Kama haupo huru ni vigumu sana
kupata mafanikio ya kweli katika nyanja yeyote ile ya kimaisha. Hebu Jichunguze
kwa umakini kama wewe ni mtu mzima 'over 18' na bado asilimia kubwa ya mambo
yako muhimu ya kimaisha huwezi kuyaamulia bila ya ushawishi kutoka kwa mtu
mwingine.
Je, ni mwenza, ni ndugu yako, ni mzazi, ni mwenye nyumba, ni
rafiki, ni jirani yako, ni mlezi wako, ni tajiri yako, au ni bosi wako kazini
anayeyadhibiti maisha yako?
Kwa kuwa hatma ya mtu yeyote
yule ipo mikononi mwake mwenyewe, haipaswi mtu mwingine ayadhibiti maisha yako kwa namna
yeyote ile. Inawezekana kwa sababu fulani mfano wa hali za kiuchumi zikamfanya
mtu maisha yake yakadhibitiwa kwa muda fulani lakini hali hiyo kamwe haipaswi
kuachwa na mhusika ikadumu milele kwa maisha yake yote. Ni lazima utafute mbinu
za kujinasua.
Unakumbuka namna nchi hasa za
Kiafrika zilivyojikomboa kutokana na ukoloni?. Basi na kwa mtu mmojammoja
inafaa pia kuwa hivyo. Ni swala la muda tu binadamu kamwe hajaumbwa kudhibitiwa
kama mnyama afugwaye. Hapa ninayo mifano halisi miwili ambayo mwenyewe binafsi
niliwahi kuishuhudia. Kabla hatukwenda kuangalia ni nini cha kufanya ikiwa
unajikuta katika hali mbayo hauna uwezo kamili wa kuyasimamia maisha yako
mwenyewe tuone kwanza mifano hiyo.
Dada mmoja, hapa nitampa jina
lisilokuwa la kwake kama ‘Mariam’,
alikuwa akifanya kazi katika duka la tajiri mmoja. Pale dukani palikuwa na
mfanyakazi mwenzake mwingine yeye nitamuita ‘Angela’. Wote wawili walikuwa wamekabidhiwa duka lile waliendeshe
huku tajiri akiwa anafika pale siku za manunuzi ya bidhaa na kufanya hesabu tu.
Ikafika kipindi fulani Mariam akawa anasumbuliwa na homa mara kwa mara kiasi
ambacho kila mtu aliyemfahamu akawa anashituka kwa jinsi alivyokuwa akikonda
siku hadi siku. Mariam alikonda hadi akafanana na mtoto mdogo.
Hata rafiki wa kiume, ‘boy
friend’ wa Mariam alianza kuingiwa na wasiwasi kwani kila mtu maeneo yale kwa
wale wa rika lake walianza kumtania na kumwambia, “kulikoni shemeji siku hizi
mbona anakonda vile, au tayari keshaukwaa?, wahini hospitali mkapime”. Mariam
alikosa kabisa raha kwani kila mtu alianza kumnyanyapaa utadhani tayari
walishampima na kutambua hali yake kiafya. Na mtu aliyeongoza unyanyapaa huo
alikuwa ni yule yule mfanyakazi mwenzake, Angela.
Angela alimkazania sana Mariam
eti, aende kituo cha afya kujua hali yake ikiwa kama alikuwa tayari
ameshaathirika na maambukizi ya vvu. Kwa kuwa kiumri Mariam alikuwa mdogo kwa
Angela basi kwa kiasi kikubwa kila aliloambiwa na Angela alikubali, “ndiyo
dada” japo wakati mwingine alikubali tu kwa shingo upande.
Ilionekana Mariam anatokea
familia duni na Angela kwa mbwembwe nyingi aliitisha mchango pale kijiweni,
(kumbuka palikuwa ni maeneo ya biashara palipokuwa na biashara nyingi) akidai
ni mchango wa matibabu ya Mariam, tumchangie kabla hajafa kwani akishakufa
kuchanga ni unafiki.
Zilipatikana fedha kidogo na
kwa msaada wa bosi wao zikatimia kiasi kama shilingi elfu hamsini hivi. Kwa
kiasi Angela alivyokuwa akishadidia suala lile la ugonjwa wa Mariamu, mtu
yeyote yule angedhani labda walikuwa ni mtu na dada yake wa damu kumbe wala
hawakuwa na uhusiano wowote ule zaidi ya kufanya kazi pamoja.
Angela alipanga siku ya
kumpeleka Mariamu hospitalini na jambo lile akawa anamweleza kila mtu huku
shauku yake kubwa ikionekana dhahiri kuwa alitaka akathibitishe kwamba Mariamu
alikuwa na ugojwa wa ukimwi. Masikini hakuna mtu yeyote aliyeonekana wala kumsaidia
Mariam kwa kumpa moyo, msaada wake mkubwa ulionekana ni kutoka kwa Angela
aliyeamua kumtafutia michango na kumpeleka kwa dokta. Mariam hakuthubutu
kupinga chochote kile hata kama aliona hatendewi vyema kwa kuhofia kuonekana
mtovu wa fadhila, ilibidi avumilie madhila yote. Kwa wakati ule ni kama vile
maisha ya Mariam yalikuwa mikononi mwa Angela.
Siku mbili kabla ya siku
waliyopanga kwenda kucheki afya ya Mariamu, Angela alisikika akimwambia Mariamu
kwamba watakapofika kwa daktari, moja kwa moja amueleze kwamba amefika pale
kupima VVU na hata kama ataogopa kumweleza dokta hivyo, basi jukumu hilo
atalifanya yeye mwenyewe Angela kwa kumfahamisha kuwa Mariamu alikuwa mdogo
wake wa kuzaliwa tumbo moja hivyo kafika pale ili pamoja na magojwa mengine
apimwe kwanza ukimwi.
Kwa kweli sakata lile toka
linaanza mpaka siku hizo mbili kabla Mariamu hajapelekwa kwa dokta kwenda
kupimwa ukimwi na Angela nilikuwa naliona. Kwa bahati nzuri rafiki wa kiume wa
Angela tulikuwa tunafahamiana na mara kadhaa hata mimi huwa nilikuwa nikipenda
kumtania juu ya kukonda kwa “shemeji
yetu Mariamu” .
Siku hiyo nilikaa naye mahali
tukajadiliana “serious” kuhusu hali
ya Mariamu na jinsi mwenzake Angela alivyokuwa akiichukulia hali ile ijapokuwa
alikuwa akijidai kuwa anamsaidia.
“Ni msaada wa namna gani huo anaompa?”
nilimuuliza boyfriend huyo wa Mariam. “Kila
binadamu anahitaji uhuru wa kujiamulia mambo yake mwenyewe anavyotaka yawe,
faragha na heshima hata ikiwa yupo mahututi” nilimueleza kwa uchungu. Baada
ya kujadili, nikamtaka amwambie Mariam kwamba nilitaka kuzungumza naye kabla
hajapelekwa hospitali siku ya Jumatatu. Mariamu siku ileile alinitafuta
tukaketi mahali, na sikuchelewa, kwanza nikamuuliza “kwani wewe Angela mna
uhusiano gani?” “Hatuna uhusiano wowote zaidi ya kufanya kazi naye hapa kwa
bosi wetu” Alinijibu Mariamu kwa hali ya unyonge.
Niliendelea kumwambia Mariamu
kwamba, hata ingelikuwa Angela ni mama yake mzazi, bado hakuwa na haki wala
ruksa ya kumlazimisha eti aende kupima afya yake ili kujua hali yake ya VVU.
Isitoshe nilimwambia Angela hata kama angetoa yeye mwenyewe zile pesa za
matibabu, bado hakuwa na haki wala uhalali wa kumtangaza kila mahali kwa namna
alivyofanya.
Nilichomshauri Mariamu ni
kwamba, akubali waende haspitalini, ila wakiwa kwa dokta akatae katakata
kupimwa ukimwi mbele ya Angela na aseme kama ni ukimwi basi ataamua mwenyewe
kwa ridhaa yake siku nyingine wala siyo kwa kulazimishwa na mtu yeyote yule.
Kweli Mariamu alifanya vilevile
kama nilivyomshauri kwa kumuumbua Angela mbele ya daktari. Daktari naye
palepale alimpa Angela elimu ya kutosha juu ya haki za msingi za binadamu
hususani kuhusiana na kujua hali ya kiafya ya mtu kama vvu. Mariamu alipata
ujasiri wa ajabu baada ya tukio lile, na akaapa kuwa hatakubali tena siku
nyingine maisha yake yawe mikononi mwa mtu wingine.
Ilikuja kubainika kumbe Mariamu
alikuwa na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na wala siyo ukimwi kama wengi walivyomdhania,
akatumia dawa kwa usahihi na sasa maisha yake yanaendelea vizuri.
Mfano wa pili, unamhusu mtu mmoja ambaye
jina lake halisi sitaweza kulitaja, bali nitamuita tu kwa utani “Mangi”. Mangi baada ya kumaliza masomo
yake na hatimaye kuanza kazi za ufundi umeme jijini Dar es salaam, aliamua kuoa
na akampata mchumba kutoka mkoani Tanga ambaye naye alikuwa akiishi jijini Dar
es salaam kwa dada yake aliyekuwa naye ameolewa.
Uamuzi wa Mangi ulikuwa ni
kinyume kabisa na matarajio ya wazazi, ndugu na jamaa zake huko Moshi ambao walitaka
Mangi akaoe nyumbani kwao kijijini alikozaliwa. Wazazi ndugu na jamaa hao
walianza chokochoko hasa baba yake mzazi aliyediriki kusema hatampa radhi
endapo ataendelea kuishi na mwanamke asiyekuwa wa kabila lake. Dada zake na
hata kaka zake wote lao llikuwa moja, kuhakikisha Mangi haishi na mwanamke
aliyemuoa.
Walimzushia mara mke wake
alikuwa mchawi, alipochelewa kuzaa wakadai hazai na mambo chungu nzima. Kipato
cha Mangi kilikuwa ni cha kawaida lakini ndugu zake walidai mwanamke huchukua
fedha na mali za ndugu yao na kupeleka upande wa mwanamke kujenga nyumbani kwao
na alikuwa amemfunga Mangi kwa dawa za kienyeji ili asiweze kumshitukia. Kwa
ujumla Mangi aliwekewa vikwazo vya ajabu ajabu mpaka mwenyewe akaanza kujutia
kumuoa yule mwanamke.
Kipindi fulani baba yake Mangi
aliugua na kwa bahati mbaya akafariki dunia. Watoto wake wote walifika Moshi
kumzika wakiwa wameongozana na wake au waume zao kasoro Mangi peke yake
aliyekwenda peke yake kwani ndugu walishaapa kwamba ikiwa mke wake angekanyaga
Moshi basi wangemkatakata kwa mapanga.
Kule Dar alikobaki mke wa
Mangi, baada ya msiba wa baba mkwe wake alidhani labda mumewe angerudi baada ya
mazishi, lakini hakumuona, alisubiri tanga liishe napo wala hakusikia simu
yake. Akaamua kumpigia Mangi namba yake nayo ilikuwa haipatikani. Kimya
kiliendelea mke wa Mangi na mwanaye mchanga Rafaeli wakiwa peke yao, mwezi,
miezi na hata mwaka ukakatika bila hata ya kujua kama Mangi alikuwa hai au
alikuwa amekufa. Hata baada ya kuwauliza baadhi ya watu waliomfahamu
walimueleza tu kwa kifupi kuwa Mangi alikuwa ameshaoa mwanamke mwingine huko
kwao Moshi na ndugu zake wenye uwezo wa pesa walikuwa wameshamjengea kila kitu,
nyumba ya kuishi pamoja na kumfungulia biashara ya kuuza nguo za mitumba katika
soko la Kiboriloni.
Mke wa Mangi aliishi kwa
uchungu muda mrefu akimkumbuka mumewe bila matumaini yeyote tena ya kuja
kuonana naye. Hatimaye alimpata mtu mwingine wakaanza tena upya maisha. Siku
moja akiwa nje ya nyumba yao maeneo ya Kimara Baruti, alimuona Mangi akija
‘amechooka’, akashtuka sana, “Baba Rafaeli ni nini ulichosahau kwetu?”
Mangi huku machozi
yakimlengalenga, alianza kumsimulia mkewe wa zamani madhila aliyokumbana nayo
baada ya kwenda kuoa kwao, alimsimulia jinsi mkewe mpya alivyomnyanyasa na
hatimaye kwenda kuolewa na tajiri mmoja huko Himo anayemiliki vituo vya mafuta.
Siyo hivyo tu alisimulia pia jinsi ndugu zake walivyomtimua kama paka katika
nyumba waliyomjengea na biashara ya mitumba kufilisika. Alieleza kuwa alikuwa
akiishi na kulala katika baraza za maduka ya watu huko Kiboriloni.
Mke wake wa zamani
alimsikitikia na kumwambia, “Baba Rafaeli mpenzi wangu, bado moyoni mwangu
nakupenda, lakini haiwezekani tena mimi kuishi na wewe, kwani tayari kuna
mwenzako keshanichukua na sasa tuna watoto wawili, tena naomba usichelewe sana
hapa kwani yu karibuni kurudi kazini sasa, kama ni mwanao Rafaeli, anasoma
shule ya boding, labda uje siku ya wiki end, nitamwambia aje nyumbani na
nitakuwa nimempa mume wangu taarifa kuwa utafika kumuona mwanao.”
Zipo sababu nyingi zinazoweza
kutufanya kukosa udhibiti wa mambo au maisha yetu kwa ujumla lakini lililokuwa
kubwa sana ni suala la kiuchumi. Ukishakuwa kiuchumi unamtegemea mtu mwingine
tayari, “automatically” wewe maisha yako anayadhibiti yule anayekuwezesha
kiuchumi. Tazama hata suala la Mariamu na Mangi hapo juu, suala la kiuchumi
“PESA” limechukua nafasi kubwa sana. Sababu nyinginezo zina uzito mdogo sana.
Athari za mtu kutokuwa na
udhibiti kamili wa maisha yake huweza kusababisha madhara mengi yakiwamo mtu
kushindwa kujiamulia mambo anayoyapendelea mwenyewe maishani mwake, au ndoto
alizokuwa nazo tangu utotoni kama vile, kujiamulia mwenza wa maisha,
kujichagulia taaluma unayopenda nk. Unaweza kufikiria ni nani atakayeweza
kutatua tatizo hilo kwako?
Hatua za kurudisha udhibiti wa Maisha yako mikononi mwako.
Kwa uhakika hakuna mtu yeyote
zaidi yako wewe mwenyewe anayeweza kuja na kukutatulia shida hiyo ya kutokuwa
na udhibiti wa maisha yako mwenyewe. Na kamwe hautaweza kubailisha hali hiyo
ikiwa wewe mwenyewe hautakuwa tayari kuwajibika kikamilifu kwa vitendo vyako.
1. Yakubali kwanza matatizo yako uliyokuwa nayo, na
kukubali maana yake ni kwamba matatizo hayo ni ya kwako na wala siyo ya mtu
mwingine. Kama kwa mfano ni matatizo ya kiuchumi, kubali kwanza kwamba wewe
ndiye mwenye hayo matatizo. Umiliki maana yake ni udhibiti na kitu kama
unakithibititi maana yake pia unao uwezo wa kubadilisha hali au mambo.
2. Anza kufanya maamuzi.
Baada ya kubaini tatizo
ulilokuwa nalo na namna ulivyokuwa tegemezi, ni wakati sasa wa kufanya maamuzi
ni eneo gani katika maisha yako unalotaka kubadilisha, kama kwa mfano ni suala
la kiuchumi basi ni wakati wa kuamua ni nini utakachofanya, labda ni biashara,
kazi au uwekezaji wowote ule utakaokuwezesha hatimaye kuwa imara na kuacha kuwa
tegemezi.
Pengine kuna vitu vinakunyima
raha kwa mfano kazi uliyokuwa nayo, biashara, mahusiano nk. hufurahishwi navyo,
basi ni wakati wa kuamua uachane navyo au uendelee navyo lakini huku ukitafuta
njia za kurekebisha hali inayokunyima raha.
3. Fanya utafiti.
Badala ya kufanya maamuzi
ilimradi tu umeyafanya, hakikisha maamuzi yako yanazingatia zile taarifa bora
kabisa ulizokuwa nazo kuhusiana na ufumbuzi wa tatizo unaloamua kulitatua. Kama
ni biashara basi hakikisha unazama katika biashara ile unayojua utamudu
kuifanya na nyenzo za kuifanya utakuwa nazo. Kwa mfano njia Mangia liyotumia
kutatua tatizo lake haikuwa sahihi, ilikuwa ni njia ya mkato iliyomsababishia
kilio na kusaga meno badala ya suluhisho.
4. Vitendo, tekeleza, Maamuzi peke yake na utafiti
pasipokuwa na vitendo halisi hakutoshi kuleta mabadiliko, fahamu malengo yako
na uweke mikakati ya kuyafikia, hakikisha pia malengo hayo ni ya kwako mwenyewe
hujashinikizwa na mtu mwingine kuyafanya.
Kuna uhusiano mkubwa sana kati
ya mafanikio ya mtu na udhibiti wa maisha yake au uhuru aliokuwa nao wa
kujiamulia mambo yake menyewe bila ya kupangiwa na mtu mwingine. Ndiyo maana
hata katika nchi zile zenye maendeleo makubwa katika ujasiriamali kama Marekani
na Ufaransa neno “UHURU” lina maana kubwa sana. Mjasiriamali anayebanwabanwa
iwe ni na serikali, mtu binafsi ama taasisi nyingine yeyote ile hawezi kufanya
jambo lolote lile la maana.
Tuchukulie mfano unamiliki
bishara lakini biashara hiyo kuna mambo ambayo ni lazima watu wengine waamue
kabla wewe hujayatekeleza, bila shaka biashara hiyo itakusumbua na hautaweza
kuifanya kwa ufanisi unaotakiwa. Mathalani katika biashara yako unatumia umeme
na mwenye nyumba ndiye anayedhibiti mita ya umeme, mwenye nyumba anaweza muda
wowote kuzima umeme akidai umeisha na wewe huna namna nyingine bali kutoa pesa
hata kama kweli umeme haukuwa umekwisha.
Mifano ya ukosefu wa udhibiti katika
eneo hili la biashara ipo mingi na ni sababu kubwa ya wajasiriamali wengi
kukwama na kutokufikia mafanikio wanayostahili katika maisha yao na dawa yake
pekee ni kuamua hata kama ni kwa uchungu kiasi gani kujiondoa katika udhibiti
wa namna hiyo, ni bora mtu ukaanza upya kitu kingine hata kama ikiwa ni kidogo
kiasi gani kwani kitaendelea kama hakuna tena udhibiti wa mtu mwingine. Kuna
watu waliachana na ubia wa biashara na kwenda kuanzisha biashara zao wenyewe
japo kwa watu wa nje ilionekana ubia ule ulikuwa unawanufaisha.
………………………………………………………………………
Ndugu Msomaji wa Blogu hii,
tumerudi tena katika ile kampeni yetu ya KUJIRUDISHIA UKUU WAKO ULIOPOTEA,
kampeni tuliyoanza nayo mwezi ule wa kwanza mwa 2017 ulipokuwa unaanza. Katika
awamu hii ya pili na ya mwisho tutahakikisha kila mtu anayefuatilia kampeni hii
basi anatimiza ndoto yake ambayo ni kujirudishia tena uwezo wake aliokuwa nao
hapo awali, iwe ni katika Nyanja yeyote ile mfano, kichumi, kiafya, kimahusiano
nk. Na kwa wale ambao basi ndio wapo katika ubora wao watapata njia sahihi za
kuhakikisha wanadumu katika ubora huo bila ya kuupoteza kwa kipindi kirefu. Fuatana
nasi kila siku katika makala zetu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, blogu
na kwa njia ya email yako.
Kwa vitabu bora kabisa vya Ujasiriamali katika lugha adhimu ya kiswahili, chagua hapa katika duka la self help books, SMART BOOKS TANZANIA. Ukihitaji kitabu chochote kile iwe ni softcopy au hardcopy wasiliana nasi kupitia namba za simu 0712202244 au 0765553030
Kupata kitabu chenye kanuni maalumu ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio katika lugha ya kiswahili bure kabisa bila malipo, bonyeza maandishi yafuatayo, KANUNI NA SIRI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO.
0 Response to "HIVI UNAJUA NI NANI ANAYEDHIBITI MAISHA YAKO?"
Post a Comment