Mpango wa biashara au mchanganuo wa biashara,
watu wengi wamekuwa wakiona kama ni jambo gumu linalohitaji mtu kuwa mtaalamu
wa biashara au mtu aliyebobea katika mahesabu ya biashara ndipo aweze kuandika
kumbe ni kinyume chake kabisa.
Wanachoshindwa kufahamu wajasiriamali ni kwamba,
kumbe kila mjasiriamali anayeanzisha biashara pasipo hata kujua yeye mwenyewe
huwa anakuwa ameshaandaa mpango wa biashara yake kichwani tayari. Tatizo moja
tu linakuja pale mtu anaposikia neno JINSI YA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA
AU MPANGO WA BIASHARA KWENYE KARATASI.
Kwa kifupi kabisa mpango au mchanganuo wa
biashara ni jumla ya mambo yote na
michakato inayotarajiwa kutekelezwa na biashara. Mambo hayo yote uyafikirie kwa
kichwa, uyaandike katika karatasi au hata uyarekodi kama sauti, vyovyote vile
yataitwa mpango wa biashara. Hivyo kufahamu mtiririko mzima jinsi
utakavyoendesha biashara yako ndiyo mpango wenyewe wa biashara na hakuna mtu
anayeweza akaanzisha biashara pasipo kufahamu anataka kufanya kitu gani au
malengo yake ni nini.
Kwa hiyo ikiwa unataka kuandika au kuandaa mpango wa biashara
utakaokuwezesha kutimiza malengo yako ya biashara uliyojiwekea, yawe ni malengo
kwa ajili ya kupata fedha mahali, benki,
kwa wawekezaji au wabia, au ni kwa malengo
tu ya kupanga mkakati imara wa kuikuza biashara yako, dondoo zifuatazo ni muhimu.
1.
Andika mchanganuo mfupi.
Lengo la kutokuandika mpango wa biashara yako
kuwa mrefu sana ni kuhakikisha mpango wako unasomwa na hadhira uliyokusudia
iusome na kama ujuavyo binadamu hatukuumbwa kusoma mamia ya kurasa, karibu kila
mtu anapenda kusoma kitu kifupi chenye maana iliyokusudiwa.
Sababu nyingine ni kwamba, mpango wa biashara
siyo kitu cha kubwaga kabatini na kuacha huko mende watafune bali ni kitu
unachopaswa kufanya marejeo mara kwa mara na kufanya marekebisho angalao kila
wiki au mwezi kulingana na matukio halisi yanavyotokea, kumbuka mpango wa
biashara ni dira tu, ukiwa mrefu sana hata wewe mwenyewe utaona uvivu kuupitia.
2. Fahamu
vizuri hadhira yako(wasomaji wa mpango wako)
Mchanganuo wako unatakiwa kuandikwa kwa
lugha ambayo ni nyepesi na inayoeleweka
barabara kwa wasomaji wako. Mathalani
biashara yako unashughulika na masuala ya kiteknolojia lakini wafadhili
au wawekezaji wako ni watu wa kawaida wasioweza kuelewa lugha za kitaalamu basi
hakikisha mpango wako unaweka maneno rahisi.
3. Usikubali
vitisho kutoka kwa watu.
Wamiliki wa biashara na wajasiriamali wengi
duniani kote siyo wataalamu wa biashara na wala wengi wao hawana digirii za
biashara, kama ulivyokuwa wewe na mimi, wanajifunza kadiri muda unavyokwenda na
biashara zao zinavyokua. Kigezo kikubwa cha mtu kuandika mpango wa biashara
yake ni ikiwa anaifahamu vizuri biashara husika, utayari wa kuifanya na
kuipenda.
Kuna watu wengine wakiwemo na baadhi ya
wataalamu wa biashara, kutokana tu na uvivu hudai mipango ya biashara ni
kupoteza wakati, ni jukumu gumu na lisilokuwa na faida. Lakini wao wenyewe
katika biashara zao kila siku hupanga mikakati na namna watakavyoboresha zaidi
biashara zao, hukubali kwa shingo upande kuwa mpango wa biashara ni muhimu
lakini wakati huohuo huponda.
Kitu wasichotambua tu ni kwamba duniani
huwezi ukafanya jambo lolote lile pasipo mipango likafanikiwa vizuri.
Unapofahamu vizuri ni nini kinachotakiwa kuwa katika mpango wako wa biashara,
hata usipoandika katika karatasi, bado unaweza ukapanga kichwani mwako na
ikatosha kuitwa ni mpango wa biashara.
Hatua
nane( 8)za kuandika mpango wa biashara yako.
Kwa haraka haraka hebu tutazame hatua nane au
unaweza kuziita vipengele vinavyounda mchanganuo wa biashara kwa mujibu wa
kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, kitabu ambacho pamoja na
masomo mengine mengi ya ujasiriamali, kimeelezea kwa undani kabisa jinsi ya
kuandka mchanganuo/mpango wa biasha yeyote ile pamoja na michanganuo yenyewe
halisi ya biashara mbalimbai
iliyokamika.
1. Muhtasari
tendaji.
Huu ni ufupisho wa mpango wako mzima wa
biashara, kurasa moja mpaka 2, ni sehemu muhimu sana unayotakiwa kuiandika kwa
umakini kumfanya msomaji wako avutike kusoma mpango wako mzima.
2.
Maelezo kuhusu biashara/kampuni
Hapa unaeleza, mfumo wa biashara kisheria,
mfano kama ni kampuni yenye dhima ya ukomo, ubia au ya mtu binafsi, historia ya
kampuni ikiwa biashara siyo mpya, wamiliki na sehemu ilipo.
3.
Maelezo kuhusu bidhaa au huduma .
Ni kitu
gani unachouza na ni mahitaji gani hasa ya wateja unayokidhi, unawatatulia
tatizo gani linalowasumbua?
4.
Soko lengwa.
Unawauzia kina nani? Soko lako muhimu ni
kundi gani, onyesha ikiwa lipo kundi moja tu au makundi zaidi ya moja na uyaelezee.
5. Mpango
wa masoko na mauzo(Mikakati)
Eleza mbinu na mikakati mbalimbali
utakazotumia ili kulifikia soko lako lengwa.
6. Vitendo
na upimaji wa matokeo
Sehemu hii unaelezea vitendo hasa hasa vile
vinavyohusika na uanzishaji wa biashara yako, mpango peke yake bila vitendo
hauna maana yeyote, taja vitendo, mtu atakayehusika pamoja na bajeti yake ni
kiasi gani.
7. Utawala
na nguvukazi
Tumia sehemu hii kuelezea timu itakayohusika
kwenye biashara yako, historia zao, ngazi ya elimu na sifa za mtu utakayependa
kumuajiri.
8. Masuala
yahusuyo fedha
Mwisho ni sehemu ya fedha ambayo wengi hudai
ni ngumu lakini siyo kweli ingawa kwa asiyekuwa na uelewa wake ana haki ya
kusema ni ngumu. Na hasa kwa biashara mpya hesabu zake ni rahisi sana. Kwa
kawaida makisio ya fedha hufanywa ya kila mwezi kwa mwaka mzima wa kwanza na
kisha kwa mwaka katika miaka miwili inayofuata.
Kisia
mauzo, gharama za mauzo mfano mishahara nk., ripoti ya faida na hasara,
mtiririko wa pesa taslimu, mizania ya biashara, sehemu na muhimu za biashara.
Vielelezo
Hii hauwezi ukasema ni sehemu au kipengele cha
mpango wa biashara lakini ni sehemu muhimu ambayo ndiyo unayotakiwa kuweka vile
vitu ambavyo usingeliweza kuviweka kwa undani katika mpango wako, vitu hivyo ni
kama vile, chati na majedwali marefu ya makisio ya hesabu zako, nyaraka
mbalimbali za kisheria kama usajili wa biashara nk.na picha na vielelezo
mbalimbali vinavyoelezea bidhaa zako.
………………………………………………………………………..
Mpenzi
msomaji wa makala hii, kwa muda mrefu sasa umekuwa ukisoma nadharia nyingi
kuhusiana na namna ya kuandika mpango wa biashara na faida zake, lakini yamkini
umekuwa ukijiuliza, “Mpango wa biashara
unanisaidiaje katika biashara yangu wakati hata taasisi za fedha hapa kwetu
mara nyingi huwa haziangalii mipango ya biashara ili kukukopesha?”
Nataka
nikutie moyo kwamba mpango wa biashara thamani yake haipo kwenye kuomba mikopo
tu peke yake, mpango wa biashara ni zana muhimu iliyokuwa na uwezo wa kumfanya
mjasiriamali aweze kuendesha biashara yake kwa ufanisi mkubwa.
Tena
siyo lazima uandike mpango wa biashara kwenye karatasi ndipo ukusaidie hapana,
kufahamu tu akilini ni kitu gani kinachotakiwa kufanya, ni hatua zipi ufuate
wakati wa kuendesha biashara yako inatosha. Na hili utalifahamu pindi
utakapopitia na kusoma michanganuo mbalimbali halisi iliyokwisha andikwa
tayari, wala haitakuchukua muda mrefu jinsi unavyofikiri.
Self Help Books Tumekuandalia kitabu kizuri kilichokuwa
na maelezo ya kutosha juu ya namna ya kuandaa mipango ya biashara kutoka A-Z,
isitoshe kina michanganuo kamili unayoweza kuichukua kama mifano na vielelezo
wakati utakapokuwa ukiandaa mpango wa biashara yako, angalizo ni kwamba usikopi, bali tumia kama vielelezo kwani kila
biashara ni tofauti, biashara ‘X’ mazingira, soko na kila kitu ni tofauti na
biashara ‘Y’.
Ununuapo
kitabu hiki, unapata na ofa ya kuingia ‘SEMINA HII YA MICHANGANUO YA BIASHARA’bure.
Bei
ya kitabu ni sh. elfu 10 softcopy na sh.elfu 20 hardcopy
Ukitaka
kuona vitabu vingine vya Self help books fungua, SMART BOOKS TANZANIA
Peter
A. Tarimo
Self
Help Books Tanzania
0712202244 &
0765553030
0 Response to "JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YAKO, DONDOO HIZI 3 NI MUHIMU SANA"
Post a Comment