Ukiniuliza ni mwanamke gani duniani mjasiriamali wa shoka
ninayemfahamu zaidi kuliko wengine wote hapa duniani, moja kwa moja picha ya
mama yangu mzazi, Fabiola Augustino
Tarimo hunijia akilili. Kuelekea maadhmisho ya siku ya mama Duniani kesho jumapili, kumbukumbu
zangu za awali kabisa katika maisha yangu ya utoto zinanikumbusha jinsi mama
alivyokuwa akihangaika na biashara ndogondogo kusudi mimi na ndugu zangu
wengine tuweze kupata mahitaji yetu muhimu yakiwemo mahitaji ya chakula, nguo,
ada za shule na hata matibabu.
Ingawa kwa mama ninazo kumbu kumbu nyingi nzuri na
zinazonisisimua sana ninapozikumbuka lakini kwa leo naona nijikite zaidi kwenye
kumbu kumbu za mama yangu kama Mwanamke na mama Mjasiriamali wa shoka ambaye
naweza nikasema kwangu mimi ndiye mwanamke ninayeweza kumpa nafasi ya kwanza
kabisa katika kumbukumbu za maisha yangu yote kama shujaa wa kuigwa mfano (Role
model) wangu katika Ujasiriamali na shughuli za biashara hapa duniani.
Sina lengo la kubeza umuhimu au juhudi za baba la hasha,
naye alikuwa akijitahidi kivyake lakini kusema ukweli, juhudi zake tu mwenyewe
bila ya mama hali ingelikuwa ngumu sana. Maisha hayakuwa rahisi, na kipato cha
baba hakikuwa kikubwa cha kuiwezesha familia kumudu mahitaji yote kwa
ukamilifu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya mama aamue kujikita katika ujasiriamali
na hasa biashara ndogondogo kwa ajili ya kuikimu familia.
Mpaka leo hii nikitazama katika mkono wangu wa kulia
chini kidogo ya kiwiko lakini kabla ya goti la mkono, kuna doa la alama fulani kama vile ya mtu aliyewahi kuungua na
moto hapo zamani, alama hii sasa imefifia kidogo lakini wakati nikiwa mtoto mdogo
ilikuwa ikionekana dhahiri. Mama wakati huo nikiwa mdogo aliwahi kunisimulia
kwamba alama ile ilitokana na yeye kukaa juani masaa mengi mno wakati akiwa
mjamzito, alinisimulia kwamba wakati nikiwa tumboni mwake alikuwa akifanya
biashara za kuuza mazao mbalimbali ya chakula kama mahindi, maharage na ndizi.
SOMA: Utamu wa lugha ya mama hauna mfano.
SOMA: Utamu wa lugha ya mama hauna mfano.
Mama alisema kwamba, ilimbidi kusafiri umbali mrefu
wakati mwingine hata kulala hukohuko kutokana na shida kubwa ya usafiri
iliyokuwepo, alikwenda maeneo ya mbali kama Arusha, Moshi mjini na Himo kwa
ajili ya kupata nafaka akauze maeneo ya Mkuu Rombo, Mashati, Useri na Tarakea.
Wakati huo usafiri uliokuwa ukitumika ni wa malori na magari ya wazi hivyo
njiani jua lilikuwa kali sana na ikawa ndiyo sababu kubwa ya mimi kupata baka
la alama niliyokuwa nayo mpaka sasa hivi mkononi mwangu.
Kumbukumbu yangu kubwa zaidi na ambayo mpaka leo hii
haijafutika akilini ingawa ilitokea nilipokuwa mdogo sana, ni ile njaa ya mwaka
1984, mwaka huo kulitokea njaa kali sana kote nchini Tanzania na nchi za jirani.
Vyakula na hasa nafaka vilikuwa adimu sana hata serikali ya awamu ya kwanza
wakati huo chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikaamua kuomba
msaada wa mahindi ya njano kutoka nchini Marekani yaliyojulikana kwa jina
maarufu kama mahindi ya Yanga. Mama wakati huo ndipo nilipotambua ujasiri
wake.
Tukio ambalo siwezi kulisahau, japo wakati linatokea
sikuwepo nyumbani, nilikuwa kwa bibi lakini wakaja kunisimulia dada na kaka
zangu ni lile la mama siku moja kuamua kuinjika jikoni chungu kilichokuwa na
chakula feki ili tu, aweze kuwaaminisha watoto wake kisaikolojia kwamba chakula
kipo, kumbe alikuwa anakwenda kukitafuta.
Alikatakata shina la chini kabisa karibu na mizizi la mgomba
kilugha huitwa(matonga) akajifanya ni
viazi na kuviweka kwenye chungu kisha akainjika jikoni pamoja na kutia magadi,
juu aliweka mfuniko na juu ya mfuniko akaweka jiwe, aliwaonya wanawe wasifunue,
wachochee moto mpaka pale atakaporejea. Baada ya muda alirejea mkononi ameshika
mfuko uliokuwa na unga. Kilichoendelea hapo kaka na dada zangu wanajua wenyewe.
Ujasiriamali wa mama haukuishia hapo, pia kipindi chote
tukisoma mimi na ndugu zangu alikuwa mashuhuri kijijini kwa biashara ya
kutengeneza na kuuza kwa jumla kinywaji maarufu cha mbege, ambacho ni
mchanganyiko wa ndizi mbivu zilizochemshwa, kutiwa maji na kukamuliwa pamoja na
kimea cha ulezi uliopikwa, wenyeji huita, kutisha mbege.
Nakumbuka mara nyingi nilivyokuwa nikimsaidia kukamua
mbege masaa ya jioni baada ya kutoka shuleni. Wakati huo huo pia mama alikuwa
akijishughulisha na kilimo na tulipokuwa shambani wote ndipo nilipojifunza
masuala mengi kuhusiana na ujasiriamali.
Kitu cha ajabu sana nilichogundua kutoka kwa mama ni kwamba,
kumbe ujasiriamali mtu anaweza akajifunza mwenyewe kutokana na mazingira na
uzoefu anaopitia katika maisha yake. Kumbuka mama aliishia darasa la 2 enzi za
mkoloni lakini kanuni muhimu za msingi za biashara na ujasiriamali alizifahamu
kupita hata mtu aliyefika chuo Kikuu.
Mama mara kwa mara tulipokuwa shambani mimi na ndugu
zangu alikuwa akituambia maneno haya,
“Mwanangu
ili uweze kupata kitu chochote kile kizuri maishani ni lazima jasho likutoke
kwanza”,-Mama
“Katika biashara yeyote ile , mtaji ni kitu
cha kuchunga sana wanangu, hakikisha unapokula usile mtaji bali kula faida tu”
–Mama
Siwezi kusahau pia jinsi mama alivyotutia moyo wanawe
pale tulipoanzisha jambo au biashara yeyote ile, nilipoanza kufuga kuku na
kilimo cha bustani wakati nikiwa bado nasoma, mama alinipa support kubwa, baba alipogundua nimekata miti yake shambani kwa ajili
ya kujengea banda la kuku alikasirika sana na kufikia hata hatua ya kunichapa
lakini mama alijitahidi kwa udi na uvumba kumpoza hasira asinichape, mpaka
ikafika hatua baba naye akaamua kuniunga mkono kwa kazi zangu baada ya kuona
zinaleta manufaa kwangu na pale nyumbani kwa ujumla.
Mama aliona uchungu sana baada ya kugundua sikuweza
kwenda kuuza mbogamboga zangu sokoni kutokana na muda wote wa mchana kuwa niko
shuleni, yeye mwenyewe alitafuta muda, akazichuma na kunipelekea sokoni,
niliporudi kutoka shuleni jioni alinipatia fedha zote alizoniuzia mbogamboga,
mayai au nyanya na kwa kweli nilifurahi mno!
Namshukuru sana mama yangu, ndiye aliyeanza kunifundisha
ujasiriamali tangu hata sijaanza shule, alinifundisha kwamba maisha ni kufanya
kazi na siyo kukaa bure. Mama ametufanya katika familia yetu wote kuwa
wajasiriamali, dada zangu, kaka na ndugu zangu wengine wote leo hii wapo
waliofanikiwa kimaisha kupitia ujasiriamali na yote ni kutokana na kuiga mfano
mzuri kutoka kwa mama yetu. Mungu azidi kumlinda na kumpa maisha marefu zaidi.
0 Response to "MWANAMKE NA MAMA MJASIRIAMALI WA SHOKA NINAYEMFAHAMU ZAIDI DUNIANI"
Post a Comment