Kuajiri wafanyakazi katika biashara ni jambo
lisiloepukika hata kidogo ikiwa mmiliki wa biashara au mjasiriamali atataka
mafanikio katika biashara yake. Wakati biashara inapoanzishwa mjasiriamai
anaweza akavaa kofia zote yeye mwenyewe kwa kufanya majukumu yote kuanzia kuwa
mkurugenzi, meneja wa biashara, mlinzi, karani, mpokeaji wageni(receptionist),
mtunza pesa(cashier), mtunza stoo(store keeper) na hata mhasibu peke yake.
Lakini kwa kadri muda unavyozidi kwenda na biashara
kupanuka zaidi, maendeleo hayo yatahitaji nguvukazi zaidi katika kuhakikisha
majukumu muhimu ya biashara yanatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa
weledi unaotakiwa. Kumbuka mjasiriamali au mmiliki wa biashara anapokuwa akivaa
kofia hizo zote kuna baadhi ya kazi ambazo anakuwa anazimudu zaidi kuliko
nyingine na nyingine anakuwa anazifanya bila ya kuwa na weledi wa kutosha ama
uzoefu unaotakiwa lakini hana budi kufanya hivyo kwani anakuwa hana chaguo
mbadala kutokana na ufinyu wa mtaji.
Baada sasa ya kuvuka hatua hiyo ya kuanza biashara na
kuingia katika hatua mpya ya upanuzi wa biashara kwa kuajiri wafanyakazi au
wasaidizi, zipo faida nyingi zitokanazo na kitendo cha kuweka wasaidizi lakini
pia kama ilivyokuwa kawaida kwa ujasiriamali changamoto ni lazima ziwepo na kwa
kuwa mjasiriamali hupaswi kuogopa changamoto unatakiwa ufahamu namna ya
kukabiliana na changamoto hizo kusudi uweze kupata mafanikio katika biashara
yako uliyokusudia kuyapata.
Moja ya changamoto kubwa mfanyabiashara au mjasiriamali
atakayokutana nayo ni gharama au mzigo wa gharama zitakazosababishwa na kuajiri
mfanyakazi au wafanyakazi katika biashara yake. Kumbuka huko nyuma mjasiriamali
huyu alizoea kufanya kila kitu peke yake na hivyo hakuwa na gharama yeyote
kuhusiana na mfanyakazi. Hata hivyo zipo changamoto zingine nyingi kama vile
wafanyakazi kukosa uaminifu, kuwa wezi na hata kufanya uzembe wa aina
mbalimbali unaoweza kusababisha biashara kutokuweza kutengeneza faida kama
inavyokusudiwa lakini nyingi ya changamoto hizo zinaweza zikapatiwa suluhisho
kupitia mbinu mbalimbali.
Kwa kiasi kukubwa matatizo ya kuajiri wasaidizi katika
biashara au changamoto zozote zile msingi wake mkubwa upo katika gharama za
biashara. Hii inamaanisha kwamba ikiwa utaajiri mfanyakazi, tayari unaongeza gharama
katika biashara, ikiwa mfanyakazi atakuibia maana yake gharama kwenye biashara
itazidi kuwa kubwa, halikadhalika ikiwa mfanyakazi atafanya uzembe wowote ule,
ni mzigo pia kwa biashara.
Hata unapompa marupurupu mfanyakazi wako pia unaongeza
gharama kwenye biashara. Hivyo basi unaweza ukaona kwaba mfanyakazi katika
biashara ni suala nyeti sana linalohitaji umakini wa hali ya juu kushughulika
nalo. Kama mjasiriamali makini unapaswa kujua mbinu zote sahihi za namna ya
kuajiri wafanyakazi na jinsi ya kuwatendea kusudi waweze kuifanikisha biashara
yako badala ya kuiua.
Gharama
halisi za wafanyakazi wako
Mara nyingi tunapowaajiri watu wa kutusaidia katika
biashara zetu huwa tunaangalia zaidi ule mshahara wa mwezi tunaokubaliana nao
tu, hatuzingatii gharama nyinginezo mbalimbali ambazo huwa tunaingia wakati
mfanyakazi huyo akiwa anaendelea kufanya kazi. Zipo gharama utakazolazimika
kumlipia mfanyakazi wako nje ya mshahara wake penda usipende ikiwa utataka
kweli mambo yaende na biashara yako iweze kufanikiwa na kinyume cha hapo basi
ndipo hukuta mambo hayaendi, wafanyakazi wanaamua kugeuka wezi, wazembe,
kutokufanya kazi kwa motisha, kuacha kazi baada ya muda mfupi na hata kula
njama na wezi au majambazi kwa ajili ya kukudhuru au kukutia hasara.
Haitoshi tu kumlipa mfanyakazi mshahara wake
mliokubaliana hasa hasa mishahara yetu hii ya kibongo ambayo mara nyingi
unakuta haitoshelezi hata gharama za maisha za mtu za nusu mwezi. Mbali hata na
gharama kwa maana ya fedha kitu cha kwanza mfanyakazi anachokihitaji ni
mazingira rafiki na wezeshi ya kazi ambayo yatamvutia mfanyakazi hata kutopenda
kukaanyumbani kwake, kila mara atamani kuwa maeneo ya kazini tu. Na hili ni
lazima likuingize gharama kidogo kwa mfano maeneo ya kazi kuwa na vivutio kama
chai, chakula, eneo zuri la mapumziko, vifaa bora vya kazi, na vitu kama
intaneti nk.
Katika biashara kubwa kuna gharama zaidi kwa mfanyakazi,
kama vile, gharama za mafunzo, kodi ya mishahara(PAYE TAX), malipo ya uzeeni,
bima za afya, gharama za sherehe na viburudisho mbalimbali, malipo na likizo
baada ya kujifungua nk. Si hivyo tu zipo gharama nyingine hata mtu huwezi
kuzifikiria kama zipo kwa mfano kumbuka hata bili za umeme, maji, jengo na simu
mfanyakazi wako atakazotumia pengine nje ya shughuli za kawaida za biashara
kama vile kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki au kuchati masula yake binafsi
nayo huongeza gharama zinazotakiwa kulipwa na wewe mmiliki wa biashara.
Unatakiwa unapopiga gharama ya mfanyakazi wako kwa mwezi basi uhakikishe na
gharama hizi nyingine unazizingatia pia.
Kwa mfano unaweza kuwa mfanyakazi unamlipa shilingi kaki
tatu kwa mwezi,utakapoamua kukokotoa gharama nyinginezo zote zilizojificha
unaweza kuja kukuta gharama halisi ya mfanyakazi huyo ni zaidi hata ya shilingi
lkaki tano kwa mwezi mmoja. Sasa hebu fikiria unao labda wafanyakazi wane au
watano itakuwa kiasi gani? Ukiwa na roho ndogo unaweza hata kuwapunguza au
kuwafukuza wote ukidhani labda utapunguza gharama kumbe wakati mwingine wala
siyo sahihi. Kujaribu kupunguza sana matumizi kwa kubana kupita kiasi gharama
unazowalipa wafanyakazi wako ni kosa kubwa sana litakalosababisha mazingira ya
kazi kuwa magumu na mwishowe wafanyakazi hao kutokufanya kazi katika ubora
unaotakiwa.
SOMA: Ajira siyo laana, bali mtaji wa uhakika kuliko aina nyingine zote za mitaji.
SOMA: Ajira siyo laana, bali mtaji wa uhakika kuliko aina nyingine zote za mitaji.
Siyo vibaya kujua ni kiasi gani wafanyakazi wako
wanakugharimu lakini hakikisha pia unawatumia kwa ufanisi unaolingana na zile
gharama unazowalipa, na kuwatumia kwa ufanisi siyo kuwawekea sheria na taratibu
kali kupindukia, ndiyo, wapo watu wasiokuwa na masikhara kabisa na wafanyakazi
wao, wao muda wote huhisi wanaweza kuwaibia, watahangaika kuweka ulinzi wa kila
aina, macctv camera, masoftware ya kila aina ya kompyuta lakini wanachoshindwa
kufahamu ni kwamba haiwezekani kabisa kudhibiti utashi wa mtu mwenye akili
timamu kama wa kwako, na njia pekee ya kufanya hivyo ili kujenga utengamano katika
biashara yako na mwishowe uzalishaji uliokuwa na tija ni kuwapa motisha
wafanyakazi wako kwa kadiri inavyowezekana, kuwawezesha, kuwapa uhuru wawe
wabunifu, kuwatia moyo, lakini
pia huku ukihakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa taratibu zinavyowataka
kufanya.
Usimamizi imara wa biashara yako uwe palepale na
mfanyakazi anayekiuka kwa makusudi taratibu zilizowekwa awajibishwe bila
kuchelewa kabla mambo hayajawa mabaya zidi.
...........................................................................................
Kwa elimu zaidi ya biashara na ujasiriamali, pata moja kati ya vitabu vifuatavyo au vyote kwa pamoja kutoka self help books Tanzania.
1
2
3
Vitabu vya kawaida vya karatasi(hardcopy) vinapatikana katika ofisi yetu, Mbezi Kwa Msuguri stendi.
Softcopy kwa njia ya e-mail, unatuma pesa na anuani yako ya email kisha tunakutumia kitabu/vitabu muda huohuo.
Bei ya vitabu kutoka juu, ni;
1. Tsh. elfu 20 hardcopy kwa sh elfu 10 softcopy.
2. Tsh. elfu 10 hardcopy kwa tsh. elfu 5 softcopy
3. Tsh. elfu 5 hardcopy kwa tsh. elfu 3 softcopy
SIMU: 0712202244 AU 0765553030
0 Response to "UKIJUA GHARAMA HALISI ZA WAFANYAKAZI KWENYE BIASHARA YAKO, UTAWAFUKUZA KAZI"
Post a Comment