UNAPOAJIRI AU KUAJIRIWA, ZINGATIA UMUHIMU WA KUJUA NI NINI UNACHOTAKA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UNAPOAJIRI AU KUAJIRIWA, ZINGATIA UMUHIMU WA KUJUA NI NINI UNACHOTAKA


Katika ulimwengu wa kazi, ajira na biashara kitu hiki makubaliano ni swala nyeti sana. Na makubaliano au mkataba hutumika katika kila nyanja ya ujasiriamali na biashara duniani kama ilivyoonyeshwa pia katika makala nyingine ya hivi karibuni iliyosema, jinsi ya kuuza wazo lako la biashara au ubunifu kwa wawekezaji na watu wengine.


Kwa kifupi kabisa makubaliano yana maanisha mapatano baina ya pande mbili tofauti kila upande ukiwa na matakwa yake(Malengo). Na katika makubaliano hayo kila upande kabla haujaja mezani inatakiwa kwanza kujiandaa kwa kujua ni vitu au malengo gani unaoyahitaji. Mfano mzuri sana ni pale mtu anapokwenda kuomba ajira.

Wote mwajiri na mwajiriwa kila mmoja anamhitaji mwenzake na huo ndiyo msingi hasa wa kusema kwamba kila mmoja anatakiwa kujua ni kitu gani anachokihitaji kutoka kwa mwenzake na matakwa hayo ni sharti yawekwe wazi wakati wa makubaliano au mkataba ikiezekana hata kwa maandishi.

Huwezi tu kwenda na kusema kwa mfano, “natafuta kazi ya hoteli” halafu ukishaambiwa “njoo uanze kesho” kesho yake unaibuka kuja kuanza kazi pasipo hata kwanza kuweka wazi unataka nini kwenye hiyo kazi. Ni kweli nafasi za kazi Tanzania siku hizi ni dili lakini isije ikawa ni kwa gharama za kutokukupata hata kile unachostahili. Unapodai mkataba, wengine watakukebehi, “kazi bongo…toka lini bongo kukawa na kazi, hapa ni kibarua tu..…kazi labda serikalini kwa wenye madigirii”


Kutokuweka wazi matakwa ya kila mmoja kabla ya ajira husababisha matatizo makubwa baina ya waajiri na waajiriwa, siyo ajira rasmi tu bali hata unapoangalia katika zile ajira zisizokuwa rasmi kama vile kazi za ndani, ajira ndogo ndogo katika biashara za watu binafsi na katika makampuni madogomadogo yasiyokuwa rasmi. Utakuta mwajiri anakubaliana tu juu juu na mfanyakazi na kwa kuwa mwajiriwa mwenyewe yeye ana shida na kazi amekaa muda mrefu bila ya kuipata sasa anashindwa kusisitiza kile anachokitaka katika makubaliano hayo.

Matokeo yake mbele ya safari, kunakuja kuibuka sintofahamu au mgogoro mkubwa. Yule mfanyakazi anashindwa kumudu mahitaji yake kutokana na maslahi ya kazi yenyewe kuwa duni. Anaanza kufanya hujuma mbalimbali kama udokozi, uvivu na kukosa morali wa kazi huku akiwaza ni vipi atamudu kuitunza pengine familia yake au hata yeye mwenyewe maisha yake hatima yake itakuwaje huko mbele.

Shilingi ina pande mbili kichwa na mwenge, hali kadhalika na kwenye makubaliano ya pande mbili mfano ajira kama tulivyotangulia kusema, mwajiri naye ana matakwa yake ambayo ni lazima anapoingia kwenye meza ya makubaliano atataka yawekwe wazi. Mwajiri naye kama alivyokuwa mwajiriwa au mfanyakazi asipofahamu ni kitu gani anachokitaka kutoka kwa yule anayetaka kumpa kazi basi ujue baadaye yataibuka matatizo. mwajiriwa anaweza kuja kuhisi anaonewa kwa kupewa majukumu ambayo tokea mwanzoni hayakuwekwa wazi. Weka mezani kila kitu unachotarajia yule unayetaka kumpa kazi aje afanye kabla ya mkataba kusudi na yeye aweze kulinganisha ikiwa vitaoana na kile anachokitaka kutoka kwako.

Hata katika makubaliano baina ya ndugu wawili kwa mfano mtu na kaka, mtu na dada yake, mjomba, shangazi nk. Usije ukakubali kuingia katika mkataba wa jambo lolote lile bila kwanza kujua kila mmoja, upande unahitaji kitu gani. Mmepeana kazi basi mapema kabisa, mwambie, “Mjomba, kaka, shangazi, mimi nitapata nini baada ya kukutimizia kazi hii?” Kumbuka hakuna kazi yeyote ile isiyokuwa na malipo duniani. Hata ikiwa ni chakula, basi mwanzoni kabisa ijulikane bayana kuwa wewe malipo yako ni ‘msosi’ utakaokuwa ukila pale kwa baba mdogo au shangazi. Vinginevyo ni kuja kulaumiana baadaye au undugu kufa pasipokuwa na sababu zozote za msingi.


Usipoweka wazi kile unachokitaka mapema ukachukulia tu upande wa pili utajua wenyewe ni makosa makubwa. Upande huo baadaye utajiona kuwa wewe ndiye unayenufaika zaidi ili hali hata kumbe siyo hivyo ni kinyume chake, kwa mfano unakaa kwa mjomba na pale unasaidia kazi zote za pale nyumbani huku na wewe ukiwa unapata milo yote ya siku kama watoto wa mjomba. Ikifika siku ukaumwa labda malaria, mjomba anaweza kujisikia ugumu wa kukupa hela ya matibabu kwa kuwa hamkukubaliana toka mwanzo afanye hivyo, na isitoshe anaweza akaona kama vile ni mzigo kwake kwakuwa tena unakula pale kwake kila siku. Hawezi kufikiria na wewe unatoa mchango mkubwa katika kazi za pale nyumbani hata pengine kuwazidi watoto wake mwenyewe.


Mifano ipo mingi karibu kila mahali katika jamii zetu tunamoishi. Makubaliano hata ikiwa siyo ya kuandikiana kwenye karatasi, hata ya mdomo yanasaidia. Kikubwa ni kila upande kujua ni nini hasa unachokitaka katika makubaliano hayo.

......................................................................................

Kwa vitabu bora kabisa vya Ujasiriamali, Biashara na Maendeleo binafsi pata vitabu hivi hapa chini;





Tuwasiliane kwa namba, 0712 202244  au 0765 553030

0 Response to "UNAPOAJIRI AU KUAJIRIWA, ZINGATIA UMUHIMU WA KUJUA NI NINI UNACHOTAKA"

Post a Comment