Mazishi ya Seth Katende(Bikira wa Kisukuma) yaliyofanyika
leo jumatano tarehe 12 Julai 2017 katika makaburi ya Kinondoni baada ya mwili
wake kuagwa rasmi katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es salaam yametoa taswira halisi ya
maisha ya kijana huyo mdogo namna alivyoishi na kila kitu alichofanya katika
miaka yake michache aliyoweza kuishi hapa duniani.
Utata
wa jina la Bikira wa Kisukuma.
Seth Katende a.k.a Bikira wa Kisukuma kwa kifupi alikuwa
Mtangazaji wa redio, mhamasishaji, mjasiriamali, mwanamitandao ya kijamii(social
media marketeer), na hata kocha wa maisha kwa vijana wenzake na makundi mengine
mbalimbali katika jamii. Seth kwa kifupi tu alikuwa ni mtu mwenye vipaji
lukuki, alikuwa kijana wa kushangaza kwa mujibu wa maelezo ya watu mbalimbali
kutoka kada tofauti waliohudhuria kumuaga pale leaders Club na baadaye mazishi
yake makaburi ya Kinondoni wakiwemo viongozi wakubwa kutoka vyama na serikalini, wanahabari na wananchi wa kawaida.
SOMA: Siri za mamillionea 10 vijana chini ya miaka 30 na utajiri wao.
SOMA: Siri za mamillionea 10 vijana chini ya miaka 30 na utajiri wao.
Mara ya kwanza kusikia jina la utani la Seth Katende
katika redio ya EFM kwa kweli jina hilo hata mimi binfsi lilinipa ukakasi
mkubwa na kusababisha nijiulize mwenyewe, “Huyu kijana ni mwanaume, itakuwaje
ajiite Bikira wa Kisukuma, haoni haya?”. Hali hiyo ikanisukuma nitake zaidi
kujua habari zake, akili yangu moja kwa moja ikiniambia “huyu inawezekana kabisa akawa
miongoni mwa wanaume mashoga maarufu kama ‘mtoto si riziki’”. Na kwa
kweli nilipo google jina lake nilishangazwa na kukutana na 'comments' nyingi
kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambazo nazo zilikuwa na dhana ileile
niliyokuwa nayo mimi. Wengine hata walienda mbali zaidi na kufikia hatua ya kumtusi.
Lakini nilizidi kuingiwa na tashwishi ya kumfahamu zaidi
kwani haikuniingia akilini kabisa watu wa EFM wampe kazi, tena ya utangazaji wa
kipindi maarufu cha Ubaoni kijana mwenye tabia na vitendo visivyokubalika na jamii kubwa
ya watu hasa Waafrika. Niliingia karibu kila mtandao wake wa kijamii ukiwemo
facebook, twitter na Instagram, lakini nilichokutana nacho huko kwa kweli
kilinistua. Ukijaribu kusoma mambo aliyokuwa akiandika Seth huwezi kabisa
kuamini kama ni yeye yule unayemuona katika picha na wala havilingani kabisa na
umri aliokuwa nao. Uthibitisho nimekuja kuupata leo pale Leaders Club.
Nilijikuta namaliza karibu usiku mzima nikisoma posts za
mtu ambaye hapo awali nilidhani alikuwa mtu wa hivihivi tu. Tena
kilichonishangaza zaidi ni kwamba kijana huyu alikuwa akifanya vitu
vinavyofanana sana na vile nifanyavyo mwenyewe kwenye mitandao, kuelimisha
na kuhamasisha juu ya elimu ya ujasiriamali na maendeleo ya mtu kwa ujumla.
SOMA: Mfahamu kijana mbunifu mkubwa wa majengo duniani aliyezaliwa Tanzania.
SOMA: Mfahamu kijana mbunifu mkubwa wa majengo duniani aliyezaliwa Tanzania.
Lakini bado nilizidi kujiuliza, hili jina Bikira wa
Kisukuma maana yake ni nnini? Alikuwa akimaanisha kitu gani, chanzo chake ni
nini, lakini mpaka leo hii sikuwa nimepata jibu lililokuwa dhahiri. Lakini
niliposikia yeye mwenyewe akilitaja redioni bila aibu yeyote, wafanyakazi
wenzake akiwemo Gadner G. Habash na Mpoki wakilitaja bila kumungunya maneno na
hata mabosi wake kama meneja wake Denis Sebo wakilitaja jina la Bikira wa
Kisukuma bila wasiwasi nikashawishika kabisa kwamba jina hilo halikuwa na jambo
lolote lile baya na lilipaswa tu kuchukuliwa kawaida kama lilivyo na kila mtu.
Utata wa jina hili la Bikira wa Kisukuma umefanya watu
wengi kuwa na tafsiri nyingi hasi na chanya, tukiachana na zile hasi kama ile
niliyokuwa nayo mwanzoni kabla sijamfahamu vizuri Seth Katende kama mtaalamu aliyebobea wa
masoko katika mitandao ya kijamii na nje ya mitandao hiyo. Miongoni mwazo ni
ile ambayo wanadai eti Seth alijiita hivyo akimaanisha kwamba yeye alikuwa na
vipaji vingi mno ndani yake ambavyo vilikuwa bado kufanya kazi, maana ya neno
bikra au bikira ni kitu ambacho bado hakijaguswa bado, bado kutumika. Hivyo
vipaji vyake yeye kama kijana kutoka Usukumani vilikuwa bado kabisa vipya.
Lakini pia mimi mwenyewe binafsi nimefikiria dhana
nyingine moja katika mtazamo wa kibiashara zaidi au kimasoko na ambayo inawezekana
kabisa kuwa ndiyo iliyomfanya Seth kutumia jina hilo, “Branding” au kwa lugha
nyingine kujijengea jina. Katika ulimwengu wa masoko, na hasahasa katika
mitandao ya kisasa ya kijamii, branding ni kitu muhimu sana. Branding au
kutengeneza jina maana yake ni kwamba, mhusika atajiita jina, kutengeneza mazingira,
logo, au alama nyingine yeyote ile ambayo itamtofautisha na watu wengine
wanaofanya kitu kinachofanana na cha kwake.
Unaweza kufanya hivyo pia kwa bidhaa au huduma unayoitoa.
Mazingira hayo ya kipekee utakayowajengea wateja au wafuasi wako akilini mwao
yanapaswa kuwa zaidi ya alama au jina, hali hiyo inatakiwa kuishi na kudumu
akilini mwao na katika mioyo yao daima NA HICHO HASA NDIYO BIKIRA WA KISUKUMA
ALICHOTAKA KIFANYIKE, NA LEO HII KUTHIBITIKA RASMI PALE LEADERS CLUB baada ya watu wengi kushuhudia jinsi walivyomfahamu Seth Katende.
SOMA: Kutafuta soko la bidhaa zako kunahitaji ubunifu mkubwa.
SOMA: Kutafuta soko la bidhaa zako kunahitaji ubunifu mkubwa.
Seth kama Mwanamasoko(Maketeer) mahiri, hakujali watu watamchukuliaje kujiita bikira ili hali
yeye ni mtoto wa kiume, wala hakuogopa ikiwa baadhi ya watu wangemchukulia na
kumhusisha isivyosahihi na watu wa mapenzi ya jinsia moja. Alichozingatia yeye
ni kampeni zake za kimasoko mitandaoni jambo ambalo alifaulu kwa asilimia zaidi
ya mia moja. Hata mimi binafsi nakiri kabisa kwamba ukakasi wa jina “BIKIRA WA
KISUKUMA” ndio ulionisukuma kumfahamu kwa undani Seth Katende.
Unapotaka kujenga jina imara la biashara yako au lako mwenyewe hupaswi kuyumbayumba, na inatakiwa kwanza wewe mwenyewe na wale wanaokuzunguka kuliamini na kulikubali jina lako vinginevyo wateja wa mbali hawataweza kufanya hivyo. Na kumbuka siyo jina kama jina ndiyo litakalojenga mahusiano mazuri na wateja bali ni zile faida kwa mteja, sifa njema au chochote kile kinachomridhisha mteja kinachoambatana na hilo jina ndicho kinachojenga huo mshikamano. Seth hata angejiita "Mfalme" lakini alichokuwa akikifanya kikawa hakiwanufaishi chochote watu, hakuna mtu yeyote angeguswa na jina hilo. Lakini vyovyote vile angejiita yeye na jina hilo likiambatana na sifa njema au faida kwa wafuasi wake bado angekumbukwa tu.
Hivyo tunajifunza kwamba, tusiyumbishwe ovyo na maoni ya watu, bali tuangalie ni kitu gani sahihi tunachokifanya kwa manufaa ya wateja wetu au jamii tuliyoamua kuihudumia. Leo hii watu wengi hawahangaiki kutaka kujua sababu za kifo cha seth katende, wala hawataki kujua chanzo cha kifo cha Bikira wa Kisukuma, bali wanataka kujua Bikira wa Kisukuma, Seth Katende ni kitu gani hasa cha tofauti alichokifanya mpaka watu wamuenzi kiasi hicho. Kilichomuua Bikira wa Kisukuma hakiwezi kuwa na uzito kama kile alichokifanya wakati wa uhai wake hapa duniani.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AMEN.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AMEN.
0 Response to "SETH KATENDE, MWANAUME UTAJIITAJE BIKIRA?"
Post a Comment