Muhogo ni zao linalochukuliwa kirahisirahisi na watu
wengi duniani siyo tu hapa Tanzania lakini ndiyo zao ambalo kuanzia mizizi
yake, shina mpaka majani, hakuna kinachotupwa, vyote huweza kutumika na
kumletea binadamu faida kubwa kiuchumi, katika maswala ya lishe na hata katika
suala zima la tiba mbadala, watu wengi hasa hapa bongo wamejenga imani kubwa
kuwa kutafuna mihogo mibichi ni tiba ya kurudisha nguvu za kiume ingawa bado
utafiti wa kutosha unahitajika kuthibitisha madai hayo.
Hakuna asiyezijua faida za muhogo angalao hata zile kuu
na mengi sana yameshaandikwa juu kilimo bora cha zao la muhogo, matumizi
mbalimbali ya zao la mihogo na jinsi muhogo ulivyokuwa na uvumilivu wa hali ya
juu katika hali ya ukame na udongo usiokuwa na rutuba ya kutosha, mihogo inao
uwezo mkubwa wa kuota na kustawi hata maeneo yaliyokuwa nusu jangwa huku
yakitoa mazao bora kama kawaida. Mihogo haishambuliwi na magonjwa mengi sana
kama mazao mengine zaidi ya ugonjwa wa batobato na ugonjwa wa michirizi ya
kahawia au matekenya ambayo yote husababishwa na virusi.
Katika mfululizo wetu wa makala za biasharazilizosahaulika lakini zenye kulipa, bado kama nilivyokwisha wahi kusema siku
nyingine, ni kwamba biashara hizi ninazosema zimesahaulika ama biashara ambazo
bado watu wengi hawajazishitukia, siyo ngeni sana bali ni biashara za kawaida
tu lakini ambazo kwa jicho la kawaida lisilokuwa la kijasiriamali mtu anaweza
asiweze kugundua fursa kubwa zilizomo ndani ya baadhi ya biashara hizo, “so I am not trying to reinvet the wheel”
bali lengo langu kubwa ni kumfanya
mjasiriamali mdogo aweze kuziona na kuzitambua fursa za ajabu zilizojificha
kwenye baadhi ya hizo biashara ndogondogo nitakazokuwa nikiziweka hapa.
Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, hebu sasa tutazame ni
jinsi gani mhogo wa kukaanga na zao la mihogo kwa ujumla wake lilivyokuwa na
fursa tamu na nzuri hasa katika jiji la Dar es salaam na hata katika mikoa yote
ya Tanzania Bara na Visiwani. Mihogo hustawi vizuri sana Tanzania karibu ukanda
wote wa pwani na Kusini mwa Tanzania kuanzia Mikoa ya Ruvuma, Pwani, Morogoro,
Dar es salaam, Zanzibar(Unguja na Pemba), Lindi na Mtwara. Zao la mhogo pia
limekuwa likisitawi vyema katika ukanda wa Maziwa makuu kama vile Mwanza
Shinyanga, Rukwa na Kigoma.
Mihogo ya kukaanga na mafuta au wengine huita chipsi dume
Dar es salaam ni biashara kubwa sana kwa sasa hasahasa kwa wafanyabiashara na
wajasiriamali wadogowadogo walioamua kujiajiri wenyewe kwa biashara za mitaji
midogo. Wanaofanya biashara hii wengi hasa ni akina mama na hata wapo wanaume
pia wanaoifanya. Uzuri wa biashara hii ya kukaanga na kuuza mihogo mtaji wake
ni kidogo na ina wateja wengi, soko la mhogo ni la uhakika ukiweza kuongeza
thamani, hununuliwa haraka na ina faida nzuri. Kwa mfano mihogo mibichi ya
shilingi elfu moja unaweza kukata vipande vya shilingi mia mia hata 30 ambavyo
utapata shilingi elfu tatu
Ukiondoa hapo gharama zingine kama za kachumbari au
chachandu, mafuta, pilipili, mkaa na chumvi, huwezi ukakosa faida halisi
shilingi elfu moja mpaka elfu moja na mia tano. Sasa hapo ni mahesabu ya fungu
moja tu la mihogo, ukiweza kuuza kiroba kizima cha mihogo utapata faida
shilingi ngapi?
Soko la mihogo ya kukaanga ni kubwa kwani watu wengi
hupendelea kuitumia kama kitafunio cha chai asubuhi na hata wengine huitumia
kama mlo rahisi wa mchana kwa wale wasiokuwa na kipato kikubwa au kwa wale
wanaoamua kubana matumizi ya kula chakula cha gharama kubwa. Ukitaka kujua
mihogo ni biashara kubwa nenda masoko ya Buguruni, Mbezi na Urafiki uone jinsi
watu wanavyoweka foleni kununua mihogo mibichi ya kwenda kukaanga.
Wengine hununua mihogo kwa ajili ya kwenda kutembeza
mitaani kwa watu wanaopenda kutafuna ikiwa mibichi. Mhogo wa nazi na samaki wa
kukaanga kama ulishawahi kuula huwezi kusahau, watu wengi hupendelea kula
muhogo ulioungwa kwa nazi hasa hasa kwenye futari wakati wa mfungo mtukufu wa
Ramadhani. Mihogo ya nazi ni chakula kinachopendwa sana hasa maeneo ya mwambao
wa Tanzania.
Ikiwa ni mjasiriamali unayefikiria biashara ndogondogo ya
kuanza Tanzania hasa maeneo ya miji kama Dar basi unaweza pia katika orodha ya
mawazo yako ya biashara utakazofanyia uchunguzi ukaiweka na hii biashara ya zao
la mihogo, inaweza ikawa ni kukaanga chipsi dume, kuuza kisamvu kilichokwisha
kuandaliwa, kuuza miti ya mbegu au mashina ya mihogo, kuuza unga wa mhogo, kutembeza
mihogo mibichi ya kutafuna mitaani, kutengeneza vitu mbalimbali kama chapatti za
mhogo, crips nk. Sababu kubwa kwanini uamue kudili na mihogo narudia tena kuwa
ni gharama zake ndogo za kuanza, kumbuka wajasiriamali wengi wana tatizo la
ukosefu wa mitaji ya kutosha kuanzisha biashara zinazohitaji mitaji mikubwa au
ya kati, vilevile ni soko lake la uhakika.
Mihogo kama zilivyokuwa biashara zingine zozote zile za
vyakula, unapoanzisha katika kiwango chochote kile iwe hata unatembeza
barabarani na sinia, siri yake kubwa ya mafanikio ni usafi wa vyombo, eneo
unalouzia, mihogo yenyewe na hata wewe mwenyewe unayeuza. Angalao hata
hakikisha unaisafisha kwa maji safi siyo ya mto, kuwa na kisu kisafi na hata
ikiwezekana unapowamenyea wateja tumia karatasi safi au tishu. Kwa wale
wanaokaanga, hakikisha chachandu yako au kama ni kachumbari basi inakuwa
salama, safi na inayovutia, halikadhalika ikiwa unauza mhogo wa kuchoma, wawekee
wateja pilipili nzuri katika chombo kisafi.
Tukiachana na mizizi, hebu tutazame shina la mhogo kama
nilivyotangulia kusema kwamba muhogo una faida kuanzia mizizi yake ambayo ndiyo
mihogo yenyewe, shina mpaka majani yake kama kisamvu cha mboga kwa ajili ya
kitoweo. Faida kubwa ya shina la mhogo ni kwamba, inatumika kama mbegu kwa
ajili ya kuzalishia mihogo mingine. Ukifungua mahali ukaamua wewe kazi yako ni
kuuza mbegu ya mhogo tu peke yake unaweza ukatajirika.
Hasahasa nyakati za mvua kama masika mshina ya mihogo
huwa dili sana na watu wengi husafiri kwenda maeneo mbalimbali inakovunwa
mihogo kwa wingi kama maeneo ya mkoa wa Pwani, Mkuranga, Rufiji na Morogoro
kuchukua miti ya mbegu ya mihogo kwa ajili ya kuja kuuza kandokando ya barabara
ya Morogoro wanakopita watu wengi wakielekea maeneo yenye mashamba ya mihogo.
Majani ya mihogo ni mboga tamu sana inayojulikana kama
kisamvu. Siku hizi kisamvu ni maarufu mno na kimekuwa kikiuzwa mpaka kwenye
supermarkets, kutangazwa kwenye mitandao na wapo watu wanaoishi kwa biashara ya
kuuza kisamvu tu.
SOMA: Biashara ndogondogo Dar za kufanya na mtaji kidogo.
SOMA: Biashara ndogondogo Dar za kufanya na mtaji kidogo.
Hizo ni fursa chache sana kuhusiana na zao la mhogo,
hatujagusa kabisa zile faida kuu za mihogo kama moja wapo ya chanzo kikubwa cha wanga duniani kwa binadamu,
unga wa muhogo hutengeneza vitu vingi ukiwemo uji wa muhogo, biskuti za mhogo,
mikate, na nk. malighafi za kutengeneza bidhaa mbalimbali viwandani ikiwemo na
nishati ya kuendeshea magari na mitambo, chakula kwa ajili ya mifugo na hata
matumizi kwa ajili ya tiba au dawa. Kuna crips za mihogo au kaukau za mhogo
nazo hupendwa sana katika maduka na supermarkets
…………………………………………………………………..
Chochote
kile ufanyacho, ni biashara, hivyo unahitaji kwa namna moja au nyingine maarifa
katika nyanja hiyo na napendekeza vitabu 3 vifuatavyo kama utachagua kujifunza
kupitia njia ya vitabu;
Njia
nyepesi zaidi na ya haraka ya kupata moja ya vitabu hivi au vyote kwa pamoja ni
kupitia E-mail kama faili za PDF au softcopy. Lakini pia vitabu vya kawaida vya
karatasi tunavyo.
Ukihitaji
wasiliana nasi kwa namba hizi hapa;
0712202244 au
0765553030
Tupo
Mbezi Kwa Msuguri karibu na stendi ya mabasi
ASANTE
SANA
Peter
Augustino Tarimo
Self
Help Books Tanzania.
0 Response to "MHOGO WA KUKAANGA UNAVYOLIPA DAR, NI BIASHARA WENGI HAWAIFAHAMU VIZURI"
Post a Comment