNZO LA TATU 3
Wakati muafaka wa kuanza biashara hautakaa utokee, ukisubiri taa zote ziwake kijani utakesha kwenye mataa.

Ukisubiri ukamilishe kila kitu ndipo uweze kuanzisha biashara, kamwe hautakaa ufanye biashara maisha yako yote. Jambo hili nina ushuhuda nalo mimi binafsi katika biashara hii ya kuuza vitabu na kutoa ushauri wa kibiashara kwa watu mbalimbali. Nimewahi kuwauzia watu wengi vitabu vyangu kikiwemo kitabu cha Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali, Siri ya mafanikio ya biashara ya duka na kile cha Mifereji 7 ya pesa.

Kuna wateja wengine hata baada ya kuwatumia vitabu mikoani waliko waliamua kufunga safari ya kuja Dar es salaam tuonane ili niweze kuwapa ushauri wa kina zaidi. Hawakuamini kama kile nilichoandika kwenye vitabu peke yake kingetosha kuwasaidia katika safari yao ya ujasiriamali. Katika vitabu vyangu karibu vyote kuna kitu kimoja au tuseme mtindo nilioutumia kuandika ambao kama umewahi kuvisoma basi unaweza ukagundua. haijalishi utasoma kurasa ngapi, tayari unakuwa umeshaanza kupata ile ‘spirit’(hamasa ya kuanza kufanya biashara)

Nashukuru kwani naweza kusema kwamba asilimia kubwa ya mirejesho ya wateja niliowahi kuwauzia vitabu vyangu wamefanikiwa, Siyo siku nyingi alikuja kijana mmoja akapaki bajaji yake ya kubebea mizigo mbele ya ofisi yangu, ilikuwa imesheheni vitu mbalimbalii vya kwenda kuuza gengeni na dukani.

Nilimfahamu kwa mara ya kwanza alipofika tena ofisini kwangu  miaka 2 iliyopita begani akiwa ameshika furushi la vitu vya kuuza gengeni kwake akataka nimuuzie vitabu vya ujasiriamali. Kwa kweli alinishangaza  kwani kijana muuza genge kununua vitabu vyote 3 vya shilingi elfu 34 halikuwa jambo la kawaida. Mara hii ya pili baada ya kumkaribisha akaniambia hivi, “Brother hujatoa tena vitabu vya aina nyingine, kwa kweli vile vimekuwa msaada mkubwa sana kwangu”

Kwa miaka hiyo 2 aliweza kutanua biashara yake kutoka genge mpaka kuwa duka kamili huku genge likiendelea kuwa pembeni, akanunua na hiyo bajaji ya mizigo achilia mbali mafanikio mengine ambayo pengine sikufanikiwa kuyajua. Kijana huyu ni mmoja kati ya wengi wanaonipa mrejesho chanya kwa mafunzo mazuri wanayoyapata katika vitabu na blogu hii.

SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?

Lakini katika upande mwingine wa shilingi kuna baadhi ya wateja ambao sasa ndio nilitaka kuwazungumzia ambao wao hata ninapokutana nao hawana furaha na ninapojaribu kuwauliza maendeleo yao kibiashara hunipa majibu ya kukatisha tamaa, huniambia mpaka sasa hawajaanzisha chochote na hata biashara yenyewe bado kutokana na sababu mbalimbali, kuna wanaosema mazingira ya kuanza bado hayajakaa vizuri, huku wengine wakidai wanasubiri muda muafaka ndipo waweze kuanza. Lakini mara zote mimi huwauliza, ni lini muda huo muafaka utakapofika?

Dhana ya kuanzisha biashara yenye mafanikio nimeielezea kwa njia nyepesi sana katika kitabu, KANUNI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO, kitabu hiki kinapatikana bure kwa msomaji yeyote wa blogu hii ingawa baadaye kitaanza kuuzwa. Ili mtu ufanikiwe katika biashara, hauhitaji maneno maneno mengi sana, wala stori au porojo nyingi zisizokuwa na manufaa. Ni vitu vichache mno unavyotakiwa uwe navyo au uvijue ndipo uweze kufanikiwa (Tafadhali jipatie kitabu hicho bure hapa kama ulikuwa bado hujakisoma)

Ukishindwa kanuni hii ya kuanzisha biashara hata kama hauna kila kitu unachohitaji, nakushauri wala usije ukajisumbua bure kununua vitabu lukuki, havitakusaidia na mwisho wa siku utajikuta haujaanza kitu chochote. Wewe anza na chochote kile ulichokuwa nacho mkononi vingine vitakuja vyenyewe mbele ya safari. Kumbuka kuna vitu vitatu, wazo, timu ya watu na mtaji. Usije ukasubiri kuwa navyo vyote vitatu ndipo uanze biashara, hata kama unacho kimoja tu wewe anza. Njia pekee ya kuweza kuanza ni kuachana na maneno matupu(kuongeaongea) na kuanza kutenda vitendo halisi. Unatakiwa utekeleze kwa vitendo na tenda sasa wakati ndio huu.

FUNZO LA NNE 4
Usiweke mategemeo yako kwenye mambo mazuri tu, jiandae na mabaya pia.

Kibinadamu tulivyoumbwa sisi ni watu wa kusali na kuomba tupate mambo mema tu, tunasahau kwamba pia kuna mikosi, bahati mbaya na matatizo mengi yanayoambatana na neema hizo. Na hivyo ndivyo ilivyo hata katika ujasiriamali, tegemea mambo mazuri, faida na kila kitu lakini pia usisahau kujiandaa na hasara na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Mafanikio katika ujasiriamali ni kama ua zuri la waridi ambalo ili ulipate basi hauna budi kwanza uchomwe na miiba ya mti wenyewe wa waridi. Unapoanzisha biashara ni lazima uelewe kuna uwezekano wa kuanguka au kufanikiwa nusu kwa nusu.

Sababu kubwa ya kukushauri ujiandae kuanguka ni kwamba, ikiwa itatokea kweli ukaanguka, basi kuanguka kwako hautakuchukulia kama balaa kwani ulishajiandaa tayari, utainuka na kuanza tena safari. Ikiwa utachukulia kuanguka huko kama janga, basi na huo ndio utakaokuwa mwisho wako wa kufanya ujasiriamali na kwenda kutafuta ajira.

Na njia bora ya kujiandaa na mabaya ni kwa wewe kuwa na njia mbadala(Plan B). Jiulize, “Hivi kama mradi huu hautafanikiwa nitafanyaje? , je nitaachana nao?, nitaanzisha mradi mwingine?, nitabadilisha mikakati ya mwanzo?.

Kuingia kwenye biashara ni kama vile kuingia kwenye msitu mnene usiojua njiani utakutana na kitu gani, hivyo ni bora ukajiandaa mapema kabla ya safari kwa kutengeneza mpango wa biashara au dira hata ikiwa mpango wenyewe utauweka akilini tu.

SOMA: Sababu 5 kwanini uandike mpango wa biashara yako.

Kuanzisha biashara toka mwanzoni kabisa mpaka juu kileleni siyo mchezo! Kuna nyakati utatakiwa kujinyima usingizi ili kukamilisha majukumu ya biashara. Utahitajika kujitolea chochote kile ulichokuwa nacho kusudi uweze kupenya kipindi kigumu cha mwanzo. Wengine kama kina Bill Gates, Steve Jobs na wengineo walidiriki hata kutoa sadaka elimu yao kusudi tu waweze kufanikisha biashara zao. Mchakato wote huo ulivyokuwa mgumu kama wewe ni mtu mwenye roho nyepesi utajikuta ukiachana na biashara.

FUNZO LA TANO 5
Mafanikio yako au kuanguka kwako katika biashara vyote 2 vinamtegemea mtu mmoja tu ambaye ni WEWE.

Funzo la 5 na la mwisho ambalo pia ni kama ushauri kwa wale wanaotarajia kuanzisha biashara au kwa waliokuwa katika biashara tayari ni kwamba, hata uwe na kila kitu kama mtaji wa kutosha, timu nzuri sana ya wasaidizi, wazo bora kabisa la biashara na mpango mzuri, lakini ikiwa hautakuwa na mtazamo sahihi wa akili, maana yake kuwa na utayari mzuri wa akili, kushikilia ndoto zako hata ikiwa utakutana na vikwazo vigumu namna gani hautaweza kufanikiwa.

Mwisho kabisa nakusihi, tegemea changamoto nyingi kabla haujafanikisha safari yako ya ujasiriamali, kitu cha msingi ni hiki hapa, “USIOGOPE KUANGUKA, BALI OGOPA SANA KUKATA TAMAA. Hatma ya maisha yao unayo wewe mwenywe, ziamini ndoto zako na kuhakikisha unapigana kufa na ukupona kusudi siku moja ndoto hizo zije kuwa kweli.”


……………………………………………………………….

Mpenzi msomaji wa blogu hii ya jifunzeujasiriamali, huu ndio wakati mzuri kabisa wa wewe kutumia muda wako wa thamani  kujifunza kitu bora kilichokuwa na manufaa makubwa kwako, siyo muda tu peke yake, angalia pia na thamani ya pesa yako, ugumu uliopitia kuipata haiingii akilini kabisa wewe kuitumia kwa kitu kisichoongeza thamani katika maish yako.

Linapokuja suala la kujifunza mbinu mbalimbali za biashara na ujasiriamali, kwanini usiokoe muda na pesa zako kwa kupata kila kitu hapa? Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, ndani yake kina kila kitu mjasiriamali yeyote anachohitaji ili kufanya biashara yenye mafanikio. 
Kina kozi zote muhimu za kuanzisha na kuendeleza biashara, namna ya kuandika mchanganuo wa biashara pamoja na michanganuo/mipango halisi ya biashara mbalimbali unayoweza kuitumia kama kielelezo au kukuhamasisha. Bei ya kitabu hiki ni sh. 20,000/= kwa kitabu cha kawaida cha karatasi. Softcopy kwa njia ya email ni sh. 10,000/=

Kama utapenda pia tuna vitabu vingine kama vile, cha BIASHARA YA REJAREJA, na kingine kiitwacho    MIFEREJI 7 YA PESA. Kwa maelezo zaidi kuhusu vitabu vyote tembelea, SMARTBOOKSTZ

Tuna Masomo ya Semina juu ya Michanganuo ya biashara pia yanayotolewa kwa mtindo wa blogu ya kulipia ambapo ni shilingi elfu 10 tu kuunganishwa na semina hiyo, bonyeza link hiyo kuingia kwenye blogu kama umeshalipia.

Vitabu hivi vyote vinapatikana katika ofisi yetu iliyopo MBEZI KWA MSUGURI, jirani kabisa na stendi ya daladala.

Kwa watu wa mikoani tunawashauri waagizie watu wanaokuja Dar es salaam, au njia nyingine tunaweza pia kuwatumia kupitia mabasi ila gharama za usafiri zitaongezeka.

Tunazo pia softcopy za vitabu hivyo vyote kwa yeyote anayependa kuvisoma kupitia e-mail yake. Tuma pesa na email tutakutumia.

Namba zetu za simu ni, 0712 202244  au  0765 553030  jina Peter Augustino Tarimo


0 Response to "MAFUNZO MATANO (5) YA JINSI YA KUANZISHA BIASHARA TOKA MWANZO MPAKA MAFANIKIO"

Post a Comment