Kila biashara ina siri yake ya mfanikio ambayo
mjasiriamali asipoizingatia basi hawezi kuona mafanikio aliyolenga kuyapata.
Kwa upande wa biashara ya chakula, inaweza ikawa ni mgahawa, hoteli, mama na
baba lishe au biashara yeyote ile inayohusisha vitu vinavyoliwa na binadamu,
siri yake kubwa ya kupata wateja wengi na wa kudumu ni kudumisha usafi wa hali
ya juu.
Mpaka naandika makala hii leo ni matokeo ya uchunguzi
wangu binafsi baada ya kuwa kila mara napita eneo fulani panapouzwa chakula
hususani kifungua kinywa nyakati za asubuhi. Mahali hapo kila nipitapo asubuhi
huwa naona pana watu na wameketi wakinywa chai, supu na vitafunwa mbalimbali.
Mimi ni mpenzi sana wa supu na kila mara huwa natamani nijiunge pale siku moja
ili na mimi nipate japo supu kidogo na chapati. Lakini kwa kuwa mara nyingi
nakuwa tayari nimeshapata kifungua kinywa nyumbani basi huwa ‘napotezea’ na kujisemea
moyoni, “lakini ipo siku tu nitapata supu
pale”
Ikaja siku hii ambapo nilitoka zangu nyumbani sijapata
chochote nikasema sasa leo ndiyo siku ya kutimiza ile dhamira yangu, ninywe
supu ya moto pale katika ile café pamoja na chapati zangu mbili au tatu. Wakati
nasogelea pale kwenye ule mgahawa, kumbuka siyo mgahawa mkubwa ni eneo tu uswahilini
la wazi lililozungushiwa ua na viti aina ya mabenchi. Niliweza kuwaona mbwa
wawili wakirandaranda eneo karibu kabisa na vyombo vinavyotumika pale
mgahawani, nikashtuka na hamu yote ya supu ikaniisha kabisa.
Nilizuga kama vile naulizia bei ya supu wakanijibu ni
shilingi elfu moja na mia tano, nikajibu asante na kugeuza kisogo nikaondoka
zangu. Nia yangu ya kunywa supu pale siku moja ikawa ndiyo imeishia palepale.
Siyo kila mtu huona kinyaa kwa wanyama kama mbwa au paka lakini ni watu wengi huwa
hawapendi wanyama hao kuwaona maeneo ya chakula, wana kawaida ya kuramba vyombo
kama sahani, masufuria na hata vijiko
ikiwa wataachiwa kiholela.
Ni vizuri kabla hujachagua eneo utakaloweka biashara yako
ya chakula basi ukahakikisha eneo hilo wanyama kama hawa hawafunguliwi ovyoovyo,
hata ikiwa jirani na hapo wapo basi tafuta njia yeyote ya kuwazuia wasikaribie
eneo lako la biashara kwani watakupotezea wateja wengi. Siyo mbwa tu kuna hata
paka nao huwa kero sana maeneo ya nayouza vyakula kwa kuwasongasonga wateja na mikia
yao wakitaka wapewe mifupa au nyama. Wakati mwingine hata hudondoshea manyoya kwenye
vyakula.
Wapo watu wengine huamua kufuga paka ndani ya maduka yao ya vyakula kwa lengo la kukomesha panya, ni lengo zuri lakini kwa mteja
anayezijua vyema tabia za mnyama huyu paka, kamwe hataweza kuwa mteja wako
mzuri wa vitu vya kupima kama unga, mchele na sukari. Paka wana tabia moja ya
ajabu sana, hupenda kujisaidia haja mchangani au katika vitu vinavyofanana na
mchanga kama vile unga, sukari na mchele.
Eneo la kuuzia chakula pia halitakiwi liwe na panya kwa
mfano mteja anaweza kuwa anakula chakula ghafla anamuona panya akikatiza njia
kwenye kona za chumba cha mgahawa, mteja huyo inaweza ikawa ndiyo siku yake ya
mwisho kufika katika mgahawa wako kwani akilini mwake atajenga picha kwamba
mapanya hurambaramba vyombo vya chakula usiku au hata kula vyakula
vilivyohifadhiwa na kwa mfanyabiashara asiyejali hawezi kutupa nyama, mboga au
tunda lililoliwa na panya badala yake atakata kidogo eneo lililoliwa na kuuza
hivyohivyo.
Inzi nao ni kikwazo kikubwa kinachowafanya wateja kuwa
mbali na biashara yako ya chakula, inzi huwa hawapendi usafi na hiyo ndiyo dawa
yao pekee ya kuwafanya wasisogee. Biashara kama ya chipsi, mishikaki, biashara
ya juisi, biashara ya nyama, biashara ya utumbo nk mara nyingi inzi hupendelea
sana biashara hizi lakini mjasiriamali makini unatakiwa ubuni njia zitakazozuia
ama kuhakikisha inzi hao hawawezi kuwa kero kwa wateja wako wanaofika kununua.
........................................................................................................
Mpenzi msomaji wa makala hii, ikiwa unapenda kujifunza biashara na ujasiriamali kwa kina kabisa, basi jipatie vitabu vya self help books kupitia email yako kwa bei rahisi kabisa ya punguzo msimu huu wa sabasaba. Ni shilingi elfu 15 tu badala ya elfu 18 kwa vitabu vyote 3 hapo chini na unatumiwa mara moja unapolipia kupitia namba 0712202244 au 0765553030 jina Peter Augustino Tarimo.
AU tembelea SMART BOOKS TANZANIA kwa maelezo zaidi.
0 Response to "BIASHARA YA KUUZA CHAKULA USIPOKUWA MSAFI UTAIONA CHUNGU"
Post a Comment