NJIA RAHISI YA KUPANGA BEI YA BIDHAA AU HUDUMA UNAYOUZA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA RAHISI YA KUPANGA BEI YA BIDHAA AU HUDUMA UNAYOUZA


Upangaji  wa bei ni jambo muhimu sana katika  kufaulu au kuanguka kwa biashara.Baada ya  kufanya utafiti na kufahamu wateja wako watarajiwa ni akina nani, sasa ni wakati wa kujua  kiasi  cha fedha utakazowatoza kwa jili ya bidhaa au huduma  utakayowauzia.


Bei  ya bidhaa  au huduma  hupangwa   kutegemeana na  moja kati ya vigezo vifuatavyo;

·       Gharama za bidhaa au huduma  inayotolewa.
·       Thamani ya bidhaa au huduma kwa mteja.
·       Bei za washindani wengine katika soko.
·       Idadi  ya wateja   wanaohitaji huduma  na hali ya soko kwa ujumla.
(1). Gharama  za bidhaa /huduma .
Kigezo hiki mfanyabiashara  hujumlisha gharama zote zilizotumika kuzalisha  bidhaa/huduma moja halafu huongeza kiasi anachoona kitampatia faida . Kwa mfano  umenunua embe kwa sh. 50/=,  ukaliuza sh. 100/= ongezeko la sh. 50/= ndiyo faida na bei ya embe itakuwa sh.100/=

Wakati mwingine inakubidi pia uweke na  gharama  za uendeshaji au gharama za kudumu, kama vile mishahara ya wafanyakazi, kodi ya pango pamoja na uchakavu. Kwa hiyo  bidhaa kama hilo embe  badala ya kuliuza sh. 100/=, pengine  litafikia hata shilingi 150/= kutokana na hizo gharama za kudumu (za uendeshaji) zilizoongezeka.

(2). Thamani ya bidhaa.
Unapanga bei ya bidhaa au huduma kwa kuangalia thamani wateja  wanayoipata kutokana na huduma au bidhaa unayotoa. Mathalani,  wewe ni fundi kompyuta, kutokana na mteja kutojua  namna ya kutengeneza  kompyuta, unaweza ukamchaji bei kubwa na akaona ni sawa, ingawa wewe hukutumia gharama kubwa sana kuitengeneza.

(3). Kuangalia washindani wengine sokoni.
Baada ya kufahamau washindani wako bei zao zikoje, ni vizuri  ukapanga bei zako zisiwe juu sana wala chini sana pasipokuwa na sababu yeyote ile ya msingi. utakapoweka  bei  zako kuwa chini sana kushinda  washindani wako ni hatari kwako kwani unaweza  usipate faida na mwishowe  biashara ikafa. Pia ukiweka bei za juu sana  unaweza ukawakimbiza wateja wakahamia kwa washindani wako na mwishowe biashara ikafa pia.

(4) Idadi  ya wateja   wanaohitaji huduma  na hali ya soko kwa ujumla.
Kigezo kingine wakati wa kupanga bei, unaweza ukazingatia idadi ya  wateja walio tayari kununua bidhaa/huduma pamoja na mazingira ya soko kwa ujumla jinsi ilivyo. Njia hii  huweza kuchukua sura tofauti tofauti kama vile;

SOMA: Namna bora ya kufanya utafiti wa soko la biashara yako.

Mitindo; Watu wengine hununua nguo au viatu kwa bei ya juu bila kujali thamani yake ilimradi tu ni mtindo unaochukuliwa ni wa kisasa na unawika kwa wakati huo.

Jina; Vitu vyenye majina  makubwa kama vile, ADIDAS, PUMA SONY, NOKIA Nk. Huuzwa kwa bei ya juu na watu huwa tayari kununua bila wasiwasi kutokana na umaarufu wake.

Upatikanaji; Usiku muuzaji wa sigara katika kioski mjini anaweza akauza  sigara moja, sh.300/= badala  ya bei ya kawaida ya sh. 150/=, na watu wakanunua kwani hawawezi kupata mahali pengine kwa urahisi usiku huo.

Ukiritimba; Ikiwa  biashara  haina mpinzani, mmiliki anaweza akauza bei aitakayo, hata kama gharama zake  siyo kubwa sana.

Ugavi na Mahitaji; Bidhaa au huduma zinapokuwa chache sokoni wauzaji hupandisha bei kuliko bei za kawaida. Zikiwa nyingi bei hushusha bei.

Kumbuka unapopanga bei, lenga bei ya juu, kwani baadaye ni rahisi zaidi uja kushusha kuliko kuanza na bei ya chini halafu baadaye  ukapandisha,  wateja watakuchukulia kama mtu mwenye tamaa na hatimaye kukuhama.Vilevile hatari ya kuuza  bei ya chini sana ni wateja kudhani kwamba  bidhaa au huduma zako  hazijapitia ukaguzi wa  viwango vinavyotakiwa kama vile TBS nk.

Kwa biashara mpya inayoanza, kupunguza sana bei ni kosa kubwa, ni bora ukaweka bei ya juu kidogo na kisha wateja ukawapoza kwa kuwaahidi  faida nyinginezo kama vile upatikanaji wa uhakika wa bidhaa/huduma, huduma bora na za haraka, huduma za kitaalamu baada ya mauzo nk. Wape sababu toufauti na bei  itakayowafanya wanunue kutoka kwako.

……………………………………………………………………

Kwa elimu ya kutosha na ya uhakika kuhusiana na ujasiriamali na biashara, jipatie vitabu mbalimbali hapa kwenye ukurasa wa SMART BOOKS TZ.

Pata hapa SEMINA KAMILI JUU YA UANDAAJI WA MICHANGANUO YA BIASHARA kwa shilingi elfu 10 tu pamoja na kitabu cha michanganuo free bila malipo.

Kwa HUDUMA nyinginezo bonyeza maandishi hayo.


0 Response to "NJIA RAHISI YA KUPANGA BEI YA BIDHAA AU HUDUMA UNAYOUZA"

Post a Comment