Waafrika karibu wote tuliokuwa na dini za kigeni na hata
wale ambao bado wanashikilia zile imani za tangu jadi walizokuwa wakiamini
mababu zetu waliotutangulia, kuna vitu ambavyo bado tunaviamini wakati mwingine
bila hata kujua tunaiamini, vitu ambavyo kimsingi havina mantiki wala ukweli
wowote ule.
(A).
IMANI POTOFU.
Watu wanazo imani nyingi potofu zisizokuwa na uthibitisho
juu ya biashara ya duka na biashara kwa ujumla wake. Wakati mwingine imani hizo
zinaweza zikawa na athari kubwa sana kwako hasa ikiwa hautatambua ukweli wake
na ukazifanya ndio zikuongoze katika suala zima la uendeshaji wa duka lako.
Baadhi ya imani hizo potofu ni kama hizi
zifuatazo;
1.
Kuna watu “chuma ulete” walio na uwezo wa kuiba mauzo uliyouza kwa njia za
kishirikina.
Hili ni suala la kiimani zaidi na sidhani kama kuna ukweli wowote, Hebu jiulize swali hili jepesi “hivi
kweli kama kuna binadamu mwenye uwezo huo, ni kwa nini asiende benki
kwenye mabilioni ya hela akawaibia ama kwenye maduka makubwa mjini aje akuibie senti zako kidogo pengine
zisizotosha hata kuunulia baiskeli?
Utakuta mara nyingi hivi ni visingizio
wanavyotoa watu baada ya kushindwa kuendesha maduka yao kwa ufanisi na wakati
mwingine mfanyakazi/msaidizi dukani anaweza akafanya hujuma na kusingizia ni
‘chuma ulete’ wanaoiba pesa.
2. Kuwatuhumu
ushirikina na kuwatilia mashaka baadhi
ya wateja bila sababu za msingi.
Utakuta mtu na
usomi wake, hata amefika chuo kikuu lakini bado hofu ya kulogwa au kuibiwa pesa
kwa njia za kishirikina hazijamuisha. Wapo watu ikifika tu usiku, atakuambia
vitu kibao hauzi hata ikiwa mteja unaviona live. Vitu kama chumvi, sindano,
nyembe, mishumaa. Magadi, udi, na hata pini watakuambia vimeisha na kumbe
vimejaa tele dukani, kisa ukiuliza wanakuambia bidhaa hizo kuna baadhi ya
wateja wanaokwenda kufanyia shughuli za kishirikina au uchawi na kupungia
majini.
Kikongwe,
mlemavu au mgonjwa wa akili akifika dukani ni mkosi wa ajabu, utasikia,
‘oo, atakuwa chuma ulete huyo! Simuuzii’,
au ‘ni ndondocha huyo katumwa aje kuchukua pesa’.
Imani hii ni kwa kila upande wapo pia wateja wenye imani
za ajabu hata akikupa pesa anapotaka kununua kitu hakupi mkononi, ataiweka juu
ya meza, sijui wanadanganywa na nani, bila shaka ni waganga wa jadi uchwara
huko mitaani. Kwa upande wa wenye maduka wao wanaogopa sana hasa kuwapa
washindani wao chenji wakihofia mauzo yao yatahamia kwao kimiujiza.
Wewe ukitaka muuza duka akupe chenji hasa nyakati za
usiku, nunua hata pipi ya shilingi mia mpe elfu kumi atakurudishia elfu tisa na
mia tisa lakini siyo akupe tu hivihivi.
(B.)
DHANA POTOFU.
Kama ilivyokuwa kwa
imani potofu pia wenye maduka ya rejareja wengi wamezikumbatia baadhi ya dhana zisizokuwa
sahihi ambazo kwa kiasi kikubwa huchangia kukwamisha mafanikio ya biashara zao.
Dhana hizo ni kama hizi hapa chini;
1.
Duka lina faida kidogo sana:
Ni kweli faida katika biashara yeyote ile ya reja reja,
siyo duka tu bali hata na kitu chochote kinachouzwa rejareja faida yake haiwezi
kuzidi asilimia 30% ya mauzo hii ina maana kwamba bidhaa ikiuzwa shilingi 100
faida yake ni Tshs. 25 na ikizidi sana ni Tshs. 30. Kwa hiyo kusema eti
biashara ya duka la rejareja haina faida au ni kidogo sana siyo sahihi kwani
utapata faida katika vitu vingi na ukichanganya
pamoja huwa kubwa.
2.
Duka halihitaji matangazo wala promosheni:
Siyo kweli kabisa dhana hii kwani matangazo ni muhimu
katika biashara ya aina yeyote ile, cha msingi tu ni aina gani ya matangazo na
promosheni utakayoifanya.
3.
Ili duka liendelee ni lazima ukae wewe, mkeo/mume au mwanao; zaidi ya hapo watakuibia na litakufa tu.
Dhana hii ina ukweli endapo utamuajiri mtu halafu
ushindwe katika suala la usimamizi hasa kwenye hesabu na vipimo kwa mfanyakazi
uliyemuweka.
4.
Maduka madogo hayana uwezo wa kushindana na maduka makubwa.
Huo ni uongo, duka hata liwe ni la mtaji wa shilingi laki
mbili bado unao uwezo wa kushindana na duka hata la ukubwa wa ‘super
market’ mbinu hapa utakayoitumia ni
kutafuta upekee wa biashara yako, huduma za kipekee kwa wateja pamoja na mandhari yakuwavutia wateja. Wateja hawatakuwa na sababu ya kwenda katika
hiyo ‘super market’ waache duka lako dogo. Wao
shida yao ni kupata huduma na siyo ukubwa wa duka.
5.
Ipo siku biashara za rejareja kwa njia ya
mtandao “intanenti” zitakuja kuzipiku kabisa biashara za maduka ya rejareja ya
kawaida.
Hakuna kitu kama hicho kitakachoweza kutokea, na si hapa
Tanzania tu bali hata na huko intanenti yenyewe ilikoanzia, watu wamethibitika
kupendelea zaidi kununua kitu wanachoweza kukiona ‘live’ na wala siyo eti
kukiona kwenye screen ya computer au
simu.
Ukitaka kupata mafanikio ya uhakika katika biashara ya
duka la rejareja au biashara nyingine yeyote ile, huna budi kuachana kabisa na
dhana na imani hizi za karne zilizopita, hii ni karne ya sayansi na teknolojia,
jiambie akilini mwako “Kama kweli imani hizi hufanya kazi jinsi
wengi wanavyoamini, mbona waafrika bado tuko nyuma hivyo kimaendeleo?” Wenzetu
wazungu na mataifa yaliyoendelea imani hizi si kama kwao hazipo hapana, bali
baada ya maendeleo na ustaarabu kushika kasi wamezipuuzilia mbali wakafanikiwa
huku sisi tukiendelea kuzikumbatia na kubakia kuwa masikini wa kutupa.
……………………………………………………………………..
Shea
na mimi uzoefu wangu binafsi wa miaka 12 katika biashara ya rejareja hususani
duka la mahitaji ya nyumbani kwa kusoma kitabu kifuatacho nilichotunga.
Kitabu cha Duka la rejareja. |
Kitabu
hiki hata ikiwa unafikiri biashara ya duka ni rahisi, utakutana na mambo mengi,
mengine pengine ulikuwa huyachukulii “serious” kumbe yana athari kubwa kwenye
biashara yako.
Softcopy
yake kwa njia ya email ni sh. Elfu 5 tu, na unaweza kutumiwa ukiwapopote pale
mara tu baada ya kulipa kupitia moja kati ya namba 0712202244 au
0765553030. Unatuma pia kwa meseji anuani yako ya baruapepe-email.
HARDCOPY
unaweza kupata ukifika ofisi yetu ilipo, MBEZI STENDI KWA MSUGURI, au unaweza
kuagiza tukakuletea popote pale kama upo Dar es salaam, lakini unatuma nauli
sh.1500/= kuonyesha kweli unahitaji kwani wapo baadhi ya watu “wanaocheat” kusema
niletee kumbe hawanunui kweli.
Kama
upo Mikoani, agiza mtu akuchukulie na kukutumia, au unaweza kutuma fedha pamoja
na gharama za usafiri tukakutumia kwa basi linalofika ulipo.
ASANTE
KWA KUSOMA
Peter
A. Tarimo
Self
Help Books Publishers Ltd
0 Response to "PUUZA IMANI NA DHANA HIZI POTOFU UFANIKIWE KATIKA BIASHARA YAKO YA DUKA LA VYAKULA"
Post a Comment