Mjasiriamali unaweza usiamini au kukubaliana na ukweli
huu, lakini ukweli utabakia kuwa ukweli daima. Mara nyingi wajasiriamali wengi
wanapofanikiwa kuvuka vikwazo vya kuanza biashara au kwa kimombo huita ‘startups’
wengi hujisahau na kuona wameweza kufika pale walipo wenyewe kwa kutumia nguvu,
maarifa na ujanja wao bila msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote yule.
Ukweli ni kwamba kwa namna moja au nyingine wajasiriamali
waliofanikiwa kama hao kuna nyakati fulani walipata misaada ya aina mbalimbali
kutoka kwa jamii inayowazunguka wakiwemo ndugu jamaa na marafiki. Misaada
ninayoizungumzia hapa siyo lazima iwe ni pesa, mtaji au rasilimali bali hata
ile kuungwa mkono tu kwa dhati peke yake nayo ni msaada, kutiwa moyo nk.
Unapokuwa katika hatua za mwanzo za biashara yako kitendo cha wale
wanaokuzunguka mfano hata wanafamilia kukupa utulivu wa nafsi na kukuacha
ufanye shughuli zako vizuri nao ni msaada.
Ili ufanikiwe kibiashara utahitaji watu kukuunga mkono,
na kitendo hata kile cha wateja kununua kutoka biashara yako nacho kinahesabika
kama msaada, hebu fikiria kama kila mtu angeghairi kununua kutoka kwako
ungelijisikiaje. Wakati mjasiriamali unapohangaika kabla hujatoka utakutana na
watu wengi wanaokupa ushauri mbalimbali mfano ni jinsi gani unaweza kupata
mtaji zaidi, mbinu mbalimbali za kupata soko, kupata msaidizi nk. Vyote hivyo
unavipata au kuvifahamu kupitia watu wengine waliokuwa na mapenzi mema kwako.
Wakati mwingine unaweza ukawa umenunua mizigo mahali
fulani na huwezi ukaibeba peke yako, ingawa utatoa pesa kidogo kwa ajili ya
vijana au watu watakaokusaidia kuibeba lakini wakati mwingine pesa unayowalipa
ni kama kifuta jasho tu, ungewalipa inavyostahili pengine mzigo wenyewe
usingepata faida, hivyo hapo unaweza ukahesabu umepata msaada.
Kwa kweli mpaka pale mtu anafikia hatua ya kupata mali au
kutajirika anakuwa amepitia uungwaji mkono kutoka kwa watu wengi ingawa pia
kunakuwa na watu wengine wachache ambao wanakuwa hawampi ushirikiano wowote na
wangetamani aanguke ili wamcheke. Lakini kwa kuwa wanaomtakia mema ni wengi
kushinda wasiomtakia mema basi ndiyo
hukuta mtu anafanikiwa.
Ni kitu
gani hicho kimoja basi Mjasiriamali
unachotakiwa kukifanya zaidi kushinda vitu vingine vyote?
Mjasiriamali unapaswa kila ufanyacho na wewe ufanye kwa
mtindo uleule unaofanyiwa na waliokuwa wengi, KUWASAIDIA WENGINE. Msaada haimaanishi pesa tu au kupoteza muda
wako bure kuwasaidia kazi watu wengine, msaada hapa unamaanisha kwamba;
kusaidia kwa kadiri ya uwezo uliokuwa nao. Misaada mingine si lazima iwe ni vitu vya kushikika, ushauri
mzuri, elimu na hata kumtakia mtu mema tu navyo ni msaada mkubwa sana.
Unapoonyesha matendo chanya kwa wengine unaasaidia kushinda hata umewapa pesa.
Utakuta mtu anaangamia au ‘kutumbukia katika shimo’, badala
ya kusaidia asiendelee kutumbukia wewe unamwacha, na kusema “mwache azame kwanza kajitakia mwenyewe”
huo siyo msaada, mwonyshe njia japo kidogo. Kama mjasiriamali msaada wako
mkubwa kabisa unatakiwa kuutoa kwa wateja wako. Wateja wako wanatakiwa wahisi
kile unachowauzia kina msaada mkubwa kwao.
Mjasiriamali pia usiwe mchoyo kuwaelekeza na wale
wanaotaka kuwa wajasiriamali kama wewe, kumbuka na wewe kuna wakati ulikuwa
hivyohivyo ukashikwa mkono kwa namna moja au nyingine na watu wengine na ndiyo
maana leo hii upo pale ulipo, hukufika hapo peke yako.
Rudisha sehemu ya kile ulichokipata kwa jamii unapofikia
hatu ya juu kabisa. Katika mlolongo huohuo wa kuhakikisha mjasiriamali unakuwa
ni mtu wa kuwasaidia watu wengine, kuna mahali unafika sasa inakuwa huna budi
kuiambia ile jamii iliyokufikisha pale ulipo asante, hapa ndiyo utakuta
matajiri, viongozi na watu wengine waliopata nafasi kimaishai wakitoa misaada
mbalimbali kwa jamii kama ujenzi wa mashule, mahospityali nk.
Wanafahamu kwamba utajiri waliokuwa nao waliwezeshwa na
jamii nzima inayowazunguka na mtazamo huu mtu anaanza kuwa nao kabla hata
hajafanikiwa kwa kuanza kujijengea mtazamo chanya kwa kila analolifanya kwa
watu wengine waliomzunguka. Na mtazamo chanya ni msaada kwa watu wengine.
Hakuna kitu kitakachokufanya ujisikie amani moyoni mwako na nafsi yako
kuridhika kama kutoa msaada kwa wengine.
.......................................................................................................
Ndugu msomaji wa makala hii, ukipenda vitabvu vyetu vya ujasiriamali, biashara na maendeleo binafsi usisite kutembelea, SMART BOOKS TANZANIA
0 Response to "KITU KIMOJA (1) MUHIMU KULIKO VYOTE MJASIRIAMALI ANACHOPASWA KUFANYA MAISHANI"
Post a Comment