Kwa haraka haraka mtu anaposikia kuhusiana na kuwekeza
katika viwanda moja kwa moja akili yake inaweza kumpeleka katika uwekezaji ama kuanzisha
kiwanda mithili ya kiwanda cha Dangote cement Mtwara, kumbe kiwanda hata ukiwa
tu unafahamu jinsi ya kutengeneza icecream unaweza kufungua kiwanda chako
kidogo kwa ajili ya kutengeneza icecream za watoto na watu wazima ukauza mtaani
kwako na hata nje ya mtaa unakoishi.
Viwanda ndiyo mhimili mkubwa katika chumi za nchi
kubwakubwa na zilizoendelea tofauti na nchi kama hizi za kwetu ambazo mhimili
mkuu ni kilimo. Hakuna shaka yeyote kwamba uzalishaji wa bidhaa viwandani ni muhimu
sana kwa nchi yeyote ile iwe imeendelea ama ni nchi iliyoko dunia ya tatu,
kwani viwandani ndiko hupatikana vifaa mbalimbali kama pembejeo za kilimo, zana
za uvuvi, madawa na kemikali za kukuzia mimea, dawa na kemikali za kuuwa wadudu
waharibifu, mashine mbalimbali, vipuri vya magari, bidhaa mbalimbali, madawa na
vifaa vya hospitalini nk.
Kwa ujumla ni kwamba karibu kila sekta nyingine zote
duniani zinategemea uzalishaji wa viwanda ili ziweze kufanya kazi sawasawa. Kwa
hiyo ikiwa unao mpango wa siku moja kuja kumiliki kiwanda basi ni vyema ukaanza
hata sasa kwa kuanza na kiwanda kidogo halafu baadaye utakapopata nguvu zaidi
kimtaji ukafungua kiwanda kikubwa kama walivyofanya matajiri wengi wakiwemo
kina Bakhresa, Reginald Mengi, Mohamed Dewji, Alihaj Ali Dangote na wengineo.
Nasema hivyo kutokana na sababu kwamba kuanzisha kiwanda
kikubwa kunahitaji uwekezaji wa fedha na rasilimali nyingi lakini na ambao pia
ikiwa bidhaa unazozalisha zinahitajika kwa wingi unaweza kutengeneza utajiri
mkubwa ndani ya kipindi kifupi sana.
Siri
7 ni kwanini kiwanda kinaweza kumtajirisha mtu haraka.
1. Kiwanda hutumia mashine kuzalisha bidhaa kwa wingi na
kwa haraka zaidi kushinda mikono ya binadamu. Tuchukulie mfano hata wa juisi ya
maembe, ukikamua juisi ya embe kwa kutumia mashine ya blenda itakuchukua muda
mfupi zaidi kuliko kama vile ungeamua kutwanga kwa kutumia kinu na kuchuja kwa
kitambaa, au kutwanga mahindi ya kande kwa kutumia kinu ni zoezi gumu na
linalogharimu muda mwingi kuliko kukoboa mahindi katika mashine.
2. Kiwanda kina uwezo wa kutengeneza bidhaa nyingi kwa
wakati mmoja ambazo unaweza ukazisambaza kwa watu wengi. Na hivyo kuwa na
wateja wengi wanaonunua bidhaa zako jambo litakalokupa faida nyingi kwa wakati
mmoja tofauti na biashara tuseme labda ya kuuza bidhaa katika eneo moja tu.
3. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha bidhaa zilizokuwa na
ubora ule ule bila ya kushuka hivyo kusababisha soko liwe la uhakika.
4. Wateja popote pale duniani wanayo tabia ya kuamini
zaidi zile bidhaa zinazotoka viwandani zikiwa na nembo pamoja na alama
zilizothibitishwa na mamlaka mbalimbali za ubora na usalama.
5. Kiwanda kina uwezo wa kufanya kazi kila siku na wakati
mwingine usiku na mchana kutokana na kutumia mashine zinazoendeshwa kwa nishati,
hivyo uzalishaji ni mkubwa na faida nayo huwa kubwa pia.
6. Kiwanda kina uwezo wa kuzifanya bidhaa zinazoharibika
upesi kudumu kwa muda mrefu zaidi na hivyo kuepusha hasara itokanayo na kuoza
kwa mazao hasa ya kilimo.
7. Kiwanda kilichosajiliwa na kupewa vibali vyote vinavyostahili
hupewa ushirikiano pamoja na usaidizi stahiki kutoka serikali kuu na serikali
za mitaa kwa jambo lolote lile linalohusiana na maendeleo ya kiwanda.
Hatua
7 za uanzishaji wa kiwanda kidogo
Unapotaka kuanzisha kiwanda hata ikiwa ni kiwanda kidogo,
inafaa mtu kufuata taratibu angalau zile muhimu ili kuhakikisha kiwanda chako
hakiji kufungiwa na serikali au mamlaka husika. Taratibu nyingi au sheria
itategemea ni kiwanda cha aina gani unachotaka kuanzisha. Kwa mfano kiwanda
kidogo cha sabuni taratibu zake zitakuwa tofauti na taratibu za uanzishaji
kiwanda tuseme labda cha kutengeneza sofa au fenicha.
Viwanda nyeti kama vile viwanda vya bidhaa zinazohusisha
moja kwa moja afya na usalama wa binadamu au mazingira taratibu zake ni lazima
zizingatiwe kwa umakini na ni vigumu kuanzisha kiwanda kama hicho bila
kuzingatia ipasavyo sheria na taratibu za kuanzisha kiwanda husika.
1. Hatua ya kwanza kabisa ukishaamua ni kiwanda cha
bidhaa gani unachotaka kuanzisha, fanya kwanza utafiti(upembuzi yakinifu) wa
soko la bidhaa yako pamoja na masuala yote yatakayohusika kuanzia mtaji
utakaohitajika, eneo la kuweka kiwanda chako, usajili na vibali kama
vinahitajika, malighafi zitakazotumika, kiasi utakachozalisha, msaidizi/wasaidizi
wa kazi kama wapo pamoja na ujuzi utakaohitaji kuwa nao kuhusiana na shughuli
za kiwanda chako.
2. Hatua ya pili ni kuandaa mpango wa biashara kulingana
na utafiti ulioufanya katika hatua iliyotangulia.
3. Tafuta pesa kwa ajili ya uanzishaji na uendeshaji wa
kiwanda chako kwani shughuli yeyote ile ya uzalishaji hata iwe ndogo kiasi
gani, bila ya kuwa na mtaji haiwezekani kuanzisha. Tumia mtaji wako uliokuwa
nao, mkopo au fedha kutokana na mchango wa mbia.
4. Hatua ya nne, fuatilia leseni na vibali vinavyohusika
kama kiwanda chako ni lazima kiwe navyo, ikiwa ni kiwanda kisichohitaji vibali
basi unaweza kufuatilia leseni tu ya kawaida ya biashara. Kulingana na ukubwa
na aina ya kiwanda utakachoanzisha, unaweza kujikuta unalazimika kwenda katika taasisi mbalimbali kama vile BRELA, TRA, Ofisi
za biashara za manispaa yako, TFDA, TBS, SIDO, NEMC nk. Mlolongo wa taasisi
hizi usikutishe kwani kwa mfano ikiwa kiwanda chako ni cha vitu kama vyakula
vile vya kawaida kama vitafunwa huna haja ya kwenda hata TFDA
5. Hatua tano ni kuandaa eneo na vifaa vya vitakavyotumika
wakati wa uzalishaji kwenye kiwanda chako. Vipo viwanda kwa mujibu wa sheria
vinatakiwa viwe kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda na kuna
viwanda vingine unaweza ukafungua eneo lolote lile ilimradi pana nafasi ya
kutosha. Nunua mshine au vifaa vinavyotakiwa.
6. Hatua ya sita, anza uzalishaji wa bidhaa zako
7. Hatua ya 7 na ya mwisho, tangaza na kuuza bidhaa zako.
Mwanzo wa ngoma ni lele, leo umeanzisha kiwanda kidogo,
baada ya muda ukishapata mtaji unaweza ukaanzisha kiwanda cha kati na hatimaye
ukamiliki kiwanda kikubwa kabisa. Unaweza kupata mafunzo na muongozo zaidi
kutoka mashirika au taasisi mbalimbali zinazohusiana na uanzishaji wa viwanda
vidogovidogo kama SIDO, VETA nk.
……………………………………………………………………...
Mpenzi msomaji wa makala katika blogu yako hii, kama unapenda
kujifunza masomo ya biashara na ujasiriamali kwa kina kabisa, unaweza
ukajipatia moja kati ya vitabu vyetu hapa, SMART BOOKS TANZANIA, pia kwa huduma
zetu nyingine tunazotoa fungua ukurasa wa HUDUMA ZETU.
Na kama ulikuwa hujakisoma
kile kitabu cha JINSI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO, bofya hayo
maandishi ili uweze kukipakua bure bila malipo yeyote.
Mwandishi na mhamasishaji wako;
Peter A. Tarimo
0712202244
0765553030
Good
ReplyDelete