Malkia wa muziki wa asili nchini Tanzania na Afrika ya
Mashariki Bibi Saida Karoli aliyetamba mwanzoni mwa miaka ya 2000 na vibao
vyake maarufu kwa lugha ya Kihaya na kiswahili vya Maria Salome(Chambua kama
Karanga), Kaisiki, Ndombolo na Mimi nakupenda, anatuthibitishia dhahiri kabisa
kwamba kufulia ama kuanguka kimaisha siyo mwisho wa dunia bali
inawezekana kabisa mtu akaibuka tena au kwa maneno mengine kujirudishia tena ukuu wako uliopotea.(#makeyourselfgreatagain)
Kama unakumbuka na upo sambamba na blogu hii, mwanzoni
mwa mwaka huu wa 2017, tulianzisha kampeni tuliyoipa jina, KUJIRUDISHIA TENA UKUU WAKO ULIOPOTEA au MAKE YOURSELF GREAT AGAIN, kampeni ambayo tulisema
itakuwa ni ya mwaka huu mzima kuhakikisha kwamba wale wote ambao wangependa
kufanya mabadiliko makubwa maishani mwao na kurudisha hali zao mbalimbali
walizokuwa nazo hapo mwanzo lakini kwa sababu mbalimbali wakaja kuzipoteza basi
wanafanya hivyo.
Ukuu wako uliopotea waweza kuwa ni hali yako kiuchumi,
afya, kiimani, mahusiano, heshima nk. Sasa hivi miezi 6 imekatika na hatuna
budi sasa kufanya tathmini ya kampeni yetu hii tulikotoka na tunakoenda miezi
mingine tena 6 ijayo. Kumbuka bado safari inaendelea na ndiyo maana ukaona leo
hii nimeamua kukuletea mfano huu wa Saida Karoli pamoja na Diamond Platnumz,
Belle 9 na Darassa, ushirikiano wao katika kibao maarufu cha muziki, chambua
kama karanga au salome wangu ambacho kilitungwa na mwana mama huyu Saida Karoli.
enzi za ukuu wake alipokuwa katika kilele cha ubora katika muziki wa asili
nchini Tanzania na Afrika wa ujumla.
Kuibuka
na kuanguka kwa Saida Karoli miaka ya 2000 Mwanzoni.
Saida mwenyeji wa Mkoa wa Kagera jirani na nchi ya Uganda
alianza shughuli zake za muziki rasmi mwaka 2001 kwa kutoa albamu iliyoitwa Maria
Salome au maarufu kama Kanichambua kama karanga(Wanchekecha) chini ya meneja
Felician Muta, mkurugenzi wa kampuni ya FM Production ltd, Saida alipata
umaarufu ndani ya kipindi kifupi na akaweza kupata mialiko sehemu mbalimbali za
Afrika Mashariki na kati kama vile Burundi, Rwanda, Uganda katika sherehe za
kutumbuiza hafla ya mfalme Kabaka na hata baadhi ya nchi za Ulaya.
Katika mahojiano yake mwenyewe na vyombo mbalimbali vya habari
nchini Saida Karoli mwenyewe anakiri kwamba sababu kubwa ya yeye kuja kuanguka
kimuziki na maisha yake kuwa duni tena kiasi cha kuamua kuishi maisha ya
kujifiha kulitokana na kushindwa kusimamia mapato yake vizuri wakati mambo
yalipokuwa mazuri. Anasimulia kwamba alikuwa haelewi ni nini maana ya mikataba
wala kudai stahili za malipo yake aliyopaswa kulipwa kutokana na mikataba
mbalimbali aliyoingia. Anadai hata kudai stahili za matumizi ya nyumbani kutoka
kwa mumewe alikuwa hajui, sembuse malipo kutokana na kazi zake za kisanii.
Kutokana na hali hiyo alifika mahali akajuikuta anaanguka
vibaya kiuchumi kiasi ambacho aliogopa hata kuonana tena na waandishi wa habari
amabao mwanzoni ndio waliochangia kwa kiasi kikubwa kumtangaza kwa jamii. Waandishi
wa habari hata hivyo hawakukata tamaa, wakaamua kumfuata hadi kijijini huko
ndanindani lakini bila mafanikio yeyote jambo lililosababisha hata wengine
kuvumisha kwamba Saida Karoli amefariki Dunia kumbe haikuwa kweli.
Kuzaliwa
tena upya kimuziki kwa Saida Karoli mwaka 2017
Ndipo mwishoni mwa mwaka 2016 September zikaanzaa kuibuka
tetesi kwamba mwanamuziki nguli nchini Tanzania wa Bongo Fleva Naseeb Abdul au
Diamond Platnumz na Reyvanny wameiba
mashairi ya wimbo wa Saida Karoli, Salome(Chambua
kama karanga) bila kumlipa chochote. Tetesi hizo hata hivyo hazikuwa na
ukweli wowote kwani baadae ilibainika kulikuwa na makubaliano fulani. Siyo
Diamond tu aliyetumia vionjo na mashairi ya Saida Karoli, Belle 9 na Darassa
pia nao wamewahi kufanya hivyo.
Lakini kumbe kitendo cha wasanii hao kutumia vionjo na
mashairi ya Saida Karoli kulikuwa na maana kubwa sana kwani ndiko
kulikomhamasisha tena upya na kumfanya Saida kuibuka tena upya. Saida Karoli
amewashukuru sana wasanii hao na kujifananisha kama vile amezaliwa tena upya
kimuziki. Baada ya kuamua kurudi tena upya Saida naye kama kurudisha fadhila
kwa wasanii hao naye ameamua kuimba katika albamu yake mpya na wimbo wa
Orugambo vionjo kutoka katika vibao mbalimbali vya wanamuziki hao, Belle 9,
Diamond na Darassa.
Katika wimbo wa Saida Karoli Orugambo, anasikika akitaja
maneno acha maneno, weka mziki ambayo ni kionjo kilichopo ndani ya kibao, Maisha
na muziki cha mwanamuziki wa bongo fleva Darassa. Mchanganyiko huo wa muziki wa
asili wa zamani kidogo na muziki wa kizazi kipya au bongo fleva umetengeneza
ladha nzuri ya kuvutia.
Kitu kikubwa tunachoweza tukajifunza kutoka kwa
wanamuziki wote hawa, Saida Karoli, Diamond, Darassa na Belle 9 ni umuhimu wa
kushirikiana katika kuhakikisha mambo yanakwenda mbele. Saida Karoli
angeendekeza ubinafsi bila shaka angeonyesha upinzani mkubwa kwa kazi zake za
muziki kukopiwa na wasanii wa kizazi kipya, lakini uvumilivu wake na kutambua
mapema fursa iliyokuwepo kwa wasanii wenye majina kukopi nyimbo zake imemsaidia
na yeye kurahisisha kazi yake ya kujirudishia tena ukuu wake uliokuwa
umepotea ukiachilia mbali malipo yeyote yale ambayo labda wamempatia.
Kwa maana hiyo hapa hakuna aliyepoteza, kila mtu amepata
na ni jambo la kupendeza sana.
Ndugu msomaji wa makala hii, kampeni yetu ya kujirudishia
tena ukuu wako uliopotea, bado inaendelea na katika nusu nyingine ya pili ya
mwaka huu iliyobakia tumeamua kuihuisha tena upya. Fuatana nasi mpaka mwisho
ili Desemba Mungu akipenda tupate shuhuda za watu wengi waliofanikiwa kurudisha
tena ukuu wao kama dada yetu Saida Karoli anavyofanya sasa.
Kampeni hii ni kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo blogu
hii ya jifunzeujasiriamali, facebook, twitter, you tube, vitabu mbalimbali vya
Self Help Books kama hivi hapa pamoja na mitandao mingine yote ya kijamii.
0 Response to "DIAMOND PLATNUMZ, BELLE 9 NA DARASSA WALIVYOMTOA TENA SAIDA KAROLI UPYA"
Post a Comment