JINSI YA KUPANGA MALENGO YA BIASHARA AU MAISHA YANAYOTIMIZIKA KWA UFANISI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUPANGA MALENGO YA BIASHARA AU MAISHA YANAYOTIMIZIKA KWA UFANISI

NAMNA YA KUWEKA MALENGO

Malengo ni nini?
Maana ya malengo hutajwa mara nyingi sana na imekuwa ikuhusianishwa na watu wengi kwa karibu sana  na siri ya mafanikio katika maisha ya binadamu. Malengo ni vitu au matokeo mahsusi mtu, kikundi ama mfumo fulani unaopanga kutimiza katika muda fulani uliopangwa. Kuna malengo ya maisha kwa ujumla, malengo ya biashara, malengo ya kazi nk.

Namna ya kujiwekea malengo.
Kwanza kabla hatujaendelea, kumbuka kwamba malengo yanaweza yakawekwa na mtu binafsi, kikundi, kampuni, serikali au taasisi yeyote ile. Sasa tutaanza kwa kuzungumzia zaidi malengo yanayowekwa na mtu binafsi(Personal Goal Setting)

Soma: Tayari malengo yako kiuchumi ya mwaka 2017 umeshayaandika mahali?

Watu wengi hujikuta wakifanya kazi kwa bidii sana lakini cha kushangaza hawaoni mafanikio yeyote yale ya maana. Sababu kubwa inayochangia hali hii ni kutojishughulisha kufikiria ni nini hasa wanachokitaka maishani mwao.

Usipofahamu unachotaka maishani, kamwe hautaweza kujiwekea malengo na matokeo yake utaishia kugusagusa kila jambo, mara leo umesomea hiki, kesho umeanzisha kile, keshokutwa umeacha umeomba kazi fulani, mtondogoo umeacha umeanzisha kile. Na hali itaendelea hivyo hivyo mpaka unakata tamaa kabisa ya mafanikio.

Mchakato wa kujiwekea malengo humsaidia mtu kugeuza ndoto yake au maono kuwa kitu halisi, humsaidia kwa kuelewa kwa uhakika kabisa ni kitu gani anachokitaka na ataweza kuelekezea nguvu zake zote katika jambo hilo ikiwa ni pamoja na kukwepa chochote kile kitakachotaka kumtoa nje ya malengo aliyojiwekea.

Kwanini kujiwekea malengo ni muhimu?
Malengo yanahitajika katika nyanja zote za kimaisha, iwe ni biashara, michezo, elimu, kazi nk. Yanakufanya uweze kukusanya maarifa na rasilimali zote kama vile muda na pesa katika kukamilisha jambo muhimu zaidi katika maisha yako.

SOMA: Uamuzi mgumu wa kuchukua mwaka huu kwa biashara yako.

Kumbuka kwamba unaweza kupata kitu chochote kile unachokitaka maishani, lakini huwezi ukapata kila kitu unachohitaji kwa wakati mmoja. Rasilimali, muda na fedha mara zote ni kidogo haziwezi kukuruhusu kufanya hivyo, kwa hiyo njia pekee iliyopo ni kuchagua lengo moja kubwa na lililokuwa muhimu kuliko mengine yote, ukaelekezea rasilimali na nguvu zako zote kwalo na matokeo yake ni lazima tu yatakuwa mazuri.

Hatua za kuweka malengo;
§  Tengeneza picha kubwa akilini ya kile unachotamani kuwa nacho maishani (ndoto/maono), labda tuseme ya mwaka mmoja, miwili au hata mitatu ijayo na kuendelea.
§  Weka Lengo kuu/Dhamira kuu ya kile unachotaka kukifikia.
§  Tengeneza malengo madogomadogo kutokana na lengo lako kuu.
§  Weka(tengeneza) mpango.
§  Tekeleza mpango.

Wana elimu ya mafanikio wengine hatua hii ya kuweka mipango katika kufanikisha malengo hutofautiana kidogo ijapokuwa wote  kwa ujumla wanakubaliana katika ndoto, malengo na utekelezaji. Kuna wanaoponda suala la kuweka mipango(Plans), kwamba mtu anaweza tu kufikia mafanikio yeyote yale ilimradi tu awe na ndoto kichwani, kisha aamini kwamba ataweza kutekeleza ndoto hiyo. Swala la utekelezaji wanaamini litakuja tu lenyewe kupitia mawazo ya ndani na nguvu kuu ya asili(Mungu)

SOMA: Maajabu ya kufikiri mnambo makubwa na kwanini uweke malengo makubwa maishani.

Wanasema kuweka mipango au malengo maana yake, tayari ni mambo unayoamini unayaweza, hivyo siyo lengo lenye changamoto tena. Kwa upande mwingine, wengine wanaamini huwezi ukafikia mafanikio pasipo kwanza kuwa na mipango madhubuti. Kwa mfano huwezi ukazingatia jinsi ya kupanga bajeti au kubana matumizi wakati unapotaka kutimiza mipango ya maisha au malengo ya biashara kama huelewi namna bora ya kufikia malengo hayo.

Mbinu za biashara mbalimbali ni lazima zihusiane na malengo na mipango hata ikiwa mtu hataki kukubaliana na ukweli huo. Kabla ya kutekeleza jambo lolote lile, kinachotangulia kwanza akilini ni malengo, kile mtu anachotaka kukifikia baada ya kutekeleza mpango huo anaoufikiria.

Lakini ni juu yako wewe ndugu msomaji uegemee mrengo gani, wa wapinga mipango au malengo, au wale wanaokubaliana na uwekaji wa malengo katika kufikia kile wanachopanga kukipata.

Hata hivyo mipango kama ilivyoelezewa kwa undani katika kitabu cha “Michanganuo ya biashara na Ujasiriamali”, siyo hakikisho asilimia 100% kwamba utafanikiwa kama ulivyopanga, ila, uwekaji wa mipango huongeza uwezekano wa mafanikio kwa kiwangi kikubwa. Ni bora kupanga kuliko kutokufanya hivyo kabisa.

Malengo mazuri ni lazima yawe na sifa zifuatazo:-
·       Yawe yanaeleweka.
·       Yawe yanapimika.
·       Yanatekelezeka.
·       Ni ya uhakika.
·       Yana muda maalumu wa kuyatekeleza.

Kwa mfano badala ya kusema, “Nataka kuwa na fedha nyingi”, sema “nataka kuwa na shilingi milioni 100 mwaka 2018”. Bila shaka lengo kama hili linaweza likatimizwa kama matayarisho ya kutosha yatafanyika.



Vipengele vingine muhimu mtu anavyopaswa kufuata ili kuweza kuweka malengo yanayotekelezeka ni kama ifuatavyo:-

·       Andika malengo yako kwenye karatasi, kwa kufanya hivyo itakusaidia uweze kuyasoma mara kwa mara na hivyo kukaa akilini.
·       Andika kila lengo kwa lugha chanya, mathalani badala ya kusema, “tutapunguza ajali”, sema, “tutazidisha hali ya usalama”
·       Eleza kwa wakati uliopo sasa, mfano usiseme, “Nitaacha kuvuta sigara” sema, “Sasa hivi naacha kuvuta sigara”
·       Weka vipaumbele, ikiwa una malengo mengi, yapange kufuatana na umuhimu ukianza na yale muhimu zaidi, hii itakusaidia kuelekeza nguvu zako nyingi kwa yale malengo yaliyokuwa na umuhimu zaidi.
·       Weka malengo makubwa, malengo madogo kila mtu anayaweza hivyo hayatakusisimua kuyakamilisha.(Think Big)
·       Lengo kubwa livunje-vunje katika malengo madogomadogo kusudi iwe rahisi kutekeleza.
·       Usiweke malengo yasiyotekelezeka, kwa mfano, mtu binafsi kuruka kwenda sayari nyingine, kuota mabawa kama ndege, kuzunguka dunia nzima ukitembea kwa miguu nk.
·       Hakikisha unadumu na malengo uliyojiwekea bila ya kukata tamaa kabisa mpaka pale utakapohakikisha umeyatimiza (Dont Give Up

*Katika kitabu cha “Michanganuo ya biashara na Ujasiriamali” malengo hasa ya kibiashara yamefafanuliwa vizuri sana katika sura inayoelezea jinsi ya kutayarisha Michanganuo ya Biashara, unaweza ukasoma pia malengo na dhamira kuu halisi za biashara mbalimbali moja kwa moja katika michanganuo na mawazo ya biashara zaidi ya 50, ukafahamu namna maneno hayo yanavyotumika.

………………………………………………………………...........

Ndugu msomaji wa makala hii, dhana hii ya Malengo pamoja na dhana nyinginezo kama vile Dhamira kuu, Maono na Dira kwa kimombo unaweza ukasema; Mission, Objectives and Vission, ambazo ni muhimu sana katika ulimwengu wa mafanikio katika kazi, biashara na maisha kwa ujumla.

Dhana hizo zimeelezewa kwa mapana sana katika kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA, Kitabu kilichojipatia umaarufu mkubwa nchini toka 2011, kwa kuwa cha kwanza Afrika Mashariki kuongelea dhana ya MIFEREJI 7 YA KIPATO. Mahali kwingine unaweza ukasikia juu ya Mifereji tofautitofauti ya Pesa au kipato kama vile mifereji 10, 12 nk. lakini Mifereji Orijino ni hii 7 katika kitabu hiki kidogo kutoka Self Help Books Tanzania.

Kama ulikuwa hujasoma kitabu hiki nakusihi kisome kina manufaa makubwa hasa kwa mtu aliyeko njia panda kati ya kujiajiri au kuajiriwa, wanaoanzisha biashara mpya, “start ups” na hata wale wote waliokwishaanzisha biashara zao kitambo na wangependa kuwa tena na mtazamo mpya ili kuhuisha biashara hizo.

MIFEREJI 7 YA KIPATO

Kinapatikana katika mifumo ifuatayo;

HARDCOPY                               sh. 5,000/=
                
SOFTCOPY kwa njia ya email  sh. 3,000/=

SIMU:          0712202244  AU  0765553030

JINA:                    Peter Augustino Tarimo

Kupata vitabu zaidi tembelea; SMART BOOKS TZ


1 Response to "JINSI YA KUPANGA MALENGO YA BIASHARA AU MAISHA YANAYOTIMIZIKA KWA UFANISI"