Una wazo la kuanzisha biashara unayoipenda ya ufugaji wa
kuku wa kienyeji kwa njia za kisasa, biashara uliyokuwa na uzoefu nayo na
ambayo unaamini itakusisimua wakati ukiifanya lakini changamoto moja inakuwa,
huna mtaji wa kutosha kuianzisha. Unaamua uende benki kukopa mkopo nako
wanakuambia uonyeshe dhamana zisizohamishika au uwe na mdhamini wa uhakika atakayekubali
kukuwekea dhamana mshahara wake kazini au nyumba yake anayoishi na familia.
Masharti hayo yote yanakufanya uahirishe kabisa wazo la
kukopa benki. Unapata habari kwa jirani yako kuwa ipo taasisi moja ya fedha,
yenyewe hukopesha lakini sharti lake kubwa ni uwe katika kikundi cha watu
wasiopungua watano mnaofahamiana vizuri na kuaminiana. Unaamua ujiunge katika
kikundi kimoja na jirani yako na hatimaye unafanikiwa kupewa mkopo wa shilingi
laki tatu.
SOMA: Kabla ya kukopa mkopo benki pambana kwanza kiume usije kuumbuka bure
SOMA: Kabla ya kukopa mkopo benki pambana kwanza kiume usije kuumbuka bure
Ukiwa unatoka hapo kaunta ya ya dirisha la taasisi ya
fedha huku mkononi umeshikilia kibunda chako cha noti za shilingi elfu kumikumi
zipatazo 30, unaanza kuwaza na kuwazua fedha hizi utazifanyia kitu gani.
Kumbuka mwanzoni wakati wa usaili wa kuchukua mkopo ulizuga unafanya biashara
ya ufugaji wa kuku wa kienyeji kisasa na kumbe wala hauna hata kibanda cha
vifaranga. Kwa kuwa ni udhamini wa kikundi, wenzako walikuonea imani kwa
kuamini hutaweza kuja kuwazingua japo walifahamu fika unaongopa biashara uliyoitaja.
Unawaza kichwani, tatizo siyo biashara ya kufanya, bali
ni kiasi cha mtaji wa kuanzisha biashara, “lakini, anyway” unajisemea
mwenyewe kichwani, “Nitaanzisha kitu chochote, mithali hela tayari nimeshaitia mkononi,
mambo yangu si kama jana”.
Unafika hapo sokoni Buguruni unaangaza angaza, huku na
kule, unaona samaki, vitunguu, nyanya, na kila aina ya mboga, unakumbuka mara
ya mwisho nyumbani familia kula samaki ilikuwa lini, unakumbuka sasa yapata
miezi zaidi ya sita hamjaonja hata dagaa, kila siku ni maharage mkibadilisha
sanasana basi ni matembele, siku ya kula kisamvu inakuwa kama mmekula nyama
vile. Baada ya kufanya hapo manuuzi kadhaa unapandisha taratibu kuelekea maeneo
ya Buguruni sheli na chama.
Wakati ukikatiza hapo maeneo ya kimboka kwa kina mama
wanaochoma kuku stendi ili ukanunue kipaja cha kuku hapo kwa kwa ajili ya
mwanao mdogo anayekulilia kila siku, “mbona baba siku hizi huniletei tena miguu
ya kuku”, unapitia kwanza
kwenye meza za wauza vitu vidogovidogo. Mara unaona dawa za mswaki, unakumbuka
nyumbani kila siku mnapiga mswaki wa kijiti kwa kutumia mkaa na majivu,
unanunua hapo dawa(whitedent) ya buku jero, mafuta ya kupaka ya mia tano(rays)
na kiwi, rangi ya viatu ya buku.
Unavuka tena barabara taratibu unatoka hapo Buguruni chama
unapanda basi la kwenda zako Gongo la Mboto unakoishi. Kuingia tu nyumbani
hivi, unapokewa kwa furaha na kabinti kako kadogo kanakoshangaa, imekuwaje leo
baba kuja na furushi la vitu kubwa namna hii mkononi wakati kila siku huja
mikono mitupu. Mama naye hachelewi anatokea kukulaki na kupokea lile furushi
moja kwa moja mpaka ndani. “Baba Mwamini leo kwani vipi?”. Unamsimulia
kila kitu, anapika, mnakula, mnalala kwa shangwe.
SOMA: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha?
SOMA: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha?
Kesho yake unapoamka na kuzihesabu zile pesa, tayari
unakuta zimeshabakia laki mbili na elfu hamsini, hapo bado haujaamua uanze kufanya
biashara gani, kila biashara unayotaka kuanzisha unaona pesa hazitoshi, ni
kidogo. Unawaza uanzishe biashara ya kusagisha mahindi kwa ajili ya kuuza unga
wa ugali wa sembe na dona lakini unagundua hautaweza kununua hata magunia
mawili ya mahindi kwa fedha zilizobakia achilia mbali gharama nyinginezo kama
mifuko ya vifungashio, kulipa watu wa mashine, ubebaji, usafiri nk.
Ukawaza uanzishe biashara ya kuuza chipsi, supu ya
kongoro, chai na vitafunio kama mandazi, chapati na silesi, lakini nayo
unagundua ukinunua jiko la chipsi, jiko la kuchomea mishikaki, sahani, vikombe,
makarai ya kukaangia na sufuria tu pesa yote imekwisha kabla hata ya kulipia
pango la sehemu yenyewe ya kufungua biashara. Kichwa sasa kinaanza kukuuma,
wiki imekatika, wenzako wanakukumbusha siku ya marejesho imewadia. Unatakiwa
upeleke marejesho shilingi elfu 20. Unachomoa tena pesa zilezile za mkopo
kurejesha.
Baada ya wiki chache pesa zote za mkopo zinakuwa
zimemalizika huku mwanaume huna hata genge la nyanya uliloanzisha barazani mwa
nyumba unayoishi. Unaanza kujuta ni kwanini hata ile siku ya kwanza zile pesa
usingeziacha vilevile zilivyo pasipo kugusa hapo hata senti tano ukasubiri
mpaka umepata kwanza biashara ya kufanya, hata ikibidi mkalala na njaa kuliko
kula pesa ya mkopo. Ukawaza na kuwazua, kwani kama usingepata hizo pesa siku
hiyo ndiyo ungelikuwa mwisho wa dunia?. Jibu likawa wala hata msingeweza kufa
kwa njaa, mbona kila siku mlikuwa mnaishi?.
Baada ya pesa zote kuisha wakati unalia na kusaga meno
huku ukifikiria ni vipi utarejesha pesa za taasisi na wenzako watakuchukuliaje,
taratibu akili inaanza kupambanua kumbe ilikuwepo njia, tena njia nzuri tu ya
kuzitumia zile pesa kwa busara pasipo hata kuzifuja kwa matumizi ya vitu vya
kupita ambavyo wala kusingeliweza kutokea madhara yeyote endapo wewe na familia
yako mngevikosa.
Si hivyo tu, unaanza kugundua kumbe kuna biashara nyingitu ndogondogo ambazo kwa kutumia mtaji kidogo uliokuwa nao ungeliweza kuanzisha
biashara yenye faida nzuri na ya haraka pasipo hata kuumiza sana kichwa. Unaanza
kukumbuka aina za ujasiriamali ambao laiti ungeliingia katu usingekuangusha
chini.
Unakumbuka biashara ya nguo, biashara ya mitumba kwenda
kununua masoko kama ilala na kutembeza mitaani, unakumbuka biashara ya urembo
ambayo huhitaji ofisi wala nini, wewe unachohitaji kuwa nacho ni kikapu chako
kidogo na rangi za kucha, kucha za bandia na superglue. Soko lako ni kina mama na
kina dada kwenye masaloon ya kike.
Unakumbuka biashara ya mazao kama vile kwenda mikoani
kama mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro na Rukwa ukanunue ndizi mbivu na maparachichi
kwa bei rahisi kisha ukiyafikisha hapa Dar unauza kwa bei ya juu. Unakumbuka
aina za biashara ndogo ndogo nyingi ambazo kwa mtaji ule wa shilingi laki tatu
jumlisha na kujibana kwa kiasi kikubwa ni lazima msingi ungeongezeka na
hatimaye kufungua biashara ya kudumu kama vile biashara ya duka nk.
Unatamani ile siku uliyochukua mkopo ingerudi tena, usingefanya mchezo, ungehakikisha baada tu ya kufika nyumbani huku ukiwa na zile laki tatu, hata kama hukuwa na biashara uliyokuwa umeshaianza na eneo la kuifanya, kesho yake ungechukua kipande cha gunia au mfuko na kwenda moja kwa moja eneo la stendi yeyote ile au popote pale wanakopita watu wengi ukatandika na kuanza biashara yeyote ile, iwe ni kuuza nyanya, mahindi ya kuchoma, biashara ya kuuza kahawa na kashata, kuuza viatu vya mitumba, kuuza vyombo, biashara ya kuuza nguo za mitumba, biashara ya kuuza vitabu vilivyokwisha tumika(used books), biashara ya mbogamboga na matunda, biashara ya kuuza miche ya matunda na miti mbalimbali nk.
Unatamani ile siku uliyochukua mkopo ingerudi tena, usingefanya mchezo, ungehakikisha baada tu ya kufika nyumbani huku ukiwa na zile laki tatu, hata kama hukuwa na biashara uliyokuwa umeshaianza na eneo la kuifanya, kesho yake ungechukua kipande cha gunia au mfuko na kwenda moja kwa moja eneo la stendi yeyote ile au popote pale wanakopita watu wengi ukatandika na kuanza biashara yeyote ile, iwe ni kuuza nyanya, mahindi ya kuchoma, biashara ya kuuza kahawa na kashata, kuuza viatu vya mitumba, kuuza vyombo, biashara ya kuuza nguo za mitumba, biashara ya kuuza vitabu vilivyokwisha tumika(used books), biashara ya mbogamboga na matunda, biashara ya kuuza miche ya matunda na miti mbalimbali nk.
Basi unaamua kufunga safari ya kutembea kwa miguu kutokea Gongo
la mboto kuelekea maeneo ya mjini lakini hata huelewi, wala huna lengo maalumu
ni wapi hasa unakoelekea. Kichwani umejawa na mawazo ajabu. Unapofika hapo
Ukonga, almanusura ugongwe na gari lililokuwa likikimbia kwa spidi kubwa, kumbe
lilikuwa ni gari la msafara wa wanajeshi baada ya kupiga honi na vingora bila
ya mafanikio wewe ukabaki katikati ya barabara kwa wingi wa mawazo.
Mara ni saa saba za mchana unajikuta upo katikati ya
makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere inapojengwa barabara ya juu, Tazara flyover.
Unashangaa shangaa pale kisha unaendelea na safari yako usikojua unakokwenda ni
wapi. Unaamua ukunje hapo Bakhresa kuelekea Buguruni. Mara unakutana na vijana
wawili ambao unawafahamu tangu mlipokuwa mkifanya kazi za kibarua kuwasaidia
mafundi ujenzi huko Tandika.
Vijana wale wakiwa na mabegi migongoni na kichwani
wamebeba vitu mfano kama makaratasi yaliyokatwa, kumbe walikuwa wamebeba mifuko
ya kufungia vitu madukani ambayo hutembeza madukani wakiwauzia wenye maduka kwa
jumla.
SOMA: Mbinu 7 za kutumia ili kuboresha biashara ya kusambaza bidhaa katika maduka ya jumla mitaani.
SOMA: Mbinu 7 za kutumia ili kuboresha biashara ya kusambaza bidhaa katika maduka ya jumla mitaani.
Baada ya kusalimiana na stori mbili tatu, unaamua
kuwasimulia maswahibu yaliyokukumba na wao bila hiyana wanaamua kukushirikisha
katika biashara ile. Unawaeleza huna hata senti tano ya kuanzia kama mtaji
lakini wanaamua kukubeba hivyohivyo, “wewe twen’zetu bwana msingi siyo ishu sana
tutakukopesha, kwanza unaweza kuchukua mzigo kwa matajiri kisha ukaja kulipa baada ya kuuza, ilimradi tu
uwe mwaminifu, sisi tutakudhamini”
Vijana wale wanakuambia.
Siku mbili, tatu, mwezi unajikuta umeshapata msingi wako
mwenyewe wa biashara ya kuuza mifuko mitaani katika maduka ya rejareja na ya
jumla. Biashara siyo mbaya kwani wateja hawakosekani kutokana na kwamba soko
lenyewe ni kubwa. Uwezo wako tu wa kutembea ndio unaoamua uuze kiasi gani.
Unashindwa kuamini macho yako pale unapozihesabu chapchap
shilingi laki tano zako mwenyewe bila hata kudaiwa na mtu yeyote baada ya
kumaliza kulipa lile deni la taasisi na mkopo wa mifuko uliyokopeshwa kama
mtaji wa kuanzia biashara ya kutembeza mifuko madukani. Unaamua sasa kufuta
akilini mwako dhana kuwa mikopo ni kitu kibaya, unajijengea fikra mpya kuwa
ubaya upo katika matumizi ya ule mkopo.
Zile shilingi laki tatu zingetosha kabisa kuanzisha
biashara ya kuuza mifuko, na tena zikabakia nyingi tu ambapo baada ya wiki moja
ungerejesha marejesho ya mkopo kwa faida ya biashara na wala siyo mkopo
wenyewe. Biashara ndogo ndogo nyingi hazihitaji ghara kubwa, hulipi pango la
chumba cha biashara wala mfanyakazi ikiwa utaamua kufanya mwenyewe. Isitoshe biashara
kama hii ya mifuko, iwe ni ile ya khaki au hata ya nailoni iliyoruhusiwa, faida
yake ni ya haraka kwani ni bidhaa inayohitajika kila siku na wateja. Ni
biashara endelevu yenye wateja wanaojirudia.
Bada ya sasa ya kupata mtaji kiasi kama milioni tatu hivi,
unaamua ukaanzishe biashara ya ndoto yako, uliyokuwa ukiipenda na kutamani
kuifanya siku zote za maisha yako, biashara ya ufugaji wa kuku wa kienyeji kwa
njia za kisasa ili uweze kupata mayai mengi na nyama kwa ajili ya kuwauzia
wateja wanaopenda mno kitoweo hiki kitamu kushinda vitoweo vingine karibu
vyote.
....................................................................................................
Kama unataka kujifunza mbinu mbalimbali za biashara na ujasiriamali kwa kina, kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI ndiyo jibu lako, kitabu hiki kwa kifupi kabisa, kina masomo yote kuanzia, ujasiriamali wenyewe kwa kina, namna ya kuanzisha biashara, uendeshaji wake kwa ujumla na namna ya kuandika mpango wa biashara. Unaweza ukasoma maelezo yake kwa undani zaidi kwa kubonyeza jina la kitabu hapo juu.
Pia unaweza kujipatia vitabu vizuri vya aina nyingine kutoka kwetu, soma ukurasa huu wa SMARTBOOKSTANZANIA kuvijua vyote kwa kina.
Tuna semina kwa njia ya blogu maalumu na email, nayo maelezo yake unaweza kuyapata hapa, DARASA LA SEMINA YA MICHANGANUO
Kwa huduma zetu zote, angalia katika Menu, HUDUMA ZETU
0 Response to "BIASHARA NDOGO RAHISI KWA WAJASIRIAMALI ZINAZOENDA NA WAKATI TULIO NAO"
Post a Comment